Ugiriki—Ile Serikali Kubwa ya Tano ya Ulimwengu
Akiwa kama chui mwenye mwendo wa kasi, aliye na mabawa, Aleksanda alitoka ndani ya Misri ili kushinda Esia Ndogo (Uturuki ya ki-siku-hizi), Palestina, Misri, na milki ya Umedi-Uajemi mpaka njia yote ile ya kufika kwenye ukingo wa India. Je! wewe ungependa kujua mengi zaidi juu ya mshindi huyu asiye wa kikawaida, na mambo ambayo Biblia ilisema juu yake?
AKIWA na umri wa miaka 20 tu, Aleksanda kijana alirithi kiti cha ufalme cha Makedoni. Miaka miwili baadaye, kwa kufuata mpangilio wa Philip baba yake, Aleksanda alijiondokea akafanye vita ya kulipa kisasi dhidi ya Waajemi wenye uweza, ambao milki yao ilikuwa upande wa mashariki. Kabla hajaacha, Aleksanda alikuwa ameshinda ulimwengu wa siku yake.
Kijana huyo mwenda-mbio mwenye maarifa ya kijeshi alikumba sehemu zote za Esia Ndogo, Siria, Palestina, Misri, Babulonia, na milki nzima ya Umedi-Uajemi mpaka kule mbali kwenye mpaka wa India ya kale! Kwa kuhesabiwa kuwa labda ndiye jemadari mkubwa zaidi wa nyakati za kale, yeye anajulikana leo kuwa Aleksanda Mkuu.
Kwa muda mfupi ajabu, Ugiriki ilikuwa imekuja kuwa ya tano ya zile serikali kubwa za ulimwengu za historia ya Biblia—kubwa kuliko yo yote iliyokuwa imeitangulia. Jambo hilo lilitukia jinsi gani? Hiyo inahusiana na Neno la Mungu jinsi gani? Inamaanisha nini kwako?
Ilitabiriwa Katika Unabii wa Biblia
Miaka mia mbili kabla ya wakati wa Aleksanda, wakati Babuloni ulipokuwa ukitawala, na ambapo Wamedi na Waajemi walikuwa bado hawajawa serikali kubwa ya ulimwengu, Danieli nabii wa Yehova alipewa njozi kubwa mbili za kiunabii ambazo zilitoa muhtasari wa historia ya ulimwengu wakati ujao. Ndipo, baada ya Babuloni kuanguka, yeye akapokea unabii wa tatu kuhusu mambo ambayo yangetukia muda mrefu baada ya wakati wake. Danieli aliandika mambo hayo. Maunabii hayo, ambayo hayakuanza kutimizwa mpaka yapata karne mbili baadaye, yana habari za wazi juu ya mambo ambayo yangetukia kwa Aleksanda na kwa ufalme wake.
Ni mambo gani yaliyofunuliwa kwa Danieli? Unaweza kupata maunabii hayo katika kitabu cha Biblia cha Danieli, kilichoandikwa wapata mwaka 536 K.W.K. Kwa ufupi, haya ndiyo mambo aliyoona kuhusiana na ile serikali kubwa ya tano ya ulimwengu, Ugiriki:
Katika njozi ya kwanza ya kiunabii, Ugiriki iliwakilishwa kuwa kama chui mwenye uwezo wa kwenda kasi. “Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne ya kiumbe anayeruka. Naye alipewa utawala kweli kweli.”—Danieli 7:6, NW.
Katika njozi ya pili ya kiunabii, mbuzi wa kiume (beberu) alionwa ‘akija kutoka machweo ya jua [magharibi] juu ya uso wa dunia nzima,” akienenda kwa mwendo wa kasi sana hivi kwamba “hakuwa akigusa dunia.” Alikuja njia yote ile mpaka kwa yule kondoo wa kiume ambaye malaika alisema “anasimamia wafalme wa Umedi na Uajemi.” Huyo mbuzi wa kiume “akaendelea na kupigisha chini yule kondoo wa kiume na kuvunja pembe mbili zake.” Danieli aliambiwa: “Yule mbuzi-mume mwenye nywele-nywele anasimamia mfalme wa Ugiriki.”—Danieli 8:5-8, 20, 21, NW.
Katika kisa cha tatu, Danieli aliambiwa kwamba mfalme wa “Uajemi... ataamsha kila kitu dhidi ya ufalme wa Ugiriki. Na kwa uhakika mfalme fulani mwenye uweza atasimama na kutawala akiwa na eneo lililoenea sana na kufanya kulingana na mapenzi yake.”—Danieli 11:2, 3, NW.
