Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 7/22 kur. 5-11
  • Kuishi Muda Mrefu Ukiwa na Afya Bora

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuishi Muda Mrefu Ukiwa na Afya Bora
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutambua Viunzi
  • Mazoea Yanayoathiri Muda Wako wa Maisha
  • Mazingira Huchangia
  • Tiba ya Gharama ya Chini na Yenye Mafanikio Sana Yapatikana
  • Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu
    Amkeni!—1999
  • Shangwe ya Ushindi na Huzuni
    Amkeni!—1997
  • Suluhisho la Duniani Pote—Je, Lawezekana?
    Amkeni!—1997
  • Ubongo Wako Hufanyaje Kazi?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 7/22 kur. 5-11

Kuishi Muda Mrefu Ukiwa na Afya Bora

WAZIA kwamba maisha ya mwanadamu ni mbio ndefu ya kuruka viunzi —mbio ambazo wakimbiaji huruka vizuizi. Wakimbiaji wote huanza mbio hizo pamoja; lakini warukapo na mara kwa mara kugonga vizuizi, wakimbiaji hupunguza mwendo, na wengi huendelea kujiuzulu mbio.

Vivyo hivyo, maisha ya mwanadamu yana mahali yanapoanzia na njiani kuna viunzi virefu. Wakati wa maisha yake mwanadamu hukabili kiunzi kimoja baada ya kingine. Kila mara arukapo yeye huwa dhaifu zaidi, punde si punde yeye huchoka. Kadiri viunzi viwavyo virefu, ndivyo anavyojiuzulu mbio upesi, au kufa. Iwapo mtu anaishi katika nchi zilizositawi, yeye hufa akiwa na umri wa miaka 75 hivi. Kipindi hiki huitwa muda wa wastani wa maisha ya mwanadamu—kinacholinganishwa na umbali ambao wakimbiaji wengi humudu.a (Linganisha Zaburi 90:10.) Hata hivyo, watu fulani huishi muda mrefu zaidi, na hata wachache hufikia ule unaodhaniwa kuwa upeo wa miaka ya mwanadamu, miaka 115 hadi 120—jambo la pekee sana kiasi cha kutangazwa kotekote ulimwenguni.

Kutambua Viunzi

Sasa watu wanaweza kuishi kwa takriban mara mbili zaidi ya walivyoweza mwanzoni mwa karne hii. Kwa nini? Kimsingi, ni kwa sababu mwanadamu ameweza kupunguza urefu wa viunzi. Lakini je, viunzi hivyo ni nini? Na je, vyaweza kupunguzwa viwe chini zaidi?

Mtaalamu wa afya ya umma wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) alieleza kwamba baadhi ya viunzi vikuu zaidi, au mambo yanayoathiri muda ambao watu wanatarajia kuishi ni mazoea, mazingira, na tiba.b Kwa hiyo, mazoea yako yawapo mazuri, mazingira yako yawapo bora, na hali yako ya tiba iwapo bora, ndivyo viunzi hivyo hushuka kwa kadiri iyo hiyo na huenda ukaishi muda mrefu. Ijapokuwa hali za watu hutofautiana sana, karibu kila mtu—kutoka kwa mkurugenzi wa benki hadi mchuuzi wa barabarani—anaweza kupunguza viunzi kwa njia fulani maishani mwake. Jinsi gani?

Mazoea Yanayoathiri Muda Wako wa Maisha

“Licha ya watu wenye mazoea mazuri ya kiafya kuishi muda mrefu, hawawi dhaifu hadi miaka michache ya mwisho ya maisha yao,” jarida The New England Journal of Medicine laripoti. Kwa kweli, kiunzi cha kwanza chaweza kupunguzwa kwa kubadili mazoea kama vile kula, kunywa, kulala, kuvuta sigareti, na kufanya mazoezi. Kwa mfano, fikiria mazoea ya kufanya mazoezi.

Mazoea ya kufanya mazoezi ya kimwili. Mazoezi ya kimwili ya kiasi yanaweza kuwa yenye faida sana. (Ona sanduku “Je, Ufanye Mazoezi Kadiri Gani na Ufanye ya Aina Gani?”) Uchunguzi unaonyesha kwamba mazoezi sahili ndani na nje ya nyumba yanaweza kuwasaidia watu wazee, kutia ndani ‘wazee wakongwe,’ kupata tena nguvu na afya bora. Kwa kielelezo, kikundi kimoja cha watu wazee wenye umri wa kati ya miaka 72 na 98 waliona kwamba baada ya kufanya mazoezi fulani ya kunyanyua uzito kwa majuma kumi tu waliweza kutembea haraka zaidi na kupanda ngazi kwa urahisi zaidi. Na hilo halishangazi! Uchunguzi uliofanywa wakati wa mazoezi ulionyesha kwamba nguvu za misuli ya wale walioshiriki zilikuwa zimeongezeka zaidi ya maradufu. Kikundi kingine kilichokuwa na wanawake wengi wenye umri wapata miaka 70, wasiozoea kufanya mazoezi walifanya mazoezi mara mbili kwa juma. Baada ya mwaka mmoja, misuli, nguvu, usawaziko, na uzito wa mifupa yao uliongezeka. “Tulipoanza, tulihofu kwamba kano zetu zingekatika, na misuli yetu kujeruhiwa,” akasema mwanafisiolojia Miriam Nelson, aliyefanya uchunguzi huo. “Lakini badala yake tukawa wenye nguvu zaidi, na afya zaidi.”

Kikitoa muhtasari wa matokeo ya uchunguzi mbalimbali wa kisayansi juu ya kuzeeka na mazoezi, kitabu kimoja chasema: “Mazoezi hupunguza mwendo wa kuzeeka, hurefusha maisha, na kupunguza kipindi cha kutegemea wengine ambacho kwa kawaida hutangulia kifo.”

Mazoea ya kufanya mazoezi ya akili. Ule msemo “Uutumie au uupoteze” yaonekana kuwa unatumika si tu kwa misuli bali pia kwa akili. Ijapokuwa kuzeeka huandamana na usahaulifu fulani, uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Marekani Inayochunguza Kuzeeka unaonyesha kwamba ubongo wa mtu aliyezeeka huwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na matokeo ya kuzeeka. Kwa hiyo, profesa wa elimu ya neva Dakt. Antonio R. Damasio akata kauli hivi: “Watu wazee wanaweza kuendelea kuwa na uwezo bora sana wa kiakili.” Ni nini kinachofanya ubongo wa watu waliozeeka uendelee kuwa na uwezo mzuri?

Ubongo una chembe za ubongo au nyuroni zipatazo bilioni 100, na chembe hizo zina trilioni nyingi za miunganisho. Miunganisho hii hutenda kama nyaya za umeme ikiwezesha nyuroni “kuwasiliana” na nyingine ili kutokeza kumbukumbu miongoni mwa mambo mengine. Ubongo uzeekapo, nyuroni hufa. (Ona sanduku “Kuchunguza Upya Chembe za Ubongo.”) Lakini, ubongo wa watu wazee bado unaweza kutenda vyema bila nyuroni zilizokufa. Wakati wowote nyuroni ifapo, nyuroni zinazoizunguka hufanyiza miunganisho mipya kati yake na nyuroni nyingine na hivyo hutimiza kazi ya nyuroni iliyokufa. Kwa njia hiyo, ubongo hubadili utendaji fulani kutoka sehemu moja hadi nyingine. Kwa hiyo, watu wengi wazee hutimiza mambo yanayohitaji kufikiri sawa na vijana, lakini huenda wakatumia sehemu tofauti za ubongo kufanya hivyo. Katika mambo fulani, ubongo wa mtu mzee hutenda kama mchezaji wa tenisi mwenye umri mkubwa ambaye hutumia ustadi kwa sababu ya kupungua kwa wepesi wake jambo ambalo huenda wachezaji vijana hawana. Lakini, licha ya kutumia mbinu tofauti na za wachezaji vijana, yule mchezaji mzee bado hupata pointi.

