Wakosa Kuvumiliwa Kwa Mara Nyingine
KWA zaidi ya miaka mitatu, kutoka 1972 mpaka 1975, Msumbiji ilikuwa kimbilio la Mashahidi wa Yehova zaidi ya elfu 30 wa nchi jirani ya Malawi. Wanaume, wanawake na watoto hao Wamalawi walikuwa na amani katika kambi kumi za watoro katika Msumbiji, baada ya kulazimika kuikimbia nchi yao kwa sababu ya mateso makali. Habari za karibuni zaonyesha kwamba, wakati wa kuandikwa kwa habari hii katika Awake! (la Januari, 8, 1976), kungali kuna hesabu kubwa waliokimbilia nchi hiyo. Mashahidi wa Yehova duniani pote wanashukuru watu wa Msumbiji kwa kuwapa kimbilio.
Walakini, kwa kuwa sasa Mashahidi wa Yehova wa Msumbiji wanashambuliwa vikali na watu fulani, kimbilio lao linaelekea kuwa mahali pa uonezi mbaya sana.
Katika Msumbiji, radio na magazeti yameeneza porojo nyingi juu ya Mashahidi wa Yehova. Wanaonyeshwa kuwa “mawakili wa Wareno Wakoloni walioachwa nyuma,” ‘makachero wa zamani wa Kireno,’ ambao lengo lao ni ‘kuharibu Serikali.’ (Noticias, Oktoba 9, 1975) Walisemekana kuwa ‘wanashikamana sana na ushupavu wa kidini . . . wakitumia hiyo kama njia ya kutolipa kodi, kutoheshimu Serikali na kuharibu mwungano na utaratibu wa Taifa,’ ili ‘kuchafua utawala,’ kulingana na yaliyosemwa na gazeti A Tribuna la Oktoba 22, 1975.
Linganisha hilo na habari nyingine iliyotoka katika chanzo tofauti. Inahusu kundi la watu wenye ghasia lililoingiza makelele katika mji mmoja kisha makutano ya watu wakakusanyika mbele ya wakuu wa mji wakipaza sauti na kusema, ‘Watu walioupindua ulimwengu wamefika huku nako na wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri.’
Habari hii ya pili ilikuwa ya miaka mia kumi na tisa iliyopita. Wakati huo mashitaka hayo yalifanywa kwa mtume wa Kikristo Paulo na mwenzi wake Sila. (Matendo 17:6, 7) Maneno hayo yaliyosemwa wakati huo yalikuwa uongo mtupu.
Maneno hayo ni ya uongo kabisa yanaposemwa juu ya Mashahidi wa Yehova, wanaojulikana sana kuwa Wakristo wenye kutii sheria katika nchi zaidi ya 200 za dunia. Mashitaka wanayofanyiwa leo katika Msumbiji yanafanana na mashitaka yale yale waliyofanyiwa Wakristo katika karne ya kwanza. Wakristo wa kweli sasa wanakosa kuvumiliwa kama zamani.
Tendo hilo la kutowavumilia Msumbiji halikuanza wakati serikali ilipobadilishwa mwaka wa 1975. Na hiyo inaonyesha kwamba madai yaliyofanywa kwamba Mashahidi wa Yehova wa huko wanatumiwa na Wareno Wakoloni ni ya uongo. Mambo ya hakika yaonyesha kwamba madai hayo si ya kweli hata kidogo.
Kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita Mashahidi wa Yehova katika Msumbiji hawavumiliwi na utawala wa kutumia nguvu. Wao walitendwa kikatili mikononi mwa PIDE (makachero wa Kireno). Sasa angalia yanayoonyeshwa kuwa mambo ya hakika:
HISTORIA YATOA USHUHUDA
Huko nyuma mwaka wa 1925 wanaume wa Msumbiji waliokuwa wakifanya kazi katika mashimo ya kuchimba dhahabu ya Afrika Kusini walipokea vitabu kadha vya Mashahidi wa Yehova vyenye kueleza mafundisho ya Biblia. Baadhi ya wanaume hao walianza kuzungumza na jirani zao juu ya mambo waliyojifunza, waliporudi makwao mwaka huo katika Vila Luisa (kaskazini ya Lourengo Marques, mji mkuu wa Msumbiji).
Hivyo, wenyeji wa Msumbiji, si wamisionari wa kigeni wala mawakili wa Wareno, ndio walioingiza nchini ujumbe wa ufalme wa Mungu ambao Mashahidi wa Yehova hupeleka duniani pote.
Wakati wa utawala wa Antonio Salazar mtumia nguvu, mwaka wa 1935, Mashahidi wawili wa Afrika Kusini, Fred Ludick na David Norman, waliingia nchini washirikiane na Mashahidi wa Msumbiji katika utendaji wao. Kukatukia nini? Karibuni walikamatwa na polisi Wareno wakafukuzwa. Wengine walifanya jitihada kama hizo mwaka wa 1938 na 1939 lakini matokeo yakawa yale yale: kufukuzwa mara moja.
Lakini, sasa wakuu Wareno walichukua hatua zaidi. Walianza kukamata watu wa Msumbiji waliokuwa wakipokea gazeti Mnara wa Mlinzi. Wengine walikaa jela hata miaka miwili kabla ya kupelekwa mahakmani. Wengine walipelekwa kwenye koloni la kuadhibia watu la Sao Tome kwa miaka kumi na miwili! Wengine walihukumiwa kifungo cha miaka kumi katika kambi za kazi katika kaskazini ya Msumbiji.
Upinzani mkali huo uliokuja chini ya utawala wa Salazar mtumia nguvu ulijaribu ushujaa na uvumilivu wa Mashahidi wa Yehova Msumbiji. Walipokutana kujifunza Biblia pamoja, sikuzote kulikuwa na hatari ya kuweza kukamatwa. Miaka ilipoendelea, wengi walikamatwa, wakapigwa, wakafungwa au wakapelekwa kwenye visiwa vya kuadhibia watu.
Jitihada za kuwafungua zilikataliwa. Mwaka wa 1955 mmoja wa Mashahidi wa Yehova kutoka Uingereza, John Cooke, alitumwa Msumbiji akafanye ombi kazi ya Mashahidi wa Yehova ipate kutambuliwa rasmi. Baada ya muda fulani aliletwa mbele ya mkaguzi wa makachero (PIDE) akaulizwa maulizo mengi sana. Alishtakiwa kuwa Mkomunisti mwenye kufanya mikutano ya siri. Ingawa mahojiano yalimsadikisha mkuu huyo kwamba Mashahidi wa Yehova si Wakomunisti, yeye alimwambia Cooke hivi: “Hata hivyo, ninyi mnapinga Kanisa Katoliki nalo Kanisa Katoliki ndilo kanisa letu. Lilitusaidia kuukuza Utawala wa Kireno!” Cooke alipewa saa 48 za kuondoka nchini.
Gazeti la kila siku la Msumbiji Noticias la Oktoba 9, 1975, lamtaja kiongozi wa Frelimo ambaye ndiye rais wa Msumbiji Samora Machel akiuliza ulizo hili (katika Massingir, Msumbiji): “Tulipofungwa na kupigwa na wakoloni Wareno, hawa Mashahidi wa Yehova walikuwa wapi?” Walikuwa wapi? Jibu la wengi wa Mashahidi wa Yehova ni kwamba walikuwa wamefungwa wakati huo na wakuu ao hao Wareno!
Kwa mfano, tumchukue Francisco Zunguza. Alitiwa gerezani katika Lourenco Marques mwaka wa 1956 kwa miezi sita; mwaka wa 1964 kwa miezi mitatu; mwaka wa 1965 kwa mwaka mmoja; na mwaka wa 1969 alitiwa katika gereza la Machava kwa zaidi ya miaka miwili. Mkewe na Mashahidi wengine kumi walikamatwa wakati huo pia.’ Walifanyiwa hivyo kwa sababu ya kuwa Mashahidi wa Yehova tu, si kwa sababu ya tendo lo lote la kutaka kufitini serikali ya Kireno.
Kutoka mwaka wa 1969 na kuendelea makachero wa Kireno (PIDE) waliongeza msako wao juu ya Mashahidi wa Yehova. Mara nyingi walitiwa nguvuni wakaulizwa maulizo. Nao wakuu Wareno na makachero walishitaki Mashahidi juu ya nini? Kwamba walikataa kushiriki kuwapiga Frelimo, chama cha wataka mapinduzi ambacho kilikuwa kimepata nguvu wakati huo na ambacho sasa ndicho serikali ya Msumbiji!
Mashahidi wa Yehova walieleza wazi kutokuwamo kwao katika siasa zote na vita vya mataifa. Msimamo wao ulipatana kabisa na maneno ya Kristo Yesu, aliyomwambia gavana wa Kirumi, Pontio Pilato: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi.”—Yohana 18:36.
Mwaka uo huo, 1969, wazee wa makundi ya Mashahidi wa Yehova kusini ya Msumbiji waliitwa wafike katika afisi za polisi. Wakaambiwa kwamba utendaji na mikutano ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa imepigwa marufuku. Ingawa walizuiwa sana, waliweza kuendelea kusonga mbele, akitenda kupatana na msimamo ambao mitume wa Kristo Yesu walichukua wakati wakuu wa Yerusalemu walipojaribu kuwalazimisha watii marufuku juu ya utendaji wao. Mitume walikabiliwa na uchaguzi wa kutii wakuu wa Kiyahudi au kutii amri ya Mungu. Ingawa walikuwa watu wenye kutii sheria, walisema kwa ujasiri kwamba, kwa kuwa amri ya wakuu ilipingana na ya Mungu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.”—Matendo 5:29.
Mwaka wa 1969 kulikuwa na lalamiko la kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuwapiga Frelimo. Lakini mwaka wa 1973 makachero (PIDE) walikamata Mashahidi kadha, na wakati huu shtaka lilikuwa kwamba walikuwa wafuasi wa Frelimo! Baba mmoja Shahidi mwenye watoto watatu alitiwa katika chumba kidogo cha gereza la Machava Machi 5,1975, kwa shtaka hilo. Aliwekwa kizuizini akiwa peke yake kwa miezi miwili, akilala sakafuni bila matandiko. Yeye ni mmoja tu wa mifano mingi kama hiyo ya kutendwa isivyo haki wakati wa miaka ya mwisho ya utawala wa Wareno Msumbiji. (Itaendelezwa)