2000—Je, Ni Mwaka wa Pekee?
JE, MWAKA wa 2000 ni wa pekee kwa njia fulani? Kwa ujumla watu wanaoishi katika nchi za magharibi huuona kuwa mwaka wa kwanza wa milenia ya tatu. Matayarisho makubwa ya kuusherehekea yameanza. Saa kubwa sana za elektroni zinawekwa ili kuhesabu sekunde zinazobaki kabla ya milenia mpya kufika. Sherehe za dansi za Mkesha wa Mwaka Mpya zinapangwa. T-shati zenye misemo juu ya mwisho wa milenia zinauzwa kwenye maduka ya vijijini na vilevile kwenye maduka makubwa ya majijini.
Makanisa, makubwa kwa madogo, yatajiunga na sherehe hizo za mwaka mzima. Mapema mwaka ujao, Papa John Paul wa Pili anatarajiwa kusafiri kwenda Israeli ili kuwaongoza Wakatoliki katika ile ambayo imeitwa “Sherehe ya yubile ya milenia ya Kanisa Katoliki.” Inakadiriwa kwamba kati ya watalii milioni mbili u nusu hadi milioni sita, wakitia ndani wanadini na wadadisi, wanapanga kuzuru Israeli mwaka ujao.
Kwa nini watu wengi hivyo wanapanga kuzuru Israeli? Akizungumza kwa niaba ya papa, Kadinali Roger Etchegaray, ofisa wa Vatikani, alisema: “Mwaka wa 2000 ni sherehe ya Kristo na maisha yake katika nchi hii. Hivyo, inafaa kwa Papa kuja hapa.” Mwaka wa 2000 unahusianaje na Kristo? Mwaka wa 2000 hufikiriwa kwa kawaida kuwa miaka 2,000 kamili tangu Kristo azaliwe. Lakini je, ndivyo ilivyo? Tutaona.
Mwaka wa 2000 ni wa maana hata zaidi kwa wafuasi wa dini fulani-fulani. Wanasadiki kwamba katika mwaka ujao au baadaye kidogo, Yesu atarudi kwenye Mlima wa Mzeituni nayo vita ya Har–Magedoni, ambayo imetajwa katika kitabu cha Ufunuo, itapiganwa katika bonde la Megido. (Ufunuo 16:14-16) Kwa kutarajia matukio hayo, mamia ya wakazi wa Marekani wanauza makao yao na karibu mali zao zote na kuhamia Israeli. Kwa manufaa ya wowote wale wasioweza kuacha makao yao, inasemekana kwamba Mweneza-evanjeli mmoja mashuhuri wa Marekani ameahidi kutangaza kurudi kwa Yesu kupitia televisheni ya rangi!
Katika nchi za Magharibi, mipango ya kuikaribisha milenia ya tatu inaongezeka. Hata hivyo, watu katika nchi nyinginezo wanaendelea na shughuli zao za kawaida. Watu hao—ambao ndio wengi zaidi ulimwenguni—hawaamini kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa ndiye Mesiya. Hata si lazima wakubali utaratibu wa kuweka tarehe wa K.K. na A.D.a Kwa mfano, Waislamu wengi hutumia kalenda yao wenyewe, na kulingana na kalenda yao mwaka ujao utakuwa 1420—wala si 2000. Waislamu huhesabu miaka kuanzia tarehe ambayo Muhammad alikimbia kutoka Mecca kwenda Medina. Kwa ujumla, watu ulimwenguni kote hutumia kalenda tofauti-tofauti zipatazo 40.
Je, mwaka wa 2000 wapaswa kuwa muhimu kwa Wakristo? Je, kweli Januari 1, 2000, ni siku yenye maana ya pekee? Maswali hayo yatajibiwa katika makala ifuatayo.
[Maelezo ya chinis]
a Katika utaratibu wa kuweka tarehe wa K.K. na A.D., matukio yaliyotokea kabla ya wakati wa kimapokeo wa kuzaliwa kwa Yesu huitwa miaka ya “K.K.” (kabla ya Kristo); nayo yale yaliyotokea baadaye huitwa miaka ya “A.D.”(Anno Domini—“katika mwaka wa Bwana wetu.”) Hata hivyo, wasomi fulani wenye ujuzi hupendelea kutumia usemi usio wa kidini “K.W.K.” (kabla ya Wakati wetu wa Kawaida) na “W.K.” (-a Wakati wetu wa Kawaida.)