Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 12/15 kur. 19-22
  • Mtihani wa Afya Kwako?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mtihani wa Afya Kwako?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Afya—Kwa Gharama Gani?
  • Ni Nguvu Zipi Zinazohusika?
  • Jihadhari!
  • Misuli—Kazi Bora za Ubuni
    Amkeni!—1999
  • Uwe na Maoni Yanayopatana na Maandiko Kuhusu Matibabu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Je, Mkristo Anaweza Kukubali Matibabu?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Dawa za Vichakani—Je! Wakristo Watafute “Mapozo” Yake?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 12/15 kur. 19-22

Mtihani wa Afya Kwako?

Watch Tower Society haipendekezi wala kuamulia watu mmoja-mmoja juu ya njia za kitiba au za kugundua magonjwa. Hata hivyo, ikiwa aina fulani za tiba zina sehemu ambazo zinatiliwa shaka na kanuni za Biblia, basi hizo zaweza kufikiriwa. Kisha kila mtu aweza kupima kile kinachohusika na kuamua jambo la kufanya.

Ndugu Wapendwa: Ningependa kujua maoni yenu. [Daktari mmoja] anaonekana kufanikiwa, lakini natilia shaka njia anayotumia. . . . Yeye hukupima ili ajue tatizo. Kisha ili ajue aina ya dawa ya kutumiwa au kiasi cha kutumiwa, yeye huweka chupa ya dawa kando ya ngozi iliyo karibu na tezi au kiungo fulani cha mwili. Yeye hujaribu kuvuta chini mkono ulionyooshwa wa mgonjwa. Aina ya dawa au kiasi cha dawa ya kutumiwa huamuliwa kwa nguvu anazohitaji katika kuvuta mkono huo chini. Wazo ni kwamba elektroni, kama ulivyo mkondo, husafiri kutoka kwenye dawa kupitia kifuniko cha chuma cha ile chupa hadi sehemu ya mwili, ikiuimarisha. Ni kama kutafuta maji kupitia fimbo ya kuyagundua yalipo?

BARUA hii kutoka Oregon, Marekani, yahusu aina ya tiba ambayo watu wengine hutumia kukadiria mahitaji ya lishe, kupima masuala ya kihisia-moyo, kuchanganua kumbukumbu, na kusuluhisha maswali juu ya maisha ya kila siku. Hata hivyo, aina hiyo ya tiba iwe ya kawaida sana kama nini, je, ni sawa kwa mwandikaji wa barua hiyo kutilia shaka?

Afya—Kwa Gharama Gani?

Tangu nyakati za kale, watu wamejaribu kuelewa sababu inayowafanya wawe wagonjwa na jinsi ya kupona. Waisraeli walikuwa na mafaa kwa sababu walijua wao ni wenye dhambi, nao walikuwa na sheria kutoka kwa Mungu zilizowasaidia kuepuka kushikwa na maradhi au kuyaeneza. (Mambo ya Walawi 5:2; 11:39, 40; 13:1-4; 15:4-12; Kumbukumbu la Torati 23:12-14) Na bado, watu wa Mungu walitafuta msaada wa matabibu waliostahili wa siku zao.—Isaya 1:6; 38:21; Marko 2:17; 5:25, 26; Luka 10:34; Wakolosai 4:14.

Hilo lilikuwa tofauti kama nini na watu wa Babiloni na Misri za kale! “Madaktari” wao walikuwa na tiba za aina fulani zilizotegemea viungo vya asili, lakini nyingi za “tiba” zao sasa zingeitwa tiba za bandia. Mwandiko wa mchoro wa Kimisri waeleza juu ya tabibu anayetibu upofu kwa mchanganyiko mbaya wa dawa ya kunywewa iliyofanyizwa kwa macho ya nguruwe, unga-unga wa wanja, udongo mwekundu, na asali. Mchanganyiko huo wa dawa ulimwagwa katika masikio ya mgonjwa! Ushuhuda fulani wa kale wadai kwamba tiba hiyo ilikuwa “bora kabisa.” Uzuzu wao au fumbo lao huenda ndio uliofanya upendwe na watu.

Mara nyingi Wababiloni na Wamisri waliomba nguvu za kifumbo.a Kuhani aliyekuwa pia tabibu angemwambia mgonjwa apumue kupitia mapua ya kondoo, akiamini kwamba kani fulani, au nishati, zingetoka kwa mgonjwa na kuingia katika kiumbe kingine na kutokeza matokeo. Kondoo huyo aliuawa, na ilisemekana kwamba ini lake lingefunua ugonjwa wa mgonjwa huyo au wakati ujao wake.—Isaya 47:1, 9-13; Ezekieli 21:21.

Bila shaka, tabibu aliyemhofu Mungu katika Israeli ya kale hangetumia mambo ya kiuchawi. Mungu aliamuru hivi kwa hekima: “Asionekane kwako . . . mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri . . . Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA.” (Kumbukumbu la Torati 18:10-12; Mambo ya Walawi 19:26; 20:27) Jambo hilo latumika kwa watumishi wa Mungu walio Wakristo leo. Inafaa kujihadhari.

Katika miaka ya karibuni watu wengi wamegeukia njia za kugundua ugonjwa na za tiba “zisizo kawaida.” Kwa ujumla hilo ni eneo la kufanya uamuzi wa binafsi. (Mathayo 7:1; linganisha Warumi 14:3, 4.) Bila shaka, lingekuwa jambo la kuhuzunisha ikiwa Mkristo yeyote angejishughulisha mno na masuala ya afya yanayobishaniwa hivi kwamba hayo yawe mambo makubwa kuliko huduma, ambayo ndiyo njia ya pekee ya kuokoa uhai. (1 Timotheo 4:16) Biblia haisemi kwamba katika ulimwengu mpya magonjwa yatatibiwa na watu kupata afya kamili kupitia njia za kitiba, dawa za mimea, ulaji maalumu, au tiba fulani maalumu. Kwa kweli, ponyo kamili litapatikana tu kwa njia ya msamaha wa dhambi kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu.—Isaya 33:24; Ufunuo 22:1, 2.

Ni Nguvu Zipi Zinazohusika?

Mkristo atafikiria nini anapojiamulia kuhusu njia ya tiba ya kupima misuli iliyotajwa hapo awali?

Njia fulani za kupima nguvu au itikio la misuli ni sehemu ya tiba za kawaida, na ni watu wachache tu wangebisha uhalali wazo. Kwa mfano, ugonjwa wa kupooza waweza kudhoofisha misuli, na tiba yao yaweza kuhusisha kile kinachoitwa kinesiolojia—“uchunguzi wa misuli na miendo ya misuli.” Kinesiolojia kama hiyo hutumiwa pia ikiwa tiba ya kuwapa nguvu wale waliopatwa na maradhi ya moyo. Watu wengi wanaelewa matibabu ya aina hiyo.

Lakini vipi juu ya kupima nguvu ya misuli kulikotajwa katika ile barua iliyo mwanzoni mwa makala hii? Aina hiyo ya “kinesiolojia” imetumiwa katika kujaribu kuchunguza kama vyakula vya aina fulani, mimea, au vitamini zinaweza kusaidia au kuumiza mtu. Kama hufanywavyo, mtu hunyoosha mkono wake, na daktari huyo husukuma mkono chini ili kupima nguvu ya misuli. Halafu mgonjwa huyo huweka lishe fulani au kitu fulani kinywani mwake, au kwenye uvungu wa tumbo, au mkononi mwake. Kisha nguvu ya misuli ya mikono hupimwa tena. Inadaiwa kwamba ikiwa anahitaji lishe hiyo, mkono wake utakuwa na nguvu zaidi, kama ni mbaya kwake, misuli yake itakuwa dhaifu zaidi.b

Wengine waliojaribu njia hii wanaamini kwamba inafanya kazi na kwamba matokeo yanategemea nguvu zilizo katika mwili. Wao wanasababu kwamba kuna mambo mengi ambayo sayansi ya kisasa haiwezi kueleza lakini yanatendeka au yaweza kuonwa. Kwa hiyo, wao hudai kwamba huenda kuna mikondo ya nishati au uchangamano kati ya nishati na vitu, hata kama matabibu hawajazigundua au kuzikubali.

Kwa upande mwingine, kitabu Applied Kinesiology chasema: “Nyakati nyingine [vitabu] hufundisha kwamba vitu vya kemikali, kama vyakula, huchanganuliwa kwa kubeba kitu hicho mkononi na kupima nguvu ya misuli. Hakuna uthibitisho wowote unaodokeza utegemeo wa aina hii ya kupima. . . . Itikadi za daktari zaweza kuwa zenye nguvu sana kiasi cha kwamba anaweza kulaghai habari sahihi za kupimwa.” “Mchunguzi mwenye ujuzi wa muda mrefu katika kupima msuli aweza kwa urahisi sana kufanya misuli ya mgonjwa ionekane kuwa dhaifu au kuwa na nguvu zaidi kulingana na jinsi anavyotaka kwa kubadili . . . kidogo tu njia ya kupima.”

Jihadhari!

Lakini, njia nyinginezo za kupima misuli huhusisha mambo mengi zaidi. Ebu fikiria kile kiitwacho “njia ya kupima ya badala.” Hilo laweza kufanywa kwa mtu mzee-mzee au mtoto aliye dhaifu mno kuweza kupimwa. Mtu wa badala anapomgusa mtoto, daktari huyo hupima mkono wa mtu huyo wa badala. Njia hiyo ya kupima imetumiwa hata kwa wanyama wapendwao; mkono wa mtu wa badala ukipimwa ukiwa umewekwa kwenye mbwa waitwao collie, German shepherd, au mnyama mwingine yeyote apendwaye aliye mgonjwa.

Si juu yetu kuhukumu matendo kama hayo, lakini huenda ukauliza, ‘Je, kani za kimwili ndizo hutokeza matokeo hayo?’ Wanasayansi wamethibitisha kuwapo kwa miali-anga, vijiwimbi, na aina kadhaa za mnururisho wa sumaku-umeme. Lakini, je, viumbe vyote, hata vitoto na wanyama wa nyumbani wapendwao, wana kani ndani yao ziwezazo kutoka na kutokeza matokeo yawezayo kupimwa kwa mtu wa pili? Wababiloni walifikiri kwamba kani zingeweza kutoka na kuathiri kondoo. Waweza kujiuliza, ‘Je, ninaamini kwamba kitu kifananacho na hicho chaweza kutendekea wanadamu au wanyama leo? Au matokeo yaweza kuelezwa kwa njia nyingine?’

Waponyaji fulani hudai kwamba wanapima “kani” za mtu kwa vyombo kama parafujo ya chuma au pendulami. Yasemekana kwamba hizo husonga wakati “mkondo wa nishati” wa mponyaji unapochangamana na ule wa mgonjwa. Daktari mmoja aliye pia mwandikaji wa habari hizi, ambaye wakati mmoja alikuwa mwanasayansi wa utafiti, nyakati nyingine hugundua ugonjwa kwa kutumia pendulami. Yeye asisitiza pia kwamba anaweza kuona “mkondo wa nishati ya binadamu” au mviringo wenye rangi unaosemwa kuwa huzingira watu mmoja-mmoja. Yeye adai kwamba anatumia “mwono wa ndani ya mwili” ili kutazama kupitia mwili na kuona vivimbe, chembe za damu, au vijiumbe vya maradhi, na kuona mambo yaliyopita.c

Kama ilivyoonyeshwa mapema, kupima kani kwa kutumia nguvu ya mkono kumetumiwa katika kukadiria hali ya kihisia-moyo. Kitabu kimoja ambacho kimeenezwa sana kilisema hivi: “Ukitamani kuongezea njia fulani ndogo ya kupima hali ya kihisia-moyo wakati uleule, uliza kwa sauti ‘Je, una tatizo?’ na upime tena. Pindi kwa pindi hilo litadhoofisha mkono ikiwa mgonjwa hafaidiki sana na ile lishe inayotumiwa kwa kupimwa huko.” Wengine hutumia njia ya kupima kama hiyo “ili kutambua umri ambao usumbufu fulani hususa wa kimwili, kihisia-moyo au kiroho” ulipotokea. Hilo hutumiwa pia katika kufanya maamuzi ya ‘ndiyo au la’ kwa mambo ya kawaida.

Yaelekea kwamba wengi ambao hupimwa misuli kwa njia hiyo (kinesiolojia) wanaweza kusema kwamba aina yao ya tiba yatofautiana na ile ambayo imetoka kufafanuliwa, na kwamba hakuna uwasiliani-roho wowote unaohusika, au kwamba wao hawapimi hali ya kihisia-moyo. Lakini, je, yale wanayofanya bado yanategemea itikadi ya kuwapo kwa kani ndani ya kila binadamu zinazoweza kupimwa au kuonwa na watu fulani tu wanaodai kuwa na uwezo wa kipekee?

Wakristo hawachukui masuala kama hayo vyepesi. Mungu alishauri Israeli: “Mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo [“nguvu hizo za kifumbo,” NW] na makutano ya ibada.” (Isaya 1:13) Taifa la Israeli lilipokuja kuasi, lilikuwa ‘likipiga ramli na kufanya uchawi.’ (2 Wafalme 17:17; 2 Mambo ya Nyakati 33:1-6) Kwa wazi walitafuta habari kupitia desturi za kipekee, nao walisema juu ya “zile ambazo ni nguvu za kifumbo.”—Zekaria 10:2, NW.

Njia fulani za kujaribu nguvu ya misuli zaweza kuwa hazina madhara, zikifanywa bila kudhuru mgonjwa au daktari. Lakini, kwa wazi mengine yanaweza kuwa na nguvu za kifumbo au zenye kupita uwezo wa kibinadamu, kama vile kuweza kuona ndani ya mwili, miviringo ya kifumbo, na matumizi ya pendulami. Wakristo hawapaswi hata kidogo kutumia nguvu za kifumbo. Hawapaswi hata kuzijaribu, kwa kuwa wao hawadadisi mambo ya ndani ya Shetani. (Ufunuo 2:24) Badala ya hivyo, kuna sababu nzuri ya kutahadhari kuhusu kitu chochote kiwezacho kuonekana kama kina uhusiano na matendo ya uwasiliani-roho, ambao Neno la Mungu lashutumu.—Wagalatia 5:19-21.

Kile ambacho daktari anafanya ni jukumu lake, na si kusudi letu kukipitia au kukihukumu kwa yale kila mmoja anadai au njia yake ya tiba. Hata kama unahisi kwamba baadhi ya matendo hayo yanahusu nguvu za kifumbo, ni wazi kwamba wengi walioyajaribu walifanya hivyo bila kukusudia, bila kujua chochote juu ya kujiingiza katika uwasiliani-roho. Huenda hilo lilikuwa wonyesho tu wa jinsi wanavyotaka sana kupata afya bora. Na bado, wengine ambao wamehusika na matendo kama hayo wameamua baadaye kwamba manufaa yoyote ya kimwili yawezayo kupatikana hayastahili kujihatarisha kiroho.

Tena, ni lazima kila mtu mmoja-mmoja aazimie jambo la kufanya kuhusu mambo ya binafsi kama hayo. Lakini, Wakristo wapaswa kukumbuka shauri la Mungu: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” (Mithali 14:15) Hilo latumika pia juu ya madai ya afya.

Shetani anatamani kukengeusha watumishi wa Mungu kutoka kwa ibada ya kweli. Ibilisi angefurahi ikiwa angefanya hivyo kwa kuwafanya Wakristo wavutiwe na mapendezi mengine. Yeye angefurahi hata zaidi iwapo wangevutiwa na vitu ambavyo ni, au vinavyoonekana kuwa, matendo ya kifumbo yanayoweza kuwaingiza katika uwasiliani-roho.—1 Petro 5:8.

Ingawa Wakristo hawako chini ya Sheria ya Kimusa, mtazamo wa Yehova Mungu kuelekea matendo ya uchawi haujabadilika. Kama ilivyotajwa mapema, Mungu aliamuru Waisraeli kwamba ‘mtu atazamaye bao, mtu atazamaye nyakati mbaya, mwenye kubashiri, msihiri, mtu alogaye kwa kupiga mafundo’ hakupaswa kupatikana miongoni mwao. “Mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA . . . Uwe mkamilifu kwa BWANA.”—Kumbukumbu la Torati 18:10-13.

Basi, ni jambo la hekima kama nini kwa Wakristo leo kudumisha kuvaa “suti kamili ya silaha kutoka kwa Mungu . . . kwa sababu tunapigana mwereka . . . dhidi ya majeshi ya roho waovu katika mahali pa kimbingu”!—Waefeso 6:11, 12, NW.

[Maelezo ya Chini]

a Watu wengi bado huwaendea shamani, wachawi, au waponyaji kama hao. Shamani ni “kuhani anayetumia uchawi kwa kutibu wagonjwa, kufunua yaliyofichwa, na kudhibiti matukio.” Mchawi au shamani, aweza kuchanganya majani na mambo ya kiuchawi (akiomba nguvu za kifumbo). Mkristo mwangalifu aliye mwaminifu-mshikamanifu angeepuka kujiingiza katika mambo ya uwasiliani-roho kama hayo, hata kama yaonekana atatibiwa.—2 Wakorintho 2:11; Ufunuo 2:24; 21:8; 22:15.

b Huo ni ufafanuzi wa ujumla, lakini njia za kupima misuli zaweza kutofautiana. Kwa kielelezo, mgonjwa aweza kuambiwa avifinye vidole vya gumba na shahada pamoja, naye daktari ajaribu kuvitenganisha.

c Yeye aandika: “Matukio hayo kama miujiza hutendekaje? . . . Mimi hutumia njia ya kuwekea mikono, kuponya kwa imani au kuponya kiroho. Si njia ya kifumbo hata kidogo, bali ni njia inayoeleweka wazi . . . Kila mtu ana mkondo wa nishati au mviringo unaozingira na kupenya mwili halisi. Mkondo huo wa nishati wahusiana sana na afya. . . . Hisi za Juu Sana za Utambuzi ni aina nyingine ya ‘kuona’ ambayo waona picha akilini mwako bila kutumia mwono wako wa kawaida. Si kitu cha kuwaziwa. Nyakati nyingine hurejezewa kuwa nguvu ya kuona yasiyoweza kuonekana.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki