“Msiba wa Usawa wa Kufanya Mambo”
“WASICHANA matineja hawafahamu ujumbe wanaowasilishiwa,” laripoti The Toronto Star. Ujumbe gani? Kwamba uvutaji sigareti ni zoea lenye kufisha. Uchunguzi wa 1991 ulifunua kwamba asilimia 25 ya wasichana Wakanada kati ya umri wa miaka 15 na 19 walikuwa wavutaji sigareti, wakilinganishwa na asilimia 19 ya wavulana katika rika hilohilo. Hata miongoni mwa watu wazima, wavutaji sigareti wa kike wanawashinda kwa idadi wavutaji sigareti wenzao wa kiume. “Utumizi wa tumbaku miongoni mwa wanawake umekuwa msiba wa usawa wa kufanya mambo,” wakaonelea madaktari wanaounga mkono shirika la Smoke-Free Canada.
Kwa nini wasichana matineja huanza kuvuta sigareti? Udadisi, msongo wa marika, na uasi huchangia. Hata hivyo, ile ambayo haipaswi kupuuzwa ni biashara ya kutangaza bidhaa, ambayo huonyesha wanawake wavutaji sigareti wakiwa wembamba. Ndiyo, wengi huvuta sigareti ili kujaribu kuzuia kula kupita kiasi, na huhofu kuongeza uzani ikiwa wataacha. Kwa kusikitisha, wanawake hawa huenda wakahangaikia sana tisho la kuongeza uzani kuliko tisho la kansa. Robert Coambs, kaimu wa profesa kwenye Chuo Kikuu cha Toronto, aliwekea mtazamo wao muhtasari hivi: “Kansa ya mapafu iko umbali wa miaka 20. Kuongeza uzani kuko hapa karibu.”
Biashara ya tumbaku pia hulenga shabaha wanawake kwa kuhusianisha uvutaji sigareti na uhuru. Hata hivyo, Jean Kilbourne, aliyekuwa mshauri kwa vikundi viwili vya Marekani vya madaktari wapasuaji, alitaarifu kwa hekima hivi: “Mtu aweza kufikiria uvutaji sigareti kuwa wenye kuweka huru tu ikiwa mtu huyo afikiria kifo kuwa uhuru wa hatimaye.”