Luka
Kulingana na Luka
1 Kwa kuwa wengi wamechukua daraka la kutunga taarifa ya mambo ya hakika yanayopewa usadiki kamili miongoni mwetu, 2 sawa na vile wale ambao tangu mwanzo walikuwa mashahidi wa kujionea na mahadimu wa ujumbe walivyotuletea haya, 3 mimi pia niliazimia, kwa sababu nimefuatisha kwa uangalifu mambo yote tangu awali kwa usahihi, kukuandikia hayo kwa utaratibu wenye kufuatana vizuri, Theofilo mtukuzwa zaidi, 4 ili upate kujua kabisa uhakika wa mambo ambayo umefundishwa kwa mdomo.
5 Siku za Herode, mfalme wa Yudea, ilitukia kukawa kuhani fulani aliyeitwa jina Zekaria wa mgawanyo wa Abiya, naye alikuwa na mke kutoka kwa mabinti za Aroni, na jina lake lilikuwa Elizabeti. 6 Wote wawili walikuwa waadilifu mbele ya Mungu kwa sababu ya kutembea bila lawama kwa kupatana na amri zote na matakwa ya kisheria ya Yehova. 7 Lakini walikuwa hawana mtoto, kwa sababu Elizabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wamesonga sana katika miaka.
8 Basi alipokuwa akitenda akiwa kuhani katika mgawo wa mgawanyo wake mbele ya Mungu, 9 kulingana na desturi ya kisherehe ya cheo cha kikuhani ikawa zamu yake kutoa uvumba alipoingia katika patakatifu pa Yehova; 10 na umati wote wa watu ulikuwa ukisali nje katika saa ya kutoa uvumba. 11 Malaika wa Yehova akaonekana kwake, akiwa amesimama kwenye upande wa kuume wa madhabahu ya uvumba. 12 Lakini Zekaria akawa mwenye kutaabika kwa hilo jambo aliloona, na hofu ikamwingia. 13 Hata hivyo, malaika akamwambia: “Usiwe na hofu, Zekaria, kwa sababu dua yako imesikiwa kwa kupendelewa, na mke wako Elizabeti atakuwa mama ya mwana wako, nawe utaita jina lake Yohana. 14 Nawe utakuwa na shangwe na mteremo mkubwa, na wengi watashangilia juu ya uzawa wake; 15 kwa maana atakuwa mkubwa mbele ya Yehova. Lakini lazima asinywe divai na kinywaji kikali hata kidogo, naye atajazwa roho takatifu moja kwa moja tangu katika tumbo la uzazi la mama yake; 16 na wengi wa wana wa Israeli atawarudisha kwa Yehova Mungu wao. 17 Pia, atakwenda mbele yake kwa roho na nguvu ya Eliya, ili kurudisha mioyo ya akina baba kwa watoto na wale wasiotii kwenye hekima itumikayo ya walio waadilifu, ili kuweka tayari kwa ajili ya Yehova watu waliotayarishwa.”
18 Naye Zekaria akamwambia malaika: “Nitakuwaje na uhakika juu ya hili? Kwa maana mimi ni mwenye umri mkubwa na mke wangu amesonga sana katika miaka.” 19 Kwa kujibu malaika akamwambia: “Mimi ni Gabrieli, asimamaye karibu mbele ya Mungu, nami nilitumwa kusema na wewe na kukutangazia habari njema ya mambo hayo. 20 Lakini, tazama! utakuwa kimya na usiweze kusema hadi siku mambo hayo yatendekapo, kwa sababu hukuamini maneno yangu, ambayo yatatimizwa wakati wayo uliowekwa.” 21 Wakati huohuo watu wakaendelea kumngoja Zekaria, nao wakaanza kustaajabia kukawia kwake katika patakatifu. 22 Lakini alipotoka hakuweza kusema na wao, nao wakafahamu kwamba alikuwa amepata tu kuona ono lizidilo nguvu za asili katika patakatifu; naye akawa anafuliza kuwatolea ishara, lakini akaendelea kuwa bubu. 23 Basi, siku za utumishi wake wa watu wote zilipotimia, akaenda zake nyumbani kwake.
24 Lakini baada ya siku hizo Elizabeti mke wake akawa mwenye mimba; naye akafuliza kujitenga mwenyewe kwa miezi mitano, akisema: 25 “Hivi ndivyo Yehova ameshughulika nami siku hizi wakati amenipa uangalifu wake ili kuondolea mbali shutumu langu miongoni mwa watu.”
26 Katika mwezi wake wa sita malaika Gabrieli alitumwa kutoka kwa Mungu hadi jiji moja la Galilaya liitwalo jina Nazareti, 27 kwa bikira aliyeposwa na mwanamume aitwaye jina Yosefu wa nyumba ya Daudi; na jina la huyo bikira lilikuwa Maria. 28 Na Gabrieli alipoingia mbele yake akasema: “Siku njema, mwenye kupendelewa sana, Yehova yuko pamoja na wewe.” 29 Lakini Maria akashtushwa sana na huo usemi na kuanza kuwazawaza hiyo ingeweza kuwa ni salamu ya namna gani. 30 Kwa hiyo malaika akamwambia: “Usiwe na hofu, Maria, kwa maana umepata upendeleo kwa Mungu; 31 na, tazama! utachukua mimba katika tumbo lako la uzazi na kuzaa mwana, nawe itakupasa kumwita jina lake Yesu. 32 Huyu atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Aliye Juu Zaidi Sana; na Yehova Mungu atampa kiti cha ufalme cha Daudi baba yake, 33 naye atatawala akiwa mfalme juu ya nyumba ya Yakobo milele, na hakutakuwa na mwisho wa ufalme wake.”
34 Lakini Maria akamwambia malaika: “Hilo litakuwaje, kwa kuwa huwa sifanyi ngono na mwanamume?” 35 Kwa kujibu malaika akamwambia: “Roho takatifu itakuja juu yako, na nguvu ya Aliye Juu Zaidi Sana itakufunika kivuli. Kwa sababu hiyo pia kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Na, tazama! Elizabeti jamaa yako yeye mwenyewe pia amechukua mimba ya mwana, katika uzee wake, na huu ni mwezi wa sita kwake, yeye ambaye huitwa kwa kawaida mwanamke tasa; 37 kwa sababu kwa Mungu hakuna tangazo lolote litakalokuwa lisilowezekana.” 38 Ndipo Maria akasema: “Tazama! Msichana mtumwa wa Yehova! Na litendeke kwangu kulingana na tangazo lako.” Ndipo malaika akaondoka kwake.
39 Basi Maria akainuka katika siku hizo akaenda hima katika nchi ya milima-milima, hadi jiji moja la Yuda, 40 naye akaingia nyumbani mwa Zekaria akamsalimu Elizabeti. 41 Basi, Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, kile kitoto kichanga katika tumbo lake la uzazi kikaruka; na Elizabeti akajazwa roho takatifu, 42 naye akapaaza sauti kwa kilio kikubwa na kusema: “Mbarikiwa ni wewe miongoni mwa wanawake, na lenye kubarikiwa ni tunda la tumbo lako la uzazi! 43 Basi ni jinsi gani kwamba pendeleo hili ni langu, nijiwe na mama ya Bwana wangu? 44 Kwa maana, tazama! mvumo wa salamu yako ulipoangukia masikio yangu, kitoto kichanga katika tumbo langu la uzazi kikaruka kwa mteremo mkubwa. 45 Mwenye furaha pia ni yeye ambaye aliamini, kwa sababu kutakuwa utimilizo kamili wa mambo yale aliyoambiwa kutoka kwa Yehova.”
46 Na Maria akasema: “Nafsi yangu yamtukuza Yehova, 47 na roho yangu haiwezi kuepuka kuwa na shangwe mno katika Mungu Mwokozi wangu; 48 kwa sababu ametazama juu ya cheo cha chini cha msichana wake mtumwa. Kwa maana, tazama! tangu sasa na kuendelea vizazi vyote vitanitamka mimi kuwa mwenye furaha; 49 kwa sababu Aliye Mwenye nguvu amenifanyia vitendo vikubwa, nalo ni takatifu jina lake; 50 na kwa vizazi baada ya vizazi rehema yake iko juu ya wale ambao humhofu. 51 Amefanya kwa uweza kwa mkono wake, ametawanya kotekote wale wenye kiburi katika kusudio la mioyo yao. 52 Ameshusha watu wa uwezo kutoka viti vya ufalme na kukweza watu wa hali ya chini; 53 ameshibisha kabisa wenye njaa kwa vitu vyema na wale waliokuwa na mali amewaacha waende bila kitu. 54 Amekuja kusaidia Israeli mtumishi wake, kukumbuka rehema, 55 sawa na vile alivyowaambia baba zetu wa zamani, Abrahamu na mbegu yake, milele.” 56 Kisha Maria akakaa pamoja naye karibu miezi mitatu, akarudi nyumbani kwake mwenyewe.
57 Sasa wakati ukawadia wa Elizabeti kuzaa, naye akawa mama ya mwana. 58 Na majirani na jamaa zake wakasikia kwamba Yehova alikuwa ametukuza rehema yake kwake, nao wakaanza kushangilia pamoja naye. 59 Na katika siku ya nane wakaja kumtahiri huyo mtoto mchanga, nao walitaka kumwita kwa jina la baba yake, Zekaria. 60 Lakini mama yake akajibu akasema: “La, hasha! bali hakika ataitwa Yohana.” 61 Ndipo wakamwambia: “Hakuna yeyote miongoni mwa jamaa zako aitwaye kwa jina hilo.” 62 Ndipo wakaanza kuuliza baba yake kwa ishara alilotaka aitwe. 63 Naye akaomba bamba na kuandika: “Yohana ndilo jina lake.” Ndipo wote wakastaajabu. 64 Mara hiyo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake ukalegea naye akaanza kusema, akimbariki Mungu. 65 Na hofu ikawa juu ya wote wale wenye kuishi katika ujirani wao; na katika nchi yote ya milima-milima ya Yudea mambo yote hayo yakaanza kuzungumzwa pande zote, 66 na wote waliosikia wakalitia katika mioyo yao, wakisema: “Kwa kweli mtoto mchanga huyu atakuwa wa namna gani?” Kwa maana kwa kweli mkono wa Yehova ulikuwa pamoja naye.
67 Na Zekaria baba yake akajazwa roho takatifu, naye akatoa unawbii, akisema: 68 “Mbarikiwa awe Yehova Mungu wa Israeli, kwa sababu ameelekeza uangalifu wake na kufanya ukombozi kuelekea watu wake. 69 Naye ametuinulia pembe ya wokovu katika nyumba ya Daudi mtumishi wake, 70 sawa na vile, kupitia kinywa cha manabii wake watakatifu tangu zamani za kale, amesema 71 juu ya wokovu kutoka kwa maadui wetu na kutoka katika mkono wa wale wote wanaotuchukia; 72 kufanya rehema kuhusiana na baba zetu wa zamani na kukumbuka agano lake takatifu, 73 kiapo ambacho aliapa kwa Abrahamu baba yetu wa zamani, 74 kutupa sisi, baada ya kuokolewa kutoka katika mikono ya maadui, pendeleo la kumtolea utumishi mtakatifu bila hofu 75 kwa uaminifu-mshikamanifu na uadilifu mbele yake siku zetu zote. 76 Lakini kwa habari yako, mtoto mchanga, utaitwa nabii wa Aliye Juu Zaidi Sana, kwa maana utakwenda kwa kutangulia mbele ya Yehova ili kufanya njia zake tayari, 77 kuwapa watu wake ujuzi wa wokovu kwa msamaha wa dhambi zao, 78 kwa sababu ya huruma nyororo ya Mungu wetu. Kwa huruma hii pambazuko litatuzuru sisi kutoka juu, 79 kuwapa nuru wale wanaokaa katika giza na katika kivuli cha kifo, kuelekeza kwa ufanisi miguu yetu katika njia ya amani.”
80 Na huyo mtoto mchanga akaendelea kukua na kupata nguvu katika roho, naye akakaa katika majangwa hadi siku ya kujionyesha waziwazi kwa Israeli.