Aksidenti ni Ajali au ni Hali?
CRISTINA, msichana wa kuvutia aliye kiolezo cha mitindo ya mavazi, hakuona basi iliyokuwa ikikaribia alipokuwa akivuka barabara Nove de Julho Avenue yenye magari mengi katika São Paulo, Brazili. Dereva alijaribu kwa vyovyote kusimamisha gari lake, lakini ilikuwa kuchelewa mno. Cristina aligongwa akafa.
Aksidenti hiyo yenye kuhuzunisha sana ilipata kuripotiwa kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti la habari la Kibrazili O Estado de S. Paulo. (Julai 29, 1990) Hata hivyo, hicho kilikuwa tu kimoja cha vifo 50,000 visababishwavyo na magari, vitukiavyo kila mwaka katika Brazili. Na ingawa maelfu wengine hulemazwa na aksidenti kama hizo, wengine huokoka bila kuumia. Basi, kwa nini msichana huyo kijana hakuokoka? Je, ilikuwa imepangwa kimbele afe siku hiyo?
Watu walio wengi wangetoa hoja kwamba ndivyo ilivyo. Wao huamini ajali, kwamba matukio makubwa, kama wakati wa kufa kwa mtu, yameamuliwa kimbele. Imani hiyo imetokeza misemo kama “Ajali haina kinga wala kafara,” “Saa yake imefika,” au “Liandikwalo ndilo liwalo.” Je! kuna ukweli wowote katika misemo kama hiyo inayoshikiliwa na watu wengi? Je! sisi ni vibaraka hoi tu wanaoongozwa na ajali?
Imani ya kwamba kila mtu ameandikiwa ajali yake, au wazo la kwamba matukio yote yanaamuliwa kimbele, ilienea miongoni mwa Wagiriki na Waroma wa kale. Hata leo wazo hilo labaki imara katika dini nyingi. Kwa mfano, dini ya Kiislamu inashikilia maneno ya Kurani: “Na nafsi yo yote haitaweza kufa ila kwa amri ya Mwenyezi Mungu kwa ajali iliyowekwa.” Imani katika ajali ni ya kawaida pia katika Jumuiya ya Wakristo nayo imekuzwa na fundisho la kadari (predestination), lililofundishwa na John Calvin. Kwa hiyo, ni jambo la kawaida kwa makasisi kuwaambia watu wa ukoo wenye majonzi kwamba aksidenti fulani ilikuwa “mapenzi ya Mungu.”
Hata hivyo, maoni ya kwamba aksidenti ni matokeo ya ajali, ni kinyume cha busara, ujuzi, na akili nzuri. Kwanza, aksidenti za gari haziwezi kuwa tokeo la mwingilio wa kimungu, kwa kuwa uchunguzi wa kikamili kwa kawaida hufunua sababu halisi. Zaidi ya hilo, takwimu zaonyesha kwa wazi kwamba kuwa mwangalifu ifaavyo—kama vile kufunga mishipi ya usalama—hupunguza kwa kadiri kubwa uwezekano wa kuwa na aksidenti ya kifo. Je! hadhari zozote za usalama zingeweza kuzuia mapenzi ya Mungu yaliyoamuliwa kimbele?
Lakini, imani katika ajali humwathiri vibaya mwamini. Je, imani hiyo haitii moyo vitendo vya kujihatirisha bure, kama vile kupuuza mipaka ya mwendo wa gari na ishara za kuongoza magari au kuendesha gari chini ya uvutano wa vileo au wa dawa za kulevya? Jambo lenye uzito zaidi ya hayo ni kwamba, imani katika kuandikiwa kwa kila mtu ajali yake hufanya watu wengine wamlaumu Mungu wakati aksidenti inapowaathiri. Wakiwa wanahisi hasira na wakiwa hoi (bila msaada), na kusadikishwa kwamba Mungu hajali, huenda hata wakapoteza imani. Kwa kufaa mshahiri Emerson alisema hivi: “Kuiamini Ajali katili ndio msiba mkali kwa uchungu maishani.”
Lakini Biblia husema nini kuhusu misiba na aksidenti? Je, inafundisha kwelikweli kwamba hiyo ni matokeo ya ajali? Kwa kuongezea, inasemaje kuhusu matazamio yetu ya wokovu? Je, tuna chaguo lolote katika jambo hilo?
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Kuiamini Ajali katili ndio msiba mkali kwa uchungu maishani.”—Ralph Waldo Emerson