Mifananisho hii ilimaanisha nini? Je! mambo haya yalitukia jinsi Danieli alivyokuwa ameambiwa yangetukia? Acha tuone.
Maunabii Yatimizwa
Katika masika ya mwaka 334 K.W.K., Aleksanda aliingia Esia kule Dardanelles (ile Hellespont ya kale) akiwa na askari 30,000 watembea-miguu na wapanda-farasi 5,000. Akiwa na mwendo wa chui mfananishwa, mwenye mabawa manne, au mwendo wa mbuzi ambaye alionekana kama kwamba hagusi chini, yeye alikumba maeneo yote ya milki ya Uajemi—iliyokuwa na ukubwa ulio mara 50 za ufalme wake mwenyewe! Je! yeye ‘angetawala akiwa na eneo lililoenea sana na kufanya kulingana na mapenzi yake’? Historia inajibu.
Kwenye Mto Graniko katika pembe ya kaskazini-magharibi ya Esia Ndogo (Uturuki ya ki-siku-hizi) Aleksanda alishinda pigano lake la kwanza dhidi ya Waajemi. Wakati wa kipupwe hicho, yeye alishinda Esia Ndogo ya magharibi. Vuli iliyofuata, kule Issus katika pembe ya kusini-mashariki ya Esia Ndogo, yeye alishinda kabisa kabisa jeshi la Kiajemi lililokadiriwa kuwa wanaume nusu-milioni, na yule mfalme mkuu, Dario 3 wa Uajemi, akakimbia, akiacha jamaa yake kwenye mikono ya Aleksanda.
Badala ya kufuatia Waajemi wenye kukimbia, Aleksanda alipiga miguu kuelekea kusini kando-kando ya pwani ya Mediterania, akishinda vituo vikuu vilivyotumiwa na kile kikosi chenye nguvu cha meli za Kiajemi. Mji Tiro wa kisiwani ulikinza kwa miezi saba. Mwishowe kabisa, akitumia mabomoko ya ule mji-bara wa zamani ambao Nebukadreza alikuwa ameharibu, Aleksanda akajenga pito la kwenda nje kwenye mji wa kisiwani. Mabakio ya pito hilo yanaonekana leo, yakishuhudiza utimizo wa unabii wa Ezekieli kwamba mavumbi ya Tiro yangesukumizwa ndani ya bahari.—Ezekieli 26:4, 12.
Akiachilia Yerusalemu, ambao ulisalimu amri yake kwa ushinde, Aleksanda alisonga kusini, akishinda Gaza na kupanua ‘eneo lake lililoenea sana’ na kufanya “kulingana na mapenzi yake” katika Misri, ambako alilakiwa kuwa mkombozi. Huko Memphisi alimtolea dhabihu Apisi ng’ombe dume, hivyo akafurahisha makuhani Wamisri. Alipiga pia msingi wa mji wa Aleksandria, ambao baadaye ulikuwa mshindani mkuu wa Athene kwa kuwa kitovu cha masomo, na bado ungali na jina lake.
Shabaha zote za mpangilio wa Philip zilikuwa zimetimizwa kwa kuzidi, lakini Aleksanda alikuwa bado hajamaliza mambo. Akiwa kama mbuzi-mume mwenye kuenenda kasi, yeye aligeuka kuelekea nyuma kaskazini-mashariki, kupitia Palestina na kupanda juu kuelekea Mto Tigri. Huko, katika mwaka 331 K.W.K., yeye alihusisha Waajemi vitani kule Gaugamela, si mbali na yale magofu yenye kumumunyika ya uliokuwa mji mkuu wa Kiashuri, Ninawi. Wanaume 47,000 wa Aleksanda walilemea jeshi la Kiajemi lililopangwa upya, la watu 1,000,000. Dario 3 alikimbia na baadaye akauawa na watu wake mwenyewe.
Akiwa anabubujika ushindi, Aleksanda aligeukia kusini na kutwaa Babuloni, mji mkuu wa Kiajemi wakati wa kipupwe. Pia alichukua ukazi wa miji mikuu huko Susa na Persepolisi, akibamba ile hazina kubwa sana ya Kiajemi na kuchoma jumba kuu la mfalme Zakse. Mwishowe kabisa, mji mkuu huko Ekbatana ulianguka mikononi mwake. Ndipo mshindaji huyo mwenye mwendo wa kasi alipoiweka chini yake sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Kiajemi, lenye kufika mbali mpaka mashariki ya Mto Indus katika Pakistan ya ki-siku-hizi. Pasipo swali, Ugiriki ilikuwa imekuja kuwa ya tano ya zile serikali kubwa za ulimwengu katika historia ya Biblia.
Pia ushindi wa Aleksanda ulieneza lugha na utamaduni wa Wagiriki katika sehemu zote za milki hii kubwa. Makoloni ya Kigiriki yalipokuwa yamesimamishwa kwa uthabiti katika bara zilizoshindwa, kile Kigiriki kilicho kawaida ya watu wote, Koine, kikawa ndiyo lugha ya kimataifa ya siku hiyo. Ndiyo lugha iliyotumiwa baadaye kuyatia katika maandishi Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ya Biblia.
Ufalme wa Aleksanda Wagawanywa
Aleksanda alitaka kujenga upya Babuloni uwe mji mkuu wa milki yake. Lakini jambo hilo halingetukia. Maunabii yalikuwa yamemsimulia yule mbuzi-mume mwenye nywele-nywele kuwa mwenye pembe kubwa moja, ambayo Danieli alikuwa ameambiwa hivi kuihusu:
“Yule mume wa wale mbuzi, kwa upande wake, alijishaua sana kufikia ukomo; lakini mara tu alipokwisha kuwa mwenye uweza, ile pembe kubwa ilivunjwa, na badala ya hiyo nne zikaendelea kuja juu kwa njia yenye kutokeza, kuelekea zile pepo nne za mbingu. . . . Yule mbuzi-mume anasimamia mfalme wa Ugiriki; na kwa habari ya ile pembe kubwa ambayo ilikuwa kati ya macho yake, hiyo inasimamia mfalme wa kwanza. Na hiyo ikiisha kuwa imevunjwa, hivi kwamba kulikuwa na nne ambazo mwishowe kabisa zilisimama badala yayo, kuna falme nne kutoka taifa lake ambazo zitasimama, lakini si kwa nguvu zake.”—Danieli 8:8 21, 22, NW.
“Wakati yeye atakapokuwa amesimama, ufalme wake utavunjwa na kugawanywa kuelekea zile pepo nne za mbingu, lakini si kwa wazaliwa wake wa baadaye na si kulingana na eneo la utawala wake ambalo kwalo alitawala; kwa sababu ufalme wake utang’olewa mizizi, hata kwa ajili ya wengine wasio hawa.”—Danieli 11:4, NW.
Kama Biblia ilivyotabiri, mshangilio wa Aleksanda wa utawala wa ulimwengu ulikuwa wa muda mfupi. Akiwa kwenye kilele chenyewe cha ushindi wake, kwenye umri wa miaka 32 tu, yalikoma maushindi ya Aleksanda yasiyo na huruma. Akiwa amepatwa na homa kali ya maleria, yeye aliendelea kula karamu mpaka kulewa, na akafa kwa ghafula katika Babuloni katika 323 K.W.K. Mwili wake ulipelekwa Misri na kuingizwa kaburini katika Aleksandria. “Ile pembe kubwa” ambayo “inasimamia mfalme wa kwanza” ilikuwa imevunjwa. Halafu ni jambo gani lilipata milki yake?
Unabii ulikuwa umesema kwamba ufalme wake ungegawanywa “lakini si kwa wazao wake wa baadaye.” Philip Arrhidayo, ndugu ya Aleksanda asiyeweza mambo, alitawala kwa muda mfupi lakini akauawa. Ndivyo ilivyotukia pia kwa Aleksanda (Allou) mwana halali wa Aleksanda na Heracles (Hercules) mwana wake wa haramu. Hivyo ndivyo ulivyofifilia mbali ukoo wa Aleksanda Mkuu, yule mmwagaji-damu mkuu.
Lililotabiriwa pia lilikuwa kwamba “kuna falme nne kutoka taifa lake ambazo zitasimama, lakini si kwa nguvu zake” na kwamba ufalme wake ‘ungegawanywa kuelekea zile pembe nne za mbingu, lakini . . . si kulingana na eneo la utawala ambalo kwalo yeye alikuwa ametawala.” Je! jambo hili lilitukia?
Baada ya muda, ile milki kubwa ya Aleksanda iligawanywa miongoni mwa majemadari wake wanne: (1) Jemadari Kasanda—Makedonia na Ugiriki. (2) Jemadari Lisimako—Esia Ndogo na Thrasi ya Ulaya. (3) Jemadari Seleuko Niketa—Babulonia, Umedi, Siria, Uajemi na mikoa ya mashariki mpaka kwenye Mto Indo. (4) Jemadari Ptolemi Lago—Misri, Libya, na Palestina. Kama ilivyokuwa imesemwa kwa unabii, kutokana na ufalme mkuu mmoja wa Aleksanda zilitokea falme nne za Kiheleni, au zilizogirikishwa.a
Wenye kudumu kwa muda mrefu zaidi kati yazo ulikuwa ule ufalme wa Kiptolemi katika Misri. Huo ulianguka mikononi mwa Roma katika 30 W.K., na hapo Roma ikachukua mahali pa Ugiriki na kuwa ya sita ya zile serikali kubwa za ulimwengu.
Matazamio ya Mbele Yaliyo Maangavu Zaidi kwa Ajili ya Aina ya Binadamu
Je! serikali kubwa za ulimwengu zenye uonevu zingepasa kuendelea kufuatana-fuatana kwa wakati usio dhahiri? Hapana, kwa maana Biblia inatuambia kwamba sisi tunaishi karibu na mwisho wa ile ya mwisho kati yazo.—Ufunuo 17:10.
Baada ya kuona serikali hizi za kibinadamu zilizo kama wanyama, Danieli aliona kitu fulani tofauti. Yeye alipewa njozi ya kutokeza kwa kupenyezwa maono yake ndani ya mbingu zenyewe, ambamo aliona “Mkale wa Siku,” Mungu mwenyewe, akiupa Ufalme, si kwa kiongozi fulani wa kibinadamu wa wakati ujao mwenye kudaka-daka vyeo, bali kwa “mtu fulani kama mwana wa binadamu”—kwa Yesu Kristo mfufuliwa, wa kimbingu!—Danieli 7:9, 10, 13, NW.
Lo! tofauti gani! Ufalme huo wa kimbingu ungepasa kutofautiana kama nini na zile za wale waliokuwa wafalme wa kibinadamu wenye kufanya vita. Danieli alisema hivi juu ya huyu “mwana wa binadamu” wa kimbingu aliyekwezwa: “Yeye alipewa utawala na fahari na ufalme, kwamba jamii za watu, vikundi vya kitaifa na lugha vipaswe vyote kumtumikia hata yeye. Utawala wake ni utawala wa kudumu kwa wakati usio dhahiri ambao hautapitilia mbali, na ufalme wake ni mmoja ambao hautaletwa kwenye uangamivu.” (Danieli 7:14, NW) Ungepaswa kuwa Ufalme wa amani na uadilifu.—Isaya 9:6, 7, NW.
Tunapotazama nyuma kuhusu pupa na jeuri ya utawala wa kibinadamu, sisi tunaweza kufurahi kama nini kwamba tayari Ufalme huu wa kimbingu umesimamishwa kwa uthabiti na kwamba utawala wao wa uadilifu duniani pote uko karibu!—Ufunuo 12:10, 12.
“Kwa maana ile njozi ni bado kwa ajili ya wakati uliowekwa rasmi, nayo inaendelea kuhema-hema ikielekea kwenye mwisho, nayo haitasema uwongo. Hata ikipasa kukawia, endelea kuitazamia; kwa maana pasipo kushindwa itakuja kuwa kweli. Hiyo haitachelewa.” —Habakuki 2:3, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Matukio ya kishindo kingi ambayo yalifuata mgawanyiko wa milki ya Aleksanda yalitabiriwa katika unabii wa “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini.” Unabii huu, ulioandikwa katika Danieli sura ya 11, unazungumziwa kirefu katika kurasa 229-48 za kitabu “Your Will Be Done on Earth, “chenye kutangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Ramani katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mweneo wa utawala wa Aleksanda
Pella
Sardisi
Isusi
Dameski
Tiro
Yerusalemu
Aleksandria
Memfisi
Tebesi
Mto Eutrati
Mto Tigri
Gaugamela
Babuloni
Ekbatana
Shushani
Persepolisi
Alexandria Eskate
Taksila
Mto Indo
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mvunjiko-vunjiko wa Milki ya Aleksanda
Bahari Kuu
KASANDA
Pella
LISIMAKO
Lisimakia
PTOLEMI LEGO
Aleksandria
SELEUKO NINIKETA
Antiokia
Seleukia
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mpaka wa pwani karibu na Aleksandria ya ki-siku-hizi
[Credit Line]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.