Je! Hirizi za Bahati Njema Zaweza Kukulinda?
KIPANDE cha fuwele kinachobebwa mfukoni mwa mwanamume Mbrazili. Sarafu ya bahati njema ya mwanariadha Mwamerika. Msalaba wa Mtakatifu Brigid ukining’inia juu ya kitanda katika nyumba ya familia ya Ailandi. Mamilioni ya watu hutumia vitu kama hivyo vikiwa hirizi za bahati njema au talasimu.a Wanaamini kwamba kuwa na hirizi hizo kwaweza kuondosha madhara na kuwaletea bahati njema.
Kwa kielelezo, fikiria Brazili. Kulingana na gazeti Veja, Wabrazili wengi hubeba “vipande vya mwamba na mawe yaliyo nusu johari yanayoonwa kuwa na nguvu za kumtwalia bahati njema na nishati za kimwili na za kiakili, yule mwenye kuyamiliki.” Wakihofu kuudhi roho za kishetani, wengine katika nchi hiyo huweka mfano wa kidini au andiko kwenye ukuta wa nyumba yao. Wengine hata hutumia Biblia ikiwa hirizi takatifu; wanaiweka kwenye meza, ikiwa imefunguliwa daima katika Zaburi 91.
Katika kusini mwa Afrika, muti, au dawa ya kienyeji, hutumiwa vivyo hivyo, si kwa sababu tu ya nguvu zayo za kuponya, bali ukiwa ulinzi dhidi ya bahati mbaya. Mara nyingi ugonjwa, kifo, hali mbaya za kiuchumi, na hata kukosa mafanikio katika mahaba huonwa kuwa tokeo la kurogwa na adui au tokeo la kukosa kuwatambikia wazazi wa kale waliokufa. Kwa kawaida muti hupatikana kutoka kwa mganga wa mashambani, anayefanyiza michanganyiko ya vitu kutoka mimea, miti, au vipande vya wanyama. Lakini, kwa ajabu, muti haumo katika maeneo ya mashambani tu; hilo zoea limeenea katika majiji ya Afrika Kusini. Wafanya biashara na wahitimu wa chuo kikuu ni miongoni mwa wale wanaotegemea muti.
Jitihada ya kutafuta bahati njema ni jambo la kawaida pia katika nchi za Ulaya. Kitabu Studies in Folklife Presented to Emyr Estyn Evans chatuarifu hivi: “Katika karibu kila mtaa au mji katika Ailandi waweza kuona vyuma vya kwato za farasi vikiwa vimefungwa kwenye au juu ya milango ya makao au majengo yaliyo kando ya nyumba.” Jambo la kawaida hata zaidi katika nchi hiyo ni ile misalaba iliyofumwa kutoka matete inayoning’inia juu ya vitanda na milango ili kuleta bahati njema. Watazamaji husema kwamba, kijuujuu, watu wengi wa Ailandi huonekana kuwa hawachukui kwa uzito ushirikina huo. Lakini, ni wachache ambao huupuuza kabisa.
Jitihada ya Kutafuta Ulinzi
Kwa nini imani hizo za kishirikina huvutia hivyo? Yaonekana ni kama zinaridhisha ule uhitaji wa msingi wa kupata usalama ambao watu huwa nao. Kwa kweli, ni wangapi wanaohisi kuwa salama wanapokuwa nyumbani mwao, acha wanapokuwa wakitembea barabarani usiku? Kuongezea hayo kuna ule mkazo wa kupata riziki na kuwatunza watoto. Naam, tunaishi katika kile kipindi ambacho Biblia huita “wakati wa taabu nyingi.” (2 Timotheo 3:1, The New English Bible) Kwa hiyo ni jambo la asili tu kwamba watu wanatamani sana kupata ulinzi.
Yaweza kuwa hivyo hasa katika tamaduni ambamo namna mbalimbali za uwasiliani-roho na uchawi zinapendwa sana. Kuhofu zile zinazodhaniwa kuwa roho za watu waliokufa (mizimu) au kuhofu kupatwa na laana ya adui kwaweza kufanya ule uitwao ulinzi wa hirizi au talasimu uonekane kuwa wa lazima. Kwa vyovyote vile, The World Book Encyclopedia yasema hivi: “Watu walio wengi wana hofu zinazowafanya wasihisi usalama. Ushirikina husaidia kushinda hofu hizo kwa kuandaa usalama. Unawahakikishia watu kwamba watapata wanachotaka na kuepuka taabu.”
Nguvu Zenye Kutilika Shaka za Talasimu
Kwa hiyo, talasimu, kago, na hirizi za aina na miundo mbalimbali zinavaliwa, kubebwa, na kuwekwa mahali fulani na watu kotekote ulimwenguni. Lakini je, yafaa kuamini kwamba hirizi iliyofanyizwa na mwanadamu inaweza kutoa ulinzi wowote wa kweli? Vitu vingi ambavyo mara nyingi hutumiwa vikiwa hirizi ni vifaa vya kibiashara vinavyofanyizwa kwa wingi. Je! si kinyume cha kusababu kuzuri na cha maoni ya kawaida kuamini kwamba kitu fulani ambacho kimefanyizwa katika kiwanda kingeweza kuwa na nguvu za kichawi? Na hata dawa ya umajimaji uliofanyizwa kipekee na mganga wa mashambani ni mchanganyiko tu wa vitu vya kawaida—mizizi, miti-shamba, na vitu kama hivyo. Kwa nini mchanganyiko wa jinsi hiyo uwe na uwezo wa kichawi? Isitoshe, je, kuna uthibitisho wowote wa kweli kwamba watu wanaotumia talasimu huishi muda mrefu zaidi—au ni wenye furaha zaidi—ya wale wasiozitumia? Je! wale wenyewe wanaozifanyiza hirizi hizo za kichawi hawapatwi na magonjwa na kifo?
Badala ya kuwapa watu ulinzi wa kweli na hisia ya kuweza kudhibiti maisha zao, kwa kweli utumizi wa kishirikina wa talasimu na hirizi huwazuia watu wasikabili matatizo yao kwa kutumia akili na kuwatia moyo watazamie bahati kuwa ndilo suluhisho la mambo yote. Kutumaini katika nguvu za talasimu kwaweza pia kumpa mwenye kuzitumia hisia bandia ya usalama. Mtu aliye chini ya uvutano wa kileo aweza kudai kwamba uthabiti wa fikira na miendo yake na nguvu zake mbalimbali haujalegea, lakini akijaribu kuendesha gari, yaelekea atajidhuru mwenyewe au wengine. Mtu anayeweka uhakika wake katika nguvu za talasimu aweza vilevile kujidhuru mwenyewe. Kwa kujidanganya kwamba analindwa, huenda akawa na mwelekeo wa kujihatarisha kipumbavu au kufanya maamuzi yasiyo yenye hekima.
Imani katika nguvu za talasimu hutokeza hatari nyinginezo nzito zisizoonekana wazi na wale mamilioni wanaozitumia. Hatari hizo ni zipi, na je, kuna njia yoyote ifaayo ya kuzuia madhara? Makala ifuatayo itashughulikia maswali hayo.
[Maelezo ya Chini]
a Kamusi ya Kiswahili Sanifu yafasili “talasimu” kuwa “kipande cha karatasi au ngozi kilicho na maandishi maalumu ambacho huangikwa ukutani au mlangoni [au kinachovaliwa] na ambacho huaminiwa na baadhi ya watu kuwa ni kinga ya madhara.”