Luka
2 Basi katika siku hizo agizo kutoka kwa Kaisari Augusto likatoka kwamba dunia yote inayokaliwa ipate kusajiliwa; 2 (usajili huu wa kwanza ulitendeka wakati Kirenio alipokuwa gavana wa Siria;) 3 na watu wote wakaanza kusafiri kwenda kusajiliwa, kila mmoja kwenye jiji lake mwenyewe. 4 Yosefu pia alipanda kwenda kutoka Galilaya, kutoka jiji la Nazareti, akaingia Yudea, kwenye jiji la Daudi, liitwalo Bethlehemu, kwa sababu ya yeye kuwa mshiriki wa nyumba na familia ya Daudi, 5 ili apate kusajiliwa pamoja na Maria, aliyekuwa ameozwa kama ilivyoahidiwa, wakati huu akiwa na mimba kubwa. 6 Walipokuwa huko, siku zikakamilika apate kuzaa. 7 Naye akamzaa mwana wake, mzaliwa wa kwanza, naye akamfunga vitambaa vya nguo na kumlaza katika hori, kwa sababu kulikuwa hakuna mahali kwa ajili yao katika chumba cha makao.
8 Katika nchi hiyohiyo kulikuwako pia wachungaji wakiishi nje na wakishika malindo usiku juu ya makundi yao. 9 Na kwa ghafula malaika wa Yehova akasimama kando yao, na utukufu wa Yehova ukamulika kuwazunguka, nao wakawa wenye hofu sana. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiwe na hofu, kwa maana, tazama! ninawatangazia nyinyi habari njema ya shangwe kubwa ambayo watu wote watakuwa nayo, 11 kwa sababu kumezaliwa kwenu leo Mwokozi, ambaye, ni Kristo Bwana, katika jiji la Daudi. 12 Na hii ndiyo ishara kwenu: Mtapata kitoto kichanga kimefungwa katika vitambaa vya nguo na kikiwa kimelala katika hori.” 13 Na kwa ghafula kukaja kuwa pamoja na yule malaika umati wa jeshi la kimbingu, ukimsifu Mungu na kusema: 14 “Utukufu katika mahali pa juu kwa Mungu, na juu ya dunia amani miongoni mwa watu wa nia njema.”
15 Kwa hiyo malaika walipokuwa wameondoka kwao kuingia mbinguni, wachungaji wakaanza kusemezana: “Na twende moja kwa moja hadi Bethlehemu tukaone jambo hili ambalo limetendeka, ambalo Yehova ametujulisha.” 16 Nao wakaenda hima wakamkuta Maria vilevile Yosefu, na kile kitoto kichanga kikiwa kimelala katika hori. 17 Walipokiona, wakajulisha juu ya usemi uliokuwa umesemwa kuhusu mtoto mchanga huyo. 18 Na wote waliosikia wakastaajabu juu ya mambo waliyoambiwa na wachungaji, 19 lakini Maria akaanza kuzihifadhi semi hizo zote, akikata kauli moyoni mwake. 20 Basi wachungaji wakarudi, wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa ajili ya mambo yote waliyoyasikia na kuyaona, sawa na walivyokuwa wameambiwa hayo.
21 Basi siku nane zilipokamilika ili kumtahiri, jina lake likaitwa pia Yesu, lile jina lililoitwa na malaika kabla ya yeye kuchukuliwa mimba katika tumbo la uzazi.
22 Pia, siku za kuwatakasa wao kulingana na sheria ya Musa zilipokamilika, wakamleta Yesu hadi Yerusalemu ili kumtoa kwa Yehova, 23 sawa na vile imeandikwa katika sheria ya Yehova: “Kila wa kiume anayefungua tumbo la uzazi lazima aitwe mtakatifu kwa Yehova,” 24 na kutoa dhabihu kulingana na yanayosemwa katika sheria ya Yehova: “Jozi moja ya njiwa-tetere au hua wachanga wawili.”
25 Na, tazama! palikuwa na mtu mmoja katika Yerusalemu aliyeitwa jina Simeoni, na mwanamume huyu alikuwa mwadilifu na mwenye kumstahi Mungu, akingojea liwazo la Israeli, na roho takatifu ilikuwa juu yake. 26 Zaidi ya hilo, alikuwa amefunuliwa kimungu na roho takatifu kwamba hangeona kifo kabla ya kuwa amemwona Kristo wa Yehova. 27 Akaja sasa katika hekalu chini ya nguvu ya roho; na wazazi walipomwingiza mtoto mchanga Yesu ili kufanya kwa ajili yake kulingana na zoea la kidesturi la sheria, 28 Simeoni mwenyewe akampokea mtoto mikononi mwake akambariki Mungu na kusema: 29 “Sasa, Bwana Mwenye Enzi Kuu, unamwacha mtumwa wako aende huru katika amani kulingana na tangazo lako; 30 kwa sababu macho yangu yameona njia yako ya kuokoa 31 ambayo umefanya tayari mbele ya vikundi vyote vya watu, 32 nuru ya kuondoa shela kwa mataifa na utukufu wa watu wako Israeli.” 33 Na baba na mama yake wakaendelea kustaajabia mambo yaliyokuwa yakisemwa juu yake. 34 Pia, Simeoni akawabariki wao, lakini akamwambia Maria mama yake: “Tazama! Huyu amewekwa kwa ajili ya kuanguka na kuinuka tena kwa wengi katika Israeli na kuwa ishara itakayonenewa vibaya 35 (ndiyo, upanga mrefu utapenyezwa ndani ya nafsi yako mwenyewe), ili mawazo ya mioyo mingi yapate kufunuliwa.”
36 Basi kulikuwako Ana nabii wa kike, binti ya Fanueli, wa kabila la Asheri (mwanamke huyu alikuwa amesonga sana katika miaka, na alikuwa ameishi pamoja na mume kwa miaka saba kutoka ubikira wake, 37 naye sasa alikuwa mjane mwenye umri wa miaka themanini na minne), ambaye alikuwa hakosi kamwe kuwa katika hekalu, akitoa utumishi mtakatifu usiku na mchana kwa mifungo na dua. 38 Na saa hiyohiyo akaja karibu akaanza kumshukuru Mungu akisema juu ya huyo mtoto kwa wale wote wenye kungojea ukombozi wa Yerusalemu.
39 Kwa hiyo walipokuwa wametekeleza mambo yote kulingana na sheria ya Yehova, wakarudi kuingia Galilaya kwenye jiji la kwao wenyewe la Nazareti. 40 Na huyo mtoto mchanga akaendelea kukua na kupata nguvu, akijawa na hekima, na upendeleo wa Mungu ukaendelea kuwa juu yake.
41 Basi wazazi wake walikuwa wenye desturi ya kwenda Yerusalemu mwaka hadi mwaka kwa msherehekeo wa sikukuu ya kupitwa. 42 Na alipokuwa mwenye umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kulingana na desturi ya msherehekeo 43 wakazikamilisha siku. Lakini walipokuwa wakirudi, mvulana Yesu alibaki nyuma Yerusalemu, na wazazi wake hawakutambua hilo. 44 Wakidhani kwamba alikuwa katika andamano lenye kusafiri pamoja, walimaliza umbali wa siku moja kisha wakaanza kumtafuta-tafuta kwa bidii miongoni mwa jamaa zao na wanaojuana nao. 45 Lakini, walipokosa kumpata, wakarudi hadi Yerusalemu, wakimtafuta-tafuta kwa bidii ya uendelevu. 46 Basi, baada ya siku tatu wakampata katika hekalu, ameketi katikati ya walimu na akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Lakini wote wale waliokuwa wakimsikiliza walikuwa katika mshangao wa daima juu ya uelewevu wake na majibu yake. 48 Basi walipomwona wakastaajabu, na mama yake akamwambia: “Mtoto, kwa nini ulitutenda kwa njia hii? Tazama, baba yako na mimi tukiwa na taabu ya akilini tumekuwa tukikutafuta.” 49 Lakini akawaambia: “Kwa nini iliwabidi kunitafuta? Je, hamkujua kwamba ni lazima mimi niwe katika nyumba ya Baba yangu?” 50 Hata hivyo, hawakufahamu usemi aliowaambia.
51 Naye akateremka kwenda pamoja nao akaja hadi Nazareti, naye akaendelea kuwa mwenye kujitiisha kwao. Pia, mama yake aliweka kwa uangalifu semi zote hizi moyoni mwake. 52 Na Yesu akafuliza kufanya maendeleo katika hekima na ukuzi wa kimwili na katika upendeleo pamoja na Mungu na wanadamu.