Kwa Kweli Ingefaa Uitazame Video No Blood—Medicine Meets the Challenge
Una habari kadiri gani kuhusu njia nyingine mbalimbali za matibabu yasiyohusisha damu? Je, unaelewa baadhi ya vitu vinavyoweza kutumiwa badala ya damu na jinsi vinavyofanya kazi? Tazama video hii na utahini ujuzi wako kwa maswali yafuatayo.—Kwa sababu video hii ina sehemu fupi zinazoonyesha upasuaji, wazazi wanapaswa kutumia busara wanapoitazama pamoja na watoto wao wadogo.
(1) Ni sababu gani kuu inayofanya Mashahidi wa Yehova wakatae kutiwa damu mishipani, nayo yapatikana wapi katika Biblia? (2) Kuhusu matibabu, tungependa nini? (3) Wagonjwa wana haki gani ya msingi? (4) Kwa nini ni jambo la kiakili na la kudhamiria kukataa kutiwa damu mishipani? (5) Mtu anapopoteza damu nyingi sana, ni mambo gani mawili ambayo madaktari wanapaswa kufanya haraka? (6) Ni hatari zipi za kitiba zinazohusiana na kutiwa damu mishipani? (7) Taja baadhi ya vifaa ambavyo wapasuaji wanaweza kutumia ili kupunguza umwagikaji wa damu nyingi wakati wa upasuaji? (8) Ungependa kujulishwa nini kuhusu tiba yoyote inayoweza kutumiwa badala ya damu? (9) Je, upasuaji tata waweza kufanywa bila kutumia damu? (10) Madaktari wengi wako tayari kuwafanyia Mashahidi wa Yehova nini, na huenda wagonjwa wote wakatibiwa vipi wakati ujao?
Bila shaka itasaidia kuitazama video No Blood pamoja na wanafunzi wa Biblia, wenzi wa ndoa au watu wa ukoo wasio Mashahidi, wafanyakazi wenzako, walimu, na wanashule wenzako ambao huenda wakauliza maswali kuhusu msimamo wetu kuhusiana na damu. Kukubali matibabu yoyote yaliyoonyeshwa katika video hii ni uamuzi wa mtu binafsi na dhamiri yake.—Ona “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika toleo la Mnara wa Mlinzi la Juni 15 na Oktoba 15, 2000.