Unajua Mbinu Zote za Matibabu Yasiyohusisha Damu?
Ulimwenguni pote, kuna ongezeko la hospitali zinazokubali kufanya upasuaji bila kutumia damu. Je, unajua vizuri mbinu zote za matibabu yasiyohusisha damu zinazopatikana? Unahitaji kujua ili uweze kufanya maamuzi yanayofaa kuhusu tiba na upasuaji. Tazama video No Blood—Medicine Meets the Challenge. Baada ya kuitazama, sali na upitie yale ambayo umejifunza ukitumia maswali yaliyo hapa chini.—Taarifa: Kwa kuwa video hiyo ina picha za watu wakifanyiwa upasuaji, wazazi wanapaswa kutumia busara wanapoitazama pamoja na watoto wao. Iwapo video hii haipatikani, pitia “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 2004 na Oktoba 15, 2000, au “Je, Wewe Uko Tayari Kukabili Hali Ngumu ya Kitiba Yenye Kujaribu Imani?” katika Huduma ya Ufalme Yetu ya Novemba 1990, na utumie maswali yanayofaa kati ya maswali yafuatayo.
(1) Ni sababu gani kuu ambayo huwafanya Mashahidi wa Yehova wakatae kutiwa damu mishipani? (2) Kuhusiana na matibabu, Mashahidi wa Yehova hupendekeza wafanyiwe nini? (3) Wagonjwa wana haki gani ya msingi? (4) Kwa nini ni jambo la usawaziko na busara kuchagua matibabu ya badala yasiyohusisha damu? (5) Mtu anapopoteza damu nyingi sana, madaktari wanapaswa kufanya mambo gani mawili haraka? (6) Taja kanuni nne za matibabu ya badala yasiyohusisha damu. (7) Madaktari wanaweza kufanya nini ili (a) kupunguza kupotea kwa damu, (b) kuhifadhi chembe nyekundu za damu, (c) kuharakisha mwili utokeze damu, na (d) kuokoa damu inayovuja? (8) Fafanua mbinu inayoitwa (a) hemodilution (uzimuaji wa damu) na ile inayoitwa (b) cell salvage (uokoaji wa chembe za damu). (9) Unapaswa kujulishwa nini kuhusu matibabu yoyote ya badala? (10) Je, upasuaji mgumu unaweza kufanywa bila kumtia mgonjwa damu? (11) Madaktari wameanza kuwa na mtazamo gani mpya?
Kuchagua baadhi ya matibabu yaliyoonyeshwa katika video hiyo ni uamuzi wa mtu binafsi unaotegemea dhamiri yake ambayo inaongozwa na Biblia. Je, umeamua kabisa ni matibabu gani ambayo wewe na watoto wako mngependa na kujaza kadi ya DPA au AMD? Ili kupata maelezo kamili kuhusu matibabu hayo, soma makala “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 2004 na Oktoba 15, 2000. Kisha tumia daftari katika nyongeza, “Nina Maoni Gani Kuhusu Visehemu vya Damu na Matibabu Yanayohusisha Damu Yangu Mwenyewe?” iliyo katika Huduma Yetu ya Ufalme ya Novemba 2006, ili kufanya uamuzi wako binafsi kuhusu matibabu ambayo ungekubali au kukataa. Mwishowe, hakikisha kwamba umeandika kwa usahihi kwenye kadi yako ya DPA au AMD matibabu ambayo umechagua. Wawakilishi wako wa kitiba na watu wa familia yako ambao si Mashahidi wanapaswa kuelewa vizuri uamuzi wako.