Kile Ambacho Jumuiya ya Wakristo Imepanda Katika Afrika
KATIKA 1867, Charles Lavigerie, Mkatoliki kutoka Ufaransa, alikuja Afrika akiwa askofu mkuu wa Algiers aliyewekwa rasmi wakati huo. “Mungu amechagua Ufaransa,” akasema, “kufanya Algeria kuwa mwanzo wa taifa kuu na la Kikristo [Afrika].”
Ndoto ya Lavigerie ilienea mbali kupita Algeria. Kwa kweli, alituma wamishonari hadi upande ule mwingine wa jangwa akiwa na lengo la “kuunganisha Afrika Kaskazini na Kati ili zishirikiane maisha ya Jumuiya ya Wakristo.”
Wakati huohuo, katika sehemu za magharibi, kusini, na mashariki za kontinenti hiyo, wamishonari Waprotestanti walikuwa wakifanya kazi tayari. Walivumilia magumu mengi, kama vile kuambukizwa tena na tena na ugonjwa wa malaria, ukiwa na ishara zao za kutetemeka, kutokwa na jasho, na mapayo. Wakidhoofishwa haraka na magonjwa ya kitropiki, wengi walikufa upesi baada ya kuwasili. Lakini wengine waliendelea kuja. “Yeyote anayesafiri katika Afrika,” akataarifu Adlai Stevenson, “hukumbushwa daima juu ya ushujaa wa wamishonari. . . . Walipambana na homa ya manjano, kuhara damu, vimelea na mawe ya kaburi niliyoona . . . , mawe yao ya kaburi—kotekote Afrika.”
Mazao ya Umishonari
Wamishonari walipopenya Afrika, walipata kwamba makabila mengi hayakuweza kusoma wala kuandika. “Kati ya lugha [za Afrika] mia nane hivi,” aeleza Ram Desai katika kitabu chake Christianity in Africa as Seen by Africans, “ni nne tu zilizokuwa katika namna ya maandishi kabla ya wamishonari kuja.” Kwa hiyo wamishonari walitunga njia ya kuandika lugha hizo ambazo hazikuwa zimeandikwa. Kisha wakatokeza vitabu vya mafundisho wakaanza kuwafundisha watu kusoma. Kwa kusudi hilo wakajenga shule kotekote Afrika.
Wamishonari walijenga hospitali pia. “Hakuna shirika jingine lolote liwezalo kufikia rekodi yao ya kazi ya kuonyesha huruma,” akiri Ram Desai. Zaidi ya utunzaji wa kitiba, Waafrika walijaribu kupata mali za kimwili za Ulaya. Baadhi ya wamishonari walianzisha vitovu vya biashara, kwani waliamini kwamba hilo lingewavuta waongofu. Kwa mfano, Misheni ya Basel kutoka Uswisi ilianzisha kampuni ya biashara katika Ghana. Walivumbua kwamba miti ya kakao ilimea vema huko, na leo Ghana ni nchi ya tatu ulimwenguni kati ya zile zinazotokeza kakao nyingi zaidi.
Ufanisi wenye kutokeza zaidi wa wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo ulikuwa kutafsiri kwao Biblia. Hata hivyo kueneza ujumbe wa Biblia huhusisha daraka jingine zito. Mtume Mkristo Paulo alionyesha hilo kwa kuuliza hivi: “Wewe umfundishaye mwingine, je! hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?” Biblia huonya kwamba wale wafundishao Ukristo ni lazima wenyewe waishi kulingana na kanuni njema zilizomo katika Neno la Mungu.—Warumi 2:21, 24.
Namna gani utendaji wa Jumuiya ya Wakristo katika Afrika? Je! imemheshimu Mungu wa Biblia, au imewakilisha vibaya mafundisho ya Kikristo?