Kuutazama Ulimwengu
Familia Zisizotazama Televisheni
Katika shule moja ambayo wengi wa wanafunzi hawatazami televisheni, walimu wanadai kwamba wao waweza kutambua kwa urahisi watoto wachache ambao hutazama televisheni sana. “Ukiona watoto wa nasari wakicheza kama mashujaa na kujifanya kuua na kukata-kata na kuumiza wengine, huo ni uthibitisho wa wazi,” akaeleza mstadi mmoja. Gazeti The Wall Street Journal liliripoti kwamba wale walioacha kutazama televisheni wamepata manufaa. Msichana mmoja mwenye miaka 17 alisema kwamba “zamani tulikuwa tukimwona baba mara nyingi kabla aende kazini. Aliporudi nyumbani alikuwa akitazama televisheni pamoja nasi, na kisha [mazungumzo ya pekee] yangekuwa ‘Lala salama baba.’ Lakini sasa twaongea nyakati zote, tuna ukaribu sana.” Yeye aliongezea kusema: “Nitakapokuwa na familia, sitakuwa na televisheni.”
Majengo Yaliyojengwa kwa Takataka?
China imegundua njia ya kipekee ya kuondoa takataka. Taasisi ya Utafiti wa Mazingira na Usafi ya Beijing hivi majuzi ilifanyiza mfumo wa kuchanganya takataka na udongo ili kutengeneza matofali. Gazeti China Today lafafanua matofali yaliyotengenezwa kuwa “matofali bora zaidi” ya kutumiwa katika ujenzi. Katika miezi michache tu, kiwanda kimoja cha matofali kilitengeneza matofali yapatayo milioni 54, “kikitumia tani 46,884 za takataka.” Baada ya kuokwa kwa joto lipatalo digrii 1,000 hadi 2,000 Sentigredi, matofali hayo yasemwa kuwa “si machafu kuliko matofali ya kawaida.”
Nchi ya Sauna
“Watu wa Finland ni watumiaji wa sauna [bafu za mvuke] zaidi ya wote ulimwenguni,” lasema gazeti Suomen Silta. Watu wengi katika Finland huoga katika bafu hiyo karibu mara moja kwa juma ili kustarehe na kujisafisha. Hali-joto huwa wastani wa digrii 80 hadi 100 Sentigredi. Kwa kawaida watu wa Finland huoga kwa maji baridi au kujitumbukiza katika ziwa mara tu baada kutoka katika bafu hiyo. Kulingana na Suomen Silta, inakadiriwa kwamba katika Finland kuna sauna zipatazo milioni 1.6. Kukiwa na idadi inayopita tu milioni tano, hilo lamaanisha kwamba nchi hiyo ya Nordi ina karibu sauna 1 kwa kila watu 3.
Kunyongwa na Chakula
Kofi mgongoni si njia bora zaidi ya kumsaidia mtu anayenyongwa na kipande cha chakula. Kulingana na Berkeley Wellness Letter, ni afadhali kujaribu kile ambacho nyakati nyingine huitwa mbinu ya Heimlich. Barua hiyo ya habari inaendelea kufafanua njia hiyo: “Simama nyuma ya mtu anayenyongwa na ufunge mikono yako kumzunguka juu ya kiuno chake. Weka ngumi yako katikati ya mfupa wa kidari na kitovu, ukiweka kidole gumba kwenye fumbatio. Shika ngumi kwa ule mkono mwingine na kisha usukume kwa haraka na kwa uthabiti kuelekea ndani na juu. Rudia-rudia mpaka chakula kitoke. Usifanye hivyo kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja, ambao huhitaji aina nyingine ya utunzi wa dharura wanaponyongwa na chakula.” Waweza kujifunza utibabu huo katika masomo ya huduma ya kwanza au ya kuhuisha watu waliozimia ambayo huandaliwa na wastadi wa mambo ya afya. Wellness Letter yasema kwamba “kufungwa kwa njia ya juu ya hewa hutokeza vifo 3,000 hadi 4,000 Marekani kila mwaka.”
Mbwa Wenye Taya Zenye Nguvu Sana
Katika New York City mwaka uliopita, kulikuwa na visa 10,753 vilivyoripotiwa vya watu kuumwa na mbwa, likasema gazeti Daily News. Kwa wastani, karibu mara moja kwa juma kulikuwa na mkabiliano baina ya polisi na mbwa uliohusu silaha. Inaripotiwa kwamba mbwa fulani waliendelea kushambulia polisi hao hata baada ya kumiminiwa risasi sita. Polisi kadhaa waliumwa, na wengine “walijeruhiwa kwa risasi zilizowarudia baada ya kugonga kitu katika hivyo vita pamoja na mbwa wakubwa wenye taya zenye nguvu,” gazeti hilo likaripoti. Wakuu wa Idara ya Polisi sasa wanahangaikia hatari ambazo risasi zilizokosa shabaha na zenye kugonga kitu na kurudi zinatokezea wanadamu wakati silaha zinatumiwa kwa mbwa wakali. Wakabiliwapo na hali hatari zinazohusu mbwa, polisi wanahimizwa kutumia njia zisizo za kuua, kama vile kuwapulizia pilipili, kunakoathiri mfumo wa kupumua.
Betri Hatari
“Kulingana na shirika la Kuzuia Upofu Utah, watu 6,000 kila mwaka huchomwa ngozi ya macho na kupata majeraha mengine ya macho kutokana na betri zilipukazo” Marekani. Gazeti Snow Country laripoti kwamba nyingi za aksidenti hizo hutokea wakati wenye magari wanapojaribu kuwasha magari yao kwa kutumia waya zilizounganishwa kwa betri ya gari jingine. Cheche kutoka kwenye betri zaweza kuwasha gesi zilizo hewani. Ili kujikinga, gazeti hilo lilipendekeza kwamba uwashapo gari kwa kutumia waya inayounganishwa kwa gari jingine, “ile waya nyeusi [iliyo hasi] yapaswa iunganishwe kwa chuma isiyo na rangi, kama vile bolti inayoonekana nje, badala ya kuiunganisha na ncha hasi ya betri hiyo. Hilo lapunguza uwezo wa umeme kurudi, jambo liwezalo kutokeza mlipuko.” Kwa kuongezea, waya zisishikane-shikane, na “wenye magari wapaswa kuvaa miwani ya kuwakinga wanapowasha magari yao kwa waya.”
Misuli Iliyopotezwa
Kuchunga ulaji kwaweza kudhuru—hasa ikiwa, katika kujaribu kupoteza mafuta ya mwili, mchunga-ulaji apoteza misuli pia. Mwandikaji wa mambo ya afya magazetini Wayne Westcott aeleza kwamba “misuli ni yenye maana sana katika mambo mengi sana tufanyayo kwa siku—usiipoteze.” Watu wasiochunga jinsi wanavyokula pia wamo hatarini ya kupoteza misuli wakiendesha maisha yasiyo na utendaji. Inakadiriwa kwamba kila baada ya miaka kumi, mtu wa kawaida asiye na utendaji hupoteza kilo 2 za misuli huku akiongeza kilo 7 za mafuta. “Kwenye kipima-uzani, hicho kingeonyesha tatizo la kuongeza uzito kwa kilo 5 (kilo 7 za mafuta kuondoa kilo 2 za misuli),” akaonelea Dakt. Westcott. “Lakini ukweli ni kwamba kwa kweli hilo ni tatizo la kilo 9 (kilo 7 za mafuta zaidi kwa kuongezea kilo 2 za misuli iliyopunguka).” Ili kudumisha afya nzuri na mwili mzuri, utendaji wa kupumua sana pamoja na mazoezi ya kupata nguvu yanapendekezwa sana.
Haki ya Kukataa Kutiwa Damu Mishipani
“Wagonjwa Wana Haki ya Kukataa Kutiwa Damu Mishipani,” kikatangaza hivyo kichwa kikuu cha gazeti Mainichi Daily News, kikiripoti juu ya pendekezo la baraza la wastadi lililopangwa na Kamati ya Maadili Kwa Ajili ya Hospitali na Hospitali za Kuzalisha za Eneo la Tokyo. Ingawa hospitali za vyuo vikuu zilizo mashuhuri tayari zimefikia uamuzi huo, huu ulikuwa ndio uamuzi wa kwanza kufanywa na serikali. Ripoti hiyo yapendekeza kwamba hospitali za Tokyo zistahi matakwa ya wagonjwa walio watu wazima wanaotaka utibabu usiohusu damu hata kama madaktari wanahisi kwamba utiaji-damu mishipani ni muhimu. “Katika hali ya mgonjwa aletwaye hospitalini akiwa hana fahamu lakini akiwa na hati inayoonyesha kwamba yeye hataki kutiwa damu mishipani, ni lazima madaktari wazingatie takwa hilo,” gazeti hilo laripoti. “Matakwa ya watoto wa shule za sekondari kuhusu utiaji-damu mishipani yatastahiwa kama kwamba wao ni watu wazima.” Hata hivyo, ripoti hiyo bado inapendekeza kwamba madaktari, wala si wazazi, ndio wana uamuzi wa mwisho juu ya utibabu wowote wa watoto wenye umri wa vidato vya chini vya shule ya sekondari na wale walio na umri mdogo zaidi.
Uwezo wa Maua
Kwa muda mrefu mimea katika kisiwa cha Madagaska imethaminiwa sana na wenyeji kwa ajili ya uwezo wayo wa kitiba. Vitu vinavyotolewa katika maua mbalimbali vimetumiwa kutibu “magonjwa kuanzia homa hadi upele-mbaya na vivimbe,” laripoti jarida Africa—Environment & Wildlife. Hata maua maridadi ya orchid ni yenye mafaa. Kwa kielelezo, aina moja (Angraecum eburneum) hutumiwa kutibu maambukizo ya virusi na katika kuzuia mimba isiharibike. Karibuni, chanzo cha dawa ya kutibu leukemia kilipatikana katika kisiwa hicho—konokono-kwekwe yenye rangi ya waridi (Catharanthus roseus). Lakini watu wataweza kunufaika na maua hayo kwa muda gani ubakio? “Jitihada inawekwa sasa,” ripoti hiyo yasema, kwa kuwa “hesabu kubwa ya aina mbalimbali ambayo hayajagunduliwa hupotea kila siku kwa sababu ya utendaji wa kibiashara kama vile kukata miti, ukulima, na uchimbaji.”
Watumiaji Tumbaku Katika India
“Kulingana na takwimu za serikali, wanaume milioni 142 na wanawake milioni 72 wenye umri upitao miaka 15 katika India hutumia tumbaku kwa ukawaida,” lasema British Medical Journal. Ripoti hiyo yaongezea kwamba “watu walio maskini hutafuna tumbaku ili kuondoa njaa.” Tumbaku ni muhimu sana kiuchumi katika India, kwa kuwa hiyo ndiyo nchi ya tatu ulimwenguni katika kukuza tumbaku, ikifuata China na Marekani, nayo imewapa maelfu ya watu kazi. Lakini, visa vya kansa ya mdomo na kansa za pharynx, kikoromeo, umio, na mapafu vimefanya ICMR (Kamati ya India ya Utafiti wa Kitiba) ihangaike. Kama vile Journal linavyoripoti, ICMR yadai kwamba “gharama ya kutibu wagonjwa wanaougua maradhi yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku itapita mapato yanayoletwa na uuzaji wa tumbaku.” Madaktari na vikundi visivyo vya kiserikali vinapendekeza kuwe na kampeni za kuelimisha watu kuhusu hatari za kiafya zitokanazo na matumizi ya tumbaku, kuondolewa kwa ukuzi wa tumbaku, na kukuzwa kwa mazao mengine.
Tatizo la Uraibu
Watu zaidi ya milioni tano nchini Ujerumani wana tabia za uraibu, kulingana na Kituo cha Ujerumani Dhidi ya Hatari za Uraibu katika Bonn. Kati ya hao, milioni 1.4 wana uraibu wa dawa mbalimbali na karibu 120,000 wana uraibu wa heroini. Watu zaidi ya 100,000 wana uraibu wa kucheza kamari. Bila shaka kikundi kikubwa zaidi kina uraibu wa kileo, laripoti Süddeutsche Zeitung, likiongezea kwamba “Wajerumani ndio mabingwa wa ulimwengu katika unywaji wa kileo.” Matumizi ya kileo katika Ujerumani hayajaongezeka tu mara tatu tangu 1950, bali kwa kulingana na makadirio zaidi ya kituo hicho, watu wapatao milioni 2.5 wanahitaji kutibiwa kwa sababu ya matumizi mabaya ya kileo.