Wagalatia
6 Akina ndugu, hata ingawa mtu achukua hatua fulani isiyo ya kweli kabla ya yeye kuijua, nyinyi mlio na sifa za ustahili wa kiroho jaribuni kumrekebisha upya mtu wa namna hiyo katika roho ya upole, huku kila mmoja wenu akifuliza kujiangalia mwenyewe, kwa kuhofu wewe pia usipate kushawishwa. 2 Endeleeni kuchukuliana mizigo yenye kulemea, na hivyo kutimiza sheria ya Kristo. 3 Kwa maana ikiwa yeyote afikiri yeye ni kitu wakati yeye si kitu, anadanganya akili yake mwenyewe. 4 Lakini acheni kila mmoja athibitishe kazi yake mwenyewe ni nini, na ndipo atakuwa na sababu ya mchachawo kwa habari yake mwenyewe peke yake, na si kwa kujilinganisha na mtu yule mwingine. 5 Kwa maana kila mmoja atachukua mzigo wake mwenyewe.
6 Zaidi ya hayo, acheni yeyote afundishwaye neno kwa mdomo ashiriki katika mambo mema yote pamoja naye atoaye fundisho la mdomo la namna hiyo.
7 Msiongozwe vibaya: Mungu si wa kudhihakiwa. Kwa maana lolote lile mtu analopanda, hilo atavuna pia; 8 kwa sababu yeye anayepanda katika mwili wake atavuna ufisadi kutokana na mwili wake, lakini yeye anayepanda katika roho atavuna uhai udumuo milele kutokana na roho. 9 Kwa hiyo acheni tusife moyo katika kufanya lililo bora, kwa maana katika majira yapasayo tutavuna ikiwa hatuchoki kabisa. 10 Basi, kwa kweli maadamu tuna wakati wenye kufaa kwa ajili ya hilo, acheni sisi tufanye lililo jema kuelekea wote, lakini hasa kuelekea wale ambao katika imani ni jamaa zetu.
11 Oneni ni kwa herufi zilizo kubwa kadiri gani nimewaandikia nyinyi kwa mkono wangu mwenyewe.
12 Wote wale watakao kufanya mwonekano wa kupendeza katika mwili ndio wale wajaribuo kuwashurutisha nyinyi mpate kutahiriwa, ili tu wasipate kunyanyaswa kwa ajili ya mti wa mateso wa Kristo, Yesu. 13 Kwa maana hata wale wanaotahiriwa wao wenyewe hawashiki Sheria, lakini wataka nyinyi mtahiriwe ili wapate kuwa na sababu ya kujisifu katika mwili wenu. 14 Isitukie hivyo kamwe kwamba mimi nijisifu, ila katika mti wa mateso wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kupitia yeye ulimwengu umetundikwa mtini kwangu na mimi kwa ulimwengu. 15 Kwa maana wala tohara si kitu wala kutotahiriwa, bali kiumbe kipya ndicho kitu. 16 Na wale wote watakaotembea kwa utaratibu kwa kanuni hii ya mwenendo, juu yao iwe amani na rehema, naam, juu ya Israeli wa Mungu.
17 Tangu sasa acheni yeyote asiwe akinitaabisha, kwa maana ninachukua juu ya mwili wangu alama za chapa ya mtumwa za Yesu.
18 Fadhili isiyostahiliwa ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho ambayo nyinyi mwaonyesha, akina ndugu. Ameni.