Mafigo Yako—Chujio la Kutegemeza Uhai
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA IRELAND
DUNIA na mwili wa binadamu vina jambo moja kwa ulingano: Ili kutegemeza uhai, vyote huhitaji chujio. Dunia huhitaji kukingwa na mashambulizi ya daima ya miale kutoka kwenye jua. Tabaka ya ozoni ya angahewa letu huchuja miale hiyo, ikiruhusu nuru yenye kutegemeza uhai ipite kuingia duniani. Na mwili wako? Nyingi za taratibu za kikemikali katika mwili wako hutoa vitu vyenye sumu na uchafu kuingia kwenye mkondo wako wa damu. Vikiachwa vibaki, vitu hivi vyaweza kukusababishia matatizo mazito, hata kifo. Vinapasa kuendelea kuchujwa na kuondolewa.
Uchujaji huu ni mojawapo ya kazi za mafigo yako. Lakini viungo hivi vidogo vyaweza kutambulishaje, kutenga, na kuondoa vitu viwezavyo kudhuru, na bado kwa wakati uleule kuhakikisha kwamba elementi muhimu zabaki ili kuulisha na kuutia nguvu mwili? Na waweza kusaidiaje mafigo yako yaendelee kukuweka ukiwa mwenye afya?
Kuna Nini Ndani ya Mafigo Yako?
Binadamu kwa kawaida wana mafigo mawili — kila moja kwenye kile upande wa uti wa mgongo katika sehemu ya chini ya mgongo. Kila moja lina urefu wa sentimeta 10, upana wa sentimeta 5, na unene wa sentimeta 2.5 na uzani wa gramu 110-170. Kugawa figo katikati kutoka juu hadi chini hufunua visehemu kadhaa vinavyoonekana wazi, ambavyo vimeonyeshwa katika michoro iliyoambatanishwa.
Ili kuona akilini jinsi figo lifanyavyo kazi, wazia stediamu yenye maelfu ya watazamaji wanaokuja kwa ajili ya tukio fulani. Kwanza, ni lazima umati huo ugawanyike katika milolongo midogo kadhaa. Kisha, watu mmoja-mmoja katika kila mlolongo wapitia malango ya ulinzi, ambapo watu mmoja-mmoja ambao hawana tikiti wanawekwa kando. Watazamaji walio na tikiti hupita hadi kwenye viti vyao walivyopangiwa.
Vivyo hivyo, elementi zote zinazofanyiza damu yako huhitaji kuzunguka kotekote katika mwili wako mzima. Hata hivyo, zifanyapo hivyo, ni lazima zipitie tena na tena katika mafigo yako kwa njia ya mishipa ya damu, ateri za figo, moja kwa kila figo. (Ona mchoro kwenye ukurasa wa 24.) Baada ya kuingia katika figo, ateri za figo hutawanyika kuwa mishipa ya damu midogo zaidi katika tabaka za ndani na za nje za figo. Hivyo, elementi tofauti-tofauti katika damu yako zinapitishwa katika “milolongo” midogo zaidi na iwezayo kushughulikiwa zaidi.
Mwishowe, damu yafika kwenye vichala vidogo mno, kila kimoja kikiwa na mishipa 40 ya damu iliyo midogo mno kama vitanzi. Kila kichala, kiitwacho kiglome, kimezungukwa na kiwambo chenye tabaka mbili kiitwacho kibumba cha Bowman.a Pamoja, kiglome na kibumba cha Bowman hufanyiza sehemu ya kwanza ya ‘lango la ulinzi’ la figo lako, nefroni—sehemu ya msingi ya uchujaji ya figo lako. Kuna zaidi ya nefroni milioni moja katika kila figo. Lakini ni ndogo sana hivi kwamba utahitaji hadubini ili kuchunguza moja!—Ona mchoro wa nefroni, ikiwa imekuzwa sana, kwenye ukurasa wa 25.
Uchujaji wa Hatua Mbili wa Damu Yako
Chembe za damu na za protini katika mkondo wako wa damu ni za muhimu. Hizo huandalia mwili wako huduma muhimu sana kama vile kuandaa oksijeni, kinga, na kurekebisha madhara. Ili kuzuia kupotezwa kwa chembe za damu na protini, hatua ya kwanza ya uchujaji huzitenganisha kutoka kwa elementi nyinginezo zote. Kazi hii ya kipekee hutimizwa na vibumba vya Bowman. Lakini jinsi gani?
Mishipa ya damu iingiayo katika kiglome hujigawanya kuwa kapilari nyingi ndogo mno zenye kuta nyembamba sana. Hivyo, msongo wa damu waweza kusukuma maji na molekuli nyinginezo ndogo kupitia viwambo vya kapilari vilivyo laini mno, kutoka kwenye mkondo wako wa damu, na kuingia katika kibumba cha Bowman na neli iliyojiviringa iliyoungana nayo. Neli hii huitwa kineli mzingo. Molekuli kubwa za protini na chembe zote za damu hubaki katika mkondo wa damu na kuendelea kutiririka kupitia kapilari.
Sasa uchujaji unakuwa mteuzi zaidi. Ni lazima mafigo yako yahakikishe kabisa kwamba hakuna chochote chenye thamani kwa mwili wako kinachoondoka! Kiowevu kinachotiririka kupitia hicho kineli mahali hapa ni mchanganyiko wa umajimaji, ulio na molekuli zilizoyeyuka zenye manufaa pamoja na uchafu na vitu visivyotakiwa. Chembe fulani hususa kwenye ukuta wa ndani wa hicho kineli hutambua molekuli zenye manufaa, kama vile maji, chumvi, sukari, madini, vitamini, homoni, na asidi amino. Hizo huondolewa kwa njia yenye matokeo kwa kufyonzwa tena kuingia kwenye ukuta wa hicho kineli na kupitishwa tena kuingia katika mfumo unaozunguka wa kapilari ili ziingie tena katika mkondo wako wa damu. Kapilari hizo huunganika tena zikiwa vena ndogo ambazo huunganika kuwa mshipa wa damu uitwao vena ya figo. Kupitia kwake, damu yako, sasa ikiwa imechujwa na kusafishwa, hutoka katika figo na kuendelea kutegemeza uhai katika mwili wako.
Kuondosha Uchafu
Lakini namna gani kiowevu kinachobaki katika kineli? Bila shaka kina vitu ambavyo mwili wako hauhitaji. Kiowevu hicho kiendeleapo kutiririka kwenye hicho kineli kuelekea kineli cha kukusanyia, au kichirizi cha kukusanyia kilicho kikubwa zaidi, chembe nyinginezo katika ukuta wa hicho kineli huachilia mnyunyizo wa ziada, kutia ndani amonia, potasi, urea, asidi uriki, na maji ya ziada. Kitu hicho cha mwisho ni mkojo.
Vichirizi vya kukusanyia kutoka nefroni tofauti-tofauti hujiunga pamoja na kuachilia mikojo kupitia matundu kwenye ncha za piramidi. Mkojo huo hupita na kuingia katika uvungu wa figo na kisha kuondoka kupitia ureta, neli inayounganisha figo na kibofu. Mkojo huhifadhiwa katika kibofu chako kabla ya kuondoshwa mwilini mwako.
Japo udogo wake usioweza kuonekana kwa macho matupu, nefroni zaidi ya milioni mbili katika mafigo yako hufanya kazi nzuri sana. The New Encyclopædia Britannica hutaarifu hivi: “Nefroni . . . huchuja maji lita tano yote yaliyo katika damu kila dakika 45.” Kufikia wakati vitu kadhaa vimefyonzwa tena na taratibu nyingi kukamilishwa, mwili wa kawaida wenye afya waweza kuondosha lita mbili hivi za uchafu kwa njia ya mkojo kila muda wa saa 24. Ni mfumo wenye kufanya kazi kwa bidii na wenye kuchuja kikamili kama nini!
Tunza Mafigo Yako!
Mafigo yako hujisafisha yenyewe na kujidumisha, yakiweza kufanya kazi kwa muda mrefu. Hata hivyo, una sehemu ya kufanya katika kuyasaidia kufanya kazi zake. Ni lazima maji mengi sana yapitie mafigo yako ili mwili wako ubaki ukiwa na afya. Kwa hakika, kunywa maji ya kutosha huonwa kuwa njia kuu ya kuzuia maambukizo ya figo na kujifanyiza kwa vijiwe vya figo.b Kunywa maji husaidia pia mifumo yako ya umeng’enyaji na mifumo ya moyo na mishipa ya damu, ataja Dakt. C. Godec, mwenyekiti wa Urology Department of Long Island College Hospital, New York.
Maji kiasi gani? Dakt. Godec na madaktari wengineo wengi hupendekeza kwamba kuongezea kupata maji katika vyakula na vinywaji vingine, kila mtu apaswa kunywa angalau lita mbili za maji kila siku. “Watu wengi wameishiwa na maji mwilini,” Dakt. Godec akaeleza Amkeni! Yeye alitaja kwamba mradi mafigo yako au moyo wako hauna maradhi, maji yanayafaa. “Lakini ni lazima unywe ya kutosha,” Dakt. Godec akasema. “Watu wengi hawafanyi hivyo.”
