Hekima ya Kuepuka Ngono na Kufunga Ndoa na Mwenzi Mmoja
KUFIKIA sasa, watu wapatao milioni 30 wameambukizwa virusi vya UKIMWI na zaidi ya watu milioni 6 wamekufa. Visa vipya vipatavyo 8,500 hugunduliwa kila siku—na kati yavyo 1,400 ni vya watoto, ambao hufa katika mwaka wa kwanza wa maisha zao. Zile ziitwazo eti kampeni za ngono-salama zimevutia uangalifu wa umma, lakini wengine huona kwamba kampeni hizo hazitoshi. “UKIMWI ni maradhi yenye kuua,” aandika Dakt. Steven J. Sainsbury katika The Tampa Tribune, “na hatua zozote zinazochukuliwa ili kuuzuia usipitishwe ni lazima ziwe zenye matokeo kabisa.”
Kuhusu matumizi ya kondomu kuwa njia ya kuzuia UKIMWI, Dakt. Sainsbury aeleza: “Twaweza kuangalia suala hili hivi. Tuseme kwamba kwa sababu zisizojulikana, kwa ghafula magari yaanza kulipuka kila wakati mtu ajaribupo kuyawasha. Wenye magari walipuliwa nchini kote. Hatimaye, serikali inatokeza suluhisho fulani. Ongezeni tu kitu hiki katika fueli, wao wasema, na uwezekano wa kulipuka utapungua kwa asilimia 90. Je, waweza kusema kwamba tatizo hilo limesuluhishwa? Je, bado ungeendelea kuendesha gari lako? Sidhani. Basi kwa nini tunakubali kondomu kuwa suluhisho la UKIMWI?”
Akitambua kwamba UKIMWI mara nyingi husababishwa na hali ya kingono, Dakt. Sainsbury atoa suluhisho: “Usifanye ngono mpaka uwe tayari kuwajibika kwa ndoa ya mwenzi mmoja ambaye hajaambukizwa. Maneno makuu ni kuepuka ngono na kufunga ndoa na mwenzi mmoja.”
Biblia huamuru waseja waepuke ngono, na wale walio katika ndoa wabaki na mwenzi mmoja. Viwango vya juu vya Biblia hukataza uasherati, uzinzi, na ugoni-jinsia-moja. (Mathayo 19:4-6; 1 Wakorintho 6:9, 10; 7:8, 9) Ingawa wengi huchambua viwango hivyo, wakisema ni vya kale au havitumiki, maadili ya Biblia yameendeleza afya njema na amani ya akili.—Isaya 48:17.