Maisha na Huduma ya Yesu
“Tazama, Mtu Huyu!”
KWA kuvutiwa na utulivu wa Yesu na akitambua kwamba hana kosa, Pilato anafuatia njia nyingine ya kumwachilia. “Kwenu kuna desturi,” anaambia umati wa watu wale, “kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka [Kupitwa, NW].”
Baraba, mwuaji mwenye sifa mbaya, amefungwa pia akiwa mfungwa-gereza, hivyo basi Pilato anauliza hivi: “Mnataka niwafungulie yupi? yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo?”
Kwa kuvutwa na usadikisho wa wakuu wa makuhani ambao wamewachochea, watu wanaomba Baraba aachiliwe lakini Yesu auawe. Bila kukata tamaa, Pilato anajibu, akiuliza tena hivi: “Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili?”
“Baraba,” wanapaaza sauti.
“Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo?” Pilato anauliza kwa kufadhaika.
Kwa mngurumo mmoja wenye kishindo cha kuziba masikio, wanajibu hivi: “Asulibiwe [acha atundikwe, NW]”! “Msulibishe! Msulibishe [mtundike, NW]!”
Kwa kujua kwamba wanadai kifo cha mtu asiye na hatia, Pilato anasihi hivi: “Kwa sababu gani? huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi [kumwadhibu] nitamfungua.”
Japo majaribio yake, umati huo wenye hasira, kwa kuchochewa na viongozi wao wa kidini, wanaendelea kupiga kelele hivi: “Asulibiwe [atundikwe, NW]”! Kwa kuchochewa sana na makuhani, umati wanataka damu. Na ebu fikiri, siku tano tu kabla ya hapo, wengine wao labda walikuwa miongoni mwa wale waliokaribisha Yesu kuingia Yerusalemu akiwa Mfalme! Muda wote huu, wanafunzi wa Yesu, ikiwa wapo, wanabaki kimya na bila kujitokeza wazi.
Pilato, akiona kwamba maneno yake ya kusihi hayafai kitu, bali kunatokea fujo, anachukua maji na kunawa mikono mbele ya ule umati, na kusema: “Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.” Hapo watu hao wanajibu hivi: “Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.”
Hivyo basi, kulingana na madai yao—naye akitaka kufurahisha umati huo kuliko kufanya analojua kuwa haki—Pilato anawafungulia Baraba. Anachukua Yesu na kuagiza avuliwe mavazi halafu apigwe mijeledi. Huku hakukuwa kupiga viboko vya kawaida. The Journal of the American Medical Association linaeleza zoea la Kiroma la kupiga mijeledi:
“Chombo cha kawaida kilikuwa kiboko kifupi (flagramu au flagelamu) chenye kamba kadhaa moja moja za ngozi-kavu au zilizosokotwa zikiwa na marefu mbalimbali, ambamo mipira midogo ya chuma au vipande vyenye ncha kali vya mifupa ya kondoo vilifungwa kwa kuachana. . . . Askari Waroma walipopiga-piga mgongo wa mfungwa kwa nguvu kamili, ile mipira ya chuma ingesababisha michubuo ya kina kirefu, na zile kamba za ngozi-kavu na mifupa ya kondoo zingekata ndani ya ngozi na sehemu zilizo chini ya ngozi ya mwili. Halafu, kupigwa mijeledi kulipoendelea, miraruko ya ngozi ingeingia chini ya nyuzi za mnofu chini kwenye mifupa ya mwili na kutokeza nyuzinyuzi zenye kuning’inia za mnofu wenye kutoka damu.”
Baada ya mpigo huu wa mateso makali, Yesu anapelekwa ndani ya jumba la gavana, na kikundi kizima cha askari kinaitwa kikusanyike. Humo askari wanarundika matukano zaidi juu yake kwa kusokota taji la miiba na kulisukuma juu ya kichwa chake. Wanatia tete katika mkono wake wa kulia, nao wanamvika vazi la zambarau, namna inayovaliwa na watu wa kifalme. Halafu wanamwambia hivi kwa dhihaka: “Salamu, Mfalme wa Wayahudi!” Pia, wanamtemea mate na kumpiga kofi usoni. Wakichukua lile tete imara kutoka mkononi mwake, wanalitumia kumpiga kichwani, hiyo ikizidi kuisukuma ndani ya ngozi ya kichwa chake ile miiba iliyochongoka ya “taji” lake lenye kumshushia heshima.
Fahari na imara ya kusifika ambayo Yesu anayo kwa kuelekeana na mtendeo mbaya huu inavutia sana Pilato hivi kwamba inamsukuma kufanya jaribio jingine la kumwachilia. “Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake,” anawaambia umati wa watu. Inawezekana kuwa anawazia kwamba sura ya hali ya kuteswa-teswa kwa Yesu italainisha mioyo yao. Yesu anapokuwa amesimama mbele ya watu hao wenye fujo wasio na moyo wa huruma, akiwa amevaa taji la miimba na lile vazi la nje la zambarau na huku uso wake wenye kutoka damu ukiwa na maumivu, Pilato anatangaza hivi: “Tazama, mtu huyu!”
Ingawa amechubuliwa na kutwangwa, hapa amesimama mtu mwenye kutokeza zaidi katika historia yote, kwa kweli binadamu wa kutokeza zaidi aliyepata kuishi! Ndiyo, Yesu anaonyesha fahari ya unyamavu na utulivu unaoonyesha ukuu ambao hata Pilato analazimika kuukubali wazi, kwa maana inaonekana maneno yake ni mchanganyiko wa heshima na huruma pia. Yohana 18:39–19:5; Mathayo 27:15-17, 20-30; Marko 15:6-19; Luka 23:18-25.
◆ Ni kwa njia gani Pilato anajaribu kufanya Yesu aachiliwe?
◆ Pilato anajaribuje kujiondoa katika daraka?
◆ Ni nini kinachohusika katika kupigwa mijeledi?
◆ Yesu anadhihakiwaje baada ya kupigwa mijeledi?
◆ Ni jaribio gani zaidi ambalo Pilato anafanya ili kumwachilia Yesu?