Je, Unaahirisha?
Kuahirisha nini? Kujaza kadi ya DPA (mamlaka ya kudumu ya uwakilishi) ambayo imeandaliwa kwa ajili ya Mashahidi waliobatizwa. Kwa kuwa ‘haujui uzima wako utakuwa namna gani kesho,’ ni muhimu uamue mapema na uandike matibabu na mbinu za kitiba ambazo utakubali ukihitaji matibabu ya dharura. (Yak. 4:14; Mdo. 15:28, 29) Video Transfusion-Alternative Health Care—Meeting Patient Needs and Rights ilitayarishwa ili kukusaidia ufanye maamuzi. Itazame, kisha upitie na kusali kuhusu kile ambacho umejifunza kwa kutumia maswali yaliyo hapa chini.—Taarifa: Kwa kuwa video hiyo ina picha za watu wakifanyiwa upasuaji, wazazi wanapaswa kutumia busara wanapoitazama pamoja na watoto wao.
(1) Kwa nini wahudumu fulani wa afya wanabadili maoni yao kuhusu kutia damu mishipani? (2) Taja aina tatu za upasuaji mgumu unaoweza kufanywa bila kumtia mgonjwa damu. (3) Ni madaktari wangapi duniani ambao wamekubali kuwatibu au kuwafanyia wagonjwa upasuaji bila kuwatia damu? Kwa nini wamekubali kufanya hivyo? (4) Uchunguzi uliofanywa majuzi katika hospitali mbalimbali umeonyesha nini kuhusu matumizi ya damu? (5) Kutiwa damu mishipani kunaweza kusababisha matatizo gani ya afya? (6) Wataalamu fulani wamekata kauli gani kuhusu manufaa ya matibabu yasiyohusisha damu? (7) Ni nini kinachosababisha upungufu wa damu? Mtu anaweza kupungukiwa damu kadiri gani na bado asiwe mahututi? Mtu mwenye upungufu wa damu anaweza kusaidiwaje? (8) Mwili wa mgonjwa unaweza kuchochewaje utengeneze haraka zaidi chembe nyekundu za damu? (9) Ni mbinu gani zinazotumiwa na madaktari ili kumzuia mgonjwa asivuje damu nyingi wakati wa upasuaji? (10) Je, mbinu za matibabu zisizohusisha damu zinaweza kutumiwa kwa mafanikio kwa watoto wachanga au wakati wa dharura? (11) Matibabu mazuri yanahusisha kanuni gani muhimu? (12) Kwa nini ni muhimu sisi Wakristo tuamue mapema tungependa matibabu gani yasiyohusisha damu? Tunaweza kufanyaje uamuzi huo?
Kuchagua baadhi ya matibabu yaliyoonyeshwa katika video hiyo ni uamuzi wa mtu binafsi unaotegemea dhamiri yake inayoongozwa na Biblia. Je, umeamua kabisa ni matibabu gani ambayo wewe na watoto wako mngependa? Matibabu hayo yamezungumziwa kwa ukamili katika “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 2004 na Oktoba 15, 2000, na nyongeza “Nina Maoni Gani Kuhusu Visehemu vya Damu na Matibabu Yanayohusisha Damu Yangu Mwenyewe?” katika Huduma Yetu ya Ufalme ya Novemba 2006. Wawakilishi wako wa kitiba na watu wa familia yako ambao si Mashahidi wanapaswa kuelewa vizuri uamuzi wako.