Mtengano Mpya
Na mleta habari za Amkeni! katika Ufaransa
JUNI 30, 1988, itakuwa tarehe ya maana katika maandishi ya kila mwaka ya Kanisa Katoliki la Kiroma. Siku hiyo, askofu mkuu Mfaransa Marcel Lefebvre aliikaidi Vatikani. Aliwaweka wakfu maaskofu wanne kwenye seminari yake ya mapokeo ya Kikatoliki katika Uswisi. Kitendo hiki kilifanya Lefebvre na wale maaskofu wapya wanne waondoshwe katika ushirika. Kilifanyiza mtengano wa kwanza katika Kanisa la Katoliki tangu 1870. Mwaka huo wale wanaoitwa eti Wakatoliki wa Zamani walijitenga na kanisa mama kwa sababu ya suala la kutokukosa kamwe kwa upapa.
Mizizi ya Mgawanyiko Huo
Ule ufa ulio kati ya Vatikani na harakati ya Kikatoliki ya Lefebvre ya bawa la kulia lisilotaka mabadiliko ya desturi za zamani ulikuwa umekuwa ukipanuka kwa muda fulani. Mizizi ya mtengano ni ya tangu huko nyuma kwenye Baraza la Vatikani la Pili, lililofanywa kuanzia 1962 kufika 1965. Papa John 23, aliyeitisha baraza hilo, aliweka malengo mawili kwa ajili ya kusanyiko hilo. Moja liliitwa aggiornamento (kufanya mamboleo), na lile jingine lilikuwa kuungamanisha tena yale yanayoitwa eti makanisa ya Kikristo.
Ingawa Askofu Mkuu Lefebvre, akiwa kasisi Mkatoliki, alishiriki katika Vatikani 2, hakukubaliana na lolote la malengo hayo mawili. Akiwa mshika mapokeo mkolevu, ni maoni yake kwamba Kanisa Katoliki halihitaji kufanyiwa mamboleo. Akikubaliana kwa moyo wote na maoni ya mapokeo ya Kikatoliki kwamba “nje ya Kanisa hakuna wokovu,” Lefebvre anasadiki kwamba njia ya pekee ambayo “Wakristo” wangeweza kabisa kuungamanishwa tena ingekuwa ni watu wote wasio Wakatoliki kushikamana na imani ya Katoliki ya Kiroma.
Kupinga Uhuru wa Kidini
Mwaka mmoja baada ya kuondoshwa kwake katika ushirika, Askofu Mkuu Lefebvre, akiongea kwa niaba ya Wakatoliki wanaoshikilia desturi za zamani ambao wanaunga mkono harakati yake, alijulisha rasmi hivi: “Sisi tunapinga kabisa lile wazo la uhuru wa kidini na matokeo yalo, hasa jitihada ya kuungamanisha dini zote pamoja, ambalo mimi binafsi naona halikubaliki.”
Yeye hakuwa akianzisha mambo mapya. Alikuwa akifuata kwa uaminifu pokeo la Kikatoliki. Katika Agosti 15, 1832, Papa Gregori 16 alichapisha ile barua ya kipapa Mirari vos, ambamo alilaani vikali uhuru wa dhamiri kuwa “maoni yenye makosa, au tuseme kichaa.” Miaka thelathini na miwili baadaye, Papa Pius 9 alichapisha fungu lake la Muhtasari wa Makosa, ambamo alilaani vikali lile wazo la kwamba “kila binadamu yuko huru kukubali na kufuata dini ambayo, kwa kutumia akili, anaamini ndiyo ya kweli.”
Kwa kukataa mwungamanisho wa dini zote pamoja, Askofu Mkuu Lefebvre alikuwa akionyesha tu ufungamano kwa kile ambacho fundisho rasmi la Kikatoliki linakiita ”upekee wa Kanisa”, yaani, kwamba liko tu kanisa ”Moja, Takatifu, la Kikatoliki na la Kimitume.”
Kachukizwa na Misa “ya Kiprotestanti”
Marekeebisho katika liturjia (kawaida rasmi ya ibada) katika mapokeo ya Kikatoliki yaliyotokezwa na Vatikani 2 ni habari yenye kumwuma sana Askofu Mkuu Lefebvre na wafuasi wake. Kasisi huyo mwasi anaona marekebisho hayo yalifanya Misa “iwe ya Kiprotestanti.” Suala si kutumia tu lugha za ki-siku-hizi badala ya Kilatini; Lefebvre anaona kwamba mambo mengi mno yamerekebishwa kwa kusudi la kuvutia Waprotestanti na kwamba hata katika Kilatini liturjia iliyokubaliwa na Papa Paulo 6 ni “ya kizushi.”
Ili kuhakikisha mwendeleo wa Misa ya Kilatini ya kimapokeo, Askofu Mkuu Lefebvre alianzisha seminari moja kule Ecône, Uswisi, katika 1970. Ilisimamiwa na Udugu wa Kipadri wa Mtakatifu Pius 10, ambao Lefebvre aliuwekea msingi mwaka uo huo. Harakati yake ilipopata mwendo, alianzisha seminari nyingine za Kikatoliki zenye kushikilia desturi katika Ulaya na zile Amerika. Huko mamia ya wanaume vijana wanapokea mazoezi ya kushikilia sana desturi kwa upadri.
Huyo kasisi mwasi ameagiza rasmi mapadri wa kimapokeo zaidi ya 200, ingawa katika 1976 alikatazwa na Papa Paulo 6 asifanye hivyo. Hawa wanaadhimisha Misa ya Kilatini katika nyumba za kitawa na makanisa ya Kikatoliki yanayokaliwa kinyume cha sheria.a Vatikani inakubali kwamba Lefebvre ana wafuasi karibu mia moja elfu wa kupigania mapokeo katika sehemu zote za ulimwengu, lakini maofisa wengine wa kanisa wanakiri kwamba idadi yenyewe inakaribia nusu milioni. Lefebvre mwenyewe anadai kwamba mamilioni ya Wakatoliki wanashiriki maoni yake.
Uhitaji wa Mwandamizi
Katika Kanisa Katoliki, askofu anaweza kuagiza rasmi mapadri. Hata hivyo, ni papa peke yake anayeweza kukubali kuagizwa rasmi kwa askofu. Kwa kukosa askofu wa kuagiza rasmi mapadri wapya, Lefebvre mzee-mzee alifahamu kwamba Udugu wake wa kipadri ulikuwa katika hatari ya kufifilia mbali baada ya kifo chake. Kwa wazi ikitumainiwa kwamba jambo hili lingetendeka, Vatikani iliingia katika mazungumzo marefu pamoja naye, mwishowe ikitoa neno mkataa. Ama yeye angekubali kuagizwa rasmi kwa askofu mwenye kuidhinishwa na Vatikani ama angeondoshwa katika ushirika, ikiwa angesonga mbele kuagiza rasmi askofu yeye mwenyewe.
Katika Juni 30, 1988, kwenye sherehe moja iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake, kasisi mwasi huyo aliwaweka wakfu maaskofu wanne watetea mapokeo. Gazeti la kila siku la Paris International Herald Tribune liliripoti hivi: “Kuwekwa wakfu kwa maaskofu wanne na Askofu Mkuu Lefebvre kulitilia shaka baraza moja la Vatikani ambamo papa alipandisha cheo maaskofu 24 wawe kwenye Jamii ya Makadinali. Vatikani ilifuta maonyesho fulani ya pekee ya muziki ili kuonyesha ‘maumivu yao ya kina kirefu’ kuhusu kitendo cha Askofu Mkuu Lefebvre. ‘Ni siku ya kuomboleza,’ Kadinali Decourtray [Mfaransa] akasema.”
Si kwamba tu mtengano huu ndani ya Kanisa Katoliki umesababisha maumivu katika Vatikani bali pia umeacha mamilioni ya Wakatoliki wenye moyo mweupe katika sehemu zote za ulimwengu wakiwa wamefadhaika na kuvurugika.
[Maelezo ya Chini]
a Ona makala “Askofu Mkuu Mwasi,” iliyochapishwa katika toleo la Desemba 22, 1987 la Amkeni! (Kiingereza).