Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 9/15 kur. 30-31
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Habari Zinazolingana
  • Kukabiliana na Madeni
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Deni! Kuingia Humo Kutoka Humo
    Amkeni!—1991
  • Matatizo ya Pesa na Madeni—Je, Biblia Inaweza Kukusaidia?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Ukopeshaji wa Pesa na Upendo wa Kikristo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 9/15 kur. 30-31

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Katika nyakati hizi zilizo ngumu kiuchumi, watu wengi na kampuni nyingi zaidi na zaidi zinajitangaza kuwa zimefilisika. Je, inafaa Kimaandiko kwa Mkristo kutafuta ulinzi wa kisheria wa kufilisika?

Jibu la swali hilo laandaa kielezi kizuri cha jinsi Neno la Mungu hutoa mwongozo utumikao kwa mambo ambayo huenda yakawa hasa ya kisasa. Nchi nyingi zina sheria za kusimamia hali ya kufilisika. Sheria hizo hutofautiana kutoka nchi hadi nchi, na si jambo la kutaniko la Kikristo kutoa shauri la kisheria kwa suala hilo. Lakini ebu tupitie mambo ya kisheria yahusuyo kufilisika.

Sababu moja ifanyayo serikali ziruhusu watu mmoja mmoja na biashara kujitangaza kuwa zimefilisika ni kwamba kufanya hivyo kwalinda kwa kiasi fulani wenye kukopesha (wadai) kutoka kwa watu au biashara zinazokopa (wadeni) lakini hazilipi madeni hayo. Kwa wadai, yaonekana kuwa njia ya pekee ni kuendea mahakama ili mdeni atangazwe kuwa amefilisika ili mali ya mdeni iweze kugawanywa kuwa malipo kidogo ya deni.

Njia nyingine ambayo sheria ya kufilisika hutenda kazi ni kuwa ulinzi kwa wadeni ambao kwa kweli hawawezi kuridhisha wadai wao. Mdeni aweza kuruhusiwa kujitangaza kisheria kuwa amefilisika, ambapo sasa wadai wake waweza kuchukua baadhi ya mali zake. Lakini, bado sheria yaweza kumruhusu abaki na nyumba yake au mali kidogo naye aendelee na maisha bila kutishwa daima na wadai wake kupoteza mali zaidi au kunyang’anywa zaidi.

Basi ni wazi kwamba sheria hizo zinakusudiwa kutoa ulinzi wa kadiri fulani kwa pande zote mbili katika mambo ya kifedha au kibiashara. Basi, ebu tuone shauri lenye msaada litolewalo na Biblia.

Ni vigumu kusoma Biblia yote bila kutambua kwamba haipendekezi kuingia katika deni. Twapata maonyo kama ya Mithali 22:7: “Tajiri humtawala maskini, naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.”

Kumbuka pia kielezi cha Yesu kwenye Mathayo 18:23-34 kilichohusu mtumwa aliyekuwa na deni kubwa sana. “Bwana akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo,” lakini bwana huyo, mfalme, akamwacha na kumhurumia. Baadaye mtumwa huyo alipokosa kuwa mwenye rehema, mfalme huyo alimwamuru ‘apelekwe kwa walinzi wa jela, hata atakapoilipa deni ile yote.’ Kwa wazi, mwendo bora zaidi upendekezwao ni kuepuka kukopa pesa.

Watumishi wa Mungu katika Israeli la kale walikuwa na shughuli za biashara, na nyakati nyingine kulikuwa na kukopesha na kukopa. Yehova aliwaamuru wafanye nini? Ikiwa mtu alitaka kukopa pesa za kuanzisha biashara au kuipanua, ilikuwa halali na jambo la kawaida kwa Mwebrania kutoza riba. Lakini, Mungu aliwahimiza watu wake wasiwe wachoyo wanapokopesha Mwisraeli mwenye uhitaji; wao hawakupaswa kupata faida kutokana na hali mbaya za wengine kwa kutoza riba. (Kutoka 22:25) Kumbukumbu la Torati 15:7, 8 yasema: “Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo . . . , mfumbulie mkono wako kwa kweli umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo.”

