Kupigana kwa Mwanadamu na Maradhi
NDIYO, ugonjwa ni adui, na mwanadamu ameendelea kupigana nao kwa muda wa karne nyingi. Katika miaka 150 iliyopita, madaktari wamepata ushindi wenye kutokeza sana. Hali ya kutunza usafi iliyositawishwa zaidi, pamoja na dawa za kuchanja na dawa nyingine, katika nchi nyingine, kumesaidia kufanya tauni za wakati uliopita kama tauni ya majipu kuanze kusahaulika.
Walakini pigano hilo halijakwisha hata kidogo. Matatizo yangalipo, mengine yayo yangalipo yajapokuwa maendeleo ya sayansi ya tiba, kama inavyoonyeshwa na kisanduku kinachofuata. Hata kama sayansi ingepata utatuzi wa maradhi yote ya kisasa, bado tauni kubwa kupita zote ingebaki—kifo. Je! faraja yo yote kutokana na hali hiyo itapatikana wakati wo wote?
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
WENGI WANAKUWA WAGONJWA ZAIDI YA INAVYOPASA KUWA KWA SABABU—
* Sehemu kubwa ya jamii ya kibinadamu inapatwa na utapiamlo (haipati chakula kinachofaa). Jambo hilo limetokeza visa vingi vya maradhi ya nyongea, ugonjwa wa kutokwa na damu katika fizi, upofu, tezi la kikoromeo na yanayofanana na hayo. Zaidi ya hayo, mtu asiyelishwa vizuri aweza kupatwa kwa urahisi na magonjwa mengine, kama kifua kikuu na mchochota wa mapafu (pneumonia). Maradhi hayo yanaweza kupunguzwa sana kwa urahisi kwa maskini kulishwa vizuri zaidi.
* Utapiamlo (ukosefu wa chakula kinachofaa) ni tisho hata kwa nchi ambazo zimesitawi. Kwa sababu gani? “Mabadiliko yametokea katika hali ya ulaji wa Waamerika ambayo yanaweza kutokeza shambulio kubwa la utapiamlo (kutokana na ulaji mwingi sana au ulaji mchache) lenye kuharibu afya katika United States kama maradhi ya kuambukia, yenye kuenea ya sehemu ya kwanza ya karne hii. Ulaji mwingi mno wa mafuta, sukari, chumvi, na vileo unatokeza kifo . . . maradhi ya moyo, ugonjwa wa ghafula, kansa, ugonjwa wa sukari, kushupaa kwa ateri (mishipa ya damu), na kunyauka kwa ini.”—“Health,” 1979.
* Shirika la Afya Ulimwenguni linakadiri kwamba asilimia 80 ya magonjwa yote katika ulimwengu yanasababishwa na ukosefu wa maji na usafi. Kati ya watu milioni 10 na milioni 25 kila mwaka wanakufa kwa sababu ya maradhi yanayoletwa na maji machafu au ukosefu wa maji. Karibu hesabu iyo hiyo ya watoto wanakufa kila mwaka kwa sababu ya mojayapo ya maradhi hayo—kuhara kunaua—kama hesabu ya watu waliouawa kila mwaka katika vita ya ulimwengu ya kwanza.
* Hewa tunayopumua inatiwa sumu na moshi unaotoka katika viwanda na motokaa. Vichwa vya magazeti vifuatavyo vinaeleza kisa hicho: “Wanaoumizwa na Uchafuzi wa Hewa katika Tokyo Waongezeka”; “Wingu la Mchanganyiko wa Moshi na Ukungu Lazuia Upumuaji wa Wagiriki”; “Moshi Wenye Sumu Wazuia Upumuaji wa Wakazi wa Mji Mkuu wa Mexico”; “Kupumua Ndani ya Nyumba Kwaweza Kuwa Hatari”; “Uchunguzi wa Amerika Waonya Juu ya Matatizo Makubwa Yanayotokana na Uchafuzi wa Hewa kwa Kaboni Dayokisaidi (carbon dioxide).” Wakati uo huo, visafishaji-hewa vikubwa vya uumbaji, miti, vinakatwa kwa kiasi kinachoanza ekari milioni 25 mpaka milioni 50 kila mwaka. Msiba wa kadiri isiyojulikana uko mbele.
* Uasherati umetokeza tauni ya kaswende na kisonono. Uvutaji sigara umesababisha tauni ya kansa ya mapafu, kusakama kwa hewa katika viungo vya ndani vya mwili, mkamba na maradhi ya mishipa ya damu ya moyo. Uchunguzi wa karibuni unaonyesha kwamba si wavutaji sigara peke yao wanaoumizwa bali pia wenzi wao wa ndoa na watoto.
* Hayo ni baadhi ya mazoea na matatizo ya ujamii yanayozuia hata maarifa ya tiba yaliyopo yasitumiwe kwa njia yenye kufaulu kuondoa magonjwa ya wanadamu.