Basi kwa Nini Kuivuta?
“Nikiwa mvutaji mimi mwenyewe, siwezi kupinga kwamba ni upumbavu mtupu kujiingiza katika tabia hiyo. Mtu yeyote mwenye akili ndogo ajua sasa kwamba kuvuta sigareti hutisha afya ya mtu. Ni tabia chafu, yenye kunyarafisha ambayo hugharimu kibunda cha pesa. . ..Kwa wavutaji sigareti, maisha ni msururu mrefu wa vijungu vichafu vya kuwekea majivu ya sigareti, vialama vichafu vya nikotini, alama za kuchomeka na gharama kubwa za usafishaji nguo—matokeo ya nguo zinazonuka moshi wa sigareti.”—Diane Francis, gazeti la Maclean’s, Kanada.
“Wavutaji sigareti wanaweza kutazamia maisha mafupi kuliko wale wasiovuta sigareti: kwa mfano, maisha ya mtu mwenye miaka 25 ambaye huvuta pakiti 2 kwa siku yatapungua kwa kiasi cha miaka 8.3 kwa kulinganisha na yale ya mtu asiyevuta sigareti. Wavutaji sigareti wanaelekea kufa kwa kansa kwa kiasi cha mara 3 zaidi ya wale wasiovuta sigareti.”—The Columbia University College of Physicians and Surgeons Complete Home Medical Guide.
“Kila mwaka sigareti huua Waamerika wengi kuliko wale waliouawa katika Vita ya Ulimwengu ya 1, Vita ya Korea, na ya Vietnam vikiwa vyote pamoja; karibu idadi ya waliokufa vitani katika Vita ya Ulimwengu ya 2. Kila mwaka sigareti huua Waamerika wengi kwa kiasi cha mara tano zaidi ya wale wanaouawa katika aksidenti za barabarani. Kansa ya mapafu peke yake huua kadiri kubwa ya watu inayolingana na ile ya wanaokufa barabarani. Biashara ya sigareti inauza silaha hatari.” (Seneta Robert F. Kennedy, Baraza la Kwanza la Ulimwengu la Uvutaji Sigareti na Afya, Septemba 11, 1967)—The Cigarette Underworld, iliyohaririwa na Alan Blum, M.D.
“Kwa kukadiria, tumbaku huua watu milioni mbili u nusu kila mwaka kotekote ulimwenguni. Ndicho kisababishi kimoja kilicho kikubwa zaidi, kinachoweza kuzuiwa ulimwenguni leo. . ..Ikitumiwa kwa namna yoyote, ni tabia iliyo hatari, ghali na yenye kukuza uzoevu.”—Dakt. Judith Mackay, mkurugenzi mkuu wa Kikoa cha Uvutaji Sigareti na Afya cha Hong Kong, aliyenukuliwa katika gazeti World Health.
“Ikiwa mkono ulionilisha wakati fulani uliopita ni biashara ya tumbaku, basi mkono huo huo umeua mamilioni ya watu na utaendelea kuua mamilioni zaidi watu wasipong’amua madhara ya sigareti. . .. Ninataka kuwasaidia watu wang’amue jinsi sigareti zilivyo zenye sumu.”—Patrick Reynolds, mjukuu wa mwanzilishi wa Kampuni ya Tumbaku R. J. Reynolds.
Basi, kwa nini mamilioni ya wanaume, wanawake, na vijana huvuta tumbaku? Kwa wengine wao jibu laweza kuwa msongo wa marika, tamaa ya kuonekana kuwa wa kisasa. Lakini kwa wengi jibu ni uzoevu tu ambao huongoza kwenye tamaa inayolazimisha kuvuta. Kama vile mamlaka moja ya kushauri ya kitiba isemavyo: “Sababu hasa ambayo hufanya watu wengi kuvuta sigareti ni kwamba wao ni wazoevu wa dawa ya kulevya yenye nguvu inayopatikana katika tumbaku—nikotini.”
Basi mvuta sigareti aweza kuwachaje uvutaji? Kwa kujipatia tamaa yenye nguvu ya kuwacha, yenye nguvu hata kuliko ile tamaa ya mwili kutaka nikotini. Kwa mtu anayejitahidi kutimiza viwango vya Kikristo, itamaanisha kukuza upendo kwa Mungu na jirani ambao huzidi tamaa ya mwili iliyo na ubinafsi.—Mathayo 22:37-40; 1 Wakorintho 13:5, 7, 8.
Kama vile ambavyo kitabu cha kitiba kilichonukuliwa mwanzoni kinavyosema: “Wavutaji sigareti wanaotaka kuwacha wanapaswa kukumbuka kwamba ile dawa ya kulevya nikotini huzoeleza tabia ya kuitumia, na wanapaswa kuwa tayari kukubali zile dalili zinazotatiza mwili wakati wa kuacha ni matokeo ya kiasili katika kuacha. Wanapaswa kukumbuka kwamba dalili zinaotatiza mwili wakati wa kuacha ni hali ya muda mfupi ambayo, ingawa haipendezi, haidhuru. Kila mtumizi wa tumbaku, hata awe mzoevu jinsi gani, aweza kuwacha kuvuta sigareti.”—The Columbia University College of Physicians and Surgeons Complete Home Medical Guide.
Ikiwa ungependa msaada katika kupata tamaa ya kuwacha inayohitajika ili kuwacha kuvuta sigareti, tafadhali uwe huru kuwasiliana na Mashahidi wa Yehova kwenye Jumba la Ufalme lao hapo ulipo au kupitia anwani za watangazaji katika gazeti hili.