Krismasi Katika Mashariki
• MIAKA IPATAYO MIA MBILI ILIYOPITA, msomi maarufu kutoka Korea alizuru Peking, China. Akikazia macho mchoro uliokuwa kwenye dari la kanisa moja, aliona Maria akiwa amemshika mtoto Yesu mikononi mwake. Yeye alisema hivi kuhusu mchoro huo wenye kushtua:
“Mwanamke fulani alikuwa amemshika mapajani mtoto mwenye umri wa miaka mitano au sita hivi, aliyeonekana mgonjwa. Inaonekana mwanamke huyo hakuwa na nguvu za kuinua kichwa, kana kwamba alimsikitikia mwanaye asiweze kumtazama. Na kule-e-e nyuma yao, kulikuweko mizuka mingi na watoto wenye mabawa walioruka kuwazunguka. Nilipowakazia macho wakiwa juu yangu, walionekana kana kwamba wangeniangukia wakati wowote. Kwa kushtuka, nikanyosha mkono wangu niwashike.”
JAMBO hilo lilitukia muda mrefu baada ya kuanza kwa yale Marekebisho Makubwa ya Kidini huko Ulaya, muda mrefu baada ya kipindi cha giza cha Enzi za Kati. Lakini watu wengi wa nchi za Mashariki waliuona Ukristo kuwa jambo geni kama vile mchoro wenyewe. Hali hiyo imebadilika jinsi gani! Mandhari ya mtoto Yesu huonyeshwa kila msimu wa Krismasi. Nchi za Mashariki zimezoea mandhari hiyo, na sasa barabara nyingi huko hupambwa kama zile za Ulaya.
Jioni ya Novemba 25, 1998, mwezi mmoja kabla ya Krismasi, barabara ya Champs Élysées jijini Paris huangazwa kwa taa zaidi ya 100,000 kwenye miti 300 kandokando ya barabara hiyo maarufu. Hali kadhalika, kwenye barabara iliyoko eneo la biashara la jiji la Seoul, Korea, mti mkubwa mno wa Krismasi unaonyeshwa kwenye duka moja kubwa na unaanza kuangaza usiku katika jiji hilo kuu. Upesi barabara zake zinapambwa kwa mapambo ya Krismasi.
Televisheni, redio, na magazeti yanatangaza habari zinazohusiana na Krismasi siku baada ya siku. Kwa kuchochewa na shamrashamra hizo za Krismasi, nchi nzima inaanza kukaribisha mwisho wa mwaka. Makanisa huko Seoul, ambayo idadi yake yawashangaza wageni wengi, yanapambwa haraka-haraka. Hivyo, Korea na nchi nyinginezo katika Mashariki zinaanza shamrashamra za Krismasi yapata wakati ule ambapo Marekani husherehekea Sikukuu ya Kushukuru mwishoni mwa mwezi wa Novemba.
Nchi nyingi za Mashariki hazionwi kuwa sehemu ya Jumuiya ya Wakristo. Kwa mfano, asilimia 26.3 tu ya watu katika Korea ndio hudai kuwa Wakristo. Asilimia 7.9 katika Hong Kong, asilimia 7.4 katika Taiwan, na asilimia 1.2 pekee katika Japani. Ni wazi kwamba watu wengi wa nchi za Mashariki si Wakristo, lakini hawapingi kusherehekea Krismasi. Kwa kweli, mara nyingi wao huonekana kuifurahia zaidi kuliko wenzao wa nchi za Magharibi. Kwa mfano, Hong Kong yajulikana sana kwa sherehe za Krismasi zenye madoido, hata ingawa wengi wa wakazi wake ni Wabuddha au wafuasi wa dini ya Tao. Hata katika China, ambako asilimia 0.1 ya watu ndio hudai kuwa Wakristo, wanaosherehekea Krismasi wanazidi kuongezeka haraka sana.
Kwa nini Krismasi husherehekewa sana hivyo katika Mashariki? Kwa nini watu wasiomkubali Yesu kuwa Mesiya wanasherehekea Krismasi, ambayo wengi wanaojidai kuwa Wakristo huiona kuwa siku ya Yesu ya kuzaliwa? Je, Wakristo wa kweli waige maoni ya watu hao kuhusu Krismasi? Tutapata majibu tunapochunguza namna Krismasi ilivyopata kupendwa sana katika Korea, nchi ya kale ya Mashariki.