Sura 1
Kwa Nini Kupendezwa na Dini Nyingine?
1-7. Ni nini baadhi ya madhihirisho ya dini mbalimbali za ulimwengu?
BILA kujali waishi wapi, bila shaka umejionea mwenyewe jinsi dini inavyoongoza maisha za mamilioni ya watu, labda na yako pia. Katika nchi ambazo Uhindu unazoewa, mara nyingi utawaona watu wakifanya puja—sherehe ambayo yaweza kuhusisha kutoa sadaka kwa vijimungu vyao, kwa namna ya nazi, maua, na matofaa. Kuhani anapaka rangi nyekundu au ya manjano, yaani tilak, kwenye vipaji vya nyuso za waumini. Mamilioni pia humiminika kila mwaka kwenye mto Ganges watakaswe na maji yao.
2 Katika nchi za Katoliki, utaona watu wakisali katika makanisa na makathedro huku wameshika kisalaba au tasbihi. Shanga za tasbihi zinatumiwa kuhesabia sala zinazotolewa kwa ujitoaji wao kwa Mariamu. Na si vigumu kutambua watawa wa kike na makasisi, wanaotofautishwa na kanzu zao nyeusi.
3 Katika mabara ya Kiprotestanti, vikanisa na makanisa ni tele, na siku ya Jumapili wafuasi kwa kawaida huvaa nguo zao bora na kukusanyika waimbe nyimbo za dini na kusikia mahubiri. Mara nyingi makasisi wao huvaa mavazi meusi na kola ya kikasisi yenye kuwatofautisha.
4 Katika nchi za Kiislamu, unaweza kusikia sauti za waadhini, wapiga mbiu Waislamu wakiipiga kwenye vinara vya misikiti mara tano kila siku, kuwaita waamini kwenye s̩alãt, au sala ya sherehe. Wao huiona Qurani Tukufu kuwa kitabu cha Kiislamu cha maandiko matakatifu. Kulingana na imani ya Kiislamu, kilifunuliwa na Mungu akapewa nabii Muhammad na malaika Gabrieli katika karne ya saba W.K.
5 Kwenye barabara za mabara mengi ya Kibuddha, watawa wa Dini ya Buddha, kwa kawaida wakiwa wamevaa majoho ya dhahabu-nyekundu, meusi, au mekundu, huonekana kuwa ishara ya mtu kuwa wa dini. Mahekalu ya kale yanayoonyesha Buddha mtulivu ni uthibitisho wa zamani za kale wa imani ya Kibuddha.
6 Dini ya Shinto ikiwa inazoewa katika Japan, inahusu maisha za kila siku kukiwa na vihekalu vya familia na matambiko kwa wazazi wa kale waliokufa. Wajapan huhisi huru kusali kwa ajili ya mambo ya kimwili kabisa, hata juu ya kufaulu katika mitihani ya shuleni.
7 Utendaji mwingine wa kidini unaojulikana ulimwenguni pote ni ule wa watu wanaoenda nyumba kwa nyumba na kusimama kwenye barabara wakiwa na Biblia na vitabu vya Biblia. Magazeti Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yakionekana wazi, karibu kila mtu anawatambua watu hao kuwa Mashahidi wa Yehova.
8. Historia ya ujitoaji kidini inaonyesha nini?
8 Unamna-namna huu mkubwa wa ujitoaji wa kidini ulimwenguni pote waonyesha nini? Kwamba kwa maelfu ya miaka ainabinadamu wamekuwa na uhitaji na tamaa ya kiroho. Binadamu ameishi na majaribu na mizigo, tashwishi na maswali yake, kutia ndani kitendawili cha kifo. Hisia za kidini zimeonyeshwa katika njia nyingi kwa watu kugeukia Mungu au vijimungu vyao, wakitafuta baraka na utulizo. Dini pia hujaribu kushughulikia maswali makubwa: Kwa nini sisi tupo hapa? Tuishije? Wakati ujao una nini kwa ajili ya ainabinadamu?
9. Ni katika njia gani watu walio wengi wana namna zao za ujitoaji kidini maishani mwao?
9 Kwa upande mwingine, kuna mamilioni ya watu wasiodai kuwa na dini yoyote wala imani yoyote katika kijimungu chochote. Wao ni waatheisti. Wengine, waagnosti, huamini kwamba Mungu hajulikani na yaelekea hawezi kujulikana. Hata hivyo, hilo kwa wazi halimaanishi kwamba wao ni watu wasio na kanuni wala maadili, kama ambavyo kudai kuwa na dini kusivyomaanisha kwamba mtu anazo. Hata hivyo, mtu akikubali dini kuwa “ujitoaji kwa kanuni fulani; utumainifu imara au uaminifu; udhamiriaji; shauku ya kufuata dini au ufungamano,” basi watu walio wengi, kutia waatheisti na waagnosti, wana namna fulani ya ujitoaji wa kidini maishani mwao.—The Shorter Oxford English Dictionary.
10. Je! dini ina mshindo juu ya ulimwengu wa kisasa? Toa kielezi.
10 Kwa kuwa kuna dini nyingi mno katika ulimwengu unaozidi kuwa mdogo zaidi na zaidi kwa sababu ya usafiri na uwasiliano wa kasi zaidi, mshindo wa imani mbalimbali huhisiwa ulimwenguni pote, tutake-tusitake. Kasirani iliyotokea mnamo 1989 kuhusu kitabu The Satanic Verses, kilichoandikwa na mtu ambaye watu wengine walimtaja kuwa ‘Mwislamu kafiri,’ ni uthibitisho ulio wazi wa jinsi fikira ya kidini yaweza kujidhihirisha kwa kiwango cha duniani pote. Kulikuwako wito kutoka viongozi wa Kiislamu kuwa kitabu hicho kipigwe marufuku na hata mtungaji wacho auawe. Ni nini kinachofanya watu wamenyuke vikali sana katika mambo ya dini?
11. Kwa nini si kosa kuchunguza imani nyingine?
11 Ili kujibu hilo, tunahitaji kujua jambo fulani juu ya chanzo cha dini za ulimwengu. Ni kama Geoffrey Parrinder anavyotoa taarifa katika World Religions—From Ancient History to the Present: “Kuchunguza dini tofauti-tofauti kwa lazima hakumaanishi mtu anakosa uaminifu kwa imani yake mwenyewe, bali huenda ikazidishwa kwa kuona jinsi watu wengine wametafuta uhalisi wa mambo na wakathawabishwa sana na jitihada yao ya kutafuta.” Maarifa huongoza kwenye kupata kuelewa, na kuelewa kwenye uvumilio wa watu wenye maoni tofauti.
Kwa Nini Kuchunguza?
12. Ni mambo gani ambayo kwa kawaida huamua dini ya mtu?
12 Je! wewe umepata kufikiri au ukasema, ‘Mimi nina dini yangu mwenyewe. Hilo ni jambo la kibinafsi kabisa. Mimi siizungumzi pamoja na wengine’? Ni kweli dini ni jambo la kibinafsi kabisa—karibu tangu kuzaliwa mawazo ya kidini au ya kiadili yanapandikizwa katika akili yetu na wazazi na watu wa ukoo. Tokeo ni kwamba, kwa kawaida sisi hufuata mafikira ya kidini ya wazazi wetu na ya wazazi wa wazazi wetu. Kwa ujumla dini imekuwa utamaduni wa familia. Matokeo ya hatua hiyo yamekuwa nini? Kwamba katika visa vingi wengine wametuchagulia sisi dini yetu. Karibu imetegemea mahali na wakati tulipozaliwa. Au, kama mwanahistoria Arnold Toynbee alivyoonyesha, kuambatana kwa mtu na imani fulani mara nyingi huamuliwa na “tukio la kijiografia la mahali alipozaliwa.”
13, 14. Kwa nini si jambo la akili kuwaza kwamba dini aliyozaliwa nayo mtu ni yenye kuidhinishwa na Mungu moja kwa moja?
13 Je! ni jambo la akili kudhania kwamba dini ambayo ilipandikizwa wakati wa mtu kuzaliwa kwa lazima ndio ukweli mzima? Kama ulizaliwa Italia au Amerika Kusini, basi, bila ya uchaguzi wowote, yaelekea ulilelewa ukiwa Mkatoliki. Kama ulizaliwa katika India, basi yaelekea moja kwa moja ulikuwa Mhindu au, kama unatoka Punjabi, labda wewe ni wa Dini ya Sikh. Kama wazazi wako walitoka Pakistan, basi kwa wazi ungekuwa Mwislamu. Na kama ulizaliwa katika nchi ya Siasa za Kijamaa katika makumi machache ya miaka yaliyopita, huenda ikawa hukuwa na uchaguzi wowote bali kulelewa ukiwa mwaatheisti.—Wagalatia 1:13, 14; Matendo 23:6.
14 Kwa hiyo, je! dini aliyozaliwa nayo mtu inakuwa moja kwa moja ndiyo ya kweli, yenye kuidhinishwa na Mungu? Kama wazo hilo ndilo lingefuatwa kwa maelfu ya miaka iliyopita, wengi kati ya ainabinadamu wangekuwa wangali wanazoea ushamani wa kikale na ibada za nguvu za uzazi za kale, kwa msingi wa kwamba ‘kilichokuwa kizuri vya kuwatosha wazazi wangu wa kale waliokufa ni kizuri vya kunitosha.’
15, 16. Kuna manufaa gani katika kuchunguza dini nyingine?
15 Kwa sababu ya unamna mpana wa wonyesho wa kidini ambao umesitawi kuuzunguka ulimwengu kwa miaka 6,000 iliyopita, angalau ni jambo lenye kuelimisha na kupanua akili kuelewa mambo ambayo wengine husadiki na jinsi itikadi zao zilivyoanza. Na kwaweza pia kufungua mataraja ya tumaini lililo imara zaidi la wakati wako ujao.
16 Katika nchi nyingi sasa, kwa sababu ya uhamiaji na kusonga-songa kwa watu, watu wa dini tofauti-tofauti hushiriki ujirani mmoja. Kwa hiyo, kuelewa maoni ya mmoja na mwenzake kwaweza kuongoza kwenye uwasiliano na mazungumzo yenye maana kati ya watu wa imani tofauti-tofauti. Labda, pia, kwaweza kuondoa ulimwenguni chuki fulani ambayo msingi ni tofauti za kidini. Ni kweli, watu wanaweza kutokubaliana sana kuhusu itikadi zao za kidini, lakini hakuna msingi wa kuchukia mtu mwingine kwa sababu tu yeye hushikilia maoni tofauti.—1 Petro 3:15; 1 Yohana 4:20, 21; Ufunuo 2:6.
17. Kwa nini hatupaswi kuwachukia wale ambao kuwaza kwao kidini hutofautiana na kwetu?
17 Sheria ya kale ya Kiyahudi ilitoa taarifa hii: “Wewe hutamchukia mtu wa jamaa yako katika moyo wako. Karipia mtu wa jamaa yako lakini usipate hatia yoyote kwa sababu yake. Wewe hutalipa kisasi wala kuwa na kinyongo juu ya watu wa nchi yako. Mpende mwenzako kama wewe mwenyewe: Mimi ndimi BWANA [Yehova].” (Mambo ya Walawi 19:17, 18, Ta) Mwanzilishi wa Ukristo alitoa taarifa hii: “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, . . . na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu.” (Luka 6:27, 35) Chini ya kichwa “Mwanamke Ambaye Ni wa Kufanyiwa Mtihani,” Qurani hutoa taarifa juu ya kanuni kama hiyo (surah 60:7): “Asaa Mwenyezi Mungu atatia mapenzi baina yenu na hao maadui zenu, na Mwenyezi Mungu ni Muweza. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu.”
18. Ni jinsi gani yale anayoamini mtu hufanya tofauti?
18 Hata hivyo, ingawa uvumilio na uelewevu vyahitajiwa, hilo halimaanishi kwamba haifanyi tofauti mtu huamini nini. Kama mwanahistoria Geoffrey Parrinder alivyotoa taarifa hii: “Nyakati nyingine husemwa kwamba dini zote zina mradi ule ule, au hizo ni njia zinazolingana za kuongoza kwenye ukweli, au hata kwamba zote zinafunza mafundisho yale yale . . . Lakini Waazteki wa kale, walionyanyua kuelekea jua mioyo yenye kudunda ya wahanga wao, kwa hakika hawakuwa na dini nzuri kama ile ya Wabuddha wapenda amani.” Kuongezea hayo, inapohusu ibada, je! Mungu mwenyewe siye anayepaswa kuamua kinachokubalika na kisichokubalika?—Mika 6:8.
Dini Ipimweje?
19. Dini yapasa kuathirije mwenendo wa mtu?
19 Ingawa dini zilizo nyingi zina fungu la itikadi au mafundisho, mara nyingi zinatokeza theolojia yenye kutatanisha sana, asiyoweza kuelewa kabwela. Hata hivyo kanuni ya kisababishi na matokeo hutumika katika kila kisa. Mafundisho ya dini yapasa kuongoza utu na mwenendo wa kila siku wa kila mwumini. Hivyo, mwenendo wa kila mtu kwa kawaida utakuwa ni mwakisho, kwa kadiri kubwa au ndogo, wa msingi wa kidini wa mtu huyo. Dini yako ina matokeo gani juu yako? Je! dini yako inatokeza mtu mfadhili zaidi? Mkarimu, mnyoofu, mnyenyekevu, mvumiliaji, na mhurumiaji zaidi? Hayo ni maswali ya kufikiri kuzuri, kwa maana kama mwalimu mmoja mkuu wa kidini, Yesu Kristo alivyotoa taarifa hii: “Kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.”—Mathayo 7:17-20.
20. Ni maswali gani yanayotokea kwa habari ya dini na historia?
20 Bila shaka historia ya kilimwengu lazima itufanye tutue na kutufanya tutake kujua dini imekuwa na jukumu gani katika vita vingi ambavyo vimetatiza ainabinadamu na kusababisha taabu isiyo na kifani. Ni kwa nini watu wengi mno wameua na kuuawa katika jina la dini? Zile Krusedi (vita vitakatifu), Mahakama za Kuhukumia Wazushi wa Kidini, mapambano katika Mashariki ya Kati na Ireland Kaskazini, machinjo kati ya Iraq na Iran (1979-87), migongano ya Wahindu na wafuasi wa Dini ya Sikh katika India—matukio hayo yote kwa hakika yanawafanya watu wanaofikiri watokeze maswali juu ya itikadi na maadili ya kidini.—Ona kisanduku chini.
21. Ni nini baadhi ya vielelezo vya matunda ya Jumuiya ya Wakristo?
21 Makao ya Jumuiya ya Wakristo yametokeza sana kwa ajili ya unafiki wayo katika uwanja huu. Katika vita vya ulimwengu viwili, Mkatoliki ameua Mkatoliki na Mprotestanti ameua Mprotestanti kwa kuchochewa na viongozi wao wa kisiasa “Wakristo.” Hata hivyo, Biblia inatofautisha matendo ya mwili na matunda ya roho. Kwa habari ya matendo ya mwili, inatoa taarifa hii: “Ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Hata hivyo waitwao Wakristo wamezoea mambo hayo kwa karne nyingi, na mwenendo wao mara nyingi umeachiliwa na makasisi wao.—Wagalatia 5:19-21.
22, 23. Kinyume cha hayo, dini ya kweli yapasa kuzaa matunda gani?
22 Kinyume cha hayo, matunda ya roho yaliyo mazuri yanasimuliwa kama: “upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Dini zote zapasa kuwa zikizaa matunda ya aina hii yenye amani. Lakini zinafanya hivyo? Je! ile yako inafanya hivyo?—Wagalatia 5:22, 23.
23 Kwa hiyo, uchunguzi wa kitabu hiki juu ya jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta Mungu kupitia dini za ulimwengu yapasa kutumika kujibu baadhi ya maswali yetu. Lakini dini yapasa kuhukumiwa kwa viwango gani? Kwa viwango vya nani?
‘Dini Yangu Ni Nzuri vya Kunitosha’
24, 25. Ni tatizo gani analotokezewa kila mtu kwa habari ya dini yake?
24 Watu wengi wanapuuza mazungumzo ya kidini kwa kusema, ‘Dini yangu ni nzuri vya kunitosha. Mimi simdhuru mtu mwingineye yote, nami husaidia niwezapo.’ Lakini hayo yatosha? Je! viwango vyetu vya kibinafsi kuhusu dini vyatosha?
25 Ikiwa dini ni “wonyesho wa imani ya mtu na heshima kubwa kwa uwezo unaozidi nguvu za kibinadamu unaotambuliwa kuwa muumba na msimamizi wa ulimwengu wote,” kama ambavyo kamusi moja inavyotoa taarifa, basi bila shaka swali lapasa kuwa hili, Je! dini yangu ni nzuri kumtosha muumba na msimamizi wa ulimwengu wote mzima? Pia, katika kisa hicho, Muumba angekuwa na haki ya kuamua ni nini mwenendo, ibada, na fundisho vyenye kukubalika au visivyokubalika. Ili kufanya hivyo, ni lazima yeye afunue mapenzi yake kwa ainabinadamu, na ufunuo huo lazima uwe unapatikana na kufikiwa kwa urahisi na wote. Kuongezea hayo, ufunuo wake, hata ingawa ulitolewa muda wa karne nyingi tofauti-tofauti, sikuzote wapasa kuwa wenye kukubaliana na kupatana. Hilo linatokeza tatizo kwa kila mtu—kuchunguza uthibitisho na mtu kujithibitishia ni nini mapenzi ya Mungu yanayokubalika.
26. Ni kitabu gani kitakatifu kinachopaswa kutumika kuwa kipimio cha ibada ya kweli? Na kwa nini?
26 Kimoja cha vitabu vya kale zaidi kinachodai kuwa na pumzi ya Mungu ni Biblia. Pia ndicho kitabu kilichoenezwa zaidi na kutafsiriwa zaidi katika historia yote. Karibu miaka elfu mbili iliyopita, mmoja wa waandikaji wacho alitoa taarifa hii: “Msifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:2) Chanzo cha uthibitisho huo kingekuwa nini? Mwandikaji uyo huyo alitoa taarifa hii: “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” Kwa hiyo, Biblia iliyopuliziwa na Mungu yapasa kutumika kuwa kipimio chenye kutegemeka cha ibada ya kweli na yenye kukubalika.—2 Timotheo 3:16, 17.
27. (a) Baadhi ya maandishi matakatifu ya dini fulani za kilimwengu ni yapi? (b) Mafundisho yayo yapaswa kulinganaje na yale ya Biblia?
27 Kisehemu cha kale zaidi cha Biblia ni cha tarehe ya mapema zaidi ya maandishi mengineyo yote ya kidini. Tora, au vitabu vitano vya kwanza vya Biblia, Sheria iliyoandikwa na Musa akiwa na pumzi ya Mungu, ni ya tarehe ya kurudi nyuma kwenye karne za 15 na 16 K.W.K. Kwa kulinganisha, maandishi ya Hindu ya Rig-Veda (mkusanyo wa nyimbo za dini) yalikamilishwa yapata 900 K.W.K. wala hayadai yana pumzi ya kimungu. “Kanuni ya Vikapu Vitatu” ya Kibuddha ni vya tarehe inayorudi nyuma kwenye karne ya tano K.W.K. Qurani, inayodaiwa kuwa ilipokewa kutoka kwa Mungu kupitia malaika Gabrieli, ilitokezwa katika karne ya saba W.K. Kitabu cha Mormon, kinachoripotiwa kuwa alipewa Joseph Smith katika United States na malaika aitwaye Moroni, kilitokezwa karne ya 19. Ikiwa baadhi ya vitabu hivi vimepuliziwa kimungu kama wanavyodai wengine, basi mambo ambayo vinatoa kwa habari ya mwongozo wa kidini hayapasi kupingana na mafundisho ya Biblia, kwani ndiyo chanzo cha awali kilichopuliziwa na Mungu. Pia vinapasa kujibu baadhi ya maswali ambayo ainabinadamu wanataka sana kujua.
Maswali Yanayotaka Jibu
28. Ni baadhi ya maswali gani yanayohitaji jibu?
28 (1) Je! Biblia hufundisha yale ambayo dini zilizo nyingi hufundisha na ambayo watu wengi huamini, yaani, wanadamu wana nafsi isiyoweza kufa na kwamba wakati wa kufa huhamia makao mengine “yanayofuata,” mbinguni, mahali penye moto wa mateso (helo), au purgatori, au kwamba hurudi kwa kuchukua umbo jingine?
(2) Je! Biblia hufundisha kwamba Bwana Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu wote mzima hana jina? Je! hufundisha kwamba yeye ndiye Mungu mmoja? au watatu-watatu katika Mungu mmoja? au vijimungu vingi?
(3) Biblia husema ni nini lililokuwa kusudi la awali la Mungu katika kuumba ainabinadamu kwa maisha duniani?
(4) Je! Biblia hufundisha kwamba dunia itaangamizwa? Au je! hutaja tu mwisho, au umalizio, wa mfumo wa ulimwengu mfisadi?
(5) Amani ya ndani na wokovu vyaweza kupatikanaje hasa?
29. (a) Kanuni ya msingi inayopasa kuongoza jitihada yetu ya kutafuta ukweli ni nini? (b) Ni majibu gani ambayo Biblia hutoa kwa maswali yetu?
29 Kila dini ina majibu tofauti-tofauti, lakini katika jitihada yetu ya kutafuta “dini safi,” hatimaye tunapaswa kufikia mikataa ambayo Mungu hutaka sisi tuifikie. (Yakobo 1:27; AS; KJ) Kwa nini twaweza kusema hivyo? Kwa sababu kanuni yetu ya msingi itakuwa hii: “Mungu aonekane kuwa amini [kweli] na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, ukashinde uingiapo katika hukumu.”—Warumi 3:4.a
30. Ni baadhi ya maswali gani yatakayofikiriwa katika sura inayofuata?
30 Kwa kuwa sasa tuna msingi wa kuchunguza dini za ulimwengu, ebu na turudi kwenye jitihada ya mapema ya ainabinadamu ya kutafuta hali ya kiroho. Twajua nini juu ya jinsi dini ilivyoanza? Ni vigezo gani vya ibada vilivyoimarishwa kati ya vikundi vya watu wa zamani sana na labda wa kikale?
[Maelezo ya Chini]
a Ikiwa wapendezwa na jibu la mara moja la Biblia kwa maswali hayo, twapendekeza uchunguze maandiko yafuatayo: (1) Mwanzo 1:26; 2:7; Ezekieli 18:4, 20; Mambo ya Walawi 24:17, 18; Mathayo 10:28; (2) Kumbukumbu la Torati 6:4; 1 Wakorintho 8:4-6; (3) Mwanzo 1:27, 28; Ufunuo 21:1-4; (4) Mhubiri 1:4; Mathayo 24:3, 7, 8; (5) Yohana 3:16; 17:3; Wafilipi 2:5-11; 4:6, 7; Waebrania 5:9.
[Blabu katika ukurasa wa 16]
Dini zote zapaswa kuzaa matunda yenye amani. Lakini zinafanya hivyo?
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Dini, Upendo na Chuki
◼ “Vita vya dini huelekea kupamba moto zaidi. Wakati watu wanapopigania eneo kwa ajili ya faida ya kiuchumi, wanafikia mahali ambapo pigano hilo halistahilishi gharama hiyo na kwa hiyo wanaridhiana. Kisabibishi kinapokuwa cha kidini, kuridhiana na kuafikiana huelekea kuwa ni uovu.”—Roger Shinn, profesa wa adili za kijamii, Union Theological Seminary, New York.
◼ “Wanaume watazozania dini, waandike kwa ajili yayo, wapigane kwa ajili yayo, wafe kwa ajili yayo; kwa vyovyote waishi kwa ajili yayo . . . Mahali ambako dini ya kweli imezuia uhalifu mmoja, dini za uwongo zimetoa kisingizio cha elfu moja.”—Charles Caleb Colton (1825).
◼ “Tuna dini ya kutufanya tuchukiane, lakini hatuna ya kutosha kutufanya tupendane.”—Jonathan Swift (1667-1745).
◼ Wanadamu hawafanyi uovu kwa ukamili na kwa uchangamfu sana kama wanavyoufanya kutokana na usadikisho wa kidini.”—Blaise Pascal (1623-62).
◼ “Kusudi halisi la dini ya juu zaidi ni kueneza mashauri ya kiroho na kweli ambazo ndizo madhumuni yayo ili kufikia nafsi nyingi iwezekanavyo, kusudi kila moja ya nafsi hizi iwezeshwe kwa njia hiyo kutimiza mwisho unaomfaa Binadamu. Mwisho unaomfaa binadamu ni kumtukuza Mungu na kumfurahia Yeye milele.”—Arnold Toynbee, mwanahistoria.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Wahindu huheshimu sana mto Ganges—huitwa Ganga Ma, au Mama Ganga
Wakatoliki wenye moyo mweupe humgeukia Mariamu katika matumizi yao ya tasbihi
Katika nchi fulani za Kibuddha, watu wa kiume walio wengi hutumika wakati fulani wakiwa watawa waliovaa kanzu za rangi nyekundu-dhahabu
Waislamu waaminifu huhiji Makka angalau mara moja
[Picha katika ukurasa wa 6]
Mashahidi wa Yehova, wanaojulikana ulimwenguni pote kwa ajili ya utendaji wao wa kuhubiri, katika jiji moja la Kijapan
[Picha katika ukurasa wa 9]
Mtoto mchanga akibatizwa katika moja la makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Je! dini ambayo mtu alizaliwa nayo kwa lazima ndiyo ya kweli?
[Picha katika ukurasa wa 11]
Dhabihu ya Kiazteki ya kutoa binadamu—je! kweli dini zote ni “njia sawa za kuongoza kwenye ukweli”?
[Picha katika ukurasa wa 13]
Katika jina la dini, mamilioni wameua na wakauawa