Je, Uko Tayari Kukabiliana na Matibabu ya Dharura?
Hali ya dharura ya kimatibabu inaweza kutokea ghafula, bila tahadhari yoyote. (Yak. 4:14) Kwa hiyo, mtu mwerevu atajitayarisha kadiri awezavyo. (Met. 22:3) Je, umeamua ni matibabu gani ambayo utakubali na kuandika maamuzi yako? Ili kukusaidia kufanya maamuzi, video ya pili yenye kichwa Transfusion-Alternative Health Care—Meeting Patient Needs and Rights, kwenye DVD ya Transfusion-Alternatives—Documentary Series, imetayarishwa. Unapoitazama, jaribu kujibu maswali yafuatayo. Kwa kuwa video hii ina sehemu fupi zinazoonyesha watu wakifanyiwa upasuaji, wazazi wanapaswa kutumia busara wanapoitazama pamoja na watoto wadogo. Iwapo video hii haipatikani, zungumzieni “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 2004 na Oktoba 15, 2000, au habari kwenye nyongeza katika Huduma Yetu ya Ufalme ya Novemba 2006.
(1) Kwa nini madaktari na wataalamu fulani wa afya wanabadili maoni yao kuhusu kuwatia watu damu? (2) Taja aina tatu za upasuaji mgumu ambao umefanywa bila kumtia mgonjwa damu. (3) Kwa nini madaktari wengi sana wanakubali kuwatibu au kuwafanyia wagonjwa upasuaji bila kuwatia damu? (4) Uchunguzi wa hivi karibuni katika hospitali mbalimbali umeonyesha nini kuhusu matumizi ya damu? (5) Kutiwa damu kunaweza kusababisha matatizo gani ya afya? (6) Wataalamu wengi wamekata kauli gani kuhusu manufaa ya matibabu yasiyohusisha damu? (7) Ni nini kinachosababisha upungufu wa damu mwilini na mtu mwenye shida hiyo anaweza kusaidiwaje? (8) Mgonjwa anaweza kupewa dawa gani ili mwili wake utengeneze chembe nyekundu haraka zaidi? (9) Ni mbinu gani zinazotumiwa ili kuzuia damu nyingi isivuje wakati wa upasuaji? (10) Je, mbinu za matibabu zisizohusisha damu zinaweza kutumiwa kwa mafanikio kuwatibu watoto wachanga au wagonjwa mahututi? (11) Matibabu mazuri yanahusisha kanuni gani muhimu?
Kwa kuwa kuchagua baadhi ya matibabu yanayoonyeshwa katika video hii ni uamuzi unaotegemea dhamiri, usingoje hadi wakati utakapopatwa na hali ya dharura, ndipo uanze kufikiria matibabu ambayo utakubali na yale utakayokataa. Ili upate habari zitakazokusaidia kufanya maamuzi ya busara, ona sura ya 7 ya kitabu “Upendo wa Mungu” na marejeo yaliyoonyeshwa, na vilevile nyongeza katika toleo la Huduma Yetu ya Ufalme la Novemba 2006. Kisha, ikiwa umebatizwa, andika matibabu ambayo umechagua kwenye kadi ya DPA au AMD (Mwelekezo wa Mapema Kuhusu Tiba) na uhakikishe kwamba unabeba kadi hiyo nyakati zote.
[Blabu katika ukurasa wa 3]
Je, umeamua ni matibabu gani ambayo utakubali na kuandika maamuzi yako?