3 Yohana
Ya Tatu ya Yohana
1 Mwanamume mzee, kwa Gayo, mpendwa, ambaye mimi nampenda kweli.
2 Mpendwa, mimi nasali kwamba katika mambo yote upate kuwa unafanikiwa na kuwa na afya njema, kama vile nafsi yako inavyofanikiwa. 3 Kwa maana mimi nilishangilia sana wakati akina ndugu walipokuja na kutoa ushahidi kuhusu kweli ambayo wewe washika, kama vile unavyoendelea kutembea katika kweli. 4 Sina kisababishi cha shukrani kilicho kikubwa zaidi kuliko mambo haya, kwamba niwe nikisikia kwamba watoto wangu waendelea kutembea katika kweli.
5 Mpendwa, wewe unafanya kazi ya uaminifu katika lolote lile ambalo wafanya kwa ajili ya akina ndugu, tena wasiojulikana, 6 ambao wametoa ushahidi kuhusu upendo wako mbele ya kutaniko. Hawa tafadhali waende zao kwa namna inayomfaa Mungu. 7 Kwa maana wao walienda kwa ajili ya jina lake, bila kuchukua kitu chochote kutoka kwa watu wa mataifa. 8 Kwa hiyo, sisi, tuko chini ya wajibu wa kuwapokea watu wa namna hiyo kwa ukaribishaji-wageni, ili tupate kuwa wafanyakazi wenzi katika kweli.
9 Niliandika jambo fulani kwa kutaniko, lakini Diotrefesi, ambaye hupenda kuwa na mahali pa kwanza miongoni mwao, hapokei kitu chochote kutoka kwetu kwa staha. 10 Hiyo ndiyo sababu, nikija, hakika nitakumbuka kazi zake ambazo yeye huendelea kufanya, akipiga-piga domo juu yetu kwa maneno maovu. Pia, akiwa haridhiki na mambo haya, wala yeye mwenyewe hawapokei akina ndugu kwa staha, na wale wanaotaka kuwapokea yeye hujaribu kuwazuia na huwatupa nje ya kutaniko.
11 Mpendwa, uwe mwigaji, si wa lililo baya, bali wa lililo jema. Yeye ambaye atenda mema hutokana na Mungu. Yeye ambaye atenda baya hajaona Mungu. 12 Demetrio ametolewa ushahidi na wao wote na ile kweli yenyewe. Kwa kweli, sisi, pia, tunatoa ushahidi, nanyi mwajua kwamba ushahidi ambao twatoa ni kweli.
13 Nilikuwa na mambo mengi ya kukuandikia wewe, lakini sitaki kuendelea kukuandikia kwa wino na kalamu. 14 Bali ninatumaini kukuona wewe moja kwa moja, nasi tutasema uso kwa uso.
Na uwe na amani.
Marafiki wakupelekea salamu zao. Wape marafiki salamu zangu kwa jina.