Majambazi Wenye Silaha Washambuliapo
KATIKA Ikoyi, kiunga cha Afrika Magharibi, kasri zimekuwa ngome. Nyingi zina kuta zenye urefu wa meta tatu, zikiwa na ncha kali katika sehemu za juu, glasi zilizochongoka, au seng’enge iliyozungushwa. Walinzi hulinda malango makubwa ambayo hufungwa kwa makomeo, vyuma, minyororo, na makufuli. Madirisha yana fito. Malango ya feleji hutenga vyumba vya kulala na zile sehemu nyingine za nyumba. Usiku, majibwa makubwa hufunguliwa yatoke katika maboma yao. Taa zenye kuangaza huondolea mbali giza, na mifumo ya kompyuta ya uchunguzi hutokeza mlio laini mambo yakiwa shwari.
Hakuna wanaotilia shaka uhitaji wa kufanya nyumba zao kuwa salama. Vichwa vya habari magazetini huripoti hivi kwa kulalamika: “Majambazi Wenye Silaha Wapora Jumuiya”; “Majambazi Wachanga Wapata Kichaa”; na “Hofu ya Ghafula, Magenge ya Mitaani Yatwaapo [Jiji Dogo].” Nchi nyingi ziko hivyo. Kama vile Biblia ilivyotabiri, kwa kweli twaishi katika nyakati za hatari.—2 Timotheo 3:1.
Kiwango cha uhalifu, kutia ndani ujambazi wa kutumia silaha, kimepanda tufeni pote. Serikali zinazidi kushindwa au kutotaka kuwatunza raia zake wenyewe. Katika nchi fulani polisi hawako tayari vya kutosha kusaidia wenye kutaka msaada, kwa kuwa ni wachache na wenye silaha chache. Wasimama-kando wengi husita kujihusisha.
Wahasiriwa, wakishindwa kutegemea msaada kutoka ama kwa polisi ama kwa umma, huachwa wajitegemee. Mzee mmoja Mkristo katika nchi moja inayoendelea alisema hivi: “Ukiomba msaada, majambazi watakulemaza au kukuua. Usitegemee msaada kutoka nje. Msaada ukija, vema, lakini usiutarajie au kuuitisha kwa sababu kuuitisha msaada kwaweza kumaanisha kuitisha matatizo zaidi.”
Kinga na Neno la Mungu
Ijapokuwa Wakristo si sehemu ya ulimwengu, wao wamo ulimwenguni. (Yohana 17:11, 16) Hivyo, sawa na watu wengine wowote, wao hujiandaa kwa kiasi fulani kwa ajili ya usalama wao. Hata hivyo, tofauti na watu wengi wasiomtumikia Yehova, watu wa Mungu hutafuta njia za kujikinga zisizokiuka kanuni za Kikristo.
Tofauti na hilo, watu katika nchi fulani za Kiafrika hutumia mizungu watafutapo kinga dhidi ya ujambazi. Mganga aweza kukata sehemu ndogo ya mkono, kifua, au mgongo wa mteja. Kisha dawa fulani ya kimizungu husuguliwa mahali hapo palipokatwa, maneno fulani ya kimizungu husemwa, na mtu huyo yadhaniwa ana kinga dhidi ya kushambuliwa na majambazi. Wengine hutia hirizi au dawa fulani za kimizungu nyumbani mwao, wakiamini kwamba “bima” kama hiyo itawafanya majambazi wasiwasumbue.
Wakristo wa kweli hawana uhusiano wowote na namna yoyote ya mizungu. Biblia hulaani vikali namna zote za uasiliani-roho, nayo yastahili kufanya hivyo, kwa kuwa mazoea kama hayo yanaweza kumhusisha mtu na roho waovu, walewale wanaoendeleza ujeuri duniani. (Mwanzo 6:2, 4, 11) Biblia hutaarifu kwa wazi hivi: “Msifanye kuloga.”—Mambo ya Walawi 19:26.
Watu wengi kwa kukata tumaini hutafuta ulinzi kwa kujihami kwa bunduki. Hata hivyo, Wakristo huyachukua maneno ya Yesu kwa uzito, aliyesema hivi: “Wale wote wauchukuao upanga wataangamia kwa upanga.” (Mathayo 26:52) Watu wa Mungu ‘wamefua panga zao zikawa majembe’ wala hawanunui bunduki ili kujilinda kutokana na ujambazi au mashambulizi.—Mika 4:3.
Vipi juu ya kupanga kuwe na walinzi wenye silaha? Ingawa lingekuwa jambo la kuamuliwa kibinafsi, kumbuka kwamba mpango kama huo huiweka bunduki mikononi mwa mtu mwingine. Mwajiri wa kazi angemtarajia mlinzi afanye nini iwapo jambazi angekuja? Je, angemtarajia mlinzi huyo ampige risasi mwizi huyo ikiwezekana ili kulinda watu na mali zilizokuwa zikilindwa?
Msimamo wanaochukua Wakristo katika kukataa mizungu na silaha kama vyombo vya kujilinda, waweza kuonekana kuwa upumbavu machoni pa wasiomjua Mungu. Hata hivyo, Biblia hutuhakikishia hivi: “Amtumainiye BWANA atakuwa salama.” (Mithali 29:25) Ijapokuwa Yehova huwalinda watu wake kwa ujumla, yeye haingilii katika kila kisa ili kuwakinga watumishi wake kutokana na ujambazi. Ayubu alikuwa mwaminifu kwa njia ya kutokeza, ingawa hivyo, Mungu aliruhusu watekaji kupora mifugo ya Ayubu, na watumishi kufa. (Ayubu 1:14, 15, 17) Mungu pia aliruhusu mtume Paulo apatwe na “hatari za kutokana na wanyang’anyi wa njia kuu.” (2 Wakorintho 11:26) Hata hivyo, Mungu huwafundisha watumishi wake waishi kwa viwango ambavyo hupunguza hatari ya kupokonywa vitu. Yeye pia huwapa ujuzi ambao huwasaidia kushughulika na majaribio ya kupokonywa vitu kwa njia ambazo zitawapunguzia uwezekano wa kujeruhiwa.
Kupunguza Tisho la Ujambazi
Mwenye hekima alisema hivi zamani za kale: “Kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi.” (Mhubiri 5:12) Yaani, huenda walio na vitu vingi wakawa wenye wasiwasi mwingi juu ya kupoteza mali zao hivi kwamba, wanakosa usingizi wakiwaza juu yavyo.
Hivyo, njia moja ya kupunguza si wasiwasi tu bali pia tisho la kupokonywa, ni kuepuka kujikusanyia mali nyingi zenye bei ghali. Mtume aliyepuliziwa aliandika hivi: “Kila kitu kilicho katika ulimwengu—tamaa ya mwili na tamaa ya macho na wonyesho wa mtu wa kujivunia njia yake ya kutegemeza maisha—hakitokani na Baba, bali hutokana na ulimwengu.” (1 Yohana 2:16) Tamaa ileile ambayo huwasukuma watu wanunue vitu vyenye bei ghali huwasukuma wengine waibe. “Na wonyesho wa mtu wa kujivunia njia yake ya kutegemeza maisha,” kwaweza kuwa mwaliko kwa wenye mielekeo ya kupora.
Mbali na kuwa mtu wa hali ya chini, ulinzi mwingine dhidi ya kupokonywa vitu ni kudhihirisha kwamba wewe ni Mkristo wa kweli. Ukiwapenda wengine, ukifuatia haki katika shughuli zako, na ukiwa na bidii katika huduma ya Kikristo, waweza kujifanyia sifa ya kuwa mtu mzuri katika jumuiya yako, anayestahili staha. (Wagalatia 5:19-23) Sifa kama hiyo ya Kikristo yaweza kuwa kinga kubwa zaidi kuliko silaha.
Majambazi Wenye Silaha Wajapo
Hata hivyo, wapaswa kufanya nini, majambazi wakifaulu kuingia nyumbani mwako na kukukabili? Kumbuka kwamba maisha yako ni muhimu kuliko mali zako. Kristo Yesu alisema hivi: “Msimkinze yeye aliye mwovu; bali yeyote akupigaye kofi kwenye shavu lako la kuume, mgeuzie lile jingine pia. Na ikiwa mtu ataka . . . umiliki wa vazi lako la ndani, acha vazi lako la nje pia limwendee.”—Mathayo 5:39, 40.
Hili ni shauri lenye hekima. Ijapokuwa Wakristo hawako chini ya wajibu wa kuwaambia wahalifu juu ya raslimali, majambazi huelekea zaidi kuwa wajeuri iwapo wanatambua kuna ukinzani, kutoshirikiana, au udanganyifu. Wengi wao, “wakiisha kuishiwa na hisia zote za adili,” wanachochewa upesi kuwa wakali na wakatili.—Waefeso 4:19.
Samuel anaishi katika jengo lenye nyumba nyingi. Majambazi walifungia jengo hilo lisiweze kufikika, nao wakaenda nyumba hadi nyumba, wakipora. Samuel alisikia milio ya risasi, milango ikivunjwavunjwa, na watu wakipiga mayowe, wakilia, na kupaaza kilio. Kuponyoka hakukuwezekana. Samuel alimwambia mkewe na wana wao watatu wapige magoti sakafuni, wainue mikono yao juu, wafunge macho, na kungoja. Majambazi walipoingia kwa nguvu, Samuel alisema nao akiwa ameinamisha macho yake chini, akijua kwamba iwapo angeangalia nyuso zao, wangefikiri kwamba angewatambulisha baadaye. “Ingieni ndani,” akasema. “Chochote mtakacho, chukueni. Mna uhuru wa kuchukua kitu chochote. Sisi ni Mashahidi wa Yehova, na hatutawakinza.” Majambazi hao walishtushwa na hilo. Kwa muda uliofuata wa saa moja hivi, jumla ya wanaume 12 wenye silaha waliingia vikundi-vikundi. Ijapokuwa walichukua vito, fedha, na vyombo vya kielektroni, familia hiyo haikupigwa wala kukatwakatwa kwa mapanga sawa na walivyofanywa wengine katika jengo hilo. Familia ya Samuel ilimshukuru Yehova kwa uhai wao.
Hili laonyesha kwamba kwa habari ya fedha na vitu vya kimwili, huenda wahasiriwa wa ujambazi wasiokinzana wakapunguza uwezekano wa kujeruhiwa.a
Nyakati nyingine kutoa ushuhuda kwa Mkristo kwaweza kuwa kinga dhidi ya kujeruhiwa. Majambazi waliposhambulia nyumba ya Ade, yeye aliwaambia hivi: “Najua mambo ni magumu kwenu, na ndiyo sababu mnafanya kazi hii. Tukiwa Mashahidi wa Yehova, twaamini kwamba siku moja kila mtu atakuwa na chakula cha kutosha kwake mwenyewe na familia yake. Kila mtu ataishi kwa amani na furaha chini ya Ufalme wa Mungu.” Hilo lilipunguza ujeuri wao. Mmoja wao alisema hivi: “Tunasikitika tumekuja nyumbani mwako, lakini ni lazima ufahamu kwamba tu wenye njaa.” Ijapokuwa walipora mali ya Ade, hawakumgusa yeye wala familia yake.
Kutulia
Si rahisi kuwa mtulivu katika hali ya hatari, ikiwa nia kuu hasa ya majambazi ni kuwatisha wahasiriwa wao ili wanyenyekee. Sala itatusaidia. Ombi letu la msaada, lijapokuwa la ukimya na fupi, laweza kusikiwa na Yehova. Biblia hutuhakikishia hivi: “Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, na masikio yake hukielekea kilio chao.” (Zaburi 34:15) Yehova hutusikia na anaweza kutupatia hekima ya kushughulika na hali yoyote kwa utulivu.—Yakobo 1:5.
Mbali na sala, msaada mwingine wa kuwa mtulivu ni kuamua kimbele utakachofanya na kile ambacho hutafanya upokonywapo. Bila shaka, haiwezekani kujua kimbele hali utakayokuwamo. Hata hivyo, ni vema kuwa na kanuni akilini, sawa na ilivyo hekima kuwa na taratibu za usalama itukiapo kwamba uko kwenye jengo ambalo limeshika moto. Ufikirio wa kimbele hukusaidia kutulia, kuepuka hofu ya ghafula, na kutojeruhiwa.
Maoni ya Mungu juu ya ujambazi yametaarifiwa waziwazi hivi: “Mimi, BWANA, naipenda hukumu ya haki, nauchukia wivi na uovu.” (Isaya 61:8) Yehova alimpulizia nabii wake Ezekieli aorodheshe ujambazi kuwa dhambi nzito sana. (Ezekieli 18:18) Hata hivyo, kitabu icho hicho cha Biblia pia huonyesha kwamba Mungu atamsamehe kwa rehema mtu atubuye na kurudisha alichopokonya.—Ezekieli 33:14-16.
Wajapoishi katika ulimwengu uliojaa uhalifu, Wakristo hushangilia katika tumaini la uhai chini ya Ufalme wa Mungu, wakati ujambazi hautakuwapo tena. Kuhusu wakati huo, Biblia huahidi hivi: “[Watu wa Mungu] wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha BWANA wa majeshi kimesema hivi.”—Mika 4:4.
[Maelezo ya Chini]
a Bila shaka, kuna mipaka ya kushirikiana. Watumishi wa Yehova hawashirikiani kwa njia yoyote inayohalifu sheria ya Mungu. Kwa mfano, Mkristo hawezi kukubali kwa hiari abakwe.