Kuutazama Ulimwengu
Ndoa Ni Afya
Kufunga ndoa “hurefusha maisha, huboresha sana afya ya kimwili na ya kihisia-moyo na huongeza mapato” ya wanawake na wanaume, ataarifu mtafiti mmoja katika The New York Times. Uchunguzi uliofanywa na profesa Linda J. Waite wa Chuo Kikuu cha Chicago wakanusha ripoti iliyochapishwa mwaka wa 1972 ukionyesha kwamba wanawake walioolewa hupatwa na mkazo zaidi wa kisaikolojia. Dakt. Waite aligundua kwamba “ndoa hubadili tabia ya watu na kuwafanya wawe bora,” kama vile kupunguza kunywa kileo. Ndoa pia yaonekana hupunguza mshuko-moyo. Kwa kweli, “waseja wakiwa kikundi walikuwa wameshuka moyo mwanzoni mwa uchunguzi huo na wakashuka moyo hata zaidi ikiwa waliendelea kuwa waseja.” Hata hivyo, Dakt. William J. Doherty, wa Chuo Kikuu cha Minnesota ataarifu kwamba takwimu huwakilisha idadi ya wastani tu, na haimaanishi kwamba ni afadhali mtu afunge ndoa au kwamba watu wanaofunga ndoa na mtu wasiyefaana watakuwa wenye furaha na afya.
Mashujaa Wajeuri
Baadhi ya violezo vya kuigwa vilivyo maarufu sana vinavyochaguliwa kwa ajili ya watoto ni mashujaa wa sinema zenye mfululizo wa mapigano, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni juu ya athari ya jeuri katika vyombo vya habari. Kati ya watoto elfu tano wa umri wa miaka 12 waliohojiwa katika nchi 23, asilimia 26 ya watoto hao waliwatanguliza mashujaa hao wa sinema “mbele sana ya watumbuizaji mashuhuri na wanamuziki (asilimia 18.5), viongozi wa kidini (asilimia 8), au wanasiasa (asilimia 3)” kuwa violezo vyao vya mwenendo, lataarifu Jornal da Tarde la Brazili. Profesa Jo Groebel, mratibu wa uchunguzi huo, asema kwamba watoto kwa wazi huwachukulia mashujaa wenye jeuri kuwa violezo vya jinsi ya kushinda hali ngumu. Kadiri watoto wanavyozoea ujeuri, Groebel aonya, ndivyo wawezavyo kuwa wenye tabia ya kupita kiasi. Yeye aongeza hivi: “Vyombo vya habari hueneza wazo la kwamba jeuri ni kitu cha kawaida, na kwamba ni yenye faida.” Groebel alikazia kwamba wazazi hutimiza fungu muhimu katika kuwaandalia watoto wao mwongozo ambao huwasaidia kupambanua habari za kubuniwa na zile za uhalisi.
Msaada wa Kielektroni kwa Wapweke
Njia ya karibuni zaidi ya mpweke kukutana na mpweke mwingine katika Japani, ni kwa kutumia “bipa ya mapenzi,” laripoti Mainichi Daily News. Bipa hiyo ina kisehemu cha kuchagua mambo mbalimbali yapendelewayo: karaoke (kuimba kwa kufuatana na muziki uliorekodiwa), marafiki, na gumzo. Tuseme kijana amtafuta msichana wa kuzungumza naye. Yeye huchagua “gumzo” kwenye bipa yake. Akiwa hatua chache karibu na msichana ambaye amechagua “gumzo” pia kwenye bipa yake ya mapenzi, bipa hizo huanza kutoa mlio na kumweka rangi ya kijani kibichi. Tayari, watu 400,000 wamenunua bipa hizo. Wale wenye shaka juu ya aina ya mtu wawezaye kukutana naye waweza kuzima milio hiyo na kutegemea mimweko ya mwangaza peke yake. Takeya Takafuji, mkurugenzi wa mipango ya watengenezaji asema hivi: ‘Iwapo mtu huyu wa makamo hakupendezi, au hutaki kuzungumza naye, basi unaenda tu zako.’
“Kisababishi Kikuu cha Vifo vya Wanawake Vijana”
Katika nchi zilizoendelea kiuchumi, maradhi ya kifua kikuu mara nyingi huwapata wanaume wenye umri wa miaka 65, charipoti kichapo Nando Times. Lakini kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), maradhi ya kifua kikuu yamekuwa “kisababishi kikuu cha vifo vya wanawake vijana tufeni pote,” yasema ripoti hiyo. “Wake, akina mama na wafanyakazi hufa wakiwa vijana,” ataarifu Dakt. Paul Dolin, wa Idara ya Programu ya Kifua Kikuu Duniani ya shirika la WHO. Wataalamu waliokusanyika Göteborg, Sweden, katika semina moja ndogo ya kitiba, walisema kwamba wanawake zaidi ya milioni 900 wana maradhi ya kifua kikuu ulimwenguni kote. Milioni moja hivi kati yao watakufa kila mwaka, wengi wakiwa kati ya umri wa miaka 15 na 44. Sababu moja ya kiwango hiki cha kifo, kulingana na gazeti la habari la Brazili O Estado de S. Paulo, ni kwamba watu wengi hukatiza matibabu kabla maradhi hayajatibiwa.
Gari Lisilochafua Hewa
Magari ndiyo vyanzo vikubwa vya uchafuzi wa hewa katika majiji makubwa ya ulimwengu. Ili kushughulikia tatizo hili, mhandisi Mfaransa amebuni gari la mjini lisilotoa sauti na lisilo na harufu na “ambalo hutumia hewa tu inayotuzunguka,” laripoti gazeti The Guardian Weekly la London. Mbuni wa injini hiyo Guy Nègre ametengeneza mota inayotumia hewa iliyobanwa. Hiyo hugharimu kiasi kisichozidi dola mbili cha matumizi ya umeme ili kulijaza tangi lake la hewa iliyobanwa, kisha, katika hali za mjini, gari laweza kwenda kwa mwendo wa juu zaidi wa kilometa 100 kwa saa, kwa muda wa saa kumi. Gari hili hutumia hewa kutoka nje wakati wa kushika breki. Kwa sababu ya mfumo wake unaochuja hewa yenye kaboni, gari hilo hutoa nje hewa safi kuliko hewa linayofyonza kutoka nje. Baada ya kufanya majaribio kwa magari mengine yasiyochafua hewa, mamlaka ya Mexico yalichagua gari hili ili lichukue mahali pa zile teksi 87,000 za mji wa Mexico.
Eneo la Milima ya Alps Lililochafuliwa
Miaka 12 baada ya aksidenti ya mtambo wa nguvu za nyuklia katika Chernobyl, Ukrainia, eneo la milima ya Alps lingali limechafuliwa sana na cheche za mnururisho zilizotokana na mlipuko wa bomu la nyuklia. Uchunguzi wa hivi karibuni ulifunua viwango vingi vya isotopu nururishi Cesium-137, laripoti gazeti la habari la Kifaransa Le Monde. Katika sehemu fulani, unururifu ulikuwa wa kiwango cha juu cha mara 50 kuliko viwango vinavyojulikana kuwa uchafu wa nyuklia vya Ulaya. Sampuli zilizochafuliwa zaidi zilitolewa katika Mbuga ya Taifa ya Mercantour, kusini-mashariki mwa Ufaransa; Matterhorn, kwenye mpaka wa Uswisi na Italia; Cortina, Italia; na Mbuga ya Hohe Tauern, Austria. Mamlaka zaomba nchi zinazoathiriwa kuchunguza viwango vya mnururisho katika maji na vyakula vinavyoshukiwa, kama vile viyoga na maziwa.
Kula Pamoja na Familia
Katika uchunguzi uliofanyiwa vijana 527, wale waliokula chakula kikuu cha siku pamoja na familia zao angalau mara tano kwa juma “hawakuelekea sana kutumia dawa za kulevya au kushuka moyo, walikuwa wakifanya vizuri shuleni na walikuwa na mahusiano bora pamoja na marika zao,” lasema gazeti la habari la Kanada Toronto Star. “Matineja ambao walifafanuliwa kuwa ‘wasio na mazoea mazuri’ walikula pamoja na familia zao mara tatu au chache zaidi kwa juma.” Mwanasaikolojia Bruce Brian asisitiza kwamba familia kula pamoja mlo mkuu wa siku ni “kitabia cha familia bora.” Kula pamoja huimarisha vifungo vya muungano wa familia, stadi za mawasiliano, na kujihisi kuwa sehemu ya wengine, yaandika ripoti hiyo, na huandaa nafasi ya kujifunza adabu za wakati wa milo na kushiriki katika mazungumzo, ucheshi, na sala. Binti wa familia moja iliyokuwa ikila pamoja asema kwamba iwapo hawangekuwa na kawaida ya kufanya hivyo, “sidhani ningekuwa na ukaribu nilio nao kwao sasa.”
Uziwi Unaosababishwa na Vipokea-Sauti Vinavyobanwa Kichwani
Uchunguzi uliofanywa na shirika la National Acoustic Laboratory la Australia ulifunua kwamba hata matumizi ya kawaida ya vipokea-sauti vinavyobanwa kichwani vya stirio vya kibinafsi vyaweza kusababisha madhara yasiyoonekana wazi ya masikio, charipoti kichapo The Courier-Mail cha Brisbane. Mtafiti Dakt. Eric LePage alisema kwamba vijana husita kuyachukua maonyo hayo kwa uzito. “Kwa kurudia-rudia, wao waweza kujihatarisha kwa kusikiza kelele nyingi sana au muziki wa sauti ya juu sana kwa miaka mingi, nao hudhani kwamba haziwezi kuwaathiri,” akasema. Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba maonyo “hayakuwa na maana sana kwa watu mpaka walipoanza kupatwa na uziwi,” likasema gazeti hilo. Utafiti huo mpya wathibitisha uchunguzi wa Ujerumani ukionyesha kwamba robo moja hivi ya wanajeshi waliosajiliwa karibuni wenye umri wa miaka 16 na 24 tayari wamedhuru uwezo wao wa kusikia kwa kusikiliza muziki wa sauti za juu na kwamba “karibu asilimia 10 ya wanafunzi wenye umri wa miaka 16 hadi 18 walikuwa wamepoteza sana uwezo wa kusikia hivi kwamba walikuwa na matatizo ya kufahamu mazungumzo ya kawaida.”
Tumbaku Yadhamini Michezo
Kwa kuwa wanabiashara wa tumbaku hutumia sana matukio ya michezo na vitumbuizo vinginevyo ili kuendeleza bidhaa zao, “ushirikiano mzuri kati ya michezo . . . na uvutaji sigareti” umetokezwa, asema Rhonda Galbally, wa Victorian Health Promotion Foundation ya Australia. Tokeo ni kwamba, ule utangazaji wenye ujanja katika michezo huwachochea watu kuvuta sigareti. Kampeni ya Utafiti wa Kansa katika Uingereza iligundua kwamba “wavulana wanaofurahia kutazama mashindano ya kimataifa ya mbio za magari kwenye televisheni wana mwelekeo maradufu wa kuanza kuvuta sigareti,” laripoti shirika la habari la Panos. “Kotekote Ulaya, makampuni ya tumbaku hutumia mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka katika kutegemeza mashindano ya magari pekee.” Na magari hayo ni matangazo ya biashara ambayo hutokea mara nyingi kwenye televisheni.
Wakulima wa Kwanza
Gazeti la habari la Kifaransa Le Monde laripoti kwamba kundi la wataalamu wa Ulaya waligundua kwamba DNA ya namna za ngano za mwituni katika Eneo Lenye Rutuba la Mashariki ya kati zilifanana sana na namna-namna za ngano zinazokuzwa kwingineko leo. Pamoja na ngano na mengine ya “mazao ya awali,” yaonekana wanyama waliofugwa mapema kama vile kondoo, mbuzi, nguruwe, na ng’ombe walifugwa pia katika eneo hilo. Wataalamu husema kwamba kutumia mazao ya nyumbani kulienea kutoka huko, na kuvuka hadi Ulaya na Asia. Kwa kupendeza, baadhi ya vijiji vya kilimo vya mapema ambapo ngano iligunduliwa maelfu ya miaka, vyasemekana kuwa katika sehemu ya kusini magharibi mwa Ziwa Van na milima ya Ararat.