Wengine hupata maji yakiwa yenye ladha zaidi yanapoongezwa ladha, kama vile limau. Wengine hupendelea ladha ya maji ya chemchemi au maji ambayo yamechujwa kupitia makaa. Kwa vyovyote, maji jinsi yalivyo au yaliyoongezwa ladha kidogo yanafaa mafigo yako kuliko kinywaji kinginecho chote. Kwa hakika, sukari katika maji ya matunda na vinywaji vilivyotiwa sukari huongeza uhitaji wa mwili wa maji. Vinywaji vilivyo na alkoholi au kafeni hufanya mwili upoteze maji.
Kuzoea kunywa lita mbili za maji kila siku kwa hakika kwaweza kuwa jambo gumu. Kwanza, watu wengi huona likiwa jambo la kutatiza au kufedhehesha kwenda msalani mara nyingi kuliko ilivyo kawaida. Lakini mwili wako utakushukuru kwa kufanya jitihada hiyo ya ziada. Kando na kukusaidia kudumisha afya, kunywa maji ya kutosha kwaweza hata kuboresha sura yako. Madaktari wanataja kwamba lishe nzuri na unywaji mwingi wa viowevu una matokeo sana kwa kufanya ngozi yako ionekane kuwa nzuri kuliko vitu vyovyote vinavyotumiwa kupaka ngozi.
Kwa kuhuzunisha, utaratibu wetu wa kuhisi kiu haujakamilika, na unakosa kufanya kazi zaidi tuendeleapo kuzeeka. Hivyo, hatuwezi kutegemea kiu pekee ili kujua tunahitaji maji kadiri gani. Waweza kuwaje na hakika kwamba unakunywa ya kutosha? Wengine huanza siku yao kwa kunywa maji gilasi mbili, na kisha baada ya vipindi fulani kunywa maji gilasi nyingine. Wengine huweka kiwekeo cha maji kiwezacho kupenyeza nuru mahali wawezapo kukiona na kukifikia — kikumbusha cha kunywa pindi kwa pindi siku yote. Hata iwe unatumia njia gani, kunywa maji mengi yaliyo safi ni njia nzuri ya kuonyesha uthamini kwa mafigo yako — chujio la ajabu likufanyalo uendelee kuwa hai.
[Maelezo ya Chini]
a Katika miaka ya mapema ya 1840, daktari mpasuaji na mwanahistolojia Mwingereza William Bowman alifafanua kibumba hiki kidogo na kazi yake. Kikaja kuitwa kwa jina lake.
b Ona Amkeni! toleo la Agosti 22, 1993, ukurasa wa 20-22, na Aprili 8, 1987, ukurasa wa 29.
[Sanduku katika ukurasa wa 25]
Nefroni—Sehemu ya Msingi ya Uchujaji
KUNA nefroni zaidi ya milioni moja katika kila figo. Huo mfumo ulio kama neli upatikanao katika kila nefroni huwa na urefu wa sentimeta 3 hivi na upana wa milimeta 0.05 tu. Hata hivyo, ikiwa ingewezekana kufumua vineli vyote vya figo moja, vingepanuka kufikia kilometa 30 hivi!
Kibumba cha Bowman hasa ni mwisho uliopinda wa kineli mzingo cha nefroni. Kineli hicho kimezungukwa na mfumo wa mishipa midogo sana ya damu iitwayo kapilari. Hicho kineli huingia katika mshipa wa kukusanyia ulio mkubwa zaidi, ambao huondoa uchafu na vitu vyenye sumu vilivyochujwa na nefroni.
[Mchoro katika ukurasa wa 24, 25]
Vena ya figo hupeleka damu iliyochujwa upya mwilini
Ateri ya figo hupeleka damu isiyochujwa kwenye figo
Piramidi za figo ni vitu vyenye umbo la pia ambavyo hupeleka mkojo kwenye uvungu wa figo
Koteksi huwa na kiglome cha kila nefroni
Uvungu wa figo ni mpare ambao hukusanya mkojo na kuuelekeza kwenye ureta
Ureta hupeleka mkojo kutoka katika figo hadi kwenye kibofu
[Mchoro katika ukurasa wa 25]
Nefroni, machujio madogo sana milioni mbili hivi yaliyo kama neli, husafisha damu
Kiglome
Mkojo hukusanywa na kineli mzingo, kisha kwenda kwenye kibofu
Kibumba cha Bowman
Mishipa ya damu