Fadhili au ufikirio kama huo ulionyeshwa katika maagizo yaliyoamuru kwamba wadai hawangeweza kutwaa vitu vilivyohitajiwa maishani kutoka kwa mdeni, kama vile jiwe la kusagia la familia au vazi la kumpasha joto wakati wa usiku.—Kumbukumbu la Torati 24:6, 10-13; Ezekieli 18:5-9.

Bila shaka, si Wayahudi wote walikubali na kutumia zisemazo sheria hizo zenye upendo kutoka kwa Mwamuzi na Mfanya-sheria wao mkuu. (Isaya 33:22) Wayahudi fulani wenye pupa waliwatenda ndugu zao kikatili. Leo, pia wadai fulani waweza kuwa wenye kudhulumu na wasiofikiri vizuri katika madai yao, hata kuelekea Mkristo mnyoofu ambaye wakati huo hangeweza kulipa deni hilo kwa sababu ya mambo yasiyotazamiwa. (Mhubiri 9:11) Kwa mkazo wao usiobadilika, wenye kudai sana, wadai wa kilimwengu waweza kumsukuma mdeni aingie katika hali ambayo ni lazima ajilinde. Kwa njia gani? Katika visa fulani, jambo la pekee ambalo wadai watatambua ni kuchukua hatua ya kisheria ya kujitangaza kuwa umefilisika. Kwa hiyo, Mkristo ambaye si mwenye pupa au mwenye kupuuza madeni yake, aweza kulazimika kuchukua hatua ya kisheria ya kujitangaza kuwa amefilisika.

Ingawa hivyo, twapaswa kuangalia upande mwingine pia wa jambo hilo. Huenda Mkristo ana deni kwa sababu tu hakujidhibiti kwa matumizi yake au kwa sababu hakufikiri vizuri kimbele katika maamuzi yake ya kibiashara. Je, awachilie tu deni alilo nalo na kupata suluhisho la kujitangaza kufilisika, kwa hiyo akiumiza wengine kwa sababu ya kutoamua mambo vizuri? Biblia haikubali hali hiyo ya kutojali mambo ya kifedha. Inahimiza mtumishi wa Mungu aache ndiyo yake iwe ndiyo. (Mathayo 5:37) Fikiria pia maelezo ya Yesu kuhusu kuhesabu gharama kabla ya kuanza kujenga mnara. (Luka 14:28-30) Kwa kupatana na hilo, Mkristo apaswa kufikiria kwa uzito mambo mabaya yawezayo kutokea kabla ya kukopa fedha. Achukuapo tu mkopo huo, yeye apaswa kutambua daraka lake la kulipa watu mmoja mmoja au kampuni zinazomdai pesa alizokopa. Ikiwa watu wengine wengi wangemwona Mkristo kuwa asiyejali daraka lake au asiyetumainiwa, huenda atakuwa ameharibu sifa nzuri ambayo amekuwa akitafuta na basi asiwe tena na ushuhuda mwema kwa watu wa nje.—1 Timotheo 3:2, 7.

Kumbuka yale Zaburi 15:4 yatuambia kuhusu aina ya mtu ambaye Yehova hukaribisha. Twasoma hivi: “Ameapa [yule akubaliwaye na Mungu] kwa hasara yake, hayabadili maneno yake.” Ndiyo, Mungu hutazamia Wakristo watendee wadai wao jinsi wao wangependa kutendwa.—Mathayo 7:12.

Basi kwa ufupi, Biblia haikatazi uwezekano kwamba katika hali mbaya sana, Mkristo aweza kuendea ulinzi wa sheria za kufilisika zitolewazo na serikali ya Kaisari. Hata hivyo, ni lazima Wakristo wajitokeze sana kuwa watu wanyoofu na wenye kutegemeka. Kwa hiyo, wao wapaswa kuwa wanyoofu kwa hali yao ya kutaka kutekeleza wajibu wao wa kifedha.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki