2 Timotheo
Ya Pili kwa Timotheo
1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kupitia mapenzi ya Mungu kulingana na ahadi ya uhai ulio katika muungano na Kristo Yesu, 2 kwa Timotheo, mtoto mpendwa:
Na kuwe fadhili isiyostahiliwa, rehema, amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Nina shukrani kwa Mungu, ninayemtolea utumishi mtakatifu kama baba zangu wa zamani walivyofanya na nikiwa na dhamiri safi, kwamba siachi kamwe kukukumbuka wewe katika dua zangu, usiku na mchana 4 nikiwa na hamu sana kukuona wewe, nikumbukapo machozi yako, ili nipate kujawa na shangwe. 5 Kwa maana nakumbuka imani iliyo katika wewe isiyo na unafiki wowote, na iliyokaa kwanza katika nyanya yako Loisi na mama yako Eunike, lakini ambayo mimi nina hakika imo pia katika wewe.
6 Kwa sababu hiihii nakukumbusha wewe kuchochea kama moto zawadi ya Mungu iliyo katika wewe kupitia kuwekwa kwa mikono yangu juu yako. 7 Kwa maana Mungu alitupa sisi si roho ya woga, bali ile ya nguvu na ya upendo na ya utimamu wa akili. 8 Kwa hiyo usiwe mwenye kuaibikia ushahidi juu ya Bwana wetu, wala juu yangu mimi mfungwa kwa ajili yake, bali chukua sehemu yako katika kupatwa na uovu kwa ajili ya habari njema kulingana na nguvu ya Mungu. 9 Yeye alituokoa na kutuita kwa wito mtakatifu, si kwa sababu ya kazi zetu, bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na fadhili isiyostahiliwa. Tulipewa hiyo kuhusiana na Kristo Yesu kabla ya nyakati zinazodumu muda mrefu, 10 lakini sasa imefanywa dhahiri kabisa kupitia udhihirisho wa Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha kifo lakini ambaye ametoa nuru juu ya uhai na kutoharibika kupitia habari njema, 11 ambayo kwa ajili yayo mimi niliwekwa rasmi kuwa mhubiri na mtume na mwalimu.
12 Kwa sababu hiihii ninapatwa pia na mambo haya, lakini siaibiki. Kwa maana najua yule ambaye nimeamini, nami nina hakika aweza kulinda kile ambacho nimeweka amana kwake hadi siku hiyo. 13 Fuliza kushika kiolezo cha maneno yenye afya ulichosikia kutoka kwangu pamoja na imani na upendo vinavyohusiana na Kristo Yesu. 14 Amana hii bora ilinde kupitia roho takatifu inayokaa katika sisi.
15 Wajua hili, kwamba watu wote katika wilaya ya Asia wamegeukia mbali kuniacha mimi. Figelo na Hermogenesi ni kati ya hao. 16 Bwana na awaruhusu kuwa na rehema watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu mara nyingi aliniletea kiburudisho, naye hakuwa mwenye kuaibikia minyororo yangu. 17 Kinyume chake, hilo, alipotukia kuwa katika Roma, alinitafuta kwa bidii yenye kuendelea na kunipata. 18 Bwana na amruhusu kupata rehema kutoka kwa Yehova katika siku ile. Na utumishi wote aliotoa katika Efeso wewe wajua vya kutosha.