Vijana Wauliza . . .
Kwa Nini Mama na Baba Hupigana Sikuzote?
Mimi nina matatizo mengi katika jamaa yetu, nami sijui la kufanya. Baba yangu hupenda kupiga kelele juu ya kila jambo dogo awezalo kupigia kelele. Na mama yangu hupiga kelele juu ya kila kijambo kidogo. Baba yangu asipopata chakula afikapo nyumbani kutoka kazini, yeye huanza tu kumpigia makelele mama yangu.—Msichana wa miaka 12.
Mimi nahangaika sana kwamba wazazi wangu watatalikiana. Bila shaka, nawapenda wote wawili nami nataka kuwa pamoja nao nyakati zote, lakini wao hupigana juu ya mambo ya kifedha na mambo mengine mengi-mengi.—Mvulana wa miaka 10.
KWA maoni yako, yawapasa wazazi wapendane na kujaliana. Yawapasa wawe na hekima yote, wajue yote, wawe wenye fadhili, wenye ufikirio. Yawapasa wapatane kabisa kuhusu karibu kila jambo. Na wakitofautiana maoni kidogo, yawapasa wazungumze mambo kwa utulivu, bila makelele, wakiwa mahali ambapo wewe husikii. Haiwapasi kabisa kubishana.
Lakini labda kwa fadhaa yako umegundua kwamba nyakati fulani wazazi hukosa maafikiano—na si sikuzote ambapo wao hufanya hivyo kwa utulivu na bila makelele. Hawa ni wazazi wako, na kuwaona wakigombana hukuumiza kwa kina kirefu kuliko vile uwezavyo kueleza. Kijana mmoja alikiri kwamba wazazi wake walipokuwa wakipigana, “nyakati fulani nilihisi ni kama matumbo yangu yanapasuka.”
Kwa Nini Wazazi Hupigana
Ingekuwa vizuri kweli kweli kama akina mama wangeshika sikuzote ‘sheria ya wema [fadhili-upendo, NW] katika ndimi zao’ na wasitamke kamwe neno kali. (Mithali 31:26) Ingekuwa vizuri hata zaidi kama akina baba ‘hawangekuwa na uchungu na’ wake zao. (Wakolosai 3:19) Lakini Biblia husema hivi: “Sisi sote tunafanya makosa [hujikwaa, NW] mara nyingi. Lakini kama mtu hakosi katika usemi wake, basi, huyo ni mkamilifu.”—Yakobo 3:2, HNWW.
Ndiyo, wazazi wako ni wasiokamilika. Kwa kawaida, huenda wao ‘wakachukuliana katika upendo.’ (Waefeso 4:2) Lakini haipasi kukushangaza ikiwa, mara kwa mara, maudhiko yajazana na kujidhihirisha kwa namna ya mzozano.
Kumbuka, pia, kwamba hizi ni “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo.” (2 Timotheo 3:1, NW) Mibano ya kutafuta riziki, kulipia gharama za matumizi, kushindana na mazingira yaliyoko mahali pa kazi—yote haya huweka mikazo mizito juu ya ndoa. Na kuna mibano maalumu wakati wazazi wote wawili wana kazi za kimwili. Kule tu kuamua ni nani atapika na kusafisha kwaweza kuwa chanzo cha ubishano.
Jinsi Kupigana Kwao Huenda Kukakufanya Uhisi
Hata kiwe ni nini huchochea hali za kutoafikiana kwa wazazi wako, huenda ukavunjika sana hisia kuwasikia wakibishana. Mwandikaji Linda Bird Francke aeleza kwamba watoto huelekea “kukweza [kuinua] wazazi wao kwenye vyeo vilivyokwezeka. Mtoto mdogo hamfikirii mama au baba yake kuwa mtu aliye na vikasoro au udhaifu wa aina yake mwenyewe, bali kuwa muundo thabiti kama mwamba ulioangushwa duniani ili tu kumtumikia yeye na kumlinda.” Kuwaona wazazi wako wakigombana hukuelewesha wazi mng’amuo fulani wenye kuumiza: kwamba wazazi hawako hata si ‘thabiti kama mwamba’ kwa kadiri ulivyofikiri. Hiyo yaweza kuutikisa msingi ule ule wenye kutegemeza usalama wako wa hisia-moyo na kuamsha hofu za namna nyingi.
Journal of Marriage and the Family yaripoti hivi: “Zaidi ya nusu ya watoto wote wenye umri wa shule ya msingi waliohojiwa katika Uchunguzi wa Kitaifa kwa Watoto hivi majuzi walisema wao huhisi wakiogopa wakati wazazi wao wawapo na mabishano.” Msichana mchanga jina lake Cindy aliweka wazo hilo hivi: “Mama yangu na baba yangu hubishana sana. Mimi huogopa sana na kwenda kulala. Sijui jambo hilo litakwisha lini.”
Mapigano juu ya pesa—mjadala ulio wa kawaida sana kati ya wenzi waliofunga ndoa—huenda yakachochea hofu za kwamba jamaa yenu inakabili uangamivu wa kifedha. Na iwapo wewe hasa ndiwe mwenye kutajwa katika pigano hilo (‘Usipomchunga zaidi, yeye atakuwa mkora!’) huenda hata ukahofu kwamba kwa njia fulani wewe walaumika kwa pigano hilo.
Yenye kusumbua fikira pia ni mapigano yasiyoisha kuhusu mambo ambayo yaonekana kuwa madogo mno. (‘Mimi nimesinywa na kuchoka kuja nyumbani na kukuta chakula hakijawa tayari!’) Mara nyingi mzozano huu wa daima hutokana na kuoneana uchungu wa kina kirefu zaidi kati ya wazazi wako. Yaeleweka kwamba huenda wewe ukaanza kuwa na wasiwasi kwamba wao wanasonga mbele wakatalikiane mahakamani. Tisho lenye kuongezeka sana la mfokeano wa ghafula “hukufanya ukose starehe nyumbani na ukose nia ya kuthubutu kuja na rafiki zako humo.”—Trouble at Home, na Sara Gilbert.
Huenda pia mahitilafiano ya wazazi wako yakafanyiza mahitilafiano yenye kuvunja moyo juu ya apaswaye kuonyeshwa uaminifu-mshikamanifu. Kama vile Journal of Marriage and the Family iwekavyo wazo hilo, “ukaribu kwa mzazi mmoja huanzisha hatari ya kukataliwa na yule mwingine.” Kwa kuhofu kusema au kutenda jambo lolote ambalo lingeweza kuonwa kuwa ni kujiunga na upande mmoja, huenda ukahisi mwenye wasiwasi wakati wowote uwapo karibu na wazazi wako, ukihofu kwamba utaburutwa ndani ya hitilafiano.
‘Je! Watatalikiana?’
Haielekei hivyo. Biblia huonyesha kwamba mkazo wa kiasi fulani huandama ndoa zote. Kwenye 1 Wakorintho 7:28, NW, Paulo aonya kwamba wale wanaofunga ndoa ‘watakuwa na dhiki katika mnofu wao,’ au “umivu na kihoro katika maisha haya ya kimwili.” (The New English Bible) Kwa hiyo ule tu uhakika wa kwamba wazazi hukosa kuafikiana, hata kwa kuwakiana sana, haumaanishi hasa kwamba hawapendani tena wala kwamba talaka yakaribia. Biblia huonyesha kwamba hata watu wenye kujaliana kwa kina kirefu waweza kuwa na mahitilafiano ya pindi kwa pindi.
Sara, mke wa Abrahamu, huonyeshwa wazi kwa wanawake Wakristo kuwa kielelezo cha ujitiisho wa mke. (1 Petro 3:6) Hata hivyo, alipohisi kwamba Ishmaeli, mwana wa Abrahamu kupitia mjakazi Hagari, alitokeza tisho kwa masilahi ya Isaka, mwana yule mwingine wa Abrahamu, alijulisha hisia zake kwa juhudi kali. “Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.” (Mwanzo 21:9, 10) Bila shaka mikazo ya hisia za ndoa iliwaka! Lakini hakuna hasara ya muda mrefu iliyotokea. Kwa uhakika, kwa kuhimizwa na Mungu, Abrahamu alikubali ombi la Sara!
Basi, yaelekea sana kwamba hali za kutoafikiana kwa wazazi wako zaonekana kuwa kubwa sana kwako kuliko zionekanavyo kwao. Margaret mchanga aligundua hilo alipojaribu kukatiza kigombano cha wazazi kwa kupaaza kelele kwamba, “Acheni kupigana!” kumbe akaambiwa, “Sisi twabishana tu.”
Hivyo mingi ya miwakiano ya kinyumbani huwa ya muda mfupi tu na husahauliwa haraka—hasa ikiwa wazazi wako ni wenye kuhofu Mungu na hutumia shauri la kwamba “iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” (Waefeso 4:32) Ndiyo, yaelekea sana kwamba wazazi wako watamaliza magumu yao bila msaada wowote kutoka kwako.
“Kwanza Wao Hubishana, Kisha Wao Huchapana”
Hata hivyo, si ole zote za ndoa ambazo hutatuliwa kwa urahisi hivyo. Uchunguzi mmoja wa miaka saba kuhusu jamaa kama 2,000 za United States ulifunua kwamba “kila mwaka karibu mtu mmoja kati ya kila sita waliooana katika United States hufanya angalau kitendo kimoja cha jeuri dhidi ya mwenzi wake. . . . Yaelekea sana kwamba huo ni mkadirio uliopunguzwa sana.” Mvulana mmoja tineja alitoa muhtasari hivi kuhusu mahitilafiano ya wazazi wake: “Kwanza wao hubishana, kisha wao huchapana.”
Ikiwa ndivyo ilivyo nyumbani kwenu, basi kuna matatizo mazito kweli kweli katika ndoa ya wazazi wako. Huenda hata kukawa kuna tisho halisi kwa usalama wako wa kimwili—au ule wa wazazi wako. Marie, mwanamke kijana ambaye mama yake alizozana kwa ukawaida na baba yake aliye mzoelevu wa pombe, akumbuka hivi: “Mimi niliogopa. Niliwaza kwamba [baba] angeumiza mama yangu au mama angeumiza [baba].”
Wa kuhangaikiwa kwa uzito pia ni wazazi ambao huepuka maonyesho ya pambano la kimwili lakini ambao hushambuliana kwa maneno wakiwa na ‘uchungu na ghadhabu na hasira na kelele na matukano.’ (Waefeso 4:31) Vilevile, wazazi ambao hurushiana vishale vya maneno yenye kudokeza kwamba hawatosheki katika ngono au hata kuhusu ukosefu wa uaminifu katika ngono hutoa ishara za wazi kwamba huenda ikawa kuna matatizo mazito ya ndoa.
Jamaa fulani hata zina vyanzo maalumu vya hitilafiano, kama vile uzoelevu wa pombe au utumizi wa dawa za kulevya. Au huenda ikawa kwamba mzazi mmoja ni Mkristo ni yule mwingine ni asiyeamini. Yesu Kristo alitabiri kwamba hali ya jinsi hiyo ‘ingesababisha mgawanyiko’ katika jamaa. Mkazo mzito wa ndoa huenda ukatokea.—Mathayo 10:35.
Basi, wewe wapaswa kufanya nini ikiwa ndoa ya wazazi wako yaonekana kuwa katika hatari halisi? Je! kuna lolote uwezalo kufanya zaidi ya kutazama ukiwa hoi tu? Habari hiyo itazungumzwa katika makala ya wakati ujao.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Miwakiano katika ndoa huthibitika kuwa yenye kusononesha sana matineja
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kutumia kanuni za Biblia hurudisha amani