Kuutazama Ulimwengu
Maradhi Mapya na Yanayoibuka
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) laonya kwamba mifoko ya maradhi, kutia na yaliyo mapya, yatisha uhai wa mamilioni ya watu. Kielelezo cha kutazamisha zaidi ni UKIMWI, maradhi yasababishwayo na virusi ambayo ilikuwa kama isiyojulikana kabisa miaka kumi iliyopita. Maradhi mengine ni virusi-hanta ya mapafu, yaliyogunduliwa majuzi kusini-magharibi mwa Marekani. Namna mpya kabisa ya kipindupindu imeibuka katika Asia. Namna mbili za homa za kutokwa na damu zimetokea katika Amerika Kusini, zote mbili zikiwa za kuua. Vielelezo vya mifoko iliyotokea katika 1993 ya maradhi ya kuambukiza yajulikanayo sana ni kutia na kipindupindu katika Amerika ya Kilatini, homa-njano katika Kenya, na kidingapopo katika Kosta Rika, na dipteria katika Urusi. Shirika la Afya Ulimwenguni linaitisha mfumo wa tufeni pote wa vitovu vya kutambua na kupambana na maradhi mapya au yanayoibuka.
Kalsiamu Haitoshi
Halmashauri ya wastadi iliyowekwa rasmi na Taasisi za Kitaifa za Afya katika Marekani ilikata shauri majuzi kwamba “nusu ya watu wazima wa Marekani hawapati kalsiamu ya kutosha, na hilo linachangia kuwako kwa watu wengi wenye mifupa ivunjikayo kwa urahisi mavunjiko yasababishayo gharama za kitiba za dola bilioni 10 kwa mwaka,” kulingana na The New York Times. Yaripotiwa kwamba, zaidi ya watu milioni 25 katika Marekani wanasumbuliwa na osteoporosi, maradhi ya mifupa. Halmashauri hiyo ilieleza katika ripoti yao kwamba kiasi cha kalsiamu kipendekezwacho kutumiwa kila siku wakati wa sasa hakitoshi. Chanzo bora zaidi cha kalsiamu katika chakula ni “vitu vitengenezwavyo kwa maziwa [hasa] na mboga chanikiwiti za majani-majani,” wakaandika wastadi hao. Hata hivyo, waliongezea kwamba “Wamarekani walio wengi huenda wakahitaji kuongezea ulaji wao kwa vibonge vya kalsiamu au vyakula vilivyotiwa kalsiamu kwa kufanyizwa viwandani.”
Mashindano ya Magari Yaendelezayo Uvutaji wa Sigareti
Kama kawaida, nchi za Ulaya zimekuwa mwenyeji wa mashindano maarufu ya mbio za magari za Formula One Grand Prix. Hata hivyo, sasa wapangaji wapendelea kufanyia matukio haya katika nchi za Kiasia kama vile Japani na China. Kwa nini? Kwa sababu sheria za Ulaya zimekuwa kali zaidi juu ya utangazaji wa tumbaku. Wadhamini wakuu wa mashindano ya mbio hizo ni kampuni za tumbaku, kwa hiyo magari ya mashindano ya mbio huonyesha matangazo ya tumbaku waziwazi. Kulingana na Asahi Evening News la Japani, kampuni moja ya tumbaku “hutumia mabilioni kadhaa ya yeni kila mwaka ikilipia timu mbili.” Imekuwa lazima matangazo juu ya magari ya mashindano ya mbio yafutwe au yafunikwe yanapokimbia katika Ulaya. Majuzi ile Grand Prix ya Kifaransa karibu iachiliwe mbali kwa sababu ya katazo moja juu ya utangazaji wa sigareti. Mataifa ya Kiasia, ambako karibu asilimia 60 ya wanaume wote walio watu wazima huvuta sigareti, sasa yachukuliwa kuwa mahali pazuri zaidi pa kutangazia sigareti juu ya magari ya mashindano ya mbio.
Pombe Tele —Chakula Hakitoshi
Katika Venezuela, watoto 726,000 wenye umri wa miaka sita na chini ni wafupi kwa kimo kuliko wapaswavyo kuwa katika umri wao kwa sababu ya utapiamlo, kulingana na gazeti la Kivenezuela El Universal. Hiyo ni asilimia ya kugutusha ya 23.8 kati ya watoto walio katika rika la umri huo, karibu 1 katika 4. Ingawa huenda ikawa hakuna chakula cha kutosha chenye lishe kwa watoto hao, nchi hiyo yaonekana kuwa ina pombe tele. El Universal laripoti kwamba miongoni mwa nchi za Amerika ya Kilatini, Venezuela ndiyo ya kwanza katika utumizi wa pombe. Katika 1991, Wavenezuela walikunywa wastani wa lita 75 kwa kila mtu.
Ushirika wa Kanisa la Uholanzi Unapungua
Uchunguzi mmoja wa majuzi waonyesha kwamba ushirika wa kanisa katika Uholanzi umekuwa ukipungua sana katika miaka 40 iliyopita. Katika 1950, laripoti Ecumenical Press Service (EPS), 3 kati ya wanaume 4 Waholanzi walikuwa washirika wa kanisa. Katika 1991 wastani wao ulikuwa umeanguka wakawa wachache kuliko 2 kutokana na 4, na watafiti watabiri kwamba punde si punde kutabaki mshirika 1 tu wa kanisa miongoni mwa kila wanaume Waholanzi 4. EPS laandika kwamba kulingana na gazeti la Kiholanzi Trouw, “miongoni mwa nchi 15 zilizochunguzwa, ni katika ile tu iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwamba tarakimu za ushirika wa kanisa na imani katika Mungu zilikuwa chini kuliko katika Uholanzi.” Hata hivyo, ijapokuwa ushirika unaoshuka, uchunguzi huo ulionyesha pia kwamba asilimia 75 ya wanaume wote Waholanzi bado huamini katika Mungu.
Majangwa Katika Ulaya
Mfanyizo-jangwa, ule mzoroto wa ardhi ya kilimo yenye rutuba kuwa majangwa, ni “mojapo matatizo yaliyo mazito zaidi ya kimazingira tufeni pote,” yadai Programu ya Kimazingira ya Umoja wa Mataifa. Gazeti The European laripoti kwamba ingawa kwa ujumla mfanyizo-jangwa hushirikishwa na Afrika, sasa wakumba kama asilimia 10 ya ardhi ya kilimo ya Ulaya. Hispania ndiyo nchi iliyoathiriwa vikali zaidi. Wanasayansi waamini kwamba ulishaji mwingi mno wa mifugo pamoja na utapanyaji wa maji ndio umefanya nchi iwe na elekeo la kukauka na kumomonyoka, ikigharimu wakulima dola kama bilioni 1.5 kwa mwaka. Tokeo zito ni kule kuhama kwa watu kwenda maeneo ya mijini, ambalo huongoza kwenye msongamano wa kupita kiasi na machafuko ya kiraia. Watabiri-anga wasema kutazidi kuwa na upungufu mbaya wa mvua kusini mwa Ulaya.
Moshi Katika Macho
Mkurugenzi wa Taasisi ya Australia ya Utafiti wa Mwono wa Kitaifa, Profesa Robert Augusteyn, adai kwamba ana ithibati isiyoweza kubishaniwa kwamba kemikali zitokazo katika moshi wa sigareti husababisha watoto-macho. Uchunguzi mmoja waonyesha kwamba wavutaji wa sigareti waelekea mara mbili au tatu zaidi kupatwa na watoto-macho kuliko watu wasio wavutaji. Kemikali zitokazo katika moshi wa sigareti hufyonzwa kwanza na mwili, lakini ndipo hizo hupenya jichoni ambako huharibu “mabomba” yakaushayo chumvi na maji ya kupita kiasi katika lenzi ya jicho. Uvimbe na mpasuko utokeao kwa sababu hiyo katika chembe za jicho hufanyiza watoto-macho. “Mimi nimeridhika kikamili. Hakuna shaka kitu fulani katika moshi wa sigareti kinazuia mabomba hayo yasifanye kazi katika lenzi,” aeleza Profesa Augusteyn.
Kutojua Kusoma Biblia Kunakoongezeka
“Kuna ukosefu wa ujuzi wa Biblia unaoongezeka katika sehemu zote za jumuiya ya Magharibi,” laripoti Ecumenical Press Service la Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Sosaiti za Biblia zakadiria kwamba asilimia 85 ya Wakristo wa Magharibi hawajasoma kamwe Biblia nzima, na uchunguzi wa maoni ya watu katika Marekani waonyesha kwamba ni asilimia 12 tu ya waenda-kanisani huko wasomao Biblia kwa ukawaida. Wanafunzi wa chuo kikuu leo, asema Fergus Macdonald, katibu mkuu wa Sosaiti ya Kitaifa ya Scotland ya Biblia, “wamekosa ufahamiano na watu wa kibiblia kama Abrahamu, Isaka na Yakobo, na majina ya mitume wa Yesu, hivi kwamba hawawezi kufahamu yaliyomo katika kazi sanifu zilizo katika fasihi ya Ulaya.”
