Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 8/15 kur. 30-31
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Kutoka Kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Kujua Yaliyo Katika Habari
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1987
  • Ndoa—Zawadi Kutoka kwa Mungu Mwenye Upendo
    “Jitunzeni Katika Upendo wa Mungu”
  • Kutayarisha Kwa Ajili Ya Ndoa Yenye Mafanikio
    Siri ya Furaha ya Familia
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 8/15 kur. 30-31

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Wakristo wapaswa kuuchukulia uchumba kwa uzito kadiri gani?

Uchumba huleta furaha, ingawa huo ni jambo zito vilevile. Hakuna Mkristo yeyote mkomavu apaswaye kuuchukulia uchumba kijuujuu tu, akifikiri kwamba anaweza kuuvunja kwa ghafula wakati wowote. Kipindi cha uchumba pia ni wakati wa wenzi hao wawili kufahamiana vizuri kabla ya ndoa.

Tunapoizungumzia habari hii, twahitaji kutambua kwamba desturi za kijamii zinazohusu ndoa, na hatua zinazoongoza kwenye ndoa, hutofautiana sana katika maeneo mbalimbali na nyakati mbalimbali. Biblia yaonyesha jambo hili.

Binti wawili wa Loti, waliokuwa bado “hawajalala na mwanamume,” walikuwa wamechumbiwa kwa njia fulani na wanaume wawili wenyeji. “Wachumba wa binti” za Loti wangewachukua, hata hivyo Biblia haituambii sababu iliyofanya uchumba huo uanzishwe na jinsi ulivyoanza. Je, binti hao walikuwa watu wazima? Je, walikuwa na daraka kubwa la kuchagua watu ambao wangewaoa? Je, walifanya uchumba kwa kuchukua hatua fulani iliyojulikana na watu? Hatujui. (Mwanzo 19:8-14, BHN) Twajua kwamba Yakobo mwenyewe alifanya mapatano na baba ya Raheli ya kumwoa Raheli baada ya kumfanyia baba huyo kazi kwa miaka saba. Ingawa Yakobo alimtaja Raheli kuwa “mke wangu,” hawakufanya ngono katika miaka hiyo. (Mwanzo 29:18-21) Mfano mwingine ni Daudi. Kabla ya kumwoa binti Sauli, ilibidi Daudi apate ushindi dhidi ya Wafilisti. Baada ya kutimiza takwa la Sauli, Daudi angeweza kumwoa binti huyo, Mikali. (1 Samweli 18:20-28) Kulikuwa na tofauti kati ya “uchumba” mbalimbali ambao umetajwa, nao pia watofautiana na desturi za nchi nyingi leo.

Sheria ya Kimusa ilikuwa na kanuni mbalimbali kuhusu ndoa na uchumba. Kwa mfano, mwanamume angeweza kuwa na wake zaidi ya mmoja; angeweza kumtaliki mkewe kwa misingi mbalimbali, ingawa yaonekana mke hangeweza kumtaliki mumewe. (Kutoka 22:16, 17; Kumbukumbu la Torati 24:1-4) Mwanamume aliyemtongoza bikira asiyechumbiwa alipaswa kumwoa ikiwa baba ya binti angekubali, naye hangeweza kamwe kumtaliki. (Kumbukumbu la Torati 22:28, 29) Sheria nyingine zilitumika katika ndoa, kama zile zilizohusu wakati ngono ipaswapo kuepukwa. (Mambo ya Walawi 12:2, 5; 15:24; 18:19) Ni kanuni zipi zilizohusu uchumba?

Hali ya kisheria ya mwanamke Mwisraeli aliyechumbiwa ilitofautiana na ya mwanamke asiyechumbiwa; kwa namna fulani aliyechumbiwa alionwa kuwa ameolewa. (Kumbukumbu la Torati 22:23-29; Mathayo 1:18, 19) Waisraeli hawangeweza kuchumbia au kufunga ndoa na watu fulani wa jamaa. Mara nyingi hawa walikuwa maharimu, lakini uchumba na ndoa fulani zilikatazwa kwa sababu ya haki za urithi. (Mambo ya Walawi 18:6-20; ona Mnara wa Mlinzi la Septemba 1, 1980, ukurasa wa 18-21, au Mnara wa Mlinzi la Machi 15, 1978, ukurasa wa 25-28, la Kiingereza.) Ni dhahiri kwamba watumishi wa Mungu hawakupaswa kuuchukulia uchumba kijuujuu tu.

