Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w02 3/1 kur. 26-30
  • Ubatizo wa Clovis—Miaka 1,500 ya Ukatoliki Nchini Ufaransa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ubatizo wa Clovis—Miaka 1,500 ya Ukatoliki Nchini Ufaransa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Milki Iliyokuwa Inadidimia
  • Mwanamume Aliyekuja Kuwa Mfalme
  • Ubishi wa Arius
  • Clovis Alikuwa Mtu wa Aina Gani Hasa?
  • Maadhimisho Yenye Ubishi
  • Miaka 1,500 ya Ukatoliki
  • Jinsi Jumuiya ya Wakristo Ilivyokuja Kuwa Sehemu ya Ulimwengu Huu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Sehemu 13: 476 W.K. na Kuendelea—Kutoka Gizani, Kikaja Kitu “Kitakatifu”
    Amkeni!—1990
  • Uasi-Imani—Njia ya Kwenda Kwa Mungu Yazibwa
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Ile Serikali Kubwa ya Sita ya Ulimwengu Roma!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
w02 3/1 kur. 26-30

Ubatizo wa Clovis—Miaka 1,500 ya Ukatoliki Nchini Ufaransa

“KATIKA jina la Papa, na ilipuke,” ukasema ujumbe uliokuwa kwenye bomu ya kujitengenezea iliyogunduliwa katika kanisa moja huko Ufaransa ambalo Papa John-Paul wa Pili alikuwa alitembelee mnamo Septemba 1996. Jambo hilo lilionyesha upinzani mkali ambao Papa alikabili wakati wa ziara yake ya tano nchini Ufaransa. Hata hivyo, mwaka huo, watu wapatao 200,000 walikuja katika jiji la Reims, Ufaransa, kuadhimisha pamoja na papa mwaka wa 1,500 tangu Mfalme Clovis wa Ufaransa ageuzwe imani kuwa Mkatoliki. Mfalme huyo alikuwa nani ambaye ubatizo wake umeitwa ubatizo wa Ufaransa? Na kwa nini kuadhimishwa kwa ubatizo huo kulisababisha ubishi?

Milki Iliyokuwa Inadidimia

Clovis alizaliwa wapata mwaka wa 466 W.K. Alikuwa mwana wa Childeric wa Kwanza, mfalme wa kabila la Salian Franks (mojawapo ya makabila ya Wafrank kutoka Ujerumani). Baada ya kushindwa na Waroma mwaka wa 358 W.K., kabila hilo liliruhusiwa kuishi katika eneo ambalo sasa ni Ubelgiji kwa masharti kwamba wangelinda mpaka na kutoa askari kwa ajili ya jeshi la Roma. Kwa sababu ya kuishi karibu na Waroma na Wagaul, kabila hilo liliiga utamaduni wa Waroma. Childeric wa Kwanza alikuwa rafiki ya Waroma, na alipigana na wavamizi wa makabila mengine ya Ujerumani, kama vile Wavisigoth na Wasaxon. Wakazi hao Waroma na Wagaul walimshukuru sana kwa jambo hilo.

Wilaya ya Roma ya Gaul ilianzia Mto Rhine, upande wa kaskazini, hadi Pyrenees, upande wa kusini. Hata hivyo, baada ya kifo cha Generali Mroma aitwaye Aetius, mwaka wa 454 W.K., wilaya hiyo iliachwa bila mtawala. Isitoshe, kuanguka kwa Romulus Augustulus, mtawala wa mwisho wa Roma, mwaka wa 476 W.K. na pia kuanguka kwa milki ya magharibi ya Roma, kulisababisha vurugu kubwa ya kisiasa katika eneo hilo. Kwa sababu hiyo Gaul ilikuwa kama tunda bivu lililokuwa tayari kuchunwa na moja ya makabila yaliyokuwa yanaishi karibu na mipaka yake. Si ajabu kwamba baada ya kurithi mamlaka ya babake, Clovis alianza kupanua mipaka ya ufalme wake. Katika mwaka wa 486 W.K., alimshinda balozi wa mwisho wa Roma aliyekuwa Gaul katika mapigano yaliyotokea karibu na jiji la Soissons. Ushindi huo ulimwezesha kutawala eneo lote katikati ya mto Somme, upande wa kaskazini, na mto Loire, upande wa kati na wa magharibi mwa Gaul.

Mwanamume Aliyekuja Kuwa Mfalme

Tofauti na makabila mengine ya Ujerumani, Wafrank walikuwa wapagani. Hata hivyo, maisha ya Clovis yalibadilika sana alipomwoa Clotilda, binti-mfalme wa Burgundia. Clotilda alikuwa Mkatoliki mwenye bidii sana, na alijitahidi sana kumgeuza mume wake awe Mkatoliki. Kulingana na historia iliyoandikwa na Gregory wa Tours katika karne ya sita W.K., Clovis aliahidi kuacha upagani ikiwa Mungu wa Clotilda angempa ushindi dhidi ya kabila la Alemanni alilopigana nalo huko Tolbiac (Zülpich, Ujerumani) mwaka wa 496 W.K. Ingawa majeshi ya Clovis yalikuwa karibu kushindwa, mfalme wa Alemanni aliuawa na jeshi lake likasalimu amri. Clovis alifikiri kwamba Mungu wa Clotilda alimpa ushindi. Kulingana na hekaya, Clovis alibatizwa na “Mtakatifu” Remigius katika kanisa la Reims, Desemba 25, 496 W.K. Hata hivyo, wengine hufikiri kwamba yaelekea alibatizwa baadaye katika mwaka wa 498/499.

Jitihada za Clovis za kunyakua ufalme wa Burgundia uliokuwa kusini-mashariki zilishindwa. Lakini alishinda vita vyake dhidi ya Wavisigoth mwaka wa 507 W.K. huko Vouillé, karibu na Poitiers. Ushindi huo ulimwezesha kutawala sehemu kubwa kusini-magharibi mwa Gaul. Kwa kutambua ushindi huo, Anastasius, maliki wa Milki ya Roma ya Mashariki, alimpa Clovis cheo cha heshima cha ubalozi. Hivyo akawa na cheo kikubwa kuliko wafalme wote wa magharibi, na utawala wake ukakubaliwa na Waroma na Wagaul.

Baada ya kuliweka eneo la Wafrank walioishi karibu na Mto Rhine upande wa mashariki chini ya utawala wake, Clovis alifanya Paris kuwa jiji lake kuu. Mwishoni mwa maisha yake, Clovis aliimarisha ufalme wake kwa kutoa sheria zilizoandikwa ambazo ziliitwa Lex Salica. Pia alifanya mkutano pamoja na baraza la kanisa huko Orléans ili kufafanua uhusiano kati ya Kanisa na Serikali. Alipokufa, yaelekea katika Novemba 27, 511 W.K., alikuwa ndiye mtawala pekee wa sehemu kubwa ya Gaul.

Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema kwamba kugeuzwa imani kwa Clovis kuwa Mkatoliki kulikuwa “jambo muhimu sana katika historia ya Ulaya magharibi.” Kwa nini kugeuzwa imani kwa mpagani huyo kulikuwa jambo muhimu hivyo? Hiyo ni kwa sababu Clovis alichagua kuwa Mkatoliki badala ya kufuata mafundisho ya Arius.

Ubishi wa Arius

Arius, aliyekuwa kasisi huko Aleksandria, Misri, alianza kueneza mafundisho tofauti kabisa kuhusu Utatu wapata mwaka wa 320 W.K. Arius alikataa fundisho kwamba Mwana alikuwa sawa na Baba. Mwana hawezi kuwa Mungu wala kuwa sawa na Baba, kwa kuwa alikuwa na mwanzo. (Wakolosai 1:15) Kuhusu roho takatifu, Arius aliamini kwamba roho ni mtu lakini aliye mdogo kuliko Baba na Mwana. Mafundisho hayo yaliyopendwa sana yalizusha ubishi mkali katika kanisa. Katika mwaka wa 325 W.K., Baraza la Nisea lilimpeleka Arius uhamishoni na mafundisho yake yakashutumiwa.a

Hata hivyo, hatua hiyo haikumaliza ubishi huo. Ubishi huo wa kimafundisho uliendelea kwa miaka 60 hivi, huku maliki waliofuata wakiunga mkono pande mbalimbali. Hatimaye, katika mwaka wa 392 W.K., Maliki Theodosius wa Kwanza alifanya Ukatoliki wa asili pamoja na fundisho lake la Utatu kuwa dini rasmi ya Milki ya Roma. Wakati huohuo Wagoth waligeuzwa imani na Ulfilas, askofu mmoja Mjerumani, na kuwa wafuasi wa Arius. Makabila mengine ya Ujerumani yalikubali upesi aina hiyo ya “Ukristo.”b

Kufikia wakati wa Clovis, Kanisa Katoliki la Gaul lilikuwa na matatizo. Wavisigoth waliokuwa wafuasi wa Arius walikuwa wakijaribu kukandamiza Ukatoliki kwa kukataa kuruhusu maaskofu wengine wachukue mahali pa wale waliokufa. Isitoshe, kanisa hilo lilikuwa karibu kugawanyika na kuwa na papa wawili, huku makasisi wa pande zenye kupingana wakiuana huko Roma. Waandishi fulani Wakatoliki walifanya hali iwe mbaya hata zaidi kwa kutokeza wazo kwamba ulimwengu ungefikia mwisho mwaka wa 500 W.K. Hivyo, kugeuzwa imani kwa mshindi huyo Mfrank kuwa Mkatoliki kulionwa kuwa jambo lifaalo, lililokuwa dalili ya “milenia mpya ya watakatifu.”

Lakini Clovis aligeuza imani kwa makusudi gani? Ingawa hatuwezi kusema kwamba makusudi yake hayakuwa ya kidini, bila shaka Clovis alikuwa na miradi ya kisiasa akilini. Kwa kuchagua kuwa Mkatoliki, Clovis aliungwa mkono na Wagaul na Waroma waliokuwa wengi na pia viongozi wa kanisa. Jambo hilo lilimfanya awe na nguvu kuliko wapinzani wake wa kisiasa. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema kwamba “ushindi wake dhidi ya Gaul ulionekana kuwa vita vya ukombozi kutoka ukandamizaji wa wafuasi wenye kuchukiwa wa Arius, ambao walionekana kuwa wazushi.”

Clovis Alikuwa Mtu wa Aina Gani Hasa?

Katika matayarisho ya mwisho-mwisho ya maadhimisho hayo ya mwaka wa 1996, askofu mkuu wa Reims, Gérard Defois, alieleza kwamba ‘kugeuzwa imani kwa Clovis ni mfano wa jambo lililofikiriwa kwa makini na kwa busara.’ Hata hivyo, mwanahistoria Mfaransa Ernest Lavisse alisema: “Kugeuzwa imani kwa Clovis hakukubadili utu wake hata kidogo; mafundisho ya Injili ya fadhili na amani hayakumfikia moyo.” Mwanahistoria mwingine alisema: “Badala ya kumwomba Odin [mungu wa Norway], alimwomba Kristo bila hata kubadili utu wake.” Kama vile Konstantino alivyofanya baada ya kule kulikoitwa eti kugeuzwa imani kuwa Mkristo, Clovis alianza kuimarisha utawala wake kwa kuwaua wapinzani wake wote. Aliwaua “watu wake wote wa ukoo, hata wa ukoo wa mbali sana.”

Baada ya Clovis kufa, watu walianza kutunga hekaya ambazo zingemfanya aonekane kuwa mtu mtakatifu na mwenye sifa nzuri badala ya kuwa mpiganaji mkatili. Masimulizi ya Gregory wa Tours, ambayo yaliandikwa karibu karne moja baadaye, yanaonekana kuwa jitihada za kimakusudi za kumlinganisha Clovis na Konstantino, aliyekuwa maliki wa kwanza Mroma kukubali “Ukristo.” Na kwa kudai kwamba Clovis alikuwa na umri wa miaka 30 alipobatizwa, Gregory anajaribu kumlinganisha na Kristo.—Luka 3:23.

Utungaji huo wa hekaya uliendelezwa na Askofu Hincmar wa Reims katika karne ya tisa. Kwa kuwa wakati huo makanisa yalikuwa yaking’ang’ania mahujaji, yaelekea masimulizi ya maisha aliyoandika kuhusu askofu aliyemtangulia, “Mtakatifu” Remigius, yalinuiwa kuliongezea kanisa lake sifa na utajiri. Anasema katika masimulizi yake kwamba njiwa mweupe alileta kichupa cha mafuta ili kumtia mafuta Clovis wakati wa ubatizo—jambo ambalo kwa wazi linarejezea kutiwa mafuta kwa Yesu kupitia roho takatifu. (Mathayo 3:16) Hivyo, Hincmar akaonyesha kwamba kulikuwa na uhusiano kati ya Clovis, Reims, na ufalme, na pia akakubaliana na wazo kwamba Clovis alikuwa mtiwa-mafuta wa Bwana.c

Maadhimisho Yenye Ubishi

Aliyekuwa Rais wa Ufaransa Charles de Gaulle alisema hivi wakati mmoja: “Kwa maoni yangu, historia ya Ufaransa inaanza na Clovis, aliyechaguliwa awe mfalme wa Ufaransa na kabila la Wafrank, ambao waliipa Ufaransa jina lao.” Hata hivyo, si kila mtu aliye na maoni kama hayo. Maadhimisho ya miaka 1,500 tangu Clovis abatizwe yalikumbwa na ubishi. Katika nchi ambamo Kanisa na Serikali zimetenganishwa rasmi tangu mwaka wa 1905, wengi waliikosoa Serikali kwa kushiriki maadhimisho hayo waliyoyaona kuwa ya kidini. Wakati baraza la jiji la Reims lilipotangaza mipango ya kulipia jukwaa ambayo ingetumiwa wakati wa ziara ya papa, shirika moja lilipeleka jambo hilo mahakamani na uamuzi huo ukafutiliwa mbali. Wengine walihisi kwamba kanisa lilikuwa likijaribu kudhibiti imani na pia raia wa Ufaransa. Jambo lililotatanisha maadhimisho hayo hata zaidi ni kwamba chama kisichopendelea mabadiliko kiitwacho National Front na makundi ya Kikatoliki yenye imani kali yalimfanya Clovis kuwa nembo yao ya uwakilishi.

Wengine walikosoa maadhimisho hayo kwa sababu za kihistoria. Walisema kwamba ubatizo wa Clovis haukugeuza imani ya Wafaransa kuwa Wakatoliki, kwa kuwa Wagaul na Waroma walifuata kwa dhati dini hiyo hata kabla ya ubatizo huo. Na walidai kwamba ubatizo huo haukuashiria kuzaliwa kwa taifa la Ufaransa. Walisema kwamba taifa la Ufaransa lilianza hasa wakati ufalme wa Charlemagne ulipogawanywa mwaka wa 843 W.K., na Charles the Bald, wala si Clovis, akawa mfalme wa kwanza wa Ufaransa.

Miaka 1,500 ya Ukatoliki

Baada ya zaidi ya miaka 1,500, Ukatoliki unaendeleaje leo nchini Ufaransa ambayo imeitwa ‘binti wa kwanza wa Kanisa Katoliki?’ Kufikia mwaka wa 1938, Ufaransa ndiyo iliyokuwa na Wakatoliki wengi waliobatizwa duniani. Sasa imeshuka hadi nafasi ya sita, nyuma ya nchi kama Ufilipino na Marekani. Na ingawa kuna Wakatoliki milioni 45 nchini Ufaransa, milioni 6 tu ndio huhudhuria Misa kwa ukawaida. Uchunguzi uliofanywa karibuni ulionyesha kwamba asilimia 65 ya Wakatoliki nchini Ufaransa “hawazingatii mafundisho ya Kanisa kuhusu ngono,” na asilimia 5 hawamwoni Yesu kuwa “mtu mwenye umuhimu wowote.” Mielekeo hiyo isiyofaa ilimfanya papa aulize hivi wakati wa ziara yake nchini Ufaransa mwaka wa 1980: “Ufaransa, umefanya nini na ahadi zako za ubatizo?”

[Maelezo ya Chini]

a Ona gazeti la Mnara wa Mlinzi, Agosti 1, 1984, ukurasa wa 24, la Kiingereza.

b Ona gazeti la Mnara wa Mlinzi, Mei 15, 1994, ukurasa wa 8-9.

c Jina Louis linatokana na jina Clovis, ambalo wafalme 19 wa Ufaransa (kutia ndani Louis wa 17 na Louis-Philippe) walipewa.

[Ramani katika ukurasa wa 27]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

WASAXON

Mto Rhine

Mto Somme

Soissons

Reims

Paris

GAUL

Mto Loire

Vouillé

Poitiers

PYRENEES

WAVISIGOTH

Roma

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 26]

Ubatizo wa Clovis kama unavyoonyeshwa katika hati ya karne ya 14

[Hisani]

© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 28]

Sanamu ya kuchongwa inayoonyesha ubatizo wa Clovis (sanamu iliyo katikati) nje ya Kanisa la Reims, Ufaransa

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 29]

Ziara ya John Paul wa Pili nchini Ufaransa ya kuadhimisha ubatizo wa Clovis ilizusha ubishi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki