Je! Maisha ya Familia Yaweza Kuwa Yenye Furaha Zaidi Bila Televisheni?
MNAMO Februari mwaka huu, The Wall Street Journal lilikuwa na makala hii: “Kuacha [Televisheni]: Familia Fulani Zinafanikiwa Bila Televisheni.” Gazeti hilo liliripoti: “Idadi ndogo ya familia za Wamerikani zinazoacha kabisa kutazama televisheni, maisha bila televisheni huendelea tu—ikiwa yenye furaha.”
Madhara ya televisheni kwa familia pia ilizungumzwa hivi karibuni katika muungano wa kusherehekea miaka 40 tangu Roger Bannister awe mtu wa kwanza kukimbia maili moja chini ya dakika nne. Kulingana na Jim Ryun, bingwa wa mbio za maili moja katika miaka ya 1966 na 1967, jambo hilo lilitajwa wakati wa mlo akiwa na Roger kabla ya Olimpiki za 1968.
“Mke wangu, Anne, nami tulikuwa tumechumbiana tufunge ndoa wakati huo,” Ryun akaeleza, “kwa hiyo Roger akatuambia kwamba alikuwa amegundua kitu ambacho kilifanya maisha ya familia yake yawe bora zaidi. Bila shaka sisi sote tulitega masikio kwa makini. Alisema kwamba alikuwa ameondoa televisheni nyumbani, na hivyo wamepata wakati zaidi wa kuzungumza na kusoma pamoja wakiwa familia.”
Ryun alisimulia: “Jambo alilosema lilikuwa na uvutano mkubwa kwetu. Tulianza kung’amua, ‘Kwa kweli hatuhitaji televisheni.’”
Watu kadhaa wamefikia uamuzi uo huo. Kwa nini? Kwa sababu ya athari za jinsi televisheni hunasa watu, hasa kwa vijana. Kulingana na mama mmoja katika Maryland, Marekani, alipokuwa akimnyonyesha binti yake mchanga mbele ya televisheni, mtoto huyo “kwa ghafula alikuwa akigeuza kichwa chake na kukikodolea macho kiwambo. Tukaamua kwamba ikiwa anafanya hivi akiwa na umri mdogo hivi, vipi akiwa mkubwa zaidi?” Kwa hiyo familia hiyo iliondoa televisheni yao.
Ikiwa huondoi televisheni kabisa, je, si jambo la akili zaidi angalau kudhibiti matumizi yayo? Karen Stevenson, mwanamke mweusi wa kwanza kupokea Msaada wa Rhodes kwa ajili ya masomo katika Chuo Kikuu cha Oxford katika Uingereza, alisema hivi juu ya maisha yake ya mapema: “Hatukuruhusiwa kutazama televisheni katikati ya juma. Kama [kulikuwa] na kipindi ambacho hasa tulitaka kutazama . . . , ilikuwa lazima tuongee na [mama] kukihusu Jumapili inayotangulia ili tukipangie.”
Vipi juu ya hali ya kutazama televisheni katika familia yako? Je! waona mafaa ya kuidhibiti, au hata kuiondoa, kwa muda?