Waisraeli walikuwa chini ya kanuni hizo zote za Sheria, lakini Wakristo hawako chini ya Sheria hiyo, kutia ndani kanuni zake zinazohusu uchumba au ndoa. (Waroma 7:4, 6; Waefeso 2:15; Waebrania 8:6, 13) Kwa hakika, Yesu alifundisha kwamba kanuni ya Kikristo inayohusu ndoa ni tofauti na kanuni ya Sheria. (Mathayo 19:3-9) Ingawa hivyo, yeye hakupunguza uzito wa ndoa, wala ule wa uchumba. Kwa hiyo, habari hii inayozungumzwa hapa, yaani uchumba miongoni mwa Wakristo, ni nzito kadiri gani?

Katika nchi nyingi, watu mmoja-mmoja hujichagulia wenyewe mtu wa kufunga ndoa naye. Mara mwanamume na mwanamke wanapoahidi kuoana, wao huonwa kuwa wamechumbiana. Kwa kawaida, hakuna hatua nyingine rasmi inayohitajika ili kuanzisha uchumba huo. Ni kweli kwamba katika maeneo fulani ni jambo la kawaida kwa mwanamume kumpa pete yule atakayekuwa mkewe kama ishara ya uchumba wao. Au ni desturi kuwatangazia jamaa na marafiki juu ya uchumba huo, kama kwenye mlo wa familia au katika kikusanyiko kingine. Mambo hayo ni uchaguzi wa kibinafsi, wala sio matakwa ya Kimaandiko. Kinachoufanya uwe uchumba ni makubaliano kati ya hao watu wawili.a

Mkristo hapaswi kujiingiza haraka-haraka katika uchumba au ndoa. Sisi huchapisha habari zinazotegemea Biblia zinazoweza kuwasaidia waseja kuamua ikiwa ni jambo la hekima kuanza kutafuta uchumba au kuchukua hatua za kufanya uchumba au kufunga ndoa.b Ushauri wa msingi katika habari hizo ni kwamba ndoa ya Kikristo ni ya kudumu.—Mwanzo 2:24; Marko 10:6-9.

Wakristo wawili wapaswa kufahamiana vema sana kabla ya kuanza kufikiria uchumba. Kila mmoja aweza kujiuliza, ‘Je, kweli naijua vema hali ya kiroho ya mtu huyo na ujitoaji wake kwa Mungu? Je, naweza kutazamia kumtumikia Mungu maisha yote nikiwa naye? Je, tunafahamu vema tabia za kila mmoja? Je, nina uhakika kwamba tutaendelea kupatana daima? Je, twafahamu mambo ya kutosha juu ya matendo ya wakati uliopita na hali za sasa za kila mmoja?’

Mara Wakristo wawili wachumbianapo, ni haki kwao na kwa wengine kutarajia kwamba ndoa itafuata. Yesu alionya hivi: “Acheni tu neno lenu Ndiyo limaanishe Ndiyo, La yenu, La.” (Mathayo 5:37) Wakristo wanaochumbiana wapaswa kuuchukulia uchumba huo kwa uzito. Hata hivyo, katika hali iliyo nadra kutokea, huenda Mkristo anayefanya uchumba akafahamu kwamba jambo fulani zito halikutajwa au lilifichwa kabla ya uchumba. Huenda likawa jambo muhimu lihusulo maisha ya zamani ya mtu huyo, hata laweza kuwa ni matendo ya uhalifu au ya ukosefu wa adili. Mkristo anayepata kuyafahamu hayo apaswa kuamua atakalofanya. Labda hao wawili wataizungumza habari hiyo kikamili na kukubali kuendelea na uchumba wao. Au huenda wakaafikiana kuukomesha uchumba huo. Ingawa kufanya hivyo huenda ukawa uamuzi wa kibinafsi—wengine hawapaswi kuingilia, kujaribu kutilia shaka, au kuhukumu jambo hilo—huo ni uamuzi mzito sana. Kwa upande mwingine, huenda yule anayepata kulifahamu jambo hilo zito akalazimika kuukomesha uchumba huo, hata ikiwa mtu yule mwingine ataka uendelee.—Ona “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Oktoba 1, 1975, au Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 1975, Kiingereza.

