Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 6/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Silaha Zisizoweza Kuua
  • Kutahiri na UKIMWI
  • Watoto Wasioelimishwa
  • Ni “Kizazi Chenye Huzuni”?
  • Tisho la Mti Mkangazi
  • Kusafirisha Nje Takataka Zenye Sumu
  • Upungufu wa Vitamini-A
  • Ubongo Usiofanya Kazi Hulegea
  • Hewa Chafu
  • Wamishonari Katika Afrika
  • Osha Mikono Yako!
  • Dini Katika Finland
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1991
  • Mataifa Maskini Yawa Mahali pa Mataifa Tajiri pa Kutupia Takataka
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 6/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Silaha Zisizoweza Kuua

Serikali ya U.S. inatafuta uwezekano wa kuanza kutumia silaha zisizoweza kuua vitani, hiyo ni kulingana na The Wall Street Journal. Tekinolojia ya kisasa huenda ikawezesha wanajeshi wa wakati ujao kutumia jenereta zenye nguvu za sumakuumeme ili kuharibu rada, simu, kompyuta, na vifaa vingine muhimu vya adui bila kuua watu. Maabara zinafanyia kazi pia “‘vizuia-mwako’ vinavyofanya injini za magari yanayokwenda zikwame, na pia kemikali zinazogeuza aina fulani-fulani za magurudumu kuwa kama maji na kuziharibu,” lasema hilo Journal. Hata hivyo, baadhi ya silaha hizo zaweza kuhatarisha sana uhai wa kibinadamu. Journal laongeza kwamba “miali ya leza yenye nguvu sana inayokusudiwa kuharibu taa za vifaru vya adui inaweza pia kulipua macho ya mwanajeshi. Silaha nyepesi za vijiwimbi zinazojaribiwa na Jeshi Maalum la U.S. zinaweza kuharibu mawasiliano ya maadui bila kufanya kelele lakini pia zinaweza kuchemsha viungo vya ndani vya mtu.”

Kutahiri na UKIMWI

Zoea la kutahiri wanaume linaonekana kuwa na mafaa katika kuzuia magonjwa yanayoambukiwa kingono, kama vile UKIMWI, lasema gazeti la Kifaransa La Revue Française du Laboratoire. Gazeti hilo lataja uchunguzi tatu mbalimbali wa kitiba unaoonyesha kwamba kutahiri wanaume (kukatwa kwa govi la juu la uume) ni jambo moja linalosaidia kuzuia mweneo wa UKIMWI. Utafiti wa maabara uliofanyiwa tumbili umeonyesha kwamba nyama ya govi la juu la uume lina chembe nyingi zaidi ambazo ni rahisi kuambukizwa vairasi ya UKIMWI kushinda sehemu nyinginezo. Kwa kuongezea, uchunguzi mmoja wa Kanada uliofanywa katika sehemu mbalimbali 140 za Afrika ulifunua kwamba kulikuwa na visa vingi zaidi vya UKIMWI miongoni mwa vikundi visivyofuata desturi ya kutahiri kuliko miongoni mwa wale wanaotahiri. Uchunguzi mwingine ulipata visa vichache vya kuambukizwa miongoni mwa wanaume waliotahiriwa wenye kuzoea ngono ya kawaida.

Watoto Wasioelimishwa

Maelfu ya watoto Wabolivia hawapokei elimu ya kutosha. Kulingana na gazeti la Bolivia Presencia, hesabu ya 1992 ilifunua kwamba kulikuwa na watoto 2,268,605 wenye umri wa kwenda shuleni katika Bolivia. Hata hivyo, rekodi za Wizara ya Elimu zaonyesha kwamba katika kipindi icho hicho, ni watoto 1,668,791 pekee walioingizwa katika shule za taifa hilo. Hiyo inamaanisha kwamba watoto 600,000 hawakupata elimu ya kutosha. Presencia laongeza kwamba kati ya wale waliojiandikisha shuleni, wanafunzi 102,652 waliacha shule mwaka huo.

Ni “Kizazi Chenye Huzuni”?

Je! ulizaliwa baada ya 1955? Basi una uwezekano wa kuugua mshuko mkubwa wa moyo wakati fulani maishani mwako kwa kiwango cha mara tatu zaidi ya babu zako. Huo ndio mkataa wa uchunguzi mmoja wa kimataifa uliohusisha zaidi ya watu 39,000 katika nchi tisa. Likiripoti juu ya uchunguzi huo, International Herald Tribune laonyesha kwamba mambo yanayochangia kushuka moyo katika siku zetu zinaweza kutia ndani mikazo ya maendeleo ya viwanda, kujihatarisha kwa vitu vyenye sumu, kuacha kuamini katika Mungu au maisha ya baadaye, na, kwa wanawake wengine, mambo yasiyoweza kutimizwa ya urembo. Tribune lataja kwamba labda ainabinadamu inaona “mwanzo wa Kizazi chenye Huzuni.”

Tisho la Mti Mkangazi

Robo milioni ya Wahindi wa Brazili katika msitu wa Amazon wako katika hatari ya kupoteza makao yao ya asili. Kulingana na mkuu wa serikali wa utumishi wa Wahindi, “tisho kubwa zaidi” latokana na biashara ya mti mkangazi. Kukatwa kwa miti ya mkangazi bila idhini kumetokeza kujengwa kwa barabara haramu zenye urefu wa kilometa 3,000 zinazopitia kusini mwa Jimbo la Pará, laripoti The Guardian la London. Kila wakati mti mmoja wa mkangazi unapokatwa, jamii nyingine za miti kufikia 20 huharibiwa. Wanapokata misitu, wafanya biashara wenye pupa hufungulia njia watu wanaokuja kukaa na wachimba dhahabu, pamoja na maelfu ya viwanda vya kukata miti. Kukiwa kumebaki ugavi wa miaka 32 tu kwa mwendo wa sasa wa ukataji, mti mkangazi, kama vile Mhindi, hauna wakati ujao mzuri.

Kusafirisha Nje Takataka Zenye Sumu

Kwa sababu ya gharama ya juu ya kuondoa sumu kwenye takataka, “nchi tajiri zinasafirishia nchi zenye umaskini takataka zenye sumu,” asema Sebastião Pinheiro wa Taasisi ya Brazili ya Mazingira na Mali Asili Zinazoweza Kutokezwa Tena. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti Veja, uchunguzi mmoja ulifunua kwamba “karibu tani milioni moja za takataka zenye sumu husafirishwa nje kila mwaka hadi nchi za Ulimwengu wa Tatu.” Takataka zenye sumu zinazoingizwa nchini hufanyiwaje? Zinaweza kuchomwa kama kuni katika vituo vipya vya nguvu za umeme. “Nchi zinazositawi hutetea wazo la kwamba ni muhimu sana kuongeza fursa za kazi hata gharama iwe nini,” asema mshauri wa shirika moja la mazingira la Brazili. Na maswali bado yanaendelea kuzushwa ulimwenguni pote. Gazeti Financial Times la London la-uliza: “Je! uamuzi juu ya mahali pa kuweka viwanda uamuliwe na makadirio ya mahali ambapo uhai wa kibinadamu unaonwa kuwa wenye thamani kidogo sana?” Veja laongeza hivi kwa kukejeli: “Jibu laonekana kuwa ndiyo.”

Upungufu wa Vitamini-A

Kila mwaka, watoto wanaofikia nusu milioni ambao hawajafikia umri wa kwenda shule hupatwa na upofu kwa sababu tu hawali chakula cha kutosha chenye vitamini-A. Theluthi mbili ya watoto hao hufa miezi michache baada ya kuwa vipofu. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni, jambo hilo latukia hasa katika sehemu fulani za Afrika, Esia, na Amerika ya Latini ambapo watu hawali sana matunda ya manjano, mboga za manjano, mboga za kijani kibichi, mboga zenye matawi makubwa, na vyakula vingine vyenye vitamini A. Ulimwenguni pote, watoto milioni 40 wanapungukiwa na vitamini-A, na kati ya hao, milioni 13 tayari wana dhara fulani la macho. Ukosefu wa vitamini-A waweza pia kuzuia ukuzi wa kimwili, waweza kuongeza uzito wa maambukizo, na kuongeza uwezekano wa vifo miongoni mwa vitoto na watoto wachanga.

Ubongo Usiofanya Kazi Hulegea

Je! muda mrefu usio na utendaji unafaa kwa ubongo? Bila shaka la, akasema Profesa Bernd Fischer katika Wonyesho Ufundi wa Kitiba katika Düsseldorf, Ujerumani. Uchunguzi wake ulionyesha kwamba “majaribio yalikuwa yameonyesha kuwa uwezo wa mtu wa kufikiri ulipungua sana baada ya muda wa saa chache tu wa ubongo kukosa utendaji,” kama ilivyoripotiwa na Der Steigerwald-Bote. Profesa huyo aliwashauri wale wanaopendelea likizo zisizokuwa na utendaji wafikirie tena. “Kama misuli isiyozoezwa,” gazeti hilo lilitaja, “baada ya likizo ndefu isiyokuwa na utendaji, chini ya hali fulani ubongo ulihitaji hadi majuma matatu ili ufikie hali yao ya kawaida ya utendaji.” Michezo, na kitu cha kupendeza cha kusomwa zilisemwa kuwa zazuia ubongo usilegee wakati wa likizo.

Hewa Chafu

“Uchafuzi wa hewa unatokeza hatari kubwa za afya zinazoendelea kuongezeka katika baadhi ya majiji makubwa zaidi ulimwenguni, na sasa hiyo ni sehemu isiyoepukika ya maisha ya mjini kila mahali.” Ndivyo yasema ripoti moja iliyochapishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira. Ripoti hiyo, iliyotegemea uchunguzi wa kisayansi katika majiji 20, yaonyesha kwamba magari ni visababishi vikubwa vya uchafuzi wa hewa. Ripoti hiyo inataja pia kwamba hesabu ya magari yanayoendeshwa ulimwenguni pote, ambayo ni karibu milioni 630 kwa wakati huu, labda itaongezeka maradufu katika miaka 20 au 30 ijayo. Uchafuzi wa hewa huathiri sana mifumo ya kupumua na ya moyo, ukitokeza magonjwa zaidi, ulemavu, na kifo.

Wamishonari Katika Afrika

Kulingana na American Journal of Tropical Medical Hygiene, visababishi vikuu vya vifo wakati huu miongoni mwa wamishonari wa Amerika katika Afrika ni aksidenti za magari, magonjwa ya kuua, na mafuta kujaa mishipani. Miongoni mwa magonjwa ya kuambukiza, mwuaji mkubwa ni mchochota-ini wa vairasi, ukifuatwa na magonjwa kama malaria, ugonjwa wa kichaa cha mbwa, homa ya matumbo, homa ya Lassa, na maambukizo ya vairasi. Hata hivyo, uchunguzi uliohusisha miaka inayoanzia 1945 hadi 1985 umeonyesha kwamba kiwango cha kifo cha wamishonari wa Amerika katika sehemu ya Afrika iliyo kusini mwa Sahara kilikuwa karibu nusu tu ya Waamerika wenzao katika United States. Jambo hilo ni kweli hata ingawa katika Afrika kuna uwezekano wa mara mbili zaidi wa kifo kutokana na aksidenti na uwezekano wa mara nne zaidi wa kuuawa kimakusudi.

Osha Mikono Yako!

Ingawa maendeleo ya kiufundi ya sayansi ya kisasa yamefanya mengi katika kukabiliana na magonjwa, wanasayansi wanasema kwamba kuosha mikono kwa sabuni ya kawaida na maji ni mojapo njia bora zaidi ya kuzuia mweneo wa magonjwa mengi ya kuambukiza. Gazeti la Kifaransa Le Figaro laripoti kwamba katika uchunguzi wa karibuni wa tabia za usafi katika Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, na Uswisi, watafiti walijifanya kuwa watu wa kurekebisha vitu au wasafisha vyoo vya umma katika hoteli, mikahawa, maofisi, shule, na viwanda. Waligundua kwamba mtu 1 kwa kila watu 4 haoshi mikono yake baada ya kwenda choo na kwamba robo ya wale wanaoosha mikono hawatumii sabuni. Wanasayansi wasema kwamba ulimwenguni pote, mkono wa binadamu bado unaonekana kuwa moja ya njia za kawaida zaidi za kueneza ugonjwa.

Dini Katika Finland

Katika Finland, watu 9 kati ya 10 ya wakazi wayo wanaokaribia milioni tano ni wafuasi wa kanisa la Lutheran State Church, lasema The European. Asilimia hiyo kubwa ya watu wa Finland wa dini hiyo ya Lutheran hulipa katikati ya asilimia 1.5 na 2.5 ya mishahara yao ikiwa kodi kwa kanisa, lakini kanisa linadai kwamba kuna upungufu mkubwa wa fedha utakaozuia kutawazwa kwa makasisi wapya mia moja na kulazimisha kufungwa kwa makanisa mengine mwaka huu. Kuna shaka kama wale wafuasi wa Lutheran zaidi ya milioni 4 katika Finland wataliokoa kanisa. The European laeleza kwamba “hakuna tamaa kubwa miongoni mwa watu wa Finland ya kujihusisha zaidi katika mambo ya Kanisa kuliko kuhudhuria sherehe za Kanisa za wakati wa Krismasi na Ista.” Gazeti hilo laongeza kwamba kwa “watu wengi wa Finland kulipa kodi ndiyo mwisho wa ushirika wao na dini inayotambulika.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki