Mileani Ya Tatu—Je! Itatimiza Matumaini Yako?
WAKATI ndio huo umeanza kuyoyoma. Saa iliyo mbele ya kitovu cha kitamaduni cha Beabourg katika Paris, Ufaransa, yaonyesha hesabu ya sekunde zinazobakia. Itafululiza tu kuyoyomesha wakati mpaka usiku-kati wa Desemba 31, 1999. Wakati huo, jambo fulani lililopata kushuhudiwa mara moja tu katika Wakati wa Kawaida wetu litatukia: kukaribisha mileani mpya, ile mileani ya tatu.
“[Mwaka] 2000, kwa njia fulani, ‘ndilo tukio kubwa kabisa lenye kutarajiwa’ kwa kadiri isiyopata kuwako katika historia ya kibinadamu,” adokeza mtafiti Bernward Joerges wa Berlin, Ujeremani. Mbona kuwe na tazamio hilo? Ingawaje, mwaka 2000 ni tarehe kama nyinginezo katika mkondo wa wakati. Mbali ya hilo, tarehe hiyo hutambuliwa na wale tu wanaofuata kalenda ya Magharibi. Kulingana na kalenda ya Kiislamu, mwaka 2000 W.K. huwadia wakati wa mwaka wa Kiislamu wa 1420; kulingana na kalenda ya Kiyahudi, ni 5760 A.M.
Lakini katika mahoji yaliyofanywa katika gazeti la kila siku la Kiswedi Dagens Nyheter, Profesa Joerges aeleza hivi: “Kwa sababu ya ukoloni na ubeberu, mpangilio wetu wa tarehe za Gregory, kuanzia na ile idhaniwayo kuwa siku ya kuzaliwa kwa Kristo, umeimarika katika sehemu kubwa za ulimwengu.” Hivyo mwaka 2000 utakuwa kitia-alama cha muhula wa tufe lote kwa sehemu kubwa ya ainabinadamu. Asema hivi Profesa Joerges: “Watu wote watahusianisha wasifu wao wa faraghani na pia kila jambo jinginelo na tukio hili.”
Hata hivyo wengi wanafikiria mengi kuliko kutia alama wakati. “Miradi mikubwa na programu za ‘kutia alama’, ambazo zalipa umaana na kuliadhimisha tukio hili tayari zaendelea katika vizio vyote vya maisha na katika tabaka zote za kijamii,” adai Joerges. Aongeza kwamba “kotekote katika tufe, wenye kutayarisha miradi mikubwa na ‘wastadi wa maonyesho’ wanaota-ota na kupangia-pangia matukio makubwa.” Watabiri wengine wasema kwamba “vitabu vya habari za karne iliyopita vitatufurikia kwa wingi sana. Vyombo vyote vya habari vitapatwa na kichaa cha kusisimukia mwanzo huo wa mileani. Kituo kimoja cha televisheni ya Ujeremani Magharibi kinapanga utangazaji wa saa 24 juu ya mapambazuko ya kotekote duniani.”
Pia vyombo vya habari vitahakikisha kufanya hekaheka ya kukitangaza sana kitoto kitakachokuwa cha mwisho kuzaliwa katika 1999 na cha kwanza kuzaliwa katika 2000. Waandishi wa habari watakuwa na hamu ya kuwatafuta wasalia wachache waliozaliwa katika karne ya 19 ili wawaulize wanahisije kuwa wameishi katika karne tatu na mileani mbili! Watu fulani hata wahisi kwamba papara-papara hii ya mileani itatokeza bumbuazi kwa halaiki ya watu. Kulingana na utabiri mmoja wa kusikitisha, igongapo ile dakika ya usiku-kati wa kuamkia Mwaka Mpya, wengi watajiua.
Ijapokuwa hivyo ni vitendo vya kupita kiasi, yaeleweka kwamba tukio hilo laamsha msisimuko. Kwa wengi katika ulimwengu wetu ulionyong’onyezwa na matata, mileani mpya hiyo yaonwa kama mmuliko wa tumaini, mwingilio wa wakati ujao ulio bora. Watu fulani hutegemea sayansi na tekinolojia kutokeza wakati ujao ambamo tutakula vizuri zaidi na tuishi muda mrefu zaidi, tufanye kazi kidogo zaidi na tukae nyumbani muda mwingi zaidi; ambamo mashine za kubonyezwa tu zitatuweka huru na kazi za ukimwa; ambamo mchanganyo wenye kudhibitiwa vizuri utageuza maji yawe mafuta ya kuwasha moto. Wao huona njozi ya wakati ujao wenye televisheni ya mkononi, simu zenye kutoa picha, mashine-faksi za rangi (za kusafirisha barua kwa kuinakili kwa mpelekewa), na simu zenye kutafsiri ujumbe dakika ile ile. Wao wanaota juu ya kupeleleza Mwezi, sayari Mars, au magimba mengine ya kimbingu, wachimbe migodi humo ili kutoa utajiri uliomo.
Lakini si wote walio na matazamio mazuri hivyo. Watafiti fulani waona kwamba mileani mpya hiyo itakaribisha wakati wa ukuzi usiodhibitiwa vizuri wa idadi ya watu ulimwenguni na kuharibika kwa mazingira. Uchafuzi wa hewa utageuza halianga ya dunia iwe na joto jingi sana. Vilima vya barafu vitayeyuka na bahari zitainuka, zikifurisha maeneo yenye mazao na watu lakini vigeuze mamilioni ya hektari za ardhi ya ukulima kuwa majangwa. Wao watabiri kwamba kutakuwako anguko la uchumi wa ulimwengu, ukosefu wa usalama wa kisiasa ambao utatikisa serikali na jumuiya, uhalifu wa chakari, na lililo baya kabisa, teketezo la kinyukilia litakalofutilia mbali uhai wote wa kibinadamu.
Watabiri wana makisio tele lakini wana uhakika haba kuhusu mileani inayokaribia. Kusema kwa usahili, matukio yasiyoonekana vizuri kule mbele ni mengi mno hivi kwamba wakati ujao hauwezi kutabiriwa kwa usahihi. Mtaalamu mwenye kutabiri wakati ujao hufananisha kufanya hivyo na kucheza sataranji (chesi): “Kabla sijapiga hatua moja ifuatayo, kwa kadiri niwezavyo natazama hatua nyingi sana za mbele zaidi. Lakini mpinzani wangu akiisha kupiga hatua yake, mimi huanza kufanya hivyo tena.”
Kuhusu yale yaliyoko hasa katika mwaka 2000, wakati ndio utajisemea wenyewe. Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba ni lazima wakati ujao wako ukose uhakika. Biblia huandaa kizibiti cha kutosha kwamba tuko karibu na mileani iliyo ya maana kuliko ile itakayoanza mnamo muda ulio chini ya mwongo mmoja. Mileani hii inayokaribia itapita kwa mbali matarajio yoyote ya kibinadamu! Hiyo yamaanisha nini hasa? Itahusisha nini ndani? Sisi twakualika wewe ufikirie makala yetu inayokuja na ujifunze mambo ambayo Biblia husema.