Tumbako na Afya Yako—Je! Kweli Mambo Haya Yana Uhusiano?
“Asante kwa Kutovuta Sigareti”—Ishara ya nyakati.
“Asante kwa Kuvuta Sigareti”—Shambulio la ukinzani katika gazeti moja la kampuni ya tumbako.
PAMBANO lenyewe laanza, huku kalamu na kompyuta za kueneza propaganda zikifanyishwa kazi. Mashirika ya utangazaji yapeleka nje jumbe zayo zenye kupingana. Vita hii hupigwa katika soko la ulimwengu. Ni ile vita ya kushindania kuuza tumbako, na mapato huwa makubwa. Mabilioni ya dola kila mwaka. Uwe au usiwe u mvutaji, wewe waathiriwa na jambo hilo.
Ni vita yenye kupigwa kuhusu mambo makubwa mawili—mambo ya uchumi na afya. Kwa wale walio dhidi ya kuvuta sigareti, afya ndilo jambo la kutangulizwa mbele kabisa. Jambo la maana ambalo huhangaikiwa na watengenezaji wakuu wa tumbako na wale wenye kushikamana sana na biashara hiyo ni uchumi, faida, na kazi. Hisia-moyo na njia za kuitikia mambo huelekea kuchemka. Kwenye uwanja mmoja wa ndege mvutaji sigareti aliomba msimama-kando mmoja moto wa kuwashia sigareti. “Pole, mimi huwa sivuti sigareti,” akajibiwa kwa weupe wa moyo. “Mimi sikukuuliza kama wewe huvuta sigareti!” mvutaji huyo kamtolea meno nje kwa kuchukizwa.
Lakini ni nini kiini hasa cha ubishi huu? Je! kweli kuvuta sigareti ni jambo baya sana kwako? Je! wewe wapaswa kuacha kuvuta?
Maonyo ya Serikali Kuhusu Afya
Suala la tumbako na kansa limejadiliwa kwa miongo ya miaka katika United States. Biashara ya tumbako imechanga mamilioni ya dola za utafiti huko nyuma katika miaka ya 1960 yakisemwa kuwa ni ya kusaidia kuchunguza vizuri ni nini hasa hutokeza uhusiano uliopo kati ya kansa na tumbako na hivyo kupata njia fulani ya kutengeneza sigareti zisizo na visababishi vya kansa. Tokeo moja labda limewagutusha watengeneza tumbako kwa kuonyesha mambo wasiyokuwa wametazamia.
Katika 1964 mpasuaji mkuu wa United States alitoa ripoti yake ya kwanza ikionya dhidi ya hatari za kuvuta sigareti. Muda wote wa tangu 1965, watengeneza sigareti wa United States wamefungwa na sheria kuchapa maandishi yenye maonyo juu ya pakiti zao. Kwanza ujumbe wenyewe haukuwa na mkazo mwingi: “Onyo: Mpasuaji Mkuu Ameamua Kwamba Kuvuta Sigareti Ni Hatari kwa Afya Yako.” Halafu katika 1985 kampuni za tumbako zikatakwa ziwe zikibadilisha-badilisha jumbe nne katika matangazo yazo na katika bidhaa zazo. Kila ujumbe waanza kwa maneno haya: “ONYO LA MPASUAJI MKUU.” Halafu zile jumbe tofauti-tofauti zasema: “Kuvuta Sigareti Husababisha Kansa ya Mapafu, Ugonjwa wa Moyo, Ugonjwa wa Kusakama kwa Hewa Katika Viungo, Na Huenda Kukatatanisha Mimba.” (Ona sanduku katika ukurasa 4.) “Huenda Kuvuta Sigareti kwa Wanawake Wenye Mimba Kukajeruhi Kijusi, Kukazalisha Mtoto Kabla Hajakomaa, Na Kufanya Mtoto Azaliwe Akiwa na Uzani Mwepesi.” “Kuacha Sasa Kuvuta Sigareti Hupunguza Sana Hatari Zenye Kupata Afya Yako.” “Moshi wa Sigareti Una Kaboni Monoksaidi.”a
Nchi fulani nyinginezo pia, mbali na United States, hutoa maonyo kuhusu sigareti. Gazeti India Today huwa na tangazo ambalo huhusisha ndani maneno haya: “ONYO LA KIKATIBA: KUVUTA SIGARETI HUDHURU AFYA.” Katika Kanada walikuwa wakisema hivi kwa maandishi madogo: “Onyo: Kanada Yenye Kuhusika na Afya na Hali Njema yashauri kwamba hatari kwa afya huongezeka kulingana na kiasi cha moshi wenye kuvutwa—epuka kuuvuta ndani.” Tangu Mei 31, 1988, kutangaza tumbako kumepigwa marufuku katika Kanada. Katika Uingereza matangazo ya sigareti huhusisha ndani maneno haya: “LAMI YA KIWANGO CHA KADIRI [au LAMI YA KIASI KIDOGO] Kama ilivyoelezwa na Serikali ya Mheshimiwa HATARI: ONYO la Serikali Kuhusu Afya: SIGARETI ZAWEZA KUHARIBU SANA AFYA YAKO.” Kutangaza tumbako kumepigwa marufuku katika Italia muda wote wa tangu 1962. (Hata hivyo Waitalia wamerudufisha uvutaji wao wa sigareti muda wa miaka 20 iliyopita!) Kukiwako maonyo mengi sana yenye kutegemea ushuhuda mwingi mno wa kisayansi, kukiwa na uchunguzi mbalimbali 50,000 muda wa miaka iliyopita, neno-mkataa haliepukiki—kuvuta sigareti ni hatari kwa afya yako!
Ingawa kuvuta sigareti ni hali ya ulimwenguni pote, si nchi zote ambazo hudai kwamba maandishi yenye maonyo yachapwe juu ya bidhaa yenyewe. Na wakati masoko yapungukiwapo na mapato katika eneo moja, yale mashirika makubwa sana ya tumbako hutumia matangazo yao yenye kubana watu sana ili kufungua masoko katika nchi nyinginezo. Je! nchi yako huathiriwa na matangazo thabiti yahusuyo tumbako? Je! sigareti za nchi za kigeni hufanywa zionekane kuwa za kuvutia zaidi? Ni kitu gani hasa husababisha yale “mauzo makubwa”?
[Maelezo ya Chini]
a Kaboni monoksaidi, ambayo ni gesi isiyo na harufu, hufanyiza asilimia 1 hadi 5 ya moshi wa sigareti nayo huchangamana sana na hemoglobini, ile molekyuli yenye kubeba oksijeni katika damu. Hupunguza ile oksijeni muhimu ipasayo kuwa inazunguka katika damu. Jambo hili laweza kuwa hatari kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa moyo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4, 5]
UVUTAJI SIGARETI na Wanawake Wenye Mimba
Hivi majuzi gazeti Nauka I Zhizn la Urusi (Sayansi na Uhai) lilitangaza kwa chapa makala iliyotungwa na Dakt. Victor Kazmin ambamo alieleza kirefu hatari ambazo hupata mama na mtoto ikiwa mama avuta sigareti wakati wa mimba. Alitaarifu hivi: “Kuvuta sigareti huleta dhara kubwa sana kwenye mwili wa mwanamke, ambao maumbile yao yaliyo tofauti sana huufanya uathiriwe kwa urahisi na vitu vyenye sumu. Ingawaje, moshi wa tumbako una vitu ambavyo ni tisho kubwa kwa afya.”
Yeye ataarifu kwamba kwa kweli akina mama wenye kuvuta sigareti waweza kutia sumu katika watoto wao. “Uchunguzi mbalimbali ambao umechanganuliwa katika maabara umeonyesha ule umajimaji wa nyungu ya uzazi ya wagonjwa hao wanawake huwa ina sumu-sumu—nikotini na kifanyizo chayo, kotinini. Lakini kama vile imegunduliwa na uchunguzi wa kutumia darubini ya kielektroni, jambo lililo la kuogopesha zaidi ni kwamba kwa wanawake wenye kuvuta sigareti wakati wa mimba hata umbo la ukanda wa kitovu hubadilika; na ni kupitia ukanda huu kwamba kijusi hupokea mahitaji yote ya uhai kutokana na mama yacho. . . .
“Ikiwa mama avuta sigareti katika majuma mawili au matatu ya kwanza baada ya kuchukua mimba, wenye kuathiriwa vibaya zaidi huwa ni mfumo mkuu wa mishipa ya fahamu ya kiinitete . . . Katika juma la nne au la tano la kuwa na mimba mfumo wa mishipa ya moyoni hukua. Halafu jambo la kwanza kuupata huwa ni kuingiwa na sumu.”
Dakt. Kazmin akata shauri gani? Kwamba “moshi wa tumbako ni hatari zaidi kwa kijusi kuliko kwa mama mwenyewe.” Je! yastahiki kuuvuta? Kumbuka lile onyo la mpasuaji mkuu wa United States: “Kuvuta Sigareti . . . Huenda Kukatatanisha Mimba.” Tena maneno hayo yamesemwa kwa upole tu.
[Hisani]
WHO/Sosaiti ya Kansa Katika Amerika
UVUTAJI SIGARETI na Kusakama kwa Hewa Mapafuni
Kusakama kwa hewa mapafuni ni ugonjwa ambao hatua kwa hatua hufanya mapafu yapoteze unyumbufu (kupanuka-panuka), na mwishowe hiyo hufanya isiwezekane kutoa nje kiasi cha kutosha cha hewa mbaya. Kichapo Columbia University College of Physicians and Surgeons Complete Home Medical Guide chaeleza hivi: “Watu [katika United States] walio na ugonjwa wa kusakama kwa hewa mapafuni hufuata kigezo fulani: Hasa wao huwa ni wanaume, kati ya miaka 50 na 70, ambao wamekuwa ni wavutaji sana kwa miaka mingi. Wakati uliopita, ugonjwa wa kusakama kwa hewa mapafuni haukuanza kusitawi katika wanawake mara nyingi kama ilivyokuwa kwa wanaume, lakini kigezo hiki kinabadilika huku wanawake wakiendelea kuwa wavutaji sana.”
Kichapo icho hicho chaongezea hivi: “Huenda kwa miaka mingi ugonjwa wa kusakama kwa hewa mapafuni ukasingizia kuwa kitu kingine. Labda mtu mwenye ugonjwa wa kusakama kwa hewa mapafuni huwa amekwisha kuwa na mafua kadhaa mabaya sana kila majira ya kipupwe kwa miaka michache, huku kila mafua yakiandamana na kikohozi kizito, na labda mchochota wa daima wa mirija ya hewa mapafuni. Mara nyingi kikohozi kile huendelea na kuwa cha daima.” Ni nini dalili nyingine za kusakama kwa hewa mapafuni?
“Kusakama kwa hewa mapafuni husitawi polepole. Ugumu kidogo wa kupumua ambao huwapo asubuhi na jioni huenda ukafuatwa baadaye na mianzo ya kukatiza-katiza utendaji mbalimbali. Huenda kutembea mwendo mfupi kukatosha kumfanya mtu apumue-pumue kwa kukosa hewa; huwa ni vigumu kutembea akipanda vidato vya ngazini. Mwishowe, mapafu yazidipo kupungukiwa na utendaji wa kuvuta hewa ndani, kuitoa nje, na kubadilisha gesi, huenda ikafika hatua ambapo kila mpumuo utataka jitihada kubwa na mgonjwa yule atakuwa hajiwezi na hawezi kutekeleza utendaji wa kikawaida.”
Kiongozi icho hicho cha kitiba chaongezea kwamba kusakama kwa hewa mapafuni kwaweza kuongoza kwenye matatizo mazito ya mishipa ya moyoni. Je! kweli yastahiki kupatwa na tatizo hilo [kwa kuvuta sigareti]? Kwa nini uondoe zawadi yako ya uhai iliyo ya thamani kubwa kwa kuibadilishana na raha ya nikotini ambayo ni ya muda tu?