Wagalatia
5 Kristo alituweka huru tuwe na uhuru wa namna hiyo. Kwa hiyo simameni thabiti, na msijiache wenyewe kufungwa tena katika nira ya utumwa.
2 Oneni! Mimi, Paulo, ninawaambia nyinyi kwamba mkiwa wenye kutahiriwa, Kristo atakuwa asiye na manufaa kwenu. 3 Zaidi ya hayo, natoa ushahidi tena kwa kila mtu anayetahiriwa kwamba yuko chini ya wajibu kuifanya Sheria yote. 4 Mwaachanishwa na Kristo, hata mwe nyinyi ni nani ambao mwajaribu kutangazwa kuwa waadilifu kwa njia ya sheria; mmeangukia mbali kutoka kwenye fadhili yake isiyostahiliwa. 5 Kwa upande wetu sisi kwa njia ya roho tunangojea kwa hamu uadilifu uliotumainiwa kama tokeo la imani. 6 Kwa maana kwa habari ya Kristo Yesu tohara haina thamani yoyote wala kutotahiriwa, ila imani itendayo kupitia upendo ina thamani.
7 Nyinyi mlikuwa mkikimbia vema. Ni nani aliyewazuia msifulize kuitii kweli? 8 Namna hii ya kushawisha si kutoka kwa Yule anayewaita nyinyi. 9 Chachu kidogo huchachusha donge lote. 10 Mimi nina uhakika juu yenu nyinyi ambao mko katika muungano na Bwana kwamba hamtakuja kufikiri tofauti; lakini anayewasababishia nyinyi taabu atachukua hukumu yake, hata awe nani. 11 Kwa habari yangu, akina ndugu, ikiwa bado ninahubiri tohara, kwa nini bado ninanyanyaswa? Basi, hakika kipingamizi chenye kukwaza cha mti wa mateso kimebatilishwa. 12 Mimi naona laiti watu wanaojaribu kuwapindua nyinyi hata wangejifanya wahasiwe wao wenyewe.
13 Bila shaka, nyinyi mliitiwa uhuru, akina ndugu; ila tu msitumie uhuru huu kuwa kichocheo kwa ajili ya mwili, bali kupitia upendo mtumikiane kama watumwa. 14 Kwa maana Sheria nzima husimama ikiwa imetimizwa katika usemi mmoja, yaani: “Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe.” 15 Lakini, ikiwa mnafuliza kuumana na kunyafuana, jihadharini kwamba msipate kuangamizana mtu na mwenzake.
16 Lakini nasema, Fulizeni kutembea kwa roho na hamtatekeleza tamaa ya kimwili hata kidogo. 17 Kwa maana mwili katika tamaa yao ni dhidi ya roho, na roho dhidi ya mwili; kwa maana hivi vyapingana, hivi kwamba mambo yaleyale ambayo mngependa kufanya hamyafanyi. 18 Zaidi ya hilo, ikiwa mnaongozwa na roho, nyinyi hamko chini ya sheria.
19 Sasa kazi za mwili ni dhahiri, nazo ni uasherati, ukosefu wa usafi, mwenendo mlegevu, 20 ibada ya sanamu, zoea la uwasiliani-roho, uadui, zogo, wivu, hasira za ghafula, magomvi, migawanyiko, mafarakano, 21 husuda, vipindi vya kulewa, sherehe zenye kelele za ulevi na ulafi, na mambo kama haya. Kuhusu mambo hayo mimi ninawaonya nyinyi kimbele, jinsi ileile kama nilivyowaonya kimbele, kwamba wale wazoeao kufanya mambo ya namna hiyo hawatarithi ufalme wa Mungu.
22 Kwa upande mwingine, matunda ya roho ni upendo, shangwe, amani, ustahimilivu, fadhili, wema, imani, 23 upole, kujidhibiti. Dhidi ya mambo ya namna hiyo hakuna sheria yoyote. 24 Zaidi ya hayo, wale walio wa Kristo Yesu walitundika mtini mwili pamoja na harara na tamaa zao.
25 Ikiwa tunaishi kwa roho, acheni sisi tuendelee kutembea kwa utaratibu pia kwa roho. 26 Acheni sisi tusiwe wenye majisifu ya bure, wenye kuchochea shindano juu ya mtu na mwenzake, tukihusudiana.