Usafishaji wa Masika juu ya Mlima Everest
Zaidi ya kuwa ndicho kilele cha juu zaidi ulimwenguni, Mlima Everest sasa wajulikana pia kuwa ndio “ua mrefu zaidi wa kutupia takataka” ulimwenguni, kulingana na gazeti UNESCO Sources. Katika miaka 40 iliyopita, wapanda-milima wameutia Everest takataka kwa karibu tani 20 za chupa za oksijeni, mahema, mifuko ya kulalia, na pakiti za vyakula. Juu ya ile miteremko ya chini zaidi, ambako mandhari-nchi ina makaratasi ya choo yanayopeperuka, sasa kile kijia cha kwenda Kambi ya Chini ya Everest ‘chajulikana kuwa kijia cha karatasi za choo.’ Juu zaidi mlimani, takataka ni nyingi ajabu. “Picha za tamasha hizi,” laandika UNESCO Sources, “zawashtua wale wadhanio kwamba Everest ni nyika inayodumisha usafi wayo wa zamani bila kuvurugwa na mwanadamu.” Ili kuondolea mlima huu uchukizo huo, serikali ya Nepal ilikubali mwaka huu kuwe na safari kadhaa za kwenda “usafishaji wa masika.”
Mwito wa Papa wa Kuhubiri
Mapema kidogo mwaka huu, Papa John Paul 2 aliambia kikundi cha Wakatoliki katika Italia kwamba wakati umefika gospeli ipelekwe moja kwa moja kwa watu. Wakatoliki katika Australia waliitikiaje? “Wakatoliki Hawataki Kutii Mwito wa Papa wa Kuhubiri,” likaandika gazeti Illawarra Mercury la Australia katika kichwa kikuu. Liliandika kwamba Wakatoliki katika nchi hiyo “hawana hamu ya kukubali kutia ule mfikio wa namna ya Mashahidi wa Yehova kwenye imani yao.” Kasisi Mkatoliki wa kienyeji Sean Cullen alisema kwamba hakuwa na uhakika kama mwito wa papa wa kuhubiri ulielekezwa kwa Wakatoliki wote au ulikuwa kwa wale walio katika Italia tu. “Sisi tungewatia watu moyo waishi kulingana na Gospeli waijuayo kupitia maisha zao wenyewe. Sina la kusema juu ya kama hilo lamaanisha kwenda kugonga-gonga milango.” Mfanyakazi aliye mwenyeji wa baraza la jiji alitoa jibu bila kuepa sana hivyo. Alisema: Uenezaji-Evanjeli “si sehemu ya akili ya Mkatoliki.”
Aksidenti za Upigaji-Mbizi wa Skyuba
Katika Marekani, “karibu watu 90 hufa kila mwaka wanapofanya upigaji-mbizi wa skyuba,” laripoti The New York Times. Maofisa wa serikali hawakubaliani na jambo la kwamba, tofauti na utendaji mwingine hatari kama urukaji wa banjii na ndege zinazoruka, hakuna sheria zinazoongoza shughuli ya upigaji-mbizi wa skyuba. Katika Marekani pekee, kuna wapiga-mbizi kati ya milioni tatu na milioni tano waliothibitishwa kwa vyeti. Maduka ya vifaa vya upigaji-mbizi wa skyuba huwathibitisha kwa vyeti watu wapatao 300,000 hadi 400,000 kila mwaka. Mwenye duka mmoja aeleza kwamba tatizo ni kwamba “wapiga-mbizi hawafuati mielekezo sikuzote.” Al Hornsby wa Shirika la Kitaalamu la Wafunzi wa Upigaji-Mbizi adai kwamba hesabu ya aksidenti za upigaji-mbizi kwa kweli inapungua. Times laripoti hivi: “Katika miaka ya katikati ya 1970, alisema, kulikuwa na vifo 12 kwa kila wapiga-mbizi 100,000, na sasa kuna vingi kidogo kuliko 2 kwa kila 100,000.”
Wezi Katika Maktaba
Majuzi uchunguzi uliofanywa na Shirika la Maktaba na Hifadhi za Taasisi za Utamaduni wa Roma. Kulingana na watafiti ni hesabu ndogo tu ya maktaba katika Italia zilindwazo kwa sasa na mifumo hodari ya kielektroni dhidi ya wizi. Tokeo ni kwamba, kila mwaka vitabu vipatavyo 100,000 ama huharibiwa ovyo visiweze kutengenezwa ama huibwa, kulingana na gazeti la Kiitalia La Repubblica. Gazeti hilo laandika kwamba hata maprofesa wa chuo kikuu wana hatia ya kuiba vitabu visivyopatikana tena sokoni lakini vilivyo na mafaa kwa machunguzi yao.