Je, Unaahirisha Kuijaza?
Kujaza nini? Kadi ya DPA (mamlaka ya kudumu ya uwakilishi) au kadi ya AMD (Mwelekezo wa Mapema Kuhusu Tiba) ambayo imeandaliwa kwa ajili ya Mashahidi waliobatizwa. Kwa kuwa ‘hujui uzima wako utakuwa namna gani kesho,’ ni muhimu uamue mapema na uandike dawa, matibabu, au mbinu za kitiba ambazo utakubali ukihitaji matibabu ya dharura. (Yak. 4:14; Mdo. 15:28, 29) Video yenye kichwa Transfusion-Alternative Health Care—Meeting Patient Needs and Rights imetayarishwa ili kukusaidia ufanye uamuzi. Itazame, kisha uipitie na kusali kuhusu mambo ambayo umejifunza kwa kutumia maswali yaliyo hapa chini.—Taarifa: Kwa kuwa video hii ina sehemu fupi zinazoonyesha watu wakifanyiwa upasuaji, wazazi wanapaswa kutumia busara wanapoitazama pamoja na watoto wadogo. Iwapo video hii haipatikani, zungumzieni “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 2004 na Oktoba 15, 2000, au “Je! Wewe Uko Tayari Kukabili Hali Ngumu ya Kitiba Yenye Kujaribu Imani?” katika Huduma Yetu ya Ufalme ya Novemba 1990.
(1) Kwa nini madaktari na wataalamu fulani wa afya wanabadili maoni yao kuhusu kutia damu mishipani? (2) Taja aina tatu za upasuaji mgumu unaoweza kufanywa bila kumtia mgonjwa damu. (3) Ni madaktari wangapi duniani ambao wamekubali kuwatibu au kuwafanyia wagonjwa upasuaji bila kuwatia damu? Kwa nini wamekubali kufanya hivyo? (4) Uchunguzi uliofanywa majuzi katika hospitali mbalimbali umeonyesha nini kuhusu matumizi ya damu? (5) Kutiwa damu mishipani kunaweza kusababisha matatizo gani ya afya? (6) Wataalamu wengi wamekata kauli gani kuhusu manufaa ya matibabu yasiyohusisha damu? (7) Ni nini kinachosababisha upungufu wa damu mwilini? Mtu anaweza kupungukiwa na damu kadiri gani na bado asiwe mgonjwa mahututi? Mtu mwenye upungufu wa damu anaweza kusaidiwaje? (8) Mgonjwa anaweza kupewa dawa gani ili mwili wake utengeneze chembe nyekundu haraka zaidi? (9) Madaktari wanatumia mbinu gani ili kuzuia damu nyingi isivuje wakati wa upasuaji? (10) Je, mbinu za matibabu zisizohusisha damu zinaweza kutumiwa kwa mafanikio kuwatibu watoto wachanga au mgonjwa mahututi? (11) Matibabu mazuri yanahusisha kanuni gani muhimu? (12) Kwa nini ni muhimu Wakristo waamue mapema watakubali matibabu gani yasiyohusisha damu? Tunaweza kufanyaje maamuzi hayo?
Kuchagua baadhi ya matibabu yanayoonyeshwa katika video hii ni uamuzi wa mtu binafsi, unaotegemea dhamiri yake inayoongozwa na Biblia. Je, umeamua kabisa ni dawa, matibabu, au mbinu gani za kitiba ambazo wewe na watoto wako mnakubali, na je, umeijaza kadi ya DPA au AMD? Habari kamili kuhusu mambo hayo zinapatikana katika sura ya 7 ya kitabu “Upendo wa Mungu” na marejeo yanayotajwa humo. Ona pia nyongeza “Nina Maoni Gani Kuhusu Visehemu vya Damu na Matibabu Yanayohusisha Damu Yangu Mwenyewe?” katika Huduma Yetu ya Ufalme ya Novemba 2006. Halafu, ndugu walio na kadi ya DPA, wanapaswa kuhakikisha wameandika kwa usahihi kwenye kadi zao matibabu waliyochagua. Wawakilishi wako wa kitiba na watu wa familia yako ambao si Mashahidi wanapaswa kuelezwa vizuri kuhusu maamuzi yako.
[Sanduku katika ukurasa wa 3]
• Je, umeamua ni dawa, matibabu, au mbinu gani za kitiba ambazo wewe na watoto wako mnaweza kukubali?
• Je, nyakati zote unabeba kadi ya DPA au ya AMD ambayo imejazwa vizuri, ili itetee msimamo wako wakati wa dharura?