Alikuwa Mtangulizi wa Mesiya
MSHIPI mpana wa ngozi ulifanya mwili wake uliochomwa na jua utokeze sana. Akivalia vazi la manyoya ya ngamia, kwa kweli alionekana kama nabii. Watu wengi walivutwa kwake katika mto Yordani. Huko, mtu huyu mwenye kustaajabisha alitangaza kwa ujasiri kwamba alikuwa tayari kubatiza watenda dhambi wenye kutubu.
Watu walishangaa! Mtu huyu alikuwa nani? Alikuwa na kusudi gani?
Yesu Kristo alisema hivi juu ya mtu huyu: “Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii. . . . Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji.” (Mathayo 11:9-11) Kwa nini Yohana alikuwa mtu wa kipekee sana hivyo? Kwa sababu alikuwa mtangulizi wa Mesiya.
Utume Wake Ulitabiriwa
Zaidi ya miaka 700 kabla ya kuzaliwa kwa Yohana, Yehova alitangaza kwamba huyu angeita kutoka nyikani: “Itengenezeni . . . njia ya BWANA; nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.” (Isaya 40:3; Mathayo 3:3) Zaidi ya miaka 400 kabla ya kuzaliwa kwa Yohana, Mungu Mweza Yote alitangaza hivi: “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya BWANA, iliyo kuu na kuogofya.” (Malaki 4:5) Jambo la kwamba Yohana Mbatizaji alizaliwa karibu miezi sita kabla ya Yesu halikutukia tu lenyewe, wala haukutukia kikawaida tu. Kama ilivyo na kuzaliwa kwa mtoto aliyeahidiwa Isaka, kuzaliwa kwa Yohana kulikuwa mwujiza, kwa kuwa wazazi wake wote wawili, Zakaria na Elisabeti, walikuwa wamepita umri wa kuzaa watoto.—Luka 1:18.
Hata kabla ya Yohana kutungwa mimba, utume wake, kazi, na njia yake ya maisha ilifunuliwa na malaika Gabrieli. Akiwa na nguvu na roho ya Eliya, Yohana angebadili watu wasiotii kutoka kwa njia ya kifo na kuwatayarisha kukubali Yesu kuwa Mesiya. Tangu kuzaliwa, Yohana alikuwa Mnadhiri, aliyejitoa kabisa kwa Mungu, naye hakuwa anywe divai wala pombe kali. Kwa kweli, chakula chake jangwani kilikuwa “nzige na asali ya mwitu.” (Marko 1:6; Hesabu 6:2, 3; Luka 1:13-17) Kama Samweli, tangu utotoni Yohana alikuwa ametengwa kwa ajili ya utumishi mtakatifu wa Mungu Aliye Juu Zaidi.—1 Samweli 1:11, 24-28.
Hata jina Yohana lilichaguliwa na Mungu. Jina la Kiebrania lililotafsiriwa “Yohana” lamaanisha “Yehova Ameonyesha Pendeleo; Yehova Amekuwa Mwenye Rehema.”
Mtoto huyo alipotahiriwa katika siku ya nane, babaye, Zakaria, alipuliziwa kimungu kutangaza hivi: “Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake; uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao. Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia.” (Luka 1:76-78) Huduma ya peupe ya Yohana ilikuwa iwe muhimu zaidi maishani mwake. Mambo mengine yote hayakuwa na maana yakilinganishwa nayo. Kwa hiyo, Maandiko yasimulia miaka 30 ya kwanza ya maisha ya Yohana katika mstari mmoja tu: “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.”—Luka 1:80.
Sauti Nyikani
Katika mwaka wa 15 wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa gavana wa Yudea, Yohana Mbatizaji alitokea nyikani akiwa na ujumbe huu wenye kugutusha: “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” (Mathayo 3:2; Marko 1:4; Luka 3:1, 2) Wakazi wa eneo hilo lote waliamshwa. Tangazo hilo lenye ujasiri liligusa mioyo ya watu waliotamani tumaini hakika. Tangazo la Yohana pia lilijaribu unyenyekevu wa mtu kwa sababu lilihitaji toba ya moyoni. Unyoofu na usadikisho wake ulisukuma umati wa watu wanyoofu na wenye mioyo ya haki kumwona kuwa mtu aliyetumwa na Mungu.
Sifa ya Yohana ikaenea upesi sana. Akiwa nabii wa Yehova, alitambulika kwa urahisi kwa mavazi yake na ujitoaji wake. (Marko 1:6) Hata makuhani na Walawi walisafiri kutoka Yerusalemu kutafuta kujua ni nini lililokuwa likitokeza upendezi huo mwingi. Tubuni? Kwa nini, na kutubia nini? Mtu huyu alikuwa nani? Wao walitaka kujua. Yohana alieleza: “Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule?”—Yohana 1:20-25.
Toba na ubatizo zilikuwa hatua za lazima kwa wale ambao wangeingia katika Ufalme. Kwa hiyo, Yohana alijibu: ‘Nabatiza watenda dhambi wenye kutubu kwa maji, lakini baada yangu mtu mwenye nguvu zaidi atawabatiza kwa roho takatifu na moto. Kwani hata sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Na mjihadhari! Amebeba pepeo mkononi mwake naye ataikusanya ngano ghalani mwake lakini atateketeza kwa moto na kuharibu makapi.’ (Luka 3:15-17; Matendo 1:5) Kwa kweli, wafuasi wa Mesiya wangepewa roho takatifu, lakini maadui wake wangepatwa na moto wa uharibifu.
“Watu wa Namna Zote” Waonywa
Wayahudi wengi wenye mioyo ya haki waliguswa moyo sana na maneno ya Yohana nao wakakiri dhambi zao waziwazi za kukosa kuwa waaminifu kwa agano la Sheria. Wao walionyesha peupe toba yao kwa kuruhusu Yohana awabatize katika Mto Yordani. (Mathayo 3:5, 6) Tokeo likawa kwamba mioyo yao ilikuwa katika hali nzuri ya kupokea Mesiya. Akiridhisha kiu yao ya kutaka ujuzi wa matakwa ya uadilifu ya Mungu, kwa furaha Yohana aliwafundisha wakiwa wanafunzi wake, hata akiwafundisha namna ya kusali.—Luka 11:1.
Kuhusu mtangulizi huyu wa Mesiya, mtume Yohana aliandika hivi: “Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote [“watu wa namna zote,” NW] wapate kuamini kwa yeye.” (Yohana 1:7) Hivyo ikawa kwamba watu wa namna zote wakaja kumsikia Yohana Mbatizaji alipokuwa ‘akiwahuburi watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba.’ (Matendo 13:24) Aliwaonya watoza-ushuru dhidi ya upunjaji. Akawaonya askari dhidi ya kunyanyasa mtu yeyote au kufanya mashtaka bandia. Naye aliwaambia hivi Mafarisayo na Masadukayo wanafiki na wenye ujitoaji: “Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.”—Mathayo 3:7-9; Luka 3:7-14.
Wakiwa jamii, viongozi wa kidini wa siku ya Yohana walikataa kumwamini nao walimshtaki kwa uwongo kuwa ana mashetani. Walikataa njia ya uadilifu iongozayo kwenye uhai wa milele. Kwa upande mwingine, watoza-ushuru na makahaba wenye dhambi walioamini ushuhuda wa Yohana walitubu na kubatizwa. Baadaye, walimkubali Yesu Kristo kuwa ndiye Mesiya.—Mathayo 21:25-32; Luka 7:31-33.
Mesiya Ajulishwa
Kwa miezi sita—tangu vuli ya 29 W.K.—Shahidi mwaminifu wa Mungu Yohana alielekeza fikira za Wayahudi kwa Mesiya aliyekuwa akija. Ulikuwa wakati wa Mfalme Mesiya kutokea. Lakini alipotokea, alikuja kwenye maji yaleyale ya Yordani akaomba abatizwe. Kwanza Yohana alikataa, kisha akakubali. Ebu wazia shangwe yake wakati roho takatifu iliposhuka juu ya Yesu na sauti ya Yehova ikasikika ikielezea ukubalifu wake wa Mwana Wake.—Mathayo 3:13-17; Marko 1:9-11.
Yohana alikuwa ndiye mtu wa kwanza kumtambua Yesu kuwa Mesiya, naye aliwajulisha wanafunzi wake mwenyewe kwa huyu Mtiwa-Mafuta. “Tazama,” akasema Yohana, “Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” Alitangaza hivi pia: “Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji.”—Yohana 1:29-37.
Kazi ya Yohana ilienda sambamba na ile ya huduma ya Yesu kwa karibu miezi sita. Kila mmoja wao alielewa kazi ambayo mwenzake alikuwa akifanya. Yohana alijiona kuwa rafiki ya Bwana-Arusi akafurahi kumwona Kristo akiongezeka huku yeye na kazi yake ikipungua.—Yohana 3:22-30.
Yesu alimtambua Yohana kuwa mtangulizi wake, aliyefananishwa na Eliya. (Mathayo 11:12-15; 17:12) Katika pindi moja, Yesu alisema: “Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.”—Luka 16:16.
Mwaminifu Hadi Mwisho
Yohana alishikwa na kufungwa gerezani kwa sababu alitangaza kweli kwa ujasiri. Hakuepa daraka lake la kufunua hata dhambi ya Mfalme Herode. Akikiuka sheria ya Mungu, mfalme huyo alikuwa akiishi maisha ya uzinzi pamoja na Herodia, mke wa ndugu yake mwenyewe. Yohana alisema jambo hilo waziwazi ili mtu huyo aweze kutubu na kupata rehema ya Mungu.
Yohana alikuwa kielelezo kizuri kama nini cha imani na upendo! Kwa kudhabihu uhuru wake binafsi, alithibitisha uaminifu wake kwa Yehova Mungu na upendo wake kwa wanadamu wenzake. Baada ya kufungwa kwa mwaka mmoja, Yohana alikatwa kichwa kutokana na hila iliyochochewa na Ibilisi na kutungwa na Herodia mwovu, ambaye ‘alikuwa amemfungia kinyongo moyoni.’ (Marko 6:16-19; Mathayo 14:3-12) Lakini mtangulizi wa Mesiya alidumisha uaminifu-maadili wake kwa Yehova naye karibuni atainuliwa kutoka kwa wafu ili afurahie maisha katika ulimwengu mpya wa Mungu wenye uadilifu.—Yohana 5:28, 29; 2 Petro 3:13.