Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 6/8 kur. 21-23
  • Mapinduzi ya Ufaransa Muono wa Kimbele wa Mambo ya Wakati Ujao

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mapinduzi ya Ufaransa Muono wa Kimbele wa Mambo ya Wakati Ujao
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jumla ya Tabaka
  • Haki za Binadamu
  • Kanisa Lagawanyika
  • Hofu Kuu na Umwagaji wa Damu
  • Kufutilia Mbali Ukristo
  • Pigano la Biblia ya Kifaransa la Kuokoka
    Amkeni!—1997
  • Sehemu 2: Wafalme, Kama Nyota, Huinuka na Kuanguka
    Amkeni!—1991
  • Utawala wa Makasisi Je! Ndilo Jibu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Ni Nini Kimepata Mamlaka?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 6/8 kur. 21-23

Mapinduzi ya Ufaransa Muono wa Kimbele wa Mambo ya Wakati Ujao

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ufaransa

Mapinduzi ya Ufaransa yalitukia miaka 200 iliyopita, katika 1789. Visababishi vyayo vilikuwa nini? Yaliacha kielelezo gani cha mambo ya wakati ujao?

“JE! NI uasi?” akauliza mfalme.

“La, Sahib, ni mapinduzi.”

Mfalme Mfaransa Louis wa 16 aliuliza swali hilo mnamo Julai 14, 1789, siku ambayo Bastille ilishambuliwa katika Paris. Alionyesha kwamba ufalme wa Ufaransa ulishindwa kutambua matukio ambayo yangetokeza mabadiliko ya kudumu katika Ufaransa na ambayo yangeandaa muono wa kimbele wa mambo ya wakati ujao.

Katika karne ya 18, njaa ilikuwa imekwisha kutokeza maasi mengi katika Ufaransa. Usiku uliotangulia mapinduzi hayo, karibu milioni 10 kati ya idadi ya watu milioni 25 walitegemea msaada wa kifadhili. Kuongezea hayo, mamlaka ya kifalme ilikuwa inazorota, usimamizi ulikuwa haujali marekebisho, na watu wenye weledi waliuliza kama mamlaka ya mfalme yapasa kuwa juu zaidi ya masilahi ya kitaifa.

Jumla ya Tabaka

Mnamo 1788 utawala huo ulikabiliwa na hali mbaya ya kifedha, kwa sehemu kubwa kwa sababu ya Ufaransa kuunga mkono Waamerika katika Vita ya Uhuru wao dhidi ya Uingereza. Mfalme alilazimika kukusanya kile kilichoitwa Jumla ya Tabaka. Ilitia ndani wawakilishi kutoka tabaka tatu za taifa: makasisi (tabaka ya kwanza); masharifu (tabaka ya pili); na akina yahe (tabaka ya tatu).

Makasisi walikuwa watu 150,000 tu, masharifu karibu 500,000, na tabaka ya tatu zaidi ya 24,500,000. Kila moja ya tabaka hizi tatu ilikuwa na kura moja. Hilo lilimaanisha kwamba akina yahe (wenye kura moja) hawangeweza kutokeza marekebisho yoyote isipokuwa makasisi na masharifu (wenye kura mbili) wakubali. Kwa hiyo makasisi na masharifu—karibu asilimia 3 ya idadi yote ya watu—wangeweza kushinda kwa kura wale wengine asilimia 97! Kuongezea hayo, makasisi na waheshimiwa walikuwa na asilimia 36 ya ardhi ikiwa mali yao na hawakupaswa kulipa kodi za ardhi.

Watu wengi hivyo walipokuwa na njaa, wawakilishi wa akina yahe walikataa utawala wa kimabavu wa serikali, na mifumo isiyo ya haki ya kodi na kupiga kura, na ukosefu wa haki na utajiri wa viongozi wa kidini wa Katoliki na pia masharifu. Hata hivyo, mfalme alionekana ni imara, kwa kuwa alidhaniwa anatawala kwa haki ya kimungu. Na watu walikuwa wangali na imani katika dini ya Katoliki. Hata hivyo, kwa muda unaopungua miaka minne, utawala wa kifalme ulipinduliwa, na hatua ya kufutilia mbali Ukristo ikaanzishwa.

Katika masika ya 1789, hatua ya kimapinduzi ilianza. Kwa sababu baadhi ya masharifu walikataa kukubali badiliko katika mfumo wa uchaguzi, makaimu wa tabaka ya tatu walijitangaza kuwa Baraza Kuu la Taifa. Hiyo ikawa alama ya ushindi wa mapinduzi ya mabwanyenye (watu wenye mali nyingi) na mwisho wa utawala wa mtu mmoja tu.

Hata hivyo, wakulima wa mashamba, walihofu njama ya mfalme na utawala wa makabaila (tabaka ya juu) ya kupindua tabaka ya tatu. Hilo lilisukuma watu wapore na kuchukua nyara maburuji ya kifalme na mashamba makubwa ya makabaila, jambo ambalo lilizorota likawa maasi ya umma. Usiku wa Agosti 4, 1789, ili kutunza utaratibu, Baraza hilo liliamua kuondoa mapendeleo ya masharifu na kufutilia mbali utawala wa mamwinyi (matajiri wenye mashamba mengi). Kwa hiyo, katika siku chache tu, misingi ya utawala wa kale ikavunjwa-vunjwa.

Haki za Binadamu

Kisha Baraza hilo lilianzisha Tangazo la Haki za Mtu. Mawazo ya uhuru, usawa, na udugu yakapigiwa mbiu. Lakini Baraza hilo lilipaswa kushinda upinzani wa makasisi kabla ya kutiwa kwa aya 10 na 11, zilizotambua haki za uhuru wa kidini na usemi.

Wengi waliamini kwamba walikuwa wamepata serikali kamilifu. Hata hivyo, wangekuja kutamaushwa, kwa sababu kanisa, likiwakilishwa na Papa Pius wa 6, alilaani vikali Tangazo hilo. Wanamapinduzi wengi pia walidharau Tangazo hilo, wakaingilia umwagaji wa damu usiotosheleza kiu.

Miaka zaidi ya 150 baadaye, katika 1948, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Tangazo la Ulimwenguni Pote la Haki za Kibinadamu, lililovuviwa na yale maandishi ya Kifaransa ya 1789. Lakini leo, kama ilivyokuwa wakati uliopita, wengi wanaounga mkono kwa maneno haki hizo wanakosa kujali kabisa kanuni zilizowekwa. Jinsi yalivyo kweli maneno ya Mhubiri 8:9: “Wanadamu fulani wana nguvu na wengine wanalazimika kuteseka chini yao.”—Today’s English Version.

Kanisa Lagawanyika

Mnamo Agosti 1789 manaibu fulani walitokeza wazo la kutaifisha mali ya kanisa. Pendekezo hilo lilikuja kuwa sheria, na serikali ilitwaa mali ya kanisa. Kuongezea hayo, Baraza hilo lilitaka makasisi waape kuwa waaminifu-washikamanifu kwa Katiba ya Kiutawala ya Makasisi ambayo lilikuwa limeitayarisha.

Kanisa liligawanyika. Kulikuwako makasisi wa serikali (asilimia 60 ya makasisi), waliokubali kiapo hicho, na makasisi waliokataa kuapa uaminifu-mshikamanifu, wakabaki waaminifu-washikamanifu kwa Roma. Mgawanyiko huo ulitokeza mapambano mengi. Mara nyingi makasisi waliokataa kiapo hicho walionwa kuwa maadui wa mapinduzi hayo na wa nchi hiyo.

Hofu Kuu na Umwagaji wa Damu

Hatari za kutoka nje pia zilitisha kuangamiza mapinduzi hayo. Tawala za kifalme za kigeni zilikuwa zinafikiria kujidukiza katika mambo ya Ufaransa ili kumrudisha mfalme kwenye kiti chake cha enzi. Kwa habari ya akina yahe, walipoteza uhakika katika Louis wa 16 wakati, mnamo Juni 21, 1791, alipojaribu kutoroka nchini.

Katika masika ya 1792, kwa sababu ya upinzani wenye kuongezeka dhidi ya mapinduzi katika nchi nyingine za Ulaya, Ufaransa ilijulisha vita dhidi ya mfalme wa Bohemia na Hangari. Vita hiyo ilisambaa Ulaya yote na ikaendelea mpaka 1799, kukiwa majeruhi zaidi 500,000 Wafaransa.

Katika Agosti na Septemba 1792, mapinduzi hayo yakawa yenye kutaka mabadiliko. Mfalme alishushwa cheo, akahukumiwa kifo, na mbiu ikapigwa kwamba kumekuwa na jamhuri. Mfalme alinyongwa Januari 21, 1793, naye malkia, Marie Antoinette, akanyongwa Oktoba 16, 1793. Makasisi wengi wasioshirikiana walihamishwa. Wanamapinduzi walihisi iliwabidi kukomboa watu wale wengine ambao walikuwa wangali chini ya tawala za kifalme za mtu mmoja. Lakini pindi nyingi mwisho wa wakombozi hao pindi nyingi ulikuwa ni wao wenyewe kuwa watawala wa mabavu.

Hata hivyo, hakuna chochote kilicholeta faraja ya magumu yaliyokuwa yamezidishwa na vita. Kufuatia agizo la kuandikisha jeshini wanaume 300,000, matata yalitokea nchini. Katika magharibi ya Ufaransa, jeshi la kifalme la Katoliki chini ya alama ya msalaba na moyo mtakatifu liliundwa. Lilitwaa uongozi wa miji katika maeneo manne na kuchinja watetea jamhuri huko.

Serikali kuu ilitumia matatizo hayo kujipa mamlaka ya kidikteta katika mikono ya “Kamati ya Usalama wa Umma,” Robespierre akiwa mshiriki mwenye kutawala. Hofu kuu ikawa ndiyo kanuni ya serikali. Mara nyingi, haki zilizowekwa katika Tangazo la 1789 zilikanyagiwa chini. Mahakama za kimapinduzi zilipitisha hukumu zaidi na zaidi za kifo, na unyongaji watu ukawa mbaya sana.

Kufutilia Mbali Ukristo

Kuanzia vuli 1793, serikali ya kimapinduzi ilianzisha mpango mkubwa wa kufutilia mbali Ukrsito. Lengo lilikuwa ni kujenga “binadamu mpya” ambaye angekuwa bila uovu. Dini Katoliki ilishtakiwa kujaribu kujifaidi na ujinga wa watu. Makanisa mengine yaliharibiwa, na hali mengine yaligeuzwa kuwa kambi za kijeshi. Makasisi walilazimishwa waache kazi yao waoe. Wale waliokataa walikamatwa na kuuawa. Wengine walitoroka nchi.

Mahali pa dini Katoliki palichukuliwa na dini ya Reason. Wengine walimwona Reason kuwa mungu-mke, “Mama ya nchi ya nyumbani.” Kisha, mahali pa ibada ya Reason pakachukuliwa na dini ya miungu iliyoingizwa kwa nguvu na Robespierre. Yeye alimaliza wapinzani wake na kusimamisha udikteta wenye ukatili. Uchu huo wa damu baadaye ulimpotezesha maisha yake mwenyewe. Julai 28, 1794 aliburutwa kupelekwa kwenye mtambo wa kunyongea akiwa anapiga yowe.

Wanasiasa waliookoka walitaka kuepuka udikteta wa mtu mmoja, kwa hiyo wakakabidhi mamlaka ya uongozi kwa washiriki watano. Lakini vita ilipoanza tena na hali ya kifedha kuzorota, kumkabidhi mamlaka mtu mmoja, Napoleon Bonaparte, kulipendelewa. Njia ya udikteta mwingine ikafunguliwa.

Mapinduzi ya Ufaransa yalipanda mawazo ambayo baadaye yalikua yakawa demokrasia na udikteta mwingi. Pia yalionyesha yanayoweza kutokea wakati mamlaka za kisiasa zinapogeukia ghafula matengenezo ya dini. Katika hilo, huenda yakaandaa muono wa kimbele wa mambo ya wakati ujao.—Ufunuo 17:16; 18:1-24.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ndani ya Kathedro Notre Dame, sherehe ya ibada ya sanamu kwa ajili ya mungu-mke Reason

[Hisani]

Bibliothèque Nationale, Paris

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Kutoka taswira ya kale, ya H. Bricher sc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki