Madaktari Wafikiria Upya Upasuaji Bila Damu
MWANAMKE mmoja Mkanada aitwaye Janet aliyekuwa na UKIMWI alimweleza mwana wake sababu ya kuwa na maradhi hayo. Mume wake alikuwa amemwambukiza maradhi hayo kabla hajafa. Yaelekea kwamba mume wake naye, aliyekuwa akiugua ugonjwa wa kutoganda kwa damu, aliambukizwa UKIMWI kupitia sehemu fulani ya damu. Maogofyo kama haya ni mojawapo tu ya mambo yanayochochea wanatiba wafikirie upya tiba ya kawaida ya kutia damu mshipani. Hata kichwa kimoja kikuu cha The New York Times mwaka huu kilitangaza: “Upasuaji ‘Bila Damu’ Wakubaliwa Zaidi.”
Mikutano kadhaa ya wanatiba imekazia kwamba watu wanazidi kupenda upasuaji bila damu. Kati ya mikutano ambayo ilifanywa mwaka jana, miwili ilikuwa Marekani (Boston na Atlanta), mmoja Kanada (Winnipeg), na mmoja Latvia (Riga), ambao ulikuwa mkutano wa kimataifa wa Ulaya Mashariki.
Baada ya kutegemea tiba ya kutia watu damu mshipani kwa zaidi ya miaka 50, kwa nini zaidi ya wataalamu 1,400 kutoka nchi 12 walihudhuria mikutano hiyo minne iliyotangaza tiba ya upasuaji bila damu kuwa “mtindo wa wakati ujao,” kama lilivyotaja gazeti moja? Mikutano hiyo ilikazia nini kuhusu dawa mpya, vifaa vipya, na mbinu mpya ambazo zingefanya kuwe na tiba mbalimbali kwa ajili ya familia yako?
Kwa Nini Tiba za Badala Zatafutwa?
Sababu kuu ni kushindwa kulinda usalama wa akiba za damu. Kwa mfano, gazeti la Globe and Mail la Januari 31, 1998, la Toronto, laeleza juu ya “msiba wa damu iliyoambukizwa” nchini Kanada uliotokea katika miaka ya 1980: “Mchochota-ini aina ya C ni maradhi yawezayo kudhoofisha ini, na hayana tiba. . . . Wakanada wapatao 60,000 huenda wameambukizwa virusi hivyo kupitia damu iliyoambukizwa, yaani, watu wapatao 12,000 wanaweza kufa kutokana na mchochota-ini ambao huambukiza watu kupitia damu.”
Japo mbinu mpya za kupima damu zimepunguza sana tisho hilo, Hakimu Horace Krever alisema yafuatayo kwenye mkutano uliofanywa Winnipeg: “Akiba ya damu nchini Kanada haijapata kamwe kuwa salama kabisa, na haiwezi kamwe kuwa salama. Matumizi ya damu hayawezi kukosa hatari.” Na hatari ya mtu kuambukizwa maradhi au kupatwa na athari mbaya sana huzidishwa na kila painti ya damu anayopokea.
Kule Riga, Dakt. Jean-Marc Debue, wa Clinique des Maussins, kule Paris, alikata kauli akisema: “Ni lazima sisi matabibu tufikirie upya njia yetu ya kawaida ya kutibu. . . . Utiaji-damu mshipani umerefusha maisha ya wagonjwa wengi, lakini pia umeharibu maisha ya wengine kwa kuwaambukiza maradhi yasiyoweza kutibika.”
Mbinu za kupima damu kwa ajili ya viini haziwezi kugundua maradhi mapya yenye kutisha na basi mbinu hizo haziwezi kutoa kinga dhidi ya maradhi hayo. Kwa mfano, Dakt. Paul Gully, wa Ottawa, Ontario, Kanada, alisema: “Mchochota-ini aina ya G ni kirusi kipya cha RNA; watu wameambukizwa maradhi hayo kupitia kutiwa damu mshipani lakini hatari zake kwa wakati huu hazijulikani.”
Hatari nyingine iliripotiwa katika toleo moja la kipekee la kitiba la gazeti Time: “Utiaji-damu mshipani waweza kudhoofisha mfumo wa kinga, . . . ukimfanya mgonjwa aweze kuambukizwa maradhi mengine kwa urahisi, hupunguza mwendo wa kupona na kurefusha kipindi cha kupata nafuu.”
Jambo jingine ni kuokoa gharama. Kulingana na gazeti Time, kila utiaji-damu mshipani waweza kugharimu dola 500 nchini Marekani. Na katika sehemu nyinginezo, akiba za damu zinapunguka kwa sababu watoaji wa damu wamepungua.
Wagonjwa wapasuliwao bila damu huokoa fedha zaidi kwa sababu hawaambukizwi sana na magonjwa na vilevile hawakai sana hospitalini. Kule Winnipeg, Durhane Wong-Rieger, wa Shirika la Wenye Matatizo ya Kutoganda kwa Damu la Kanada, alisema hivi kuhusu upasuaji bila damu: “Twahisi ni muhimu sana. Ni nafuu na bila shaka unaweza kuboresha afya ya wagonjwa.”
Pia wagonjwa mbalimbali wanazidi kudai wafanyiwe upasuaji bila damu. Dakt. David Rosencrantz wa Hospitali za Legacy Portland (Oregon, Marekani), alisema kwamba hapo awali “asilimia 100 ya wale waliotujia walikuja kwa sababu za kidini.” Lakini, sasa angalau asilimia 15 hupendelea tiba za badala ya utiaji-damu mshipani, wala si kwa sababu ya dhamiri ya kidini.
Maoni Mbalimbali
Kwenye mikutano hiyo minne, jambo moja kubwa lililokubaliwa kwa ujumla ni kwamba ni salama sana kutumia damu yako mwenyewe kuliko kutumia damu iliyotolewa na watu wengine. Basi, wengine wanapendekeza kujiwekea akiba ya damu yako kabla ya kufanyiwa upasuaji. Lakini, wengi walisema kwamba hakuna wakati wa kuweka akiba ya damu katika hali za dharura. Pia kuna suala la kidini la Mashahidi wa Yehova kupinga matumizi ya damu yoyote iliyowekwa akiba.a
Dakt. Bruce Leone, wa Chuo Kikuu cha Duke, North Carolina, Marekani, aliuambia mkutano wa Kanada: “Kutoa [damu yako mwenyewe] kabla ya kufanyiwa upasuaji ni ghali, ni kazi nyingi, hakuondoi magonjwa ya kawaida ambayo husababishwa na kutiwa damu mshipani [ambayo huwa ni kosa la wahudumu, yaani kosa linalotokea ofisini au katika utaratibu wa tiba] na huhitaji muda mwingi kabla ya upasuaji.”
Wanatiba wengi hutetea kuendelea kutafuta tiba na mbinu ambazo zinaweza kupunguza kabisa utiaji-damu mshipani. Wao wabisha kwamba mtu apaswa kutiwa damu mshipani katika hali za dharura pekee. Kwa upande mwingine, sasa wengine hawatumii kamwe damu katika tiba yao. Wao wataja upasuaji mgumu sana—wa kubadilisha mfupa wa nyonga, upasuaji mkubwa wa ubongo, upasuaji wa moyo wa vitoto vichanga na watu wazima—uliofanywa bila utiaji-damu mshipani, na wagonjwa wakapona haraka.
Kufikia wakati huu, zaidi ya hospitali 100 ulimwenguni pote zina mipango ya tiba bila damu, na kati ya hizo zaidi ya 70 ziko Marekani. Hata sasa kuna zaidi ya madaktari 88,000 ulimwenguni pote ambao wanawatibu wagonjwa wasiotaka damu.
Mbinu Mpya
Kwenye mkutano wa Atlanta, wasemaji wengi walikiri kwamba walisitawisha mbinu mpya kwa mara ya kwanza walipokuwa wakiwatibu Mashahidi wa Yehova.b Wengi walikubaliana na Dakt. James Schick wa Encino-Tarzana Regional Medical Center, Los Angeles, aliyesema kwamba kwa sababu ya mbinu mpya alizositawisha alipokuwa akitibu watoto wa Mashahidi wa Yehova waliozaliwa kabla ya wakati wao, sasa amepunguza matumizi yake ya damu kwa asilimia 50 kwa watoto wachanga wote anaowatibu. Bila shaka, mbinu hizo mpya pia zimewafaidi watu wazima.
Dakt. Jean-François Hardy, wa Taasisi ya Moyo ya Montreal, alisema: “Upasuaji bila damu hauwezi kufaulu kwa msaada wa mbinu moja tu ya kitiba . . . Badala yake, inaweza kufaulu tu kwa kutumia mbinu mbalimbali pamoja.”
Miongoni mwa mbinu mpya ni (1) matayarisho ya kabla ya upasuaji, (2) kuzuia damu isivuje wakati wa upasuaji, na (3) utunzaji wa baada ya upasuaji. Bila shaka, njia zote za upasuaji hutegemea sana wakati, yaani, kama kuna wakati wa kutosha wa kuzidisha chembe nyekundu za damu za mgonjwa ili kumtayarisha kwa upasuaji au hakuna wakati kwa sababu ni lazima upasuaji wa dharura ufanywe.
Njia bora ya kufanya upasuaji bila damu ni tiba ya kabla ya upasuaji ambayo huzidisha idadi ya chembe nyekundu za damu na kuboresha afya kwa ujumla. Hiyo yatia ndani kutumia vibonge vya chuma vyenye nguvu nyingi na vitamini na vilevile, inapowezekana, erythropoietin zilizofanyizwa, dawa ambayo huchochea uboho wa mfupa wa mgonjwa kutengeneza chembe nyekundu za damu haraka zaidi. Tekinolojia ambayo ina uwezo wa kuchunguza mambo madogo-madogo huwezesha kutoa damu kidogo tu ili kupimwa na bado mambo mengi yajulikane kutokana na damu hiyo kidogo. Hilo ni muhimu sana kwa watoto wachanga na kwa wagonjwa wenye umri mkubwa ambao wamepoteza damu nyingi sana.
Maji ni muhimu sana, nayo huingizwa mshipani ili kuzidisha kiasi cha damu. Pia chombo cha oksijeni hutumiwa katika hospitali fulani ili kusaidia kuongeza mahitaji ya oksijeni ya mgonjwa ambaye amepoteza damu nyingi sana. Kule Atlanta, Dakt. Robert Bartlett alieleza kwamba chombo cha oksijeni ni kizuri sana lakini lazima kitumiwe kwa uangalifu kwa sababu oksijeni nyingi mno ni sumu.
Kwa hatua ya pili, kuzuia damu isivuje wakati wa upasuaji, kuna vifaa vingi vipya na tekinolojia mpya. Hizo husaidia kupunguza kuvuja kwa damu; hazikati sehemu kubwa mwilini, zikipunguza kiasi cha damu kinachotoka na mshtuko wa mwili; au husaidia mara moja kunasa na kutumia tena damu ya mgonjwa mwenyewe ambayo ingalivuja wakati wa upasuaji. Fikiria chache tu kati ya mbinu hizo mpya.
◼ Chuma chenye kutumia umeme husaidia kuzuia mishipa isivuje damu.
◼ Kigandishaji chenye mwali wa gesi ya agoni husaidia kukomesha mvujo wa damu wakati wa upasuaji.
◼ Kisu cha mtikiso hutumia mtikisiko na msuguano ili kukata na kusababisha damu igande kwa karibu wakati uo huo mmoja.
◼ Wakati wa upasuaji fulani, dawa kama vile tranexamic acid na desmopressin hutumiwa mara nyingi kuzidisha kuganda kwa damu na kupunguza kuvuja kwa damu.
◼ Dawa za nusukaputi hupunguza kuvuja kwa damu kwa kupunguza msongo wa damu.
Jambo muhimu vilevile ni maendeleo yanayofanyiwa mashine zinazosaidia kuhifadhi damu wakati wa upasuaji. Wakati wa upasuaji, mashine hizi huchukua damu hiyo mara moja na kuitumia wakati uo huo, bila kuihifadhi.c Mashine mpya zaweza kutenganisha damu katika sehemu-sehemu na kuitumia tena inapohitajika zikiwa zingali zimeunganishwa kwenye mgonjwa.
Baada ya mkutano wa Riga na baada ya ku-sikia uhitaji wa Latvia, Mashahidi wa Yehova nchini Sweden walitoa mashine mbili za kuhifadhi chembe za damu zipelekwe Latvia. Kufika kwa mashine ya kwanza na manufaa za upasuaji bila damu kulitokeza idili sana nchini Latvia hivi kwamba tukio hilo lilionyeshwa kwenye televisheni ya taifa huko.
Utunzaji wa baada ya upasuaji mara nyingi hutia ndani mbinu zilezile za kuzidisha kiasi cha damu zinazotumiwa kabla ya upasuaji. Lakini, mara nyingi ni rahisi kuwatunza wagonjwa ambao hawakutiwa damu mshipani kuliko wale waliotiwa damu mshipani. Kwa nini?
Matokeo Yenye Kutokeza
Ingawa mbinu zinazoondoa matumizi ya damu mara nyingi huhitaji kazi nyingi kabla ya upasuaji na wakati wa upasuaji, madaktari-wapasuaji wameona kwamba wagonjwa hunufaika kwa sababu ya kupona haraka baada ya kufanyiwa upasuaji. Wao hawapatwi na matatizo ambayo mara nyingi huwapata watu wenye kutiwa damu mshipani. Imethibitishwa kwamba wagonjwa ambao hawakutiwa damu hawakai sana hospitalini.
Dakt. Todd Rosengart wa The New York Hospital-Cornell University Medical Center, alisema kwamba mbinu yao yenye kuchukua hatua nane ya kuhifadhi damu ilifanya waweze kufanya upasuaji mgumu wa moyo bila wasiwasi na bila damu. Dakt. Manuel Estioko, wa Good Samaritan Hospital kule Los Angeles, alisema walipata “ujuzi mwingi kwa kufanya mamia ya upasuaji wa moyo bila damu.” Dakt. S. Subramanian aliripoti kwamba alipata mafanikio kwa kuwafanyia watoto upasuaji wa moyo bila kuwaongeza damu kwenye Hospitali ya Watoto ya Miami.
Upasuaji unaohusu mifupa, hasa kubadilisha mfupa wa nyonga, ni mgumu sana. Lakini, Dakt. Olle Hägg, wa Hospitali ya Uddevalla nchini Sweden, aliripoti katika Riga kwamba kutumia kwa pamoja “mbinu za upasuaji na ustadi” kumewafanya wapunguze kuvuja kwa damu kwa kiasi kikubwa kwa wagonjwa ambao ni Mashahidi wa Yehova. Kwa kweli, Bw. Richard R. R. H. Coombs, wa Imperial College School of Medicine, London, alisema kwamba “asilimia 99.9 ya upasuaji wote unaohusu mifupa waweza kufanywa bila . . . kutiwa damu mshipani.”
Wakati Ujao
Idadi ya hospitali na madaktari wanaotumia mbinu za upasuaji bila damu yaendelea kuongezeka. Na mikutano ambamo watu huelezana ujuzi kama huo imekuwa yenye mafaa sana, kwa kuwa matabibu hujifunza njia za badala za kutibu ambazo zimejaribiwa kwa mafanikio na zinatumiwa kwa kawaida.
Dakt. Richard Nalick, wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Southern California, alisema: “Watu wanaozidi kuongezeka hutaka tiba na upasuaji bila damu . . . Tiba na upasuaji bila damu ni njia ya kisasa na haipasi kueleweka vibaya kuwa ‘tiba ya badala’ ambayo si bora.”
Matatizo yanayohusu utiaji-damu mshipani yazidipo kuongezeka na umma kuzidi kudai tiba ya badala, wakati ujao wa upasuaji bila damu waonekana kuwa mzuri.
[Maelezo ya Chini]
a Mashahidi wa Yehova hukubali tiba kwa ajili yao wenyewe na kwa watoto wao. Lakini, kwa kutegemea katazo la wazi la Biblia la kutoingiza damu mwilini, wao hukataa kutiwa damu mshipani. (Mwanzo 9:3, 4; Matendo 15:28, 29) Kwa habari zaidi, ona broshua Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?, iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Mazungumzo juu ya mbinu mbalimbali zilizotajwa kwenye mikutano hiyo kamwe si mapendekezo ya Amkeni! Sisi twaripoti tu matukio hayo.
c Kwa matumizi yafaayo ya mashine kama hizo na fungu la dhamiri, msomaji anaweza kusoma Mnara wa Mlinzi la Machi 1, 1989, ukurasa wa 30-31.
[Picha katika ukurasa wa 20, 21]
Madaktari wanaozidi kuongezeka wanaheshimu matakwa ya wagonjwa wao kuhusu upasuaji bila damu