Je, Maisha Yako Ni Makimwa? Waweza Kuyabadili!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA
MARGARET na Brian walikuwa katika miaka yao ya katikati ya 50, fursa nzuri sana ilipotokea: kustaafu mapema pamoja na malipo ya ujira wa uzeeni mwafaka. Ni wakati huo walipoamua kuelekea kusini kufurahia jua na fuo za Mediterania. Hakuna mahangaiko tena, hakuna mafadhaiko tena—maisha ya starehe yaliwangoja kwenye shale yao ufuoni mwa bahari!
Baada ya miaka miwili ndoto yao ilienda mrama. Brian alieleza hivi: “Yote yalionekana kukosa maana—siku baada ya siku bila lolote la kufanya. Bila shaka ningeogelea, nicheze golfu kidogo au tenisi, na kuongea kama kasuku kwa yeyote ambaye angenisikiliza. Kuhusu nini? Upuuzi tu.”
Gisela, mama fulani aliye katika miaka ya 20, ana kisichana kirembo. Kwa kawaida, wakati wa alasiri mama na bintiye, huenda kwenye bustani la starehe, ambapo binti hucheza kwenye vilima vya changarawe, akiwa amenywelea shughuli kikamili, kwa furaha akifanya vitumbua na vigome vya changarawe. Wakati huo, mama hukaa kwenye benchi iliyo karibu bustanini na kukiangalia kienda-dema chake. Au kwa kweli yeye akiangalia? Hapo hukaa, masikio yake yakiwa yamekazwa kwenye redio yake yenye kubebeka. Kupitia kwa moshi wa sigareti yake, katu haoni mtoto wake tena. Amepatwa na ukimwa kiasi cha kutokwa na machozi.
Peter, mwanafunzi fulani wa sekondari mwenye umri wa miaka 17, hukaa chumbani mwake, akiwa amezungukwa na vidude bora vya karibuni zaidi vya elektroni. Afungua mmojapo ya michezo yake ya vidio, kuvumbua tu kwamba kamwe humpendezi tena. Tayari ameucheza mamia ya nyakati, na sasa ajua mbinu zote za kuucheza. Je, asikize muziki fulani? Hata hivyo, hakuna mrekodi alionao ambao hajapata kuusikiliza madazani ya nyakati. Ana ukimwa kupindukia, yeye hulalama hivi: “Sijui la kufanya.”
Je, Wapitisha Wakati?
Hakika, si kila mmoja huwa na siku duni na hafifu. Bado wengi waishi maisha yenye furaha na yenye maana, wakitafuta ujazo kwa kujifunza mambo mapya, kwa kuridhisha silika yao ya ubuni, na kwa kusitawisha mahusiano mema pamoja na watu wengine—na hata wenye maana zaidi, pamoja na Mungu.
Hata hivyo, ukimwa huathiri watu wa tabaka zote—Mjerumani 1 kwa kila 3 ni mkimwa, kulingana na uchunguzi wa majuzi. Yupi mwenye tamaa ya fahari ambaye kwa kutotulia hutamba maeneo yote yajulikanayo ya utumbuizo mjini, kijana asiye na kazi ambaye hupitisha wakati na muziki wenye sauti ya juu na pombe ya bei rahisi, mfanya-kazi mwenye umri wa makamo wa kazi ya mikono ambaye hutumia miisho-juma akitazama televisheni, karani ajihisiye kukosa uhakika aachapo ofisi yake—wote waugua tatizo moja: ukimwa.
Wanafalsafa wa kale waliita taedium vitae (uchovu wa maisha katika Kilatini). Katika Kijerumani ni Langeweile (muda mrefu). Saa ambazo hujikokota, kazi ambayo huonekana kuwa isiyo na maana, kule kutamani “kujinasua kutoka kwayo yote” ni dalili za kawaida sana za ukimwa.
Hata walio matajiri hupatwa. Baada ya kueleza mtindo wa maisha wa matajiri, Roger Rosenblatt wa gazeti la Time alionelea hivi: “Baada ya kupata nyumba kubwa na shamba kubwa na wanyama wakubwa, burudani na watu, ni nini wengi wa waponda-mali wa ulimwengu hutangaza? Kwamba wana ukimwa. Ukimwa.”
Wakati mmoja ilifikiriwa kwamba starehe iliyoongezeka ingekuwa tiba kamili ya ukimwa. Kisio hilo lilikuwa kwamba hali za binadamu za kufanya kazi, kumaliza ukawaida wenye kuchosha wa wakati uliopita, na kiasi cha kutosha cha wakati wa starehe kingefanya maisha yathawabishe kwa mwanadamu wa kawaida. Lakini, kwa kusikitisha, si rahisi hivyo. Kuamua la kufanya na wakati wote huu wa starehe kumethibitika kuwa kugumu kuliko ilivyotarajiwa. Wengi hukamia juma zima kuwa na mwisho-juma wenye kufurahisha, kupata tu kwamba ufikapo hautimilizi matarajio yao.
Matokeo Hasi ya Ukimwa
Watu fulani hutafuta kuepuka ukimwa kwa kujiingiza wenyewe katika utendaji wa kupita kiasi. Waraibu fulani wa kazi walikuwa hivyo kwa sababu hawakujua kamwe la kufanya na wakati wao walipokuwa hawako ofisini. Wengine huzamisha ukimwa wao katika alkoholi au hutafuta msisimuko kwa kujaribia dawa za kulevya. Wengi wa magwiji waigizaji wa vitumbuizo vya ulimwengu walionywelea katika shughuli hujazia utupu, vifijo viishapo, na dawa za kulevya kama vile kokeni. Ukimwa umetambulishwa kuwa mojapo ya sababu za idadi inayozidi kuongezeka ya akina mama matineja ambao hawajaolewa, wengi ambao huenda walifikiri kwamba watoto wangeyajazia maisha yao matupu.
Ukimwa wahusianishwa hata na kiwango cha uhalifu kinachoongezeka. Gazeti Time lilionelea kwamba idadi ya vijana huacha shule kwenye miaka 16 na hawana lolote la kufanya na wale ambao hawajaajiriwa wa Ulaya Magharibi, wakilinganishwa na marika wao wanaofanya kazi, ‘wana uelekeo mkubwa wa kujiua, kupatwa na utumizi mbaya wa dawa za kulevya, uelekeo zaidi wa kupata mimba nje ya kifungo cha ndoa na mbetuko zaidi wa kuvunja sheria.’ Hili laonekana kuhakikisha tena ule msemo wa kale kwamba ‘Shetani huwatafutia la kufanya wasio na la kufanya.’—Linganisha Waefeso 4:28.