Watu wazee wanaweza kufanya nini ili kudumisha uwezo wao? Baada ya kuchunguza zaidi ya watu 1,000 wenye umri wa kati ya miaka 70 na 80, mtafiti wa hali ya kuzeeka Dakt. Marilyn Albert alipata kwamba mazoezi ya akili ni mojawapo ya mambo yanayoamua watu wazee watakaodumisha uwezo mkubwa wa kufikiri. (Ona sanduku “Kudumisha Uwezo wa Kufikiri.”) Mazoezi ya akili hudumisha utendaji wa ‘miunganisho’ ya ubongo. Kwa upande mwingine, watafiti husema kwamba kudhoofika kwa akili huanza “watu wanapostaafu, wanapoamua kulegea, na wanaposema haiwalazimu kuhangaishwa na matukio ya ulimwengu.”—Inside the Brain.

Kwa hiyo habari njema ni kwamba, aeleza mwanasayansi anayechunguza kuzeeka Dakt. Jack Rowe, “mambo tunayoweza kudhibiti au yale tunayoweza kubadili yanapaswa kuboresha uwezo wetu wa kufurahia miaka ya uzeeni.” Isitoshe, bado haijawa kuchelewa mno kuanza kuwa na mazoea mazuri. “Hata ikiwa umekuwa na mazoea mabaya ya kiafya muda mrefu katika maisha yako kisha ukabadili maisha yako katika miaka ya baadaye,” asema mtafiti mmoja, “bado unapaswa kufurahia angalau faida fulani za kudumisha maisha bora.”

Mazingira Huchangia

Iwapo msichana ambaye amezaliwa London leo angerudishwa London wakati wa Enzi za Kati, muda ambao angetarajia kuishi ungekuwa nusu ya muda anaoishi sasa. Tofauti hiyo ingesababishwa na badiliko la ghafula la viunzi viwili virefu—mazingira na tiba, wala haingesababishwa na badiliko la ghafula la hali za kimwili za msichana huyo. Fikiria kwanza mazingira.

Mazingira ya kiasili. Hapo kale, mazingira ya kiasili ya mwanadamu—kwa mfano makao yake, —yalikuwa hatari sana kwa afya. Hata hivyo, katika miongo ya majuzi, hatari zilizosababishwa na mazingira ya kiasili zimepunguzwa. Usafi bora, maji salama, na kupungua kwa wadudu waharibifu katika nyumba kumeboresha mazingira ya mwanadamu, afya yake, na kumerefusha maisha yake. Matokeo ni kwamba katika sehemu nyingi duniani, sasa mwanadamu anaweza kuishi muda mrefu zaidi.c Lakini kupunguza urefu wa kiunzi hiki hutia ndani mengi zaidi ya kuboresha mazingira yako ya kiasili. Huhusisha pia kudumisha mazingira yanayofaa kijamii na kidini.

Mazingira ya kijamii. Mazingira yako ya kijamii hufanyizwa na watu—wale unaoishi nao, kufanya kazi nao, kula nao, kuabudu nao, na kucheza nao. Mazingira yako ya kiasili huboreka unapopata maji safi; na vivyo hivyo, huenda mazingira yako ya kijamii yakaboreka unapopata mashirika mazuri, tukitaja jambo moja tu muhimu. Kuweza kushiriki na wengine shangwe, majonzi, miradi, na mafadhaiko yako, hupunguza kimo cha kiunzi cha mazingira na hurefusha maisha yako.

Hata hivyo, jambo lililo kinyume na hilo ni kweli pia. Kutokuwa na marafiki huenda kukasababisha upweke na kujitenga. Utaelekea kudhoofika unapoishi na watu wasioonyesha kuwa wanakujali. Mwanamke mmoja aliyekuwa akiishi katika makao ya kutunzia watu wazee alimwandikia hivi mjuani wake: “Nina umri wa miaka 82 na nimekuwa katika makao haya kwa muda mrefu wa miaka 16. Tunatunzwa vema, lakini nyakati nyingine mimi hulemewa na upweke.” Kwa kusikitisha, hali ya mwanamke huyu inafanana na ya watu wengi wazee, hasa katika nchi za Magharibi. Kwa kawaida wao huishi katika mazingira ya kijamii yanayowakubali bila kuwathamini. Matokeo ni kwamba “upweke ni mojawapo ya hali kubwa zinazohatarisha hali njema ya watu wazee katika nchi zilizositawi,” asema James Calleja, wa Shirika la Kimataifa Linalochunguza Kuzeeka.

Ni kweli kwamba huenda usiweze kukomesha hali zinazokufanya uwe mpweke—kama vile kustaafishwa kwa lazima, kupungua kwa uwezo wa kutembea, kupoteza marafiki wa muda mrefu, au kifo cha mwenzi—lakini bado unaweza kuchukua hatua fulani ili kupunguza urefu wa kiunzi hiki hadi kimo kinachofaa. Kwanza, kumbuka kwamba kuhisi upweke hakusababishwi na umri wa uzee; baadhi ya vijana huhisi upweke pia. Kuzeeka si chanzo cha tatizo hili—kujitenga na jamii ndiko chanzo. Unaweza kufanya nini ili ukabiliane na mwelekeo wa kujitenga?

“Wafanye watu wapendezwe na ushirika wako,” ashauri mjane mmoja mzee. “Watu wengi hawapendi kushirikiana na mtu mwenye manung’uniko. Unahitaji kujitahidi kuwa mchangamfu. Ni kweli kwamba inahitaji jitihada, lakini jitihada zako hutokeza manufaa. Ukiwa mwenye fadhili nawe utaonyeshwa fadhili.” Yeye aongezea hivi: “Ili kuhakikisha kwamba nina jambo la kuzungumza pamoja na watu ninaokutana nao, vijana au wazee, mimi hujitahidi kusoma habari za karibuni katika magazeti yenye kuarifu na kufuatilia habari zinazoripotiwa.”

Hapa pana madokezo mengine: Jifunze kupendezwa na mambo yanayowapendeza watu wengine. Uliza maswali. Uwe mkarimu kadiri iwezekanavyo. Iwapo huna vitu vya kimwili, unaweza kujitoa mwenyewe; kuna furaha katika kutoa. Andika barua. Jihusishe katika hobi fulani. Kubali mialiko ya kuzuru watu wengine au ya utendaji mwingine wa mbali. Yafanye makao yako yawe na uchangamfu na yenye kupendeza wageni. Jitahidi kusaidia watu wanaohitaji msaada na uwasaidie.

Mazingira ya kidini. Uthibitisho mwingi unadokeza kwamba utendaji wa kidini huwasaidia watu wazee kupata “umaana na kusudi maishani” na kupata “furaha,” “hisi ya kuthaminiwa,” “uradhi zaidi maishani,” na “hisi ya kuwa sehemu ya jamii na kuwa na hali njema.” Kwa nini? Kitabu Later Life—The Realities of Aging chaeleza: “Imani ya kidini huwafanya watu wawe na mambo ya kufuatia maishani na utaratibu fulani wa mitazamo, kanuni, na itikadi ambazo huwasaidia kufasiri na kuelewa ulimwengu unaowazunguka.” Kwa kuongezea, utendaji wa kidini huwakutanisha watu waliozeeka pamoja na watu wengine na hivyo “hupunguza uwezekano wa kujitenga na jamii na hali ya upweke.”

Kwa Louise na Evelyn, wote wakiwa ni wajane wenye umri wa miaka 80 na washiriki wa kutaniko moja la Mashahidi wa Yehova, uchunguzi huu unathibitisha tu yale ambayo wamejua kwa miongo mingi. “Katika Jumba la Ufalme letu,d mimi hufurahia kuzungumza na wengine, wazee kwa vijana,” asema Louise. “Mikutano huwa yenye kuelimisha. Tunaposhirikiana baada ya mikutano, sisi hufurahia ucheshi pia. Ni wakati wa kuchangamsha.” Evelyn pia hunufaika na utendaji wake wa kidini. “Kwenda kuzungumza na majirani wangu juu ya Biblia,” yeye asema, “hunifanya nisijitenge. Lakini zaidi ya hayo, hunifanya niwe mwenye furaha. Kuwasaidia wengine wajue kusudi halisi la maisha ni kazi yenye kuridhisha.”

Kwa wazi, Louise na Evelyn wana kusudi maishani. Hisi zao za kuwa na hali njema hupunguza urefu wa kiunzi cha pili—mazingira—na huwasaidia kuishi bila kukata tamaa.—Linganisha Zaburi 92:13, 14.

Tiba ya Gharama ya Chini na Yenye Mafanikio Sana Yapatikana

Maendeleo katika sayansi ya kitiba katika karne hii yamepunguza sana urefu wa kiunzi cha tatu, tiba—lakini si ulimwenguni pote. Katika nchi kadhaa zilizo maskini, yasema The World Health Report 1998, “muda wa maisha unaotarajiwa ulipungua kati ya mwaka wa 1975-1995.” Mkurugenzi mkuu wa WHO alisema kwamba “watu 3 kati ya 4 katika nchi maskini zaidi wanakufa leo kabla ya kufikia umri wa miaka 50—muda wa maisha ambao watu walitarajia kuishi nusu karne iliyopita.”

Ijapokuwa hivyo, idadi kubwa ya vijana na wazee katika nchi maskini wanapunguza urefu wa kiunzi hiki kwa kutumia tiba iliyoko na wanayoweza kugharimia. Kwa kielelezo, fikiria mbinu mpya ya kutibu kifua kikuu (TB).

Ulimwenguni pote, kifua kikuu husababisha vifo vya watu kuliko jumla ya vifo vyote vinavyosababishwa na UKIMWI, malaria, na maradhi ya kanda za joto—watu 8,000 kila siku. Watu 95 kati ya 100 wenye kifua kikuu, huishi katika nchi zinazositawi ulimwenguni. Watu milioni 20 sasa wanaugua kifua kikuu, na watu wapatao milioni 30 wanaweza kufa kutokana na kifua kikuu kwa miaka kumi ijayo, idadi inayolingana na jumla ya watu wote katika Bolivia, Kambodia, na Malawi.

Si ajabu kwamba shirika la WHO lilifurahi kutangaza katika mwaka wa 1997 kwamba lilikuwa limebuni mbinu ya kutibu kifua kikuu kwa miezi sita bila uhitaji wa kulazwa hospitalini au kupata tiba ya kisasa. “Kwa mara ya kwanza,” kikasema kichapo The TB Treatment Observer cha WHO, “ulimwengu una vifaa na mbinu zenye kutegemeka za kukomesha kifua kikuu si tu katika nchi tajiri, bali pia katika nchi maskini zaidi ulimwenguni.” Mbinu hii—iliyoelezwa na wengine kuwa “maendeleo makubwa zaidi kuhusu mambo ya afya katika mwongo huu”—inaitwa DOTS.e

Ijapokuwa gharama ya mbinu hii ni chini zaidi ya tiba ya kawaida ya kifua kikuu, matokeo ni mazuri, hasa kwa wale wanaoishi katika nchi zinazositawi. “Hakujapata kuwa na mbinu nyingine ya kudhibiti na kuponya sana kifua kikuu kama mbinu hii,” asema Dakt. Arata Kochi, mkurugenzi wa Mpango wa WHO wa Ulimwenguni Pote wa Kudhibiti Kifua Kikuu. “Mbinu ya DOTS huponya kwa asilimia 95 ya wagonjwa, hata katika nchi maskini zaidi ulimwenguni.” Kufikia mwisho wa mwaka wa 1997, mbinu ya DOTS ilikuwa inatumiwa katika nchi 89. Leo idadi hiyo imeongezeka hadi 96. Shirika la WHO linatumaini kwamba mbinu hii itafikia mamilioni ya watu maskini katika nchi zilizo maskini, hilo litawawezesha kupunguza urefu wa kiunzi cha tatu katika mbio za maisha.

