Alipigania Imani Yake
MIAKA mitatu iliyopita Caridad Bazán Listán, mmoja wa Mashahidi wa Yehova katika Cádiz, Uhispania, alihitaji upasuaji wa haraka. Mawe ya nyongo yalikuwa yakisababisha homa na yalikuwa yakitia damu yake sumu. Alipolazwa katika hospitali ya huko, alieleza msimamo wake wenye msingi wa Biblia wa kukataa kukubali kutiwa damu mishipani. Madaktari walikubali kufanya upasuaji bila damu. Hata hivyo, kabla tu ya yeye kupelekwa ndani ya chumba cha upasuaji, madaktari walimwomba atie sahihi hati fulani. Ilionyesha kwamba walikuwa na nia ya kustahi uamuzi wake kuhusu damu lakini ikiwa hali ya dharura ingetukia, walitaka ruhusa yake ya kutumia utaratibu wowote wa kitiba uonwao kuwa wa lazima.
Mzee mmoja wa kundi aliyekuwapo kwenye hospitali pamoja na mwana wa Caridad, aliye Shahidi pia, walimweleza Caridad juu ya maana hasa ya kutia sahihi fomu ya jinsi hiyo. Sahihi yake ingaliwapa madaktari mamlaka ya kumtia damu iwapo hali ya dharura ingalitukia. Matabibu walipokuja kumpeleka ndani ya chumba cha upasuaji, alieleza kwamba asingetia sahihi karatasi hiyo. Bila kukawia alirudishwa kwenye chumba chake na kubanwa sana ili abadili uamuzi wake.
Baada ya mazungumzo kadhaa waliamua kumwita hakimu wa korti ili aweze kumsadikisha, lakini hilo halikufaulu. Caridad alieleza kwamba alihisi angekuwa na hatia mbele za Mungu ikiwa angewaruhusu wampe damu. Alionyesha kwamba chini ya Sheria ya Kimusa, ikiwa mwanamke angelalwa kinguvu, hangeonwa kuwa mwenye hatia ikiwa angekinza kwa kupiga makelele ili kupata msaada. (Kumbukumbu la Torati 22:23-27) “Madaktari wanapuuza mapenzi yangu na wanajaribu kuchafua dhamiri yangu,” akasema, “kwa hiyo ni lazima nikinze kana kwamba walikuwa wakinilala kinguvu.”
Saa kadhaa zilipita, na mwishoni madaktari wakakubali kumpasua bila damu. Katika chumba cha upasuaji, Caridad aliomba ruhusa ya kusali kwa Yehova. Alifanya hivyo, na upasuaji ukawa wenye mafanikio.
Hata hivyo, baadaye hali ya Caridad ikawa mbaya zaidi, na madaktari wakaamua kupuuza mapenzi yake na kumtia damu mishipani kwa lazima. Hivyo, daktari na mwuguzi mmoja walitayarisha kumtia damu mishipani. Ijapokuwa hali yake dhaifu, Caridad alikinza kwa nguvu zake zote. Hata akaweza kuiuma ile mrija ambamo damu ingepitia. Mwishoni, daktari huyo aliaibishwa sana na lile walilokuwa wakifanya hivi kwamba aliacha kulifanya. “Siwezi kuendelea kufanya hivi. Nimeshindwa!” akasema.
Caridad aliokoka taabu hiyo akapona bila matatizo mengine. Madaktari na wauguzi pia walivutiwa sana na imani na moyo wake mkuu. Yote hayo yalitukia wakati Caridad alipokuwa na umri wa miaka 94.