Wagalatia
3 Enyi Wagalatia wasio na akili, ni nani huyo aliyewaleta nyinyi chini ya uvutano mwovu, nyinyi ambao machoni penu Yesu Kristo alionyeshwa waziwazi akiwa ametundikwa mtini? 2 Hili peke yake nataka kujifunza kutoka kwenu: Je, mlipokea roho kwa sababu ya kazi za sheria au kwa sababu ya kusikia kwa njia ya imani? 3 Je, nyinyi hamna akili kiasi hicho? Baada ya kuanza katika roho sasa mnakuwa wenye kutimilizwa katika mwili? 4 Je, mlipatwa na mateso mengi sana bila kusudi? Ikiwa kwa kweli ilikuwa bila kusudi lolote. 5 Kwa hiyo, yeye awapaye nyinyi roho na kufanya kazi zenye nguvu miongoni mwenu, je, yeye hufanya hivyo kwa sababu ya kazi za sheria au kwa sababu ya kusikia kwa njia ya imani? 6 Kama vile Abrahamu “alivyoweka imani katika Yehova, na ikahesabiwa kwake kuwa uadilifu.”
7 Hapana shaka mwajua kwamba wale washikamanao sana na imani ndio wale walio wana wa Abrahamu. 8 Sasa Andiko, likitangulia kuona kwamba Mungu angetangaza watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa sababu ya imani, lilitangaza habari njema kimbele kwa Abrahamu, yaani: “Kupitia wewe mataifa yote yatabarikiwa.” 9 Kwa sababu hiyo wale washikamanao sana na imani wanakuwa wenye kubarikiwa pamoja na Abrahamu mwaminifu.
10 Kwa maana wote wale wategemeao kazi za sheria wako chini ya laana; kwa maana imeandikwa: “Mwenye kulaaniwa ni kila mtu asiyeendelea katika mambo yote yaliyoandikwa katika hati-kunjo ya Sheria kusudi ayafanye.” 11 Zaidi ya hayo, kwamba kwa sheria hakuna yeyote ambaye hutangazwa kuwa mwadilifu kwa Mungu ni dhahiri, kwa sababu “mwadilifu ataishi kwa sababu ya imani.” 12 Sasa Sheria haishikamani sana na imani, bali “yeye azifanyaye hakika ataishi kwa njia yazo.” 13 Kristo kwa kununua alituachilia kutokana na laana ya Sheria kwa kuwa laana badala yetu, kwa sababu imeandikwa: “Mwenye kulaaniwa ni kila mtu aliyeangikwa juu ya mti.” 14 Kusudi lilikuwa kwamba baraka ya Abrahamu ipate kuja kwa ajili ya mataifa kupitia Yesu Kristo, ili tupate kupokea roho iliyoahidiwa kupitia imani yetu.
15 Akina ndugu, nasema kwa kielezi cha kibinadamu: Agano lililohalalishwa, ingawa ni la mwanadamu, hakuna yeyote aliwekaye kando au kuambatisha maongezo kwalo. 16 Sasa ahadi zilisemwa kwa Abrahamu na kwa mbegu yake. Haisemi: “Na kwa hizo mbegu,” kama katika kisa cha nyingi za namna hiyo, bali kama katika kisa cha moja: “Na kwa mbegu yako,” ambaye ni Kristo. 17 Zaidi, mimi nasema hili: Kuhusu agano lililohalalishwa na Mungu hapo kwanza, Sheria ambayo imekuja kuwapo miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kubatilisha ahadi. 18 Kwa maana ikiwa urithi ni kwa sababu ya sheria, hauwi tena kwa sababu ya ahadi; lakini Mungu amempa huo Abrahamu kwa fadhili kupitia ahadi.
19 Basi, kwa nini Sheria? Iliongezwa kufanya mikiuko-sheria iwe dhahiri, mpaka mbegu iwasili ambayo kwayo ahadi ilikuwa imetolewa; na ilipitishwa kupitia kwao malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20 Sasa hakuna mpatanishi ambapo ni mtu mmoja tu ahusika, bali Mungu ni mmoja tu. 21 Kwa hiyo, je, Sheria ni dhidi ya ahadi za Mungu? Hilo lisitukie kamwe! Kwa maana ikiwa sheria ingalitolewa iwezayo kutoa uhai, kwa kweli uadilifu ungalikuwa umekuwa kwa njia ya sheria. 22 Lakini Andiko lilikabidhi mambo yote pamoja kwenye kifungo cha dhambi, ili ahadi inayotokana na imani kuelekea Yesu Kristo ipate kupewa kwa wale wanaodhihirisha imani.
23 Hata hivyo, kabla ya imani kuwasili, tulikuwa tukilindwa chini ya sheria, tukikabidhiwa pamoja kifungoni, tukitazama kwenye imani iliyokusudiwa kufunuliwa. 24 Kwa sababu hiyo Sheria imekuwa mfunzi wetu ikiongoza kwa Kristo, ili tupate kutangazwa kuwa waadilifu kwa sababu ya imani. 25 Lakini sasa kwa kuwa imani imewasili, sisi hatuko tena chini ya mfunzi.
26 Kwa kweli, nyinyi nyote ni wana wa Mungu kupitia imani yenu katika Kristo Yesu. 27 Kwa maana nyinyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. 28 Hakuna Myahudi wala Mgiriki, hakuna mtumwa wala mtu huru, hakuna wa kiume wala wa kike; kwa maana nyinyi nyote ni mtu mmoja katika muungano na Kristo Yesu. 29 Zaidi ya hayo, ikiwa nyinyi ni wa Kristo, kwa kweli nyinyi ni mbegu ya Abrahamu, warithi kuhusiana na ahadi.