Marko
15 Na mara hiyo kwenye pambazuko makuhani wakuu pamoja na wanaume wazee na waandishi, hata Sanhedrini yote, wakaendesha ushauriano, nao wakamfunga Yesu na kumwongoza na kumkabidhi kwa Pilato. 2 Kwa hiyo Pilato akamtokezea swali: “Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?” Kwa kumjibu akasema: “Wewe mwenyewe wasema hilo.” 3 Lakini makuhani wakuu wakaendelea kumshtaki juu ya mambo mengi. 4 Sasa Pilato akaanza kumuuliza tena, akisema: “Je, huna jibu la kutoa? Ona ni mashtaka mangapi wanaleta dhidi yako.” 5 Lakini Yesu hakutoa jibu zaidi, hivi kwamba Pilato akaanza kustaajabu.
6 Basi, kutoka msherehekeo hadi msherehekeo alikuwa na kawaida ya kuwafungulia mfungwa mmoja, ambaye waliomba kwa bidii wapewe. 7 Wakati huo kulikuwa na aliyeitwa kwa kawaida Baraba akiwa katika vifungo pamoja na wachochezi wa uasi, ambao katika uchochezi wao wa uasi walikuwa wamefanya uuaji-kimakusudi. 8 Kwa hiyo umati ukapanda kuja na kuanza kufanya ombi la bidii kulingana na lile alilokuwa na kawaida ya kuufanyia. 9 Pilato akawajibu, akisema: “Mwataka mimi niwafungulie mfalme wa Wayahudi?” 10 Kwa maana alijua kwamba ni kwa sababu ya husuda makuhani wakuu walikuwa wamemkabidhi kwake. 11 Lakini makuhani wakuu wakauchochea umati ili umfanye awafungulie Baraba, badala yake. 12 Tena kwa kujibu Pilato alikuwa akiwaambia: “Basi, nitafanya nini na yeye mmwitaye mfalme wa Wayahudi?” 13 Mara nyingine tena wakapaaza kilio: “Mtundike mtini!” 14 Lakini Pilato akaendelea kuwaambia: “Kwani, alifanya jambo gani baya?” Bado wao wakapaaza kilio hata zaidi: “Mtundike mtini!” 15 Ndipo Pilato, akitaka kuutosheleza umati, akawafungulia Baraba, na, baada ya kufanya Yesu apigwe mijeledi, akamkabidhi atundikwe mtini.
16 Sasa askari-jeshi wakamwongoza kumwingiza uani, yaani, katika ikulu ya gavana; nao wakaita kikosi chote cha askari pamoja, 17 nao wakampamba kwa vazi la zambarau na kusuka taji la miiba wakaliweka juu yake. 18 Nao wakaanza kumsalimu: “Siku njema, wewe Mfalme wa Wayahudi!” 19 Pia, wakawa wakimpiga kichwani kwa tete na kumtemea mate na, wakikunja magoti yao, wakawa wakimsujudia. 20 Mwishowe, walipokuwa wamemfanyia ucheshi, wakamvua lile vazi la zambarau na kumvisha mavazi yake ya nje. Nao wakamwongoza atoke ili wamtundike mtini. 21 Pia, wakashurutisha mpita-njia kufanya utumishi, Simoni fulani wa Kirene, aliyekuwa akija kutoka mashambani, baba ya Aleksanda na Rufo, ili auchukue mti wake wa mateso.
22 Kwa hiyo wakamleta mahali pale Golgotha, ambalo humaanisha, litafsiriwapo, Mahali pa Fuvu la Kichwa. 23 Hapa wakajaribu kumpa divai iliyotiwa dawa ya kulevya ya manemane, lakini hakuipokea. 24 Nao wakamtundika mtini na kugawanya mavazi yake ya nje kwa kupiga kura juu yayo kuhusu nani achukue nini. 25 Sasa ilikuwa saa ya tatu, nao wakamtundika mtini. 26 Na mwandiko wa shtaka dhidi yake uliandikwa juu, “Mfalme wa Wayahudi.” 27 Zaidi ya hayo, walitundika mtini wapokonyaji wawili pamoja naye, mmoja kwenye upande wake wa kuume na mmoja kwenye upande wake wa kushoto. 28 —— 29 Na wale waliokuwa wakipitia hapo walikuwa wakisema naye kwa maneno yenye kuudhi, wakitikisa vichwa vyao na kusema: “Po! Wewe mtaka-kuangusha chini hekalu na mjenzi walo katika muda wa siku tatu, 30 jiokoe mwenyewe kwa kuteremka kutoka kwenye mti wa mateso.” 31 Kwa namna kama hiyo pia makuhani wakuu walikuwa wakifanya ucheshi miongoni mwao wenyewe pamoja na waandishi na kusema: “Wengine aliokoa; mwenyewe hawezi kujiokoa! 32 Acheni Kristo Mfalme wa Israeli ateremke sasa kutoka kwenye mti wa mateso, ili tupate kuona na kuamini.” Hata wale waliotundikwa mtini pamoja naye walikuwa wakimshutumu.
33 Ilipokuwa saa ya sita giza likawa juu ya nchi yote hadi saa ya tisa. 34 Na kwenye saa ya tisa Yesu akapaaza kilio kwa sauti kubwa: “Eli, Eli, lama sabakthani?” ambayo humaanisha, yatafsiriwapo: “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniachilia mbali?” 35 Na baadhi ya wale waliosimama karibu, waliposikia hilo, wakaanza kusema: “Ona! Anamwita Eliya.” 36 Lakini mtu fulani akakimbia, akalowesha sponji kwa divai iliyochacha, akaiweka juu ya tete, na kuanza kumnywesha, akisema: “Acheni iwe hivyo kwake! Acheni tuone kama Eliya aja kumshusha chini.” 37 Lakini Yesu akatoa kilio kikubwa akaisha. 38 Na pazia la patakatifu likapasuliwa vipande viwili kutoka juu hadi chini. 39 Sasa, wakati yule ofisa-jeshi aliyekuwa amesimama kando akimtazama alipoona alikuwa ameisha chini ya hali hizo, akasema: “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
40 Kulikuwa pia na wanawake wakiona kwa umbali, miongoni mwao Maria Magdalene na vilevile Maria mama ya Yakobo Mdogo na Yosesi, na Salome, 41 waliokuwa na kawaida ya kuandamana naye na kumhudumia alipokuwa katika Galilaya, na wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja wakipanda pamoja naye hadi Yerusalemu.
42 Sasa kwa kuwa ilikuwa jioni-jioni, na kwa kuwa ilikuwa Matayarisho, yaani, ile siku ya kabla ya sabato, 43 kukaja Yosefu wa Arimathea, mshiriki mwenye kusifika wa Baraza, ambaye yeye mwenyewe pia alikuwa akiungojea ufalme wa Mungu. Akajipa moyo kuingia mbele ya Pilato na kuomba apewe mwili wa Yesu. 44 Lakini Pilato akataka kujua kama alikuwa mfu tayari, na, akiita yule ofisa-jeshi kwake, akamuuliza kama tayari alikuwa amekufa. 45 Kwa hiyo baada ya kuhakikisha kutoka kwa huyo ofisa-jeshi, akampa Yosefu hiyo maiti. 46 Basi akanunua kitani bora na kumshusha chini, akamviringisha katika kitani bora na kumlaza katika kaburi lililokuwa limechimbwa katika tungamo-mwamba; naye akabingirisha jiwe hata kwenye mlango wa lile kaburi la ukumbusho. 47 Lakini Maria Magdalene na Maria mama wa Yosesi wakaendelea kutazama mahali alipokuwa amelazwa.