Utawala wa Kibinadamu Wapimwa Katika Mizani
Sehemu 1: Kuelekeza Fikira Kwenye Serikali
MABADILIKO makubwa sana ya kisiasa katika Ulaya wakati wa 1989 yaligeuza fikira za ulimwengu kwa njia ya kipekee sana kwa habari ya serikali. Jarida moja la habari lilionyesha kwamba “1989 utakumbukwa si kuwa mwaka ambao Ulaya ya Mashariki ilibadilika bali kuwa mwaka ambao Ulaya ya Mashariki kama ambavyo tumeijua kwa miongo mingi ilifikia mwisho.”
Akiongezea zaidi, Francis Fukuyama mmoja wa wafanya kazi wa Idara ya Serikali ya U.S. ya kupanga miongozo, hivi majuzi aliandika kwamba “huenda ikawa tunayoshuhudia si mwisho tu wa vita vya maneno, au kupita kwa kipindi fulani cha historia ya baada ya vita, bali mwisho wa historia: yaani, upeo wa mageuzi ya mawazo ya kisiasa ya ainabinadamu.”
Maoni hayo, yajapokuwa yenye kubishika, bado yanaelekeza fikira zetu kwenye maswali fulani ya maana sana. Kwa kielelezo, yaweza kusemwa nini juu ya karne nyingi za utawala wa kibinadamu zilizokwisha kupita? Je! ainabinadamu amefikia ule upeo katika wakati ambao aweza kusema juu ya “mwisho wa historia”? Hasa wakati ujao umewekea serikali akiba gani? Na matukio hayo ya wakati ujao yatakuwa na tokeo gani juu yetu mmoja mmoja?
Jinsi Watu Wanavyoona Juu ya Serikali
Mamilioni ya watu wamekoseshwa tumaini na viongozi wao wa kisiasa. Iko hivyo si kwa wale tu wanaoishi katika Ulaya bali, kwa viwango vyenye kutofautiana, ndivyo ilivyo pia kwa raia kila mahali. Kwa kielelezo, tuangalie nchi za Amerika ya Latini.
Jarida la kibiashara lijulikanalo la Kijerumani lilieleza hali ya kisiasa huko mwishoni mwa 1988 kuwa “kama rundo la mabomoko.” Likitaja mambo waziwazi, lilisema: ‘Uchumi wa Argentina unafumukana. Brazili yatishia kuwa isiyotawalika. Peru imekuwa hohehahe. Uruguay imevurugika. Ecuador inajaribu kuchanganua ile ambayo bila shaka ni hali ya dharura. Colombia na Venezuela zinadumisha kawaida ya kidemokrasi yenye kutikisika-tikisika. Katika Mexico uthabiti wa chama chenye kutawala ambacho kimetawala bila kupingwa kwa miaka 50 unavunjika-vunjika kwa uwazi kabisa. Miaka ya 1980 tayari yatajwa kuwa ‘mwongo uliopotezwa.’
Katika sehemu fulani umaarufu wa wanasiasa umepungua kuliko wakati mwingineo wote. Wakati watu wa Austria walipoulizwa wafuatanishe kazi 21 kwa kulingana na cheo cha heshima, waliorodhesha wanasiasa katika mahali pa 19. Kura za kutafuta maoni ya umma katika Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani zafunua kwamba asilimia 62 ya raia zayo walioulizwa wanakubali kuwa tumaini lao kwa wanasiasa ni kidogo.
Profesa Reinhold Bergler, mkurugenzi wa Taasisi ya Saikolojia kwenye Chuo Kikuu cha Bonn, aonya kwamba “vijana wanakaribia kupa kisogo serikali, siasa na wanasiasa.” Yeye asema kwamba asilimia 46 ya vijana hao huona wanasiasa kuwa watu ambao “hupayuka-payuka,” na asilimia 44 huwaona kuwa walio wafisadi.
Mtafuta kura ya maoni mmoja aliye Mwamerika, akiandika katika miaka ya 1970, aliandika hivi: “Kuna imani ya kwamba mfumo (wa kisiasa) ni usiojali na wenye udanganyifu sana hivi kwamba hauwezi kutumiwa na wapiga kura kwa ajili ya makusudi yao. Kwa hiyo, hesabu ya watu katika United States wanaohisi kwamba wanasiasa “kwa kweli hawajali wewe unapatwa na nini” imeongezeka kwa mfululizo kutoka asilimia 29 katika 1966 hadi asilimia 58 katika miaka ya 1980. Gazeti la Kijerumani Stuttgarter Nachrichten hutetea ukadiriaji huo, likisema hivi: “Wanasiasa wengi sana hufikiria kwanza faida zao wenyewe na kisha, yawezekana labda, zile za waliowapigia kura.”
Basi kuongezeka kwa ubaridi wa kisiasa kwaeleweka. Katika 1980 ni asilimia 53 pekee ya raia za U.S. wanaostahili kupiga kura walioenda kwenye uchaguzi. Iliripotiwa kuwa huko kulikuwa ni kushuka kwa tano kwa mfululizo. Kufikia 1988 hesabu ya wapiga kura ilikuwa imeshuka kufikia asilimia 50 pekee.
Wanasiasa wanaona tatizo hilo. Kiongozi mmoja wa ulimwengu ajulikanaye sana alikiri: “Kuna unafiki mwingi . . . katika maisha ya kisiasa.” Akieleza sababu, yeye alisema: “Ni wa lazima ili kuingia cheoni na ili kubaki cheoni.” Mnenaji alikuwa nani? Aliyekuwa hapo kwanza rais wa U.S. Richard Nixon. Kwa sababu ya kashifa zilizofupiza urais wake, ni watu wachache watakaotilia shaka kwamba yeye alijua aliyokuwa akisema.
Kasoro za kisiasa hufanya watu wenye mioyo ya kufuatia haki washangae kama serikali nzuri yawezekana kwa vyovyote. Je! hatungekuwa afadhali zaidi bila ya serikali yoyote? Je! labda yawezekana ‘kutokuwa na serikali’ ndilo jibu?
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
“Wakati ambapo hakuna mwelekezo wa ustadi, watu huanguka.”—Mithali 11:14, “NW”