Kwa kubadili mazoea yake, kuboresha mazingira yake, na kuboresha tiba yake, kwa kweli mwanadamu amefaulu kurefusha muda wa wastani wa maisha na muda wa maisha anaotarajia kuishi. Swali ni, Je, siku moja mwanadamu ataweza kurefusha muda wa upeo wa maisha yake vilevile—labda hata kuishi bila kikomo?

[Maelezo ya Chini]

a Japo semi “muda unaotarajiwa wa maisha” na “muda wa wastani wa maisha” hutumiwa mara nyingi kwa maana ileile, kuna tofauti kati ya semi hizi mbili. “Muda unaotarajiwa wa maisha” hurejezea idadi ya miaka ambayo mtu anaweza kutarajia kuishi, huku “muda wa wastani wa maisha” ukirejezea idadi ya wastani ya miaka halisi ambayo watu wa eneo fulani huishi. Kwa hiyo, makadirio ya muda unaotarajiwa wa maisha hutegemea muda wa wastani wa maisha.

b Kwa kuongezea mambo hayo yanayobadilika, bila shaka umbile la mwanadamu la kurithiwa na lisilobadilika huathiri afya yake na urefu wa maisha yake. Hili litazungumzwa katika makala ifuatayo.

c Kwa habari zaidi juu ya jinsi ya kuboresha mazingira ya nyumbani kwa kuchukua hatua sahili, ona makala “Kutimiza Takwa la Usafi” na “Kinachoamua Afya Yako—Lile Uwezalo Kufanya,” katika makala za Amkeni! za Mei 8, 1989 (au Septemba 22, 1988, kwa Kiingereza), na Aprili 8, 1995.

d Mahali ambapo Mashahidi wa Yehova hufanyia mikutano yao ya kila juma huitwa Jumba la Ufalme. Watu wote wanakaribishwa katika mikutano hii bila malipo.

e Neno DOTS ni ufupi wa maneno directly observed treatment, short-course (tiba ya muda mfupi ya kuzingatia na kutazama wagonjwa). Kwa habari zaidi juu ya mbinu ya DOTS, ona makala “Kinga Mpya Dhidi ya Kifua Kikuu,” katika Amkeni! la Mei 22, 1999.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

JE, UFANYE MAZOEZI KADIRI GANI NA UFANYE YA AINA GANI?

“Ni jambo linalofaa kuwa na mradi wa kufanya mazoezi ya kiasi kwa dakika 30 kila siku,” yasema Taasisi ya Kitaifa Inayochunguza Kuzeeka (NIA). Lakini si lazima ufanye mazoezi kwa dakika 30 katika kipindi kimoja. Kufanya mazoezi kwa vipindi vitatu vifupi vya dakika 10 kila kimoja husemekana kuwa na manufaa sawa na kufanya mazoezi yale yale kwa kipindi kimoja cha dakika 30. Unaweza kufanya mazoezi ya aina gani? Kijitabu Don’t Take It Easy: Exercise! cha taasisi ya NIA chapendekeza hivi: “Mazoezi makali yanayofanywa kwa muda mfupi, kama vile kupanda ngazi badala ya lifti, au kutembea badala ya kupanda gari, kwaweza kufikia dakika 30 za mazoezi kila siku. Kukusanya majani, kucheza kwa bidii pamoja na watoto, kutunza bustani, na hata kufanya kazi za nyumbani kwaweza kufanywa katika njia ambayo inachangia jumla ya wakati unaofanya mazoezi kila siku.” Bila shaka, ni jambo la hekima kupata ushauri wa daktari wako kabla hujaanza kufuata mpango maalumu wa mazoezi.

[Picha]

Mazoezi ya kimwili ya kiasi yanaweza kuwasaidia watu wazee kupata tena nguvu

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]

KUDUMISHA UWEZO WA KUFIKIRI

Uchunguzi wa kisayansi uliohusisha maelfu ya watu wazee ulionyesha mambo kadhaa yanayosaidia kudumisha uwezo wao wa kufikiri. Yanatia ndani “kusoma sana, kusafiri, kujishughulisha sana na mambo ya kijamii, elimu, kujiunga na klabu, na vyama vya kitaaluma.” “Fanya mambo mbalimbali mengi iwezekanavyo.” “Endelea na kazi yako. Usistaafu.” “Zima televisheni.” “Jifunze kozi fulani.” Yaaminika kwamba mbali na kuboresha hali ya mtu utendaji huo hutokeza pia sinapsi mpya kwenye ubongo.

[Picha]

Mazoezi ya akili husaidia kudumisha uwezo wa kufikiri

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

MADOKEZO YA KIAFYA KWA WATU WANAOZEEKA

Taasisi ya Kitaifa Inayochunguza Kuzeeka, kitivo cha Idara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani, yasema kwamba “uwezekano wa kudumisha afya bora na kuishi muda mrefu waweza kuboreshwa” kwa kufuata mashauri bora kama yafuatayo:

● Kula mlo kamili, unaotia ndani matunda na mboga.

● Iwapo wewe ni mnywaji wa vileo, unywe kwa kiasi.

● Usivute sigareti. Haijawa kuchelewa mno kuacha.

● Fanya mazoezi kwa ukawaida. Pata ushauri wa daktari kabla hujaanza kufuata mpango maalumu wa mazoezi.

● Wasiliana na familia na marafiki.

● Dumisha utendaji kazini, michezoni, na katika jumuiya.

● Uwe na mwelekeo mzuri maishani.

● Fanya mambo yanayokufurahisha.

● Uchunguzwe kwa ukawaida na daktari.

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

KUZICHUNGUZA UPYA CHEMBE ZA UBONGO

“Hapo awali tulifikiri kwamba chembe za ubongo hufa kila siku ya maisha yako na katika kila sehemu ya ubongo,” asema Dakt. Marilyn Albert, profesa wa akili na neva. “Hilo si kweli—chembe fulani hufa unapozeeka, lakini si kwa wingi, na hilo hutukia katika sehemu fulani tu za ubongo.” Isitoshe, uchunguzi wa karibuni unadokeza kwamba hata imani ya muda mrefu ya kwamba chembe mpya haziwezi kukua katika ubongo wa mwanadamu, “ilikosea kabisa,” laripoti Scientific American la Novemba 1998. Wanasayansi wa neva wanasema kwamba sasa wana uthibitisho wa kwamba hata watu waliozeeka “hufanyiza mamia ya nyuroni mpya.”

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

JE, UNAPOZEEKA UNAKUWA MWENYE HEKIMA?

“Wazee ndio walio na hekima, na katika kuishi siku nyingi iko fahamu,” Biblia yasema. (Ayubu 12:12) Je, ni kweli? Watafiti walichunguza sifa zifuatazo katika watu wazee, “ufahamu, uwezo wa kufanya maamuzi vizuri, maoni sawa ya akilini na uwezo wa kubainisha kanuni zinazopingana na kubuni mbinu za kutatua matatizo.” Kulingana na kichapo U.S.News & World Report, uchunguzi huo ulionyesha kwamba “kwa kawaida watu wazee huwapita vijana katika kuwa na hekima, kutoa shauri la busara, na la ndani sana.” Uchunguzi unaonyesha pia kwamba “ingawa mara nyingi wazee huhitaji muda mrefu wa kufanya uamuzi kuliko vijana, kwa kawaida uamuzi wao unakuwa bora.” Kwa hiyo, kama vile kitabu cha Biblia cha Ayubu kinavyodokeza, kwa kweli kuzeeka kunatokeza hekima.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Maisha ya mwanadamu ni kama mbio za kuruka viunzi vingi

[Picha katika ukurasa wa 9]

“Wafanye watu wapendezwe na ushirika wako,” ashauri mjane mmoja

[Picha katika ukurasa wa 10]

“Kuwasaidia wengine wajue kusudi halisi la maisha ni kazi yenye kuridhisha.”—Evelyn

[Picha katika ukurasa wa 10]

“Katika Jumba la Ufalme letu, mimi hufurahia kuzungumza na wengine, wazee kwa vijana.”—Louise

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki