“Katika Hatari za Baharini”
KATIKA giza la usiku, meli inayobeba watu 276 yakaribia kisiwa kimoja katika Mediterania. Wanabaharia na abiria wamechoka kwa kurushwa huku na huku katika maji yenye dhoruba kwa siku 14. Wanapoona ghuba wakati wa mapambazuko, wanajaribu kupeleka chombo hicho pwani. Lakini omo yasakama kiasi cha kutoweza kusonga, na mawimbi yavunja tezi vipande vipande. Wote kwenye meli hiyo waiacha na wafaulu kufika kwenye fuo za Malta kwa kuogelea au kwa kushikilia kwa nguvu mbao na vitu vingine. Wakiwa wamepata baridi na kuchoka, wanajivuta kutoka katika mawimbi hayo yaliyochafuka. Paulo, mtume Mkristo, yuko miongoni mwa abiria hao. Anasafirishwa hadi Roma ili kufanyiwa kesi.—Matendo 27:27-44.
Kwa Paulo, kuvunjikiwa meli kwenye kisiwa cha Malta hakukuwa kisa cha kwanza chenye kutisha uhai. Miaka michache mapema, aliandika hivi: “Mara tatu nilipata kuvunjikiwa na meli, usiku mmoja na mchana mmoja nimetumia katika kilindi.” Aliongezea kwamba alikuwa “katika hatari za baharini.” (2 Wakorintho 11:25-27) Kusafiri baharini kulikuwa kumemsaidia Paulo kutimiza daraka lake alilopewa na Mungu la kuwa “mtume kwa mataifa.”—Waroma 11:13.
Je, usafiri wa baharini ulikuwa umeenea kadiri gani katika karne ya kwanza? Je, huo ulitimiza fungu gani katika kuenezwa kwa Ukristo? Je, ulikuwa salama kadiri gani? Ni vyombo vya aina gani vilivyotumiwa? Nao abiria walishughulikiwaje?
Uhitaji wa Roma wa Biashara ya Baharini
Waroma waliita Mediterania Mare Nostrum, yaani, Bahari Yetu. Kudhibiti njia za baharini kulikuwa jambo muhimu sana kwa Roma, si kwa sababu za kijeshi tu, bali pia kwa sababu nyingine. Majiji mengi ya Miliki ya Roma ama yalikuwa bandari ama yalihudumiwa na bandari. Kwa mfano, Roma ilikuwa na bandari katika Ostia iliyokuwa karibu, ilhali Korintho ilitumia Lechaeum na Kenkrea, na Siria ya Antiokia ilihudumiwa na Seleukia. Miunganisho mizuri ya baharini kati ya bandari hizo ilihakikisha kuwepo kwa mawasiliano ya haraka kati ya majiji muhimu na ilifanya iwe rahisi kutawala ifaavyo majimbo ya Roma.
Roma pia lilitegemea biashara ya usafirishaji wa meli ili kupata chakula chake. Likiwa na watu wapatao milioni moja hivi, Roma lilikuwa na mahitaji makubwa mno ya nafaka—kati ya tani 250,000 na tani 400,000 kwa mwaka. Nafaka hiyo yote ilitoka wapi? Flavius Josephus amnukuu Herode Agripa wa Pili akisema kwamba Afrika Kaskazini ililisha Roma kwa miezi minane ya mwaka, ilhali Misri ilipeleka nafaka ya kutosha kutegemeza jiji hilo kwa miezi minne iliyobaki. Maelfu ya vyombo vya baharini yalitumiwa kupeleka chakula jijini humo.
Biashara hiyo ya baharini iliyositawi sana iliandaa aina zote za bidhaa kwa ajili ya kutosheleza upendeleo wa anasa wa Roma. Madini, mawe ya ujenzi, na marumaru yalisafirishwa kwa meli kutoka Saiprasi, Ugiriki, na Misri, na mbao zilisafirishwa kutoka Lebanoni. Divai ilitoka Smirna, njugu zikatoka Damaski, na tende zikatoka Palestina. Marhamu na mpira zilipakiwa Kilikia, sufu ikapakiwa Mileto na Laodikia, vitambaa vikapakiwa Siria na Lebanoni, vitambaa vya zambarau vikapakiwa Tiro na Sidoni. Rangi zilipelekwa kutoka Thiatira na vioo kutoka Aleksandria na Sidoni. Hariri, pamba, pembe ya tembo, na manukato vililetwa kutoka China na India.
Ni jambo gani linaloweza kusemwa kuhusu meli iliyovunjikia Malta ambayo Paulo alikuwa amepanda? Ilikuwa meli ya nafaka, “mashua kutoka Aleksandria ikisafiri kuelekea Italia.” (Matendo 27:6, New World Translation of the Holy Scriptures—With References, kielezi-chini) Makundi ya meli za nafaka yalimilikiwa kibinafsi na Wagiriki, Wafoinike, na Wasiria, walioziongoza na kuziandalia vifaa. Hata hivyo, meli hizo zilikodiwa na Serikali. “Kama ilivyokuwa katika kukusanya kodi,” asema mwanahistoria William M. Ramsay, “serikali iliona kuwa ni rahisi kuwapa wanakandarasi kazi hiyo kuliko kujipangia watu na vifaa vingi sana vilivyohitajika kwa utumishi huo mkubwa.”
Paulo alikamilisha safari yake ya kwenda Roma akiwa katika chombo kilichokuwa na sanamu yenye jina “Wana wa Zeusi.” Hiyo pia ilikuwa meli ya Aleksandria. Iliegeshwa Puteoli katika Ghuba ya Naples, bandari ambamo makundi ya meli za nafaka yaliegeshwa kwa ukawaida. (Matendo 28:11-13) Kutoka Puteoli—ambayo siku hizi ni Pozzuoli—mizigo ama ilisafirishwa kupitia nchi kavu ama ilisafirishwa kwa mashua ndogo kuelekea kaskazini kandokando ya ufuo halafu kuingia Mto Tiber hadi katikati ya Roma.
Abiria Katika Meli ya Mizigo?
Kwa nini Paulo na walinzi wake wa kijeshi walisafiri kwa meli ya mizigo? Ili kujibu swali hilo, twahitaji kujua kilichomaanishwa na kusafiri baharini ukiwa abiria siku hizo.
Katika karne ya kwanza W.K., hakukuwa na meli yoyote ya abiria. Vyombo vilivyotumiwa na wasafiri vilikuwa meli za bidhaa. Na watu wa aina zote—kutia ndani maofisa wa Serikali, wasomi, wahubiri, wachawi, wasanii, wanariadha, wafanya-biashara, watalii, na pilgrimu—huenda walisafiri kwa meli hizo.
Kulikuwepo, bila shaka, mashua ndogo zilizosafirisha abiria na mizigo karibu na fuo. Huenda Paulo alitumia chombo cha aina hiyo ili ‘kuvuka aingie Makedonia’ kutoka Troasi. Huenda vyombo vidogo vilimsafirisha kwenda na kutoka Athene zaidi ya mara moja. Huenda pia Paulo alitumia vyombo vidogo katika safari yake ya baadaye kutoka Troasi hadi Patara kupitia visiwa vilivyo karibu na ufuo wa Asia Ndogo. (Matendo 16:8-11; 17:14, 15; 20:1-6, 13-15; 21:1) Kutumia vyombo vidogo vya aina hiyo kuliokoa wakati, lakini havingeweza kusafiri mbali sana na nchi. Kwa hiyo meli zilizomsafirisha Paulo kwenda Saiprasi na halafu Pamfilia na zile alizosafiria kutoka Efeso hadi Kaisaria na kutoka Patara hadi Tiro, lazima ziwe zilikuwa kubwa kadiri fulani. (Matendo 13:4, 13; 18:21, 22; 21:1-3) Chombo kilichovunjika Paulo akiwamo huko Malta pia kingeonwa kuwa kikubwa. Meli ya aina hiyo ingeweza kuwa kubwa kadiri gani?
Maandishi fulani yalisababisha msomi mmoja kusema hivi: “[Meli] iliyo ndogo zaidi ambayo ingewafaa watu wa zamani ilikuwa yenye tani 70 hadi 80. Meli yenye ukubwa uliopendwa zaidi, angalau katika enzi ya Ugiriki, ilikuwa yenye uzito wa tani 130. Meli yenye uzito wa tani 250, ingawa ilionekana mara nyingi, kwa hakika ilikuwa kubwa kupita wastani. Katika nyakati za Roma meli zilizotumiwa katika utumishi wa usafirishaji wa kifalme zilikuwa kubwa hata zaidi, ukubwa uliopendwa ulikuwa tani 340. Meli kubwa zaidi zilizosafiri baharini zilifikia uzito wa tani 1300, au labda kubwa zaidi kuliko hizo.” Kulingana na ufafanuzi ulioandikwa katika karne ya pili W.K., meli ya kubeba nafaka Isis ya Aleksandria ilikuwa yenye urefu wa meta 55, na yenye upana wa karibu meta 14, na ngama yenye kina cha meta 13 hivi, na huenda ingeweza kubeba tani zaidi ya elfu moja za nafaka na labda abiria mia kadhaa.
Wasafiri walitunzwaje wakiwa katika meli ya nafaka? Kwa kuwa meli hizo hasa zilikuwa za mizigo, abiria walipewa ufikirio wa pili. Hawakupewa chakula wala huduma, isipokuwa maji. Wangelala juu ya sitaha, labda wakiwa ndani ya mahema yaliyopigwa usiku na kung’olewa kila asubuhi. Ingawa huenda wasafiri waliruhusiwa kutumia jiko kwa upishi, ingewabidi wajiandalie wenyewe kila kitu kilichohitajika kupikia, kulia, kuogea, na kulalia—kuanzia sufuria na vikaango hadi matandiko.
Usafiri wa Baharini —Ulikuwa Salama Kadiri Gani?
Kwa kuwa walikosa vifaa—hata dira—mabaharia wa karne ya kwanza waliendesha meli hasa kwa kutumia macho. Kwa hiyo, usafiri ulikuwa salama zaidi wakati hali ya kuona ilipokuwa nzuri kabisa—kwa ujumla kuanzia mwisho-mwisho wa Mei hadi katikati ya Septemba. Wakati wa miezi miwili ya kabla na baada ya wakati huo, huenda wafanya-biashara wangejasiria kusafiri. Lakini wakati wa majira ya baridi, mara nyingi ukungu na mawingu vilisitiri alama za ardhini na jua wakati wa mchana, na nyota wakati wa usiku. Usafiri wa baharini ulionwa kuwa umefungwa (Kilatini, mare clausum) kuanzia Novemba 11 hadi Machi 10, isipokuwa katika hali za lazima kabisa au za dharura. Wale waliosafiri wakiwa wamechelewa wakati wa majira hayo walikabili hatari ya kukaa katika bandari ya ugenini wakati wa majira ya baridi.—Matendo 27:12; 28:11.
Ijapokuwa ulikuwa hatari na wa kutegemea majira, je, usafiri wa baharini ulitoa manufaa yoyote kuliko usafiri wa nchi kavu? Kwa kweli ndiyo! Usafiri wa baharini haukuchosha sana, ulikuwa wa gharama ndogo, na wa haraka zaidi. Wakati pepo zilielekea upande unaofaa, meli ingeweza kusafiri labda kilometa 150 kwa siku. Kiwango cha kawaida cha kwenda safari ndefu kwa miguu kilikuwa kilometa 25 hadi 30 kwa siku.
Upepo ulitegemewa sana ili kusafiri kwa kasi baharini. Safari ya kutoka Misri hadi Italia ilikuwa mfululizo wa kung’ang’ana dhidi ya pepo za mbisho, hata katika majira bora zaidi. Kwa kawaida njia fupi zaidi ilikuwa kupitia Rodesi au Mira au bandari nyingine yoyote kwenye ufuo wa Likia katika Asia Ndogo. Baada ya kukabili dhoruba na kupotea njia pindi moja meli ya nafaka, Isis, ilitia nanga katika Piraeus siku 70 baada ya kung’oa nanga huko Aleksandria. Kukiwa na pepo zinazovuma kutoka kaskazini-magharibi zikiisukuma meli hiyo kutoka nyuma, mkondo wa kurudi kutoka Italia huenda ungefanywa katika muda wa siku 20 hadi 25. Kwa kutumia njia ya ardhini, safari kama hiyo kwenda upande wowote ingehitaji zaidi ya siku 150 kukiwa na hali nzuri ya hewa.
Habari Njema Zapelekwa Mbali Ng’ambo ya Bahari
Kwa wazi, Paulo alijua hatari za kusafiri baharini wakati wa majira yasiyofaa. Hata alitoa shauri dhidi ya kusafiri mwisho-mwisho wa Septemba au mapema Oktoba, akisema hivi: “Wanaume, nahisi kwamba uendeshaji utakuwa na dhara na hasara kubwa si ya shehena na mashua tu bali pia ya nafsi zetu.” (Matendo 27:9, 10) Hata hivyo, ofisa-jeshi aliyeshika usukani akayapuuza maneno hayo, na jambo hilo likatokeza kuvunjikiwa meli huko Malta.
Kufikia mwisho wa kazi yake ya umishonari, Paulo alikuwa amevunjikiwa meli angalau mara nne. (Matendo 27:41-44; 2 Wakorintho 11:25) Na bado, mahangaiko yasiyofaa juu ya matukio ya aina hiyo hayakuwazuia wahubiri wa mapema wa habari njema wasisafiri baharini. Walitumia kikamili njia zote za usafiri zilizokuwepo wakati huo ili kueneza ujumbe wa Ufalme. Na kwa kutii amri ya Yesu, ushahidi ulitolewa kwa mapana na marefu. (Mathayo 28:19, 20; Matendo 1:8) Kwa sababu ya bidii yao, imani ya wale waliofuata mfano wao, na mwongozo wa roho takatifu ya Yehova, habari njema zimefika sehemu za mbali zaidi sana za dunia inayokaliwa.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.