Wafilipi
3 Mwishowe, ndugu zangu, endeleeni kushangilia katika Bwana. Kuwaandikia nyinyi mambo yaleyale si jambo lenye kunitaabisha, bali ni lenye usalama kwenu.
2 Jihadharini na hao mbwa, jihadharini na wafanyakazi wa ubaya, jihadharini na wale waukatakatao mwili. 3 Kwa maana sisi ndio wale wenye tohara halisi, wanaotoa utumishi mtakatifu kwa njia ya roho ya Mungu na tuna kujisifu kwetu katika Kristo Yesu na hatuna uhakika wetu katika mwili wenye nyama, 4 ijapokuwa mimi, kama kuna yeyote, nina sababu za kuwa na uhakika pia katika mwili.
Ikiwa mtu yeyote mwingine hufikiri ana sababu za kuwa na uhakika katika mwili, mimi ni zaidi: 5 katahiriwa siku ya nane, katokana na ukoo wa familia ya Israeli, wa kabila la Benyamini, Mwebrania aliyezaliwa kutoka kwa Waebrania; kwa habari ya sheria, Farisayo; 6 kwa habari ya bidii, nikilinyanyasa kutaniko; kwa habari ya uadilifu ulio kwa njia ya sheria, mmoja aliyejithibitisha mwenyewe kuwa bila lawama. 7 Lakini vitu vilivyokuwa mapato ya faida kwangu, hivyo nimeviona kuwa hasara kwa sababu ya Kristo. 8 Naam, kama ilivyo, kwa kweli naona vitu vyote kuwa hasara kwa sababu ya thamani iliyo bora zaidi ya ujuzi wa Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa sababu yake nimekubali hasara ya vitu vyote nami naviona kuwa takataka nyingi, ili niweze kupata Kristo 9 na kupatikana katika muungano naye, nikiwa, si na uadilifu wangu mwenyewe, ambao hutokana na sheria, bali ule ambao ni kupitia imani katika Kristo, uadilifu utokao kwa Mungu juu ya msingi wa imani, 10 ili kumjua yeye na nguvu ya ufufuo wake na kushiriki katika mateso yake, kujinyenyekeza mwenyewe hadi kifo kama chake, 11 ili kuona kama kwa vyovyote huenda nikaufikia ufufuo wa mapema zaidi kutoka kwa wafu.
12 Si kwamba tayari nimepokea au tayari nimefanywa kuwa mkamilifu, bali ninafuatia kuona kama pia huenda nikashika lile ambalo kwa ajili yalo mimi pia nimeshikwa na Kristo Yesu. 13 Akina ndugu, bado mimi sijifikirii mwenyewe kuwa nimekwisha kulishika hilo; bali kuna jambo moja juu ya hilo: Nikisahau mambo ya nyuma na kujinyoosha mbele kwenye mambo ya mbele, 14 ninafuatilia sana kuuelekea mradi kwa ajili ya tuzo la mwito wa Mungu wa kwenda juu kwa njia ya Kristo Yesu. 15 Basi, acheni wengi wetu kadiri tulivyo wakomavu, tuwe na mtazamo huu wa akili; na mkiwa na mwelekeo wa akili ulio tofauti katika jambo lolote, Mungu atawafunulia nyinyi mtazamo huo. 16 Kwa vyovyote, kwa kadiri ambayo tumefanya maendeleo, acheni tuendelee kutembea kwa utaratibu katika kawaida hiyohiyo.
17 Kwa muungano iweni waigaji wangu, akina ndugu, na fulizeni kuwaangalia wale wanaotembea katika njia ilinganayo na kielelezo mlicho nacho katika sisi. 18 Kwa maana kuna wengi, nilikuwa na kawaida ya kuwataja mara nyingi lakini sasa nawataja pia kwa kutoa machozi, wanaotembea kama maadui wa mti wa mateso wa Kristo, 19 na mwisho wao ni uangamizo, na mungu wao ni tumbo lao, na utukufu wao huwa katika aibu yao, nao wameweka akili zao juu ya vitu vilivyo juu ya dunia. 20 Kwa habari yetu, uraia wetu uko katika mbingu, ambako kutoka huko pia tunangoja kwa hamu mwokozi, Bwana Yesu Kristo, 21 ambaye ataufanya upya mwili wetu uliotwezwa ili upatanishwe na umbo la mwili wake wenye utukufu kulingana na utendaji wa nguvu aliyo nayo, hata kutiisha vitu vyote kwake mwenyewe.