Kuna sababu nzuri ya kutatua masuala kama hayo kabla ya kuingia katika ndoa. Yesu alisema kwamba msingi pekee wa Kimaandiko wa talaka unaomweka mtu huru kuoa tena ni por·neiʹa, ambayo ni ukosefu mbaya sana wa adili katika ngono unaofanywa na huyo mwenzi mwingine wa ndoa. (Mathayo 5:32; 19:9) Yeye hakusema kwamba ndoa ya kisheria yaweza kuvunjwa kwa talaka ikiwa mtu apata kujua juu ya tatizo au kosa zito lililofanywa kabla ya arusi.

Kwa kielelezo, katika siku ya Yesu kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupata ukoma. Ikiwa mwanamume Myahudi angegundua kwamba mwenzake alikuwa (iwe kwa kujua au kutojua) na ukoma alipomwoa, je, angekuwa na msingi wa kumtaliki? Huenda Myahudi aliye chini ya Sheria akamtaliki kwa sababu hiyo, lakini Yesu hakusema kwamba hatua hiyo yafaa kwa wafuasi wake. Fikiria hali mbalimbali za wakati huu. Huenda mwanamume aliyeambukizwa kaswende, malengelenge ya viungo vya uzazi, virusi vya UKIMWI, au ugonjwa mwingine hatari wenye kuambukiza akaoa pasipo kufichua ukweli huo. Huenda aliambukizwa ugonjwa huo kupitia ukosefu wa adili katika ngono kabla ya uchumba au wakati wa uchumba. Mke kufahamu baadaye kuhusu ugonjwa wa mume huyo au ukosefu wake wa adili wa wakati uliopita (hata kufahamu kuhusu uhanithi wake au kutoweza kwake kufanya ngono) hakubadili uhakika wa kwamba sasa wao wameoana. Maisha mabaya ya wakati uliopita si msingi wa Kimaandiko wa kuvunja ndoa, na ndivyo ilivyo pia ikiwa mke alikuwa ameambukizwa ugonjwa fulani au hata kuficha mimba ya mwanamume mwingine wakati wa kuolewa. Sasa wao wameoana na kujitoa wenyewe kwa mmoja na mwenzake.

Ni kweli kwamba hali zenye kuhuzunisha kama hizo ni nadra, lakini vielelezo hivyo vyapasa kuongeza uzito kwa jambo kuu: Uchumba haupaswi kuchukuliwa kijuujuu tu. Kabla ya uchumba na pia wakati wa uchumba, Wakristo wapaswa kujitahidi kufahamiana vema. Wapaswa kusema ukweli kuhusu yale ambayo mwenzi yule mwingine ataka kujua au ana haki ya kujua. (Katika nchi fulani sheria huwataka wenzi wafanyiwe uchunguzi wa kitiba kabla ya ndoa. Huenda wengine wakataka uchunguzi kama huo ufanywe ili waweze kufahamu.) Kwa hiyo, shangwe na uzito wa uchumba utatimiza kusudi lenye kuheshimika hao wawili wakaribiapo ndoa, ambayo ina shangwe na uzito hata zaidi.—Mithali 5:18, 19; Waefeso 5:33.

[Maelezo ya Chini]

a Katika jamii fulani wazazi bado hupanga uchumba wa watoto wao. Huenda hilo likafanywa wakati fulani kabla hao wawili hawajakuwa tayari kuoana. Kwa wakati huo wao hutambuliwa kama waliochumbiana, au walioposana, ingawa hawajaoana bado.

b Ona vitabu Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, sura ya 28-32, na Siri ya Kupata Furaha ya Familia, sura ya 